Profesa Maghembe katumwa kuivuruga Loliondo?

PROFESA Jumanne Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii, ameendelea kutoa kauli zinazoidhalilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jeuri hiyo anaitoa wapi? Maghembe, kwa mfano, ametoa kauli dhidi ya raia wa Tanzania wanaoishi katika vijiji vilivyopo tarafa za Loliondo na Sale katika Wilaya Ngorongoro.

Hivi karibuni, akifahamu kuwa anaingilia kazi ya kamati iliyoundwa na waziri mkuu, Profesa Maghembe aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kuwaambia; “Sehemu ya kilomita za mraba 1,500 za Pori Tengefu la Loliondo zitabaki kuwa hifadhi tu. Shughuli za binadamu ni marufuku ili kuokuoa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kulinda Mto Grumeti.”

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alionyesha wazi kusikitishwa kwake na mwenendo wa Maghembe. Gambo alimwonya Maghembe, bila kumtaja jina, kuacha kuingilia mgogoro unaoshughulikiwa na waziri mkuu. Gambo, akionyesha ghadhabu alisema, “Serikali inaendeshwa kiitifaki. Anapotoa maelekezo waziri mkuu,  makamu wa rais au rais pekee ndiyo wenye mamlaka kuyahoji maelekezo hayo.”

Maghembe alikaa kimya. Hata hivyo, Februari 4, 2017, R.F. Gowelle, aliandika barua yenye kumbukumbu namba PM/P/2/569/29 na kuisaini kama Kaimu Katibu wa Waziri Mkuu. Barua hiyo ilisheheni vitisho na hujuma dhidi ya vijiji vya wafugaji vilivyopo katika Pori Tengefu la Loliondo. Gowelle anaandika kuwa Pori Tengefu la Loliondo “Limevamiwa na mifugo mingi sana kupita uwezo wake wa kuibeba.”

Bahati nzuri Wilaya ya Ngorongoro ina viongozi. Viongozi hao hawanywi juisi ya maboga. Haraka sana walilifuatilia jambo hili kwa waziri mkuu. Matokeo yake Gowelle aliagizwa kuandika barua kuifuta barua yake ya awali.

Februari 17, 2017, Gowelle aliandika; “Waziri Mkuu ameagiza maelekezo ya barua hii yatekelezwe tofauti na maelekezo ya awali kupitia barua yenye Kumb. Na. PM/P/2/569/29 ya tarehe 3 Februari 2017.” Hakuna barua iliyoandikwa tarehe 3 Februari 2017 yenye Kumb. Na. PM/P/2/569/29 kuhusu mgogoro wa Loliondo. Gowelle pekee ndiye anafahamu kwa nini hataki kuitaja barua yake ya tarehe 4 Februari 2017.

Gowelle anasaini barua ya tarehe 17 Februari 2017 kama Katibu wa Waziri Mkuu. Gowelle alikuwa na vyeo viwili kati ya tarehe 4 Februari 2017 na tarehe 17 Februari 2017; yaani Kaimu Katibu wa Waziri Mkuu na kisha Katibu wa Waziri Mkuu?

Vile vile kuna utata katika barua hizi mbili zilizoandikwa na Gowelle. Ukizitazama kwa umakini, hata kama wewe siyo mtaalamu wa saini, utabaini kuwa kuna tofauti nyingi sana za saini katika barua hizo mbili. Au hiyo ilikuwa ni mbinu ya kupora ardhi kwa kufoji nyaraka? Kama ndivyo, haya siyo matumizi mabaya ya ofisi ya waziri mkuu?

Ikiwa Gowelle ndiye mwandishi wa barua hizo mbili ni nani alimtuma kwanza? Gowelle alikuwa anatekeleza maslahi ya nani kuandika barua ya kudhulumu wananchi bila idhini ya waziri mkuu? Gowelle atajiuzulu? Mamlaka husika zitamuwajibisha?

Serikali ya Dk. John Magufuli inapigana vita dhidi ya ufisadi. Baadhi ya viongozi wenye nyadhifa mbalimbali, wanalipwa kwa kodi, katika Serikali ya Magufuli wanatetea ufisadi unaonuka na wa zaidi ya miaka 20 unaondelea katika Pori Tengefu la Loliondo.

Pori Tengefu la Loliondo, mashariki mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lina ukubwa wa kilomita mraba 4,000; kama mara 17 ya eneo lote la Jiji la Dar es Salaam.

Pori hilo lipo katika vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Olorien, Maaloni, Arash, Malambo na Piyaya. Sheria ya serikali za mitaa, tawala za mikoa, namba 7 ya mwaka 1982 inavitambua vijiji hivyo. Sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inalinda ardhi ya vijiji hivyo. Sheria ya wanyamapori namba 23 ya mwaka 1974 ilianzisha Pori Tengefu la Loliondo kwenye ardhi ya vijiji hivi. Sheria hii haikubadilisha hadhi ya vijiji hivi wala haki za ardhi za vijiji husika. Mkurugenzi wa wanyamapori anasimamia wanyamapori na kugawa vitalu vya uwindaji kwa kampuni za uwindaji.

Kashfa ya Loliondogate ilianza 1992 serikali ilipompa kibali cha uwindaji mwana-mfalme Brigedia Mohamad Al-Ali kinyume cha sheria. Sheria iliagiza kuwa kampuni ndiyo inapewa kibali cha uwindaji, siyo mtu binafsi kama serikali ilivyompa Al-Ali.

Tarehe 11 Novemba 1992 Waziri wa Utalii, Maliasili na Mazingira, Abubakar Mgumia, alimpa kibali cha uwindaji kinyume cha sheria Brigedia Al-Ali ili awinde katika Pori Tengefu la Loliondo kwa miaka 10, sheria hairuhusu kibali zaidi ya miaka mitano.

Kwanza, Waziri Mgumia alivunja kifungu namba 4(1-2) cha Sheria ya Mashirika ya Umma namba 17 ya 1969 iliyoagiza kuwa kampuni binafsi ni lazima zilete wageni wao kuwinda kupitia shirika la umma, Tanzania Wildlife Corporation, kwa kifupi TAWICO.

Pili, Waziri Mgumia alivunja Sheria ya Wanyamapori namba 12 ya 1974 kwa kulipokonya shirika la umma, TAWICO, Pori Tengefu la Loliondo 1992. Wizara iliipa kibali cha uwindaji kwa miaka mitano TAWICO kuanzia Januari 1991 hadi Desemba 1996.

Mkurugenzi wa wanyamapori wakati huo, Muhidin Ndolanga, alipinga uharamia huo. Ndolanga alisema haingii akilini kulipokonya shirika la umma eneo tena kwa kuvunja sheria. Ndolanga alitabiri pia kuwa wanyamapori Loliondo wangetoroshwa kwenda nje.

Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 kashfa hii ya Loliondogate ikapata sura mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Mwezi Julai 2009 serikali ilichoma moto makazi ya wafugaji katika vijiji halali na kuwafanyia wafugaji kila aina ya ukatili. Lengo la uharamia huo ilikuwa ni kuilinda kampuni ya uwindaji kutoka Dubai. Kampuni hiyo ndiyo chanzo cha mgogoro wa ardhi katika tarafa za Loliondo na Sale.

Tarehe 20 Januari 1993 gazeti la Mfanyakazi lilichapisha habari yenye kichwa cha habari “Tanzania ‘inavyoliwa’ na Waarabu.” Habari ile, iliyoandikwa na marehemu Stan Katabalo, ilidai kuwa tarehe 18 Januari 1993 dege lenye namba za usajili A6-HRM kutoka Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu lilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Dege lile lilikuja kuwachukua wanamfalme Al-Ali na mawindo yao pamoja na wanyama waliowakamata wakiwa hai bila kibali cha Serikali ya Tanzania.

Gazeti la New York Times la tarehe 13 Novemba 1993 liliandaka habari iliyodai kwamba wawindaji kutoka familia ya kifalme ya Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu waliwinda wanyama kikatili Tanzania. Wanyama wale walikuwa ni pamoja na wanyama walio katika hatari ya kutoweka kabisa duniani kama vile duma na mbwa mwitu.

Alipobanwa na vyombo vya habari, Mgumia, alikiri kuwa wageni wale wa kifalme walifanya uhalifu. Waliwinda wanyama wengi kuliko wale walioruhusiwa kisheria.

Waliwakamata wanyama hai kinyume cha sheria. Mgumia alikiri pia kuwa baadhi ya wanyama wale walifia KIA kwa mujibu wa Sunday News la tarehe 21 Machi 1993. Haina tofauti na wale twiga walisaofirishwa kwenda Pakistan miaka ya hivi karibuni.

Tarehe 20 Novemba 1992, ikiwa ni ndani ya siku 10 tu tangu Waziri Mgumia alipompa kibali cha uwindaji Brigedia Al-Ali kinyume cha sheria, mkataba uliwekwa saini na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ngorongoro. Viongozi wa vijiji sita walikataa, katakata, kuridhia Brigedia Al-Ali kuwinda kwenye ardhi ya vijiji vyao.

Mawakala wa wapora ardhi ya wafugaji Loliondo kila siku wanaibuka na propaganda nyingine dhidi ya wafugaji. Waingereza wanasema, “Ukitataka kumnyonga mbwa mpe jina baya.” Madai ya mawakala wa wapora ardhi kuwa wafugaji wanaharibu mazingira Loliondo yanalenga kupotosha umma ili kuhalalisha uporaji wa ardhi ya vijiji vya wafugaji. Wafugaji walipoteza kilomita za mraba karibu 15,000 kupisha Hifadhi ya Serengeti. Mchango wao katika uhifadhi Tanzania hauna kifani.


0754 453 192

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *