Raha na karaha za mitandao ya kijamii

WIKI iliyopita, Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, ilimhukumu kijana mmoja mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti kijana wa kiume ambaye ni mwanafunzi katika shule moja ya sekondari jijini. Utekelezaji wa kosa hilo la ulawiti umethibitishwa kuwa ulichochewa na mawasiliano ya wawili hao kupitia mtandao wa Facebook ambako ndiko walikofahamiana hadi kufikia kutenda kosa hilo.

Niliposoma habari hiyo kwenye gazeti moja, ikanikumbusha matukio kadha ya kiuhalifu yanayochochewa na mitandao ya kijamii. Aidha ikanikumbusha pia taarifa moja ya utafiti iliyotolewa majuma mawili yaliyopita ikieleza kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kusababisha watumiaji kukumbwa na magonjwa ya akili.

Nakumbuka mwaka 2012, mahakama moja ya Afrika Kusini, ilimtia hatiani kijana aitwaye Thabo Bester maarufu kama ‘Magagula’ na kuhukumiwa kifungo cha miaka 50 jela kwa kupatikana na hatia ya kuwapora, kuwabaka na kuwaua wanawake kadhaa nchini Afrika Kusini baada ya kuunganishwa na mtandao huo huo wa Facebook.

Magagula, kijana mtanashati, alitafutwa na polisi kwa ubakaji na mauaji ya wasichana warembo kwa muda mrefu, lakini baadaye alijisalimisha polisi jijini Johannesburg baada ya kuona jitihada zake za kujificha haziwezi kufua dafu. Wasichana watatu waliripotiwa kutendewa unyama na baadaye kuuawa na Magagula baada ya kufahamiana kupitia Facebook.

Uhalifu kupitia Facebook umewahi kukikumba pia kikundi kimoja cha muziki Afrika Kusini, ambacho kilitapeliwa Rand 3,000 na watu waliojifanya waandaaji wa tamasha la muziki nchini humo. Yapo matukio mengi ya uhalifu ambayo yamechochewa na mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook, Whatsapp, Telegram, Tango, IMO, Instagram na mingineyo mingi inayoibuka kila kukicha.

Mitandao hii ya kijamii huanzishwa kwa nia njema lakini ubaya huja kwenye matumizi yake. Ilikuwa ni Februari 2004 ambapo Facebook ilianzishwa na Mark Zuckerberg wakati huo akiwa ni mmoja wa wanafuzi katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.

Lengo la awali kabisa la kuanzisha Facebook ilikuwa ni kwa wanafunzi kuwasiliana kwa urahisi na kubadilishana nyaraka mbalimbali kwa ajili ya masomo yao. Baada ya kukua, mtandao huu ukatumika kama njia ya kuwaunganisha ndugu, jamaa na marafiki waliopoteana kwa miaka mingi.

Hadi sasa tafiti mbalimbali zimefanywa na zinaendelea kufanywa na wanazuoni juu ya matumizi ya Facebook na mitandao mingine ya kijamii. Mwaka 2009, Jane Lewis na Anne West kutoka London School of Economics nchini Uingereza, walifanya utafiti kuhusiana na wanafunzi wanaoutumia mtandao huu wa kijamii. Moja ya mambo waliyobaini ni kwamba pamoja na kuwa neno ‘rafiki’ ndilo huwaunganisha watumiaji, lakini ukweli ni kwamba kuna zaidi ya urafiki katika muunganiko huo. Wapo maadui wanawasiliana kwenye mitandao ya kijamii kwa kivuli cha urafiki.

Ni jambo la kawaida kumkuta mtumiaji ana marafiki 5,000 kwenye facebook na maelfu wengine kwenye mitandao mingine ya kijamii. Lakini ni kweli wote ni marafiki? Wote wana nia na malengo yanayofanana? Wanasaikolojia wanaeleza kuwa hata ukiwa na marafiki wengi kiasi gani kwenye mitandao ya kijamii, ni marafiki kati ya 150 na 260 tu ndio ambao mnaweza kufahamiana ndani na nje ya ya mitandao ya kijamii. Na hao ndio marafiki wa kweli, sio wale maelfu uliounganishwa nao.

Watafiti Jane na Anne walibaini kuwa idadi kubwa ya marafiki katika Facebook na mitandao ya kijamii, haionyeshi kuwa wewe ni maarufu sana ama mkarimu ndani na nje  ya mtandao huo, bali ni dalili ya mtumiaji kutokuwa na vigezo vya watu wanaostahili na wasiostahili kuwa marafiki zake. Hii ni moja ya adha ya Facebook, kujionyesha hadharani udhaifu wako wa kutokuchuja jema na baya.

Hivi sasa watumiaji wa mitandao ya kijamii hutumia saa kadhaa kwa siku wakiperuzi kurasa moja baada ya nyingine mitandaoni. Ufanisi wa kazi umeshuka kwa kiasi kikubwa huku baadhi ya fisi zikiweka katazo la matumizi ya simu ama mitandao ya kijamii nyakati na mahala pa kazi. Matumizi haya yamesababisha uraibu ambao watafiti wanaeleza kuwa hali hiyo ndio husababisha hata watu kupata kichaa na magonjwa ya akilii kutokana na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani, umebaini kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za talaka, na asilimia 81 ya ongezeko hilo, imesababishwa na mitandao ya kijamii. Wenza wengi wamejikuta sio waaminifu wanapokuwa watumiaji wa mitandao hii ya kijamii, na matokeo yake kuwa na ugomvi mwingi na kuishia kutalikiana.

Tukitazama suala la uhalifu, tumeona hapo awali jinsi Magagula na kijana wa OUT walivyofanikiwa kutumia Facebook kutekeleza uovu wao. Magagula alitumia Facebook kuwapata wasichana warembo Afrika Kusini, lakini mwisho wa siku lengo lake lilikuwa ni kuwaibia, kuwabaka kisha kuwaua. Wapo watu wengi kama Magagula ambao wamepata teknolojia mpya ya kutenda uhalifu na njia hiyo ni kutumia mitandao ya kijamii.

Licha ya uhalifu, mitandao ya kijamii imekuwa kichocheo kikubwa katika kusambazwa picha zisizofaa na kuwaingiza vigogo na watu maarufu katika kashfa na kuvunjiwa heshima. Miezi michache iliyopita, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini na mpigania uhuru kupitia Jeshi la ANC (Umkhonto we Sizwe), Kebby Maphatsoe, alijikuta akiingia katika kashfa kubwa baada ya picha zake za utupu kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii nchini kote. Picha hizo zinadaiwa kupigwa hotelini na mwanamke (sio mkewe) ambaye aliingia naye hotelini hapo.

Ukiangalia mwenendo huu wa mitandao ya kijamii na matumizi yake, utaona dhahiri kuwa teknolojia inayokuja kwa nia njema, sasa inaanza kutupeleka kubaya kutokana na matumizi yasiyo sahihi. Inabidi jamii ijitazame upya ili kuepuka kutokea makubwa zaidi ya yale aliyoyafanya Magagula ama aliyoyafanya kijana mwanafunzi wa OUT ama kashfa iliyomkumba Maphatsoe na kumharibia sifa yake kwa familia yake na umma mzima wa Waafrika Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *