Profesa atia neno kwa waliojichora tattoo, je, wanaweza kushiriki uchangiaji damu?

Na Jacquiline Mrisho

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, ametoa ufafanuzi dhidi ya taarifa zilizosambaa kwamba watu waliojichora michoro mwilini, maarufu kama tattoo, hawastahili kuchangia damu.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, hakuna uhusiano uhusiano wa kisayansi kati tattoo na uchangiaji damu. Na kwa hiyo, wenye tattoo wanaweza kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa damu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Juni 15, 2017, Profesa Janabi alifafanua kuwa damu inapochukuliwa kutoka kwa mwananchi ni lazima ichunguzwe ili kubaini kama iko sawa kwa ajili ya wagonjwa wenye upungufu wa damu.

“Wananchi wanatakiwa waelewe kuwa kinachoambukiza magonjwa sio tattoo bali ni wale wadudu waliopo katika damu, hivyo tunawashauri wananchi wote waendelee kuchangia damu,” alisema Profesa Janabi.

Alifafanua kuwa jumla ya watoto takribani 150 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo, na kwa hiyo, uchangiaji wa damu unahitajika ili kusaidia utekelezaji wa suala hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, awashukuru waliojitokeza kuchangia damu kwa hiari, akisema wamefanya jambo la maana katika kuokoa maisha ya wengine.

“Suala la kuchangia damu sio la mtu mmoja pia linatakiwa lifanyike kila siku kwa sababu hakuna mtu anayejua lini ataumwa au kupungukiwa damu mwilini kiasi cha kuhitaji kuongezewa damu. Kwa hiyo yatupasa tuchangie damu kwa hiari,” alisema DC Sophia.

Naye Mkurugenzi wa Huduma ya Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Praxeda Ogweyo, alisema kwa siku hospitali hiyo hupokea jumla ya lita 50 hadi 60 za damu wakati mahitaji ya hospitali ni lita 100 hadi 120 kwa siku.

“Hospitali inajitahidi kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchangia damu, tumeunda timu kwa ajili ya kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa manufaa ya maisha yetu sote,” alisema Praxeda.

Alitoa rai kwa wananchi, wizara mbalimbali, mashirika, taasisi na shule kufika katika kituo cha kutoa damu cha hospitali hiyo ili kuchangia damu. Vile vile amewataka Watanzania kuamini kuwa damu inayotolewa na kitengo hicho ni salama kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa.

June14 ya kila mwaka ni siku ya uchangiaji damu inayoadhimishwa duniani kote. Kwa Halmashauri ya Ilala jijini Dare s Saalam vituo vinavyotoa huduma ya uchangiaji wa damu ni Mnazi Mmoja, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Karume Mchikichini, Hospitali ya Amana pamoja na JKCI.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *