Rais Magufuli: Fyekavichwa magoliati kuokoa Edeni inayoteketea [2]

“Wakajazwa kasumba za utamaduni wa kimagharibi… wakawa kama kasuku mbele ya ndugu zao” (Franz Fanon, katika “The Wretched of the Earth”/Viumbe Waliolaaniwa).
MIAKA ya 1990 – 2000 kilikuwa kipindi cha mabadiliko makubwa katika uchumi na siasa za dunia ambapo Afrika na nchi za dunia ya tatu kwa ujumla, zilinaswa katika utando mpya wa ukoloni mamboleo na ubeberu wa kimataifa ulioficha makucha ndani ya mabadiliko hayo.
Nchi za Afrika, pengine kuliko nchi zingine duniani, ziliingiliwa kirahisi kutokana na uchumi wake ulioharibika na kwa sababu ya viongozi dhaifu, walafi, mafisadi na mamluki wa nchi za magharibi kutosimama imara kutetea wanyonge wa nchi zao.
Kwao usaliti kwa nchi na wananchi wao kwa “vipande thelathini vya dinari” ilikuwa sifa na staili mpya ya kuongoza kwa madai ya kupanua wigo wa mahusiano ya kimataifa (bila uchambuzi wa madhara yake) chini ya dhana ya utandawazi. Tanzania ambayo hapo mwanzo ilisifika duniani kwa mawazo na fikra za kimapinduzi kwa wanyonge, haikusalimika kwa ujio wa ukoloni huo mpya.
Nani asiyejua, kabla ya hapo, jinsi jamii ya kisomi ya Kitanzania, hususani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kilivyokuwa kitovu cha fikra na harakati za kimapinduzi ambapo mifumo ya siasa, utawala na uchumi wa dunia,vilivyoweza kuwekwa mezani na kuchambuliwa kama karanga kubainisha mifumo kandamizi isiyofaa kwa maendeleo ya binadamu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa mstari wa mbele wa harakati hizo?
Chambuzi hizo za kimapinduzi ndizo zilizozaa sera zenye utu na ubinadamu kwa nchi: Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Tanzania ilikuwa bingwa wa haki za binadamu na usawa wa kimataifa. Kile pekee kwa Dar es Salaam kuwa Makao Makuu ya harakati za Ukombozi barani Afrika, na kwa Mwalimu Nyerere kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ushirikiano wa Nchi Masikini duniani (South –South Commission), ni ushahidi tosha wa hayo.
Aidha, kama si ubeberu wa kimataifa kuzivuruga nchi za Afrika Mashariki, kuanzia na mapinduzi ya kijeshi ya Idi Amin dhidi ya serikali ya mwanaharakati, Dk. Milton Obote nchini Uganda mwaka 1972, azma ya kuona Shirikisho imara la nchi za Afrika Mashariki likiundwa kwa ushawishi mkubwa wa Tanzania, ingetimia mapema.
Hadi Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC) kuelekea Shirikisho ikivunjika mwaka 1976, ilikuwa kubwa, yenye nguvu na mafanikio kuliko hata ilivyokuwa Jumuiya Nchi za Ulaya (EEC sasa EU). Adui wa yote haya ni ubeberu wa kimataifa kwa kuwatumia viongozi mamluki kutibua juhudi zetu za kujikomboa.
Nani hakujua nguvu ya ushawishi wa Mwalimu na Tanzania kwa viongozi wa Afrika juu ya harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni-mamboleo na ubeberu wa kimataifa, kiasi kwamba kila alipopiga yowe ya vita nao waliitikia hima?; alipopiga chafya nao wakapata mafua?.
Mfano, Mwalimu alipoanzisha Azimio la Arusha, Ujamaa na Kujitegemea; Rais wa Misri, Gamal Abdel Nasser alitunga “The Charter” kwa mfumo, maudhui na madhumuni hayo hayo; Sekou Toure wa Guinea akasimika “The Guinean Revolution”; wakati Obote alianzisha “The Common Man’s Charter”; Dk. Keneth Kaunda wa Zambia “Zambian Humanism”. Naye Rais Jomo Kenyatta wa Kenya akaibuka na “Session Paper Number 10” iliyoandaliwa na wakala mmoja wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) aliyekuwa akifanya kazi chini ya Waziri wa Mipango ya Maendeleo ya Uchumi wa Kenya, Tom Mboya.
Hata madikteta walishika mafua Mwalimu alipopiga chafya, kama Jenerali Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC) aliyelazimika kuanzisha kile alichokiita “African Authenticity”. Tanzania ilikuwa tanuri la ukombozi wa kweli; ilikuwa bustani ya Edeni ambamo binadamu/Mtanzania huru aliishi kwa usawa, matumaini na amani.
Kuondoka madarakani kwa Mwalimu mwaka 1985 kulitoa mwanya wa kutunguliwa kwa Azimio la Arusha, Ujamaa na Kujitegemea kwa shinikizo la mashirika ya ubeberu wa dunia – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na kwa watawala kuahidiwa misaada kwa sharti la kufufua demokrasia na uchumi; eti kwamba sera za “utu” na usawa hazikuwa na tija katika kukuza uchumi wa nchi, ila kwa njia ya soko huria na ubinafsishaji usiojali.
Tukaambiwa, serikali haipaswi kupanga na kusimamia uchumi wa nchi kwa manufaa ya watu wake; kwamba nguvu ya soko huria itafanya kazi hiyo. Ilikuwa mithili ya nyoka Ibilisi wa msahafu kumdanganya Adamu kula tunda la mti wa mema na mabaya bustanini Edeni alilokatazwa na Mungu.
Cha kushangaza ni kwamba, ni WB na IMF haohao ambao miaka ya 1960 walipiga vita sera za soko huria kwa nchi za dunia ya tatu kwa kusisitiza umuhimu wa serikali katika kupanga na kusimamia uchumi kuleta maendeleo ya kweli. Na kwa msingi huo, mwaka 1965, Rais wa WB wa wakati huo, Robert McNamara, aliisifia Tanzania kwa mipango thabiti ya uchumi akisema ilikuwa mfano wa kuigwa na nchi zote za dunia ya tatu.
Iweje miaka ya 1990 WB na IMF haohao waje na shinikizo la sera za soko huria kwa madai kwamba s erikali kupanga uchumi ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo?
Ikatolewa orodha ndefu ya masharti ya kufuatwa ili tustahili kupewa misaada, yakiwa ni pamoja na: Kupunguza thamani ya fedha, ikaitwa “fedha ya madafu”; kuondoa ruzuku kwa bidhaa muhimu kwa mlaji; kupunguza kodi kwa bidhaa kutoka nje; na kuongeza bei ya bidhaa za kilimo zisiweze kupenya soko la nje kwa sababu ya kuwa aghali.
Masharti mengine ni kubinafsisha au kufunga mashirika ya umma ili kuruhusu sekta binafsi kutamba; kuondoa Tume ya Bei ili wasio na uwezo kifedha wanyukwe kwa bei zisizodhibitiwa; serikali kupunguza matumizi, kupunguza kukopa na hivyo kusitisha utoaji huduma au ruzuku kwa wananchi kama vile elimu na tiba; kuondoa vizuizi kwa “wawekezaji” kuhamishia (kutoroshea) nje fedha, na masharti mengine lukuki.
Nasi kwa ujinga wetu, mwaka 1986 tukazilaki kwa furaha bila udadisi sera hizo za kurekebisha uchumi (SAPs); na mwaka 1992, tukalitungua Azimio la Arusha kwa mzinga wa Azimio la Zanzibar.
SAPs zilitanguliwa na zoezi la kupigwa msasa viongozi na wasomi nchini waweze kucheza ngoma kwa mhemko kwa mdundo wa WB na IMF. Warsha na makongamano yakapewa kipaumbele badala ya mipango ya maendeleo kana kwamba nchi haikuwa na wasomi ila kwa kurudishwa “darasani” kujifunza upya; fulana, kofia na vipeperushi na wawezeshaji, vikatafuna sehemu kubwa ya mikopo na nchi kuingia madeni yasiyolipika.
Kwenye warsha na makongamano, injili iliyohubiriwa ni “maendeleo ya vitu” na si “maendeleo ya watu” kwa sababu uchumi wa soko ni unyama kwa kila mmoja kuishi na kubakia hai kwa ukali wa meno yake; eti kwamba “Ujamaa” na haki sawa zilikuwa njozi za juzi za Usoshalisti na Ukomunisti.
Semina na makongamano haya yaliwahusu pia viongozi wa kisiasa ambapo wao, Mawaziri na Wakuu wa Mikoa walipelekwa nje ya nchi; au zilifanyika kwenye hoteli za kitalii kama Ngurdoto na si kwenye kumbi za Kiserikali tena, kama vile Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa, Arusha (AICC), kuwaonesha wakubwa hao “utukufu” na harufu ya mitaji kwa uhai si wa jamii tena, bali kwa “kila mtu na lwake” hivi kwamba asiye nacho ajilaumu yeye na Mungu wake.
Makongamano, warsha na semina za SAPs zenye kufadhiliwa na WB na IMF zilizalisha wanasiasa na wasomi “mazezeta”, mateka wa ukoloni mamboleo kwa usaliti mkubwa kwa watu wao. Kati ya hao, baadhi yao walianza kusifia na kuimba “utukufu” wa utandawazi; wengine kwa ujinga, kujikomba na kwa kusaliti umma wa wanyonge, walisherehekea “maslahi” ya siasa na uchumi huria kwa kuwania malisho mapya binafsi kwa mgongo wa jamii.
Kwa tabaka hili lenye kujazwa kasumba ya mambo mapya ya “majuu”, ambalo kwa makosa tunaliita “wanasiasa wasomi”, masuala ya usawa na haki za kijamii yakawa hayaingiii akilini mwao na kuchukuliwa kama masalia ya kijamaa ya juzi yasiyotakiwa; maadili na miiko ya uongozi ikatoweka; mkataba wa kijamii kati ya watawala hao na wananchi (Social Contract) ukabezwa kwa viongozi kujifanyia mambo wapendavyo bila hofu ya kuhojiwa wala kuwajibishwa; wakataka kutumikiwa badala ya kutumikia.
Kufikia hapo, nchi ikawa imetekwa kupitia viongozi na wasomi mamluki kuthibitisha anachokisema Franz Fanon kwamba: “Wakachaguliwa vijana walioonekana wanaweza kutegemewa, nao wakajazwa kasumba za utamaduni wa kimagharibi uliojaa maneno yasiyo na maana yoyote, yakawajaa kinywani, wakawa kama kasuku mbele ya ndugu zao….”.
Kwa kuwa chini ya sera za WB na IMF “Maendeleo” maana yake ni maendeleo ya vitu na si ya watu, viongozi sasa walijikita zaidi katika kujitajirisha kwa kufukuzia utajiri binafsi na vitu badala ya maendeleo ya wananchi na kuzaa fungate kati ya utajiri na uongozi, na kile kinachoweza kuitwa “utajiri kununua siasa na siasa kununua utajiri” kwa maana ya viongozi kujitajirisha kwa nyadhifa zao, na wenye fedha kununua uongozi kwa njia ya rushwa.
Miongoni mwa hao walikuwa vijana wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere wasiobanduka ubavuni mwake kipindi chake!.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, aliyepigiwa debe na Mwalimu Nyerere kukalia kiti hicho mwaka 1995 akimnadi kama “Mr. Clean” (mtu msafi), anasifiwa na nchi za magharibi, WB na IMF kwa kuwatukana watu wake mwenyewe (Watanzania) kwa kuwaita “wajinga, wenye wivu na wavivu wa kufikiri” kwa kushindwa kumwelewa juu ya “manufaa” ya utandawazi na sera za mashirika hayo.
Na kwa kuwatukana hivyo watu wake, Mkapa alizawadiwa Uenyekiti Mwenza wa Tume ya Dunia ya Utandawazi, yeye na Mama Tarja Hallonen wa nchi tajiri ya Finland.
Lini na wapi nchi masikini na nchi tajiri zikazungumza lugha moja, maana bila kuzifukarisha nchi za dunia ya tatu, utajiri kwa nchi zinazojiita tajiri utakuwa ni ndoto! Iweje wasomi wetu leo kufungua mazungumzo na Goliati au Lishing’weng’we kama si ghiliba na usaliti uliopitiliza?
Kwa ushawishi wa ubepari wa kimataifa, nchi yetu imekuwa moja ya nchi masikini duniani yenye kupokea mikopo mikubwa ya kifedha na ya kiufundi, kiasi kwamba, utii na uwajibikaji wa viongozi umehama kutoka kwa wananchi wanaowaongoza kwenda kwa wafadhili na wafanyabiashara wakubwa wanaoweza kulainisha mifuko yao bila kuhofia gadhabu ya umma unaoumia kwa sababu tu “kaka mkubwa” anawalinda wasaliti hao, mithili ya msemo wa kimsahafu kwamba: “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa baba yenu (ubepari, ubeberu wa kimataifa) ameona vema kuwapa ule (ulaji, uporaji wa jasho la wanyonge) ufalme” (Luka 12:32).
Maswali yanayoulizwa leo na wasaliti hawa ni ya kushangaza kwamba, badala ya kujikita juu ya namna masikini walivyosukumwa kwenye lindi la umasikini na wanaendelea kuwa hivyo; wao wanajikita kuhesabu idadi ya masikini kwa kuhoji, “ni wangapi walio masikini: masikini wa kati, masikini sana; na itachukua muda gani kuumaliza umasikini kwa kutembeza bakuli la “ombaomba?”.
Kwa msingi wa maswali haya, nchi yetu iliyokuwa ya kimapinduzi, imegeuzwa chaka la mazezeta,“masikini” kwa kujitakia, wanajipanga mstari, vibakuli mkononi kusubiri misaada ya kupunguza makali ya umasikini kwa kutelekezwa na wasaliti, huku sekta binafsi,yenye kuabudu maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu ikipigiwa debe na kusifiwa kama “injini au treni ya maendeleo”.
Mgogoro wa sasa katika uchumi wa dunia hautokani na mapenzi ya Mungu, bali ni mkakati wa siasa za ubepari uliojikita kwenye maovu pacha, ulafi wa mali, uchoyo na maadili duni miongoni mwa viongozi kwa kushirikiana na uchafu wa kitabaka wa nchi za Magharibi kuruhusiwa kuweka na kusimamia ajenda ya maendeleo badala ya ajenda hiyo kuwekwa na wananchi wenyewe.
Viongozi hawa, kwa kuvimbiwa vinono vya “majuu”,wamediriki kuwaita watu wao “wajinga” na “wavivu wa kufikiri” wanapohoji juu ya sera hizi.
Ndiyo maana hatukushangaa kuona serikali mbili za awamu za mwisho, zikiwaalika nchini, Manungayembe ya uchumi wa kibepari na soko huria kama Jeffrey Sachs na Gordon Brown, kuja kutuhubiri injili ya utandawazi zenye kutetea sera za uporaji rasilimali kwa nchi masikini unaofanywa na nchi za magharibi; eti kwamba wanataka kuutupa umasikini wetu kwenye jumba la Makumbusho ubakie historia. Ni uzezeta huu unaofanya baadhi ya viongozi wetu kurandaranda kwenye miji mikuu ya mataifa makubwa, wakimwaga “umombo” uchwara kujipendekeza waonekane “watoto wazuri”, wenye adabu, watii na waitika wito wa ajenda ya maendeleo iliyotekwa nyara na nchi hizo.
Na wanaporejea nyumbani kujipanga mstari na bakuli mkononi kusubiri misaada kutoka nchi hizo, na kwa kufungua milango hadi bawaba ya mwisho kwa “wawekezaji” kutoka nchi hizo,hicho tunachopata (ikiwa ni pamoja na vyandarua tena kwa masharti ya kuuza uhuru wa nchi), ni kiduchu mara 90 ya kile tunachoporwa kwa njia ya “uwekezaji” usiojali kupitia mikataba mibovu na ya kifisadi.
Uropokaji wa kina Sachs na Brown (Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, mchumi) unapingwa vikali na Wazungu wenzao kama William Easterly ambaye katika kitabu chake “The Whiteman’s Burden” akisema, “Dhana ya maendeleo inayopigiwa debe na kina Sachs na Brown haina mashiko kwa nchi za dunia ya tatu kwa kuwa ni ya kibeberu na kinyonyaji, hivi kwamba, maendeleo ya uchumi yanayosemwa kupatikana ni kwa tabaka la walio nacho (wenye mitaji) pekee na kamwe hayamfikii wala hayana maana kwa mtu wa chini”.
Na huo ndio ukweli wenyewe; kwamba wakati tunaambiwa na wanasiasa kuwa uchumi wetu unakua kwa mwendo wa kupaa, wananchi wetu wanaendelea kuwa masikini kuliko mwanzo, na pengine masikini zaidi kuliko walivyokuwa kabla ya Uhuru !
Kuna mantiki katika malalamiko ya Waziri wa Fedha wa Uganda, kwenye mkutano mmoja wa Kimataifa juu ya “Mikataba ya Uwekezaji wa Makampuni ya kuhodhi ya Kimataifa (MAI), kama alivyonukuliwa na John Pilger, katika kitabu chake “Hidden Agenda” (1988) – “Ajenda Iliyofichika”, akisema: “Tuliambiwa, kama tutakuwa na demokrasia, tutapata mapesa; tukaiga demokrasia kwa tafsiri yao, lakini hakuna mapesa yaliyotolewa. Tukaambiwa, kama tungekuwa na mipango ya kurekebisha uchumi (SAPs), uwekezaji kutoka nje ungefurika; tukarekebisha uchumi wetu kwa masharti yao, lakini hakuna fedha iliyokuja”.
“Tena tukaambiwa, kama tungekuwa na soko huria na kubinafsisha sekta ya umma, uwekezaji ungekuja; tukakaribisha soko huria na kubinafsisha taasisi za umma, lakini hakuna kilichotokea. Sasa tunaambiwa, tutapata mapesa kama tukiingia mikataba na makampuni makubwa ya kimataifa ya kuhodhi!. Ninyi (wazungu) ni walaghai wakubwa, mnajaribu kuidanganya Afrika”.
Heri ya waziri huyu mzalendo wa Uganda, aliyeng’amua mapema ulaghai huo wa nchi za magharibi kwa manufaa ya taifa lake. Na sisi tusemeje juu ya viongozi na wasomi mateka wa ulaghai huu kufikia kuwaita watu wao “wavivu wa kufikiri”?.

One thought on “Rais Magufuli: Fyekavichwa magoliati kuokoa Edeni inayoteketea [2]”

  1. Ali Ben Himidi says:

    Upinzani Wa TANZANIA Visiwani Na Bara ,Wanapaswa Kujitathmini /Wajione,Wajikosowe ,Wajilaani
    Kwa Kujisuta Kwenye Ukweli Wa Yaliyomo Kwenye Makala Hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *