WIKI iliyopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara mahususi katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Tabora akiwa na ajenda moja kuu: mapambano dhidi ya mauaji yanayoshamiri nchini ya walemavu wa ngozi (Albino).
Sitaki kurejea yale yote yaliyojiri kwenye ziara hiyo ila jambo moja kubwa ambalo limezua mjadala katika jamii. Hili ni kauli yake ya ‘jino kwa jino’ kwa maana kwamba wauaji wa walemavu wa ngozi pindi wanapokamatwa ‘ready handed’ basi hakuna haja ya kuwapeleka polisi( ila nao wauwawe).
Hii ni kauli nzito kutolewa na kiongozi mzito wakati huu ambao nchi iko katika hekaheka ya kujaribu kukomesha mauaji ya hawa ndugu zetu ambao kwa miaka mingi tumeishi nao bila matatizo.
Nianze kwa kukiri kabisa kwamba kwa mtu yeyote ambaye ni muumini wa utawala bora kwa maana ya utawala unaoheshimu na kuzingatia sheria, kuua ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya msingi ya binadamu ambayo ni kuishi. Hii hahitaji kuwa mwanasheria ili kuwa mtetezi wa haki za binadamu na utawala bora.
Lakini kuna jambo moja la msingi ambalo mpaka sasa linatatiza sana kuhusu hizi haki za binadamu na watu wanaozitetea kwa nguvu zao zote. Kwamba kuua mtu hakuna tatizo ila kuua mtu aliyeua ni kosa kubwa!
Hapo ndipo ninapoungana na Waziri Mkuu Pinda. Kwamba iweje mtu mmoja awe na haki ya kuua lakini abaki na haki yake ya kuishi? Hivi huyu aliyeuawa hakuwa na haki ya kuishi? Na kama anayo kwa nini asitetewe basi? Na kama amenyimwa haki yake ya kuishi kwa nini huyu aliyemnyima naye asipokonywe (auawe) haki yake kama alivyomfanyia mwenzake?
Hivi hapa ugomvi au utata unatoka wapi? Kabisa haingii akilini kama mtu anamuua mwenzake halafu mtu mwingine anamtetea kwamba huyu aliyeuwa ana haki ya kuishi!!! Hivi huyu aliyeuawa alikuwa hana haki ya kuishi? Au huyu aliyeuawa alikuwa nguruwe na huyu aliyeua ndiyo binadamu (mkuki kwa nguruwe...)? Kama si hivyo si dawa ya moto ni moto (jino kwa jino)? Nani hasa anamtetea huyu aliyeuawa? Haki yake itatetewa kwa kumfunga muuaji maisha? Maana watetezi wa haki za binadamu wanapinga pia adhabu ya kifo! Hawataki auawe wakati yeye ameua!
Ni katika mantiki hiyo ya kawaida unaweza kusema kwamba Waziri Mkuu alikuwa sahihi. Kilichotokea kwa Pinda ni kwamba aliweka pembeni cheo chake na kubakia na uhalisia kama binadamu. Alizungumza kama binadamu wa kawaida ambaye ameguswa na kukerwa na mauaji ya ndugu zetu Albino.
Katika hali ya kawaida huwezi kumkamata mtu aliyeua ndugu yako halafu ukampeleka polisi ukasubiri uwe shahidi? Na huko kwenye sheria huenda wakamwona hana hatia! Kama mtu anamfumania mke wake anamuua aliyefumaniwa halafu mahakama inamhukumu kifungo cha miaka kumi kwa kuua bila kukusudia iweje huyu aliyeua ndugu yako wa damu! Hivi kati ya kufumania na kuua kipi kikubwa!? Na katika hili tuweke siasa na usomi wetu pembeni, tujiweke katika uhalisia wetu.
Kweli unamkamata mtu ameua ndugu yako na ana kiungo chake, utavumilia mpaka umpeleke polisi huku ukiacha kiwiliwili cha ndugu yako hakina viungo vyake!?
Ndiyo maana nasema kwamba kitu pekee ambacho Pinda anaweza kulaumiwa ni kutamka hayo maneno hadharani. Kauli ya kiongozi ni agizo, hivyo kwa kiongozi kuagiza watu waue katika hali ya kawaida haileti picha nzuri hata kama amekerwa kwelikweli na vitendo vya mauaji ya Watanzania wasiokuwa na hatia.
Kama kiongozi angetafuta namna ya kutoa hayo maelekezo bila kuutangazia umma. Najua hata hao wanaomkosoa watakuwa wanatumia kigezo hiki lakini mioyoni mwao nafsi zitakuwa zinawasuta kwamba si rahisi kumvumilia mtu aliyeua ndugu yako eti kwa sababu ya utawala wa sheria!
Hapa ndipo umuhimu matumizi kama ya sharia unahitajika. Ndiyo, kuna vitu vingine ukianza kufuata sheria utashindwa. Ukianza kufuata haki za binadamu katika kupambana na mauaji kama haya ya albino, utashindwa. Haya ni mauaji ya kundi fulani katika jamii (minority genocide) hivyo hayana tofauti na mauaji ya Watusi ya mwaka 1994.
Haya si mauaji ya kawaida. Ni mauaji ambayo tusipochukua hatua madhubuti, jamii fulani itaangamizwa nchini huku sisi tukijifanya watetezi wa haki za binadamu! Hebu tusio Albino tujiweke kwenye nafasi yao, tufikirie hatua gani tutachukua iwapo tutakutana na muuaji wa Albino. Haya mambo tusiyachukulie kwa wepesi, kwa vile tunapata mkate wa kila siku wa kupiga zomali ya kutetea haki za binadamu.
Hili ni janga la kitaifa hivyo tufumbe macho na tulimalize kwa njia yoyote ile ili kuwanusuru wenzetu vinginevyo historia itatuhukumu.
Hata kwenye Biblia kuna wakati Mwenyezi Mungu alikuwa anateketeza kizazi chote baada ya kuona maasi yamezidi. Kwa waliosoma vitabu vya Waamuzi na Wafalme wanaona jinsi Mungu alivyokuwa anaagiza au kuwapa nguvu waamuzi na wafalme kuteketeza maadui zao. Nani anajua haki ya kuishi kuliko Muumba. Kama yeye anaruhusu kuua, iweje leo tuseme haiwezekani kuua mtu ambaye ameua Albino au mtu mwingine?
Mauaji ya Albino ni maasi katika jamii yetu hivyo ili kutokomeza tatizo hili ni vyema kutumia mbinu yoyote. Hii ni vita ambayo, mambo kama haki za binadamu inabidi tuweke pembeni.
Najua haiwezekani kuruhusu raia kujichukulia hatua mikononi, lakini katika hili la mauaji ya Albino ni tatizo maalumu.
Ni maalumu kwa sababu kundi hili la watu linatishiwa kutoweka. Sote tunakubaliana kwamba mauaji yanapolenga kundi fulani ama kwa sababu ya kabila, rangi, jinsia, hayo si mauaji ya kawaida. Kwa hiyo hata mapambano dhidi yake, lazima yasiwe ya kawaida. Ni mapambano maalumu yenye kuhitaji mbinu mbalimbali. Hii ni vita ambayo haina macho.
Naomba kuhitimisha kwa kusema, Pinda yuko sahihi kwa kauli yake kama Mtanzania mwenye uchungu wa kweli na ndugu zetu Albino. Tatizo hapa ni cheo chake na mahali alipotolea hiyo kauli. Kama kiongozi zipo njia nyingi za kufanya maamuzi bila kulazimika kutamka hadharani. Sote tunashuhudia matukio ya kibaka kuchomwa moto baada ya kukwapua simu ya mkononi au kitu kidogo tu lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, sembuse mtu aliyeua Albino!
Kila mmoja anao wajibu wa kupambana na mauaji haya ya ndugu zetu Albino. Na iwapo kila moja atatimiza wajibu wake inawezekana. Tuache kushupalia kauli kama za Pinda. Tusikae na kusubiri kukosoa kauli kama hizi kwa lengo la kujipatia umaarufu (cheap popularity). Badala yake tuwe mstari wa mbele kukemea hawa wanaogeuza binadamu wenzao kama ngazi ya kujitajirisha. Kukosoa tu hakutasaidia katika vita hii tuliyoianza.
Turejee na tujikite kwenye tatizo lenyewe ili tulimalize na kuwasaidia hawa wenzetu ambao kwa kweli wanahitaji msaada wa kila mmoja wetu ili nao wafaidi haki yao ya kuishi kwa amani kama sisi.
Toa maoni yako