Rambirambi za ajali ya wanafunzi kaa la moto

MALUMBANO yameibuka baina ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na baadhi ay viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu matumizi ya fedha za rambirambi kwa ajili ya familia za wanafunzi 32 waliofariki dunia katika ajali ya basi dogo la Shule ya Lucky Vicent.

Katika ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu, walimu wawili na dereva wa basi hilo aina ya Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T 871 BYS pia walipoteza maisha na kufanya idadi ya waliofariki kuwa 36.

Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Rhotia katika mteremko mkali na wenye kona nyingi wa mto Marera ambapo dereva wa basi hilo akiwa katika mwendo mkali alishindwa kumudu usukani wa gari na kutumbukia korongoni.

Hata hivyo wiki moja baada ya ajali Mkuu wa Mkoa ameingia katika malumbano na viongozi wa chama hicho cha upinzani akidaiwa “kuhodhi” shughuli zote za msiba huo na hakuna uwazi katika matumizi ya michango ya rambirambi kwa wafiwa iliyochangwa na wadau mbalimbali.

Malumbano hayo yalianza baada ya Gambo kupitia mitandao ya kijamii hasa ukurasa wake wa mtandao wa Face book kutoa mchanganuo wa fedha zilizopatikana na jinsi zilivyotumika.

Katika mchanganuo huo Gambo alieleza kuwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita walipokea shilingi milioni 215 na wamegawa kwa kila familia ya  wafiwa kiasi cha shilingi 3,850,000 kama rambirambi.

Kwa mujibu wa Gambo fedha hizo ni nje ya gharama zingine zilizotolewa na serikali kugharimia mazishi ya wanafunzi hao, ikiwa ni pamoja na kusafirisha miili, kununua majeneza na kuwalipa madereva posho ya kusafirisha miili hiyo.

Katika maelezo yake Gambo pia amerekodiwa katika video inayomwonyesha akitoa ufafanuzi wa mchanganuo huo na Raia Mwema imepata nakala hiyo.

“Hadi sasa tumepokea kiasi cha shilingi milioni 215 kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao walitoa shilingi milioni 100, Baraza la Wawakilishi na  Wizara ya Elimu ya Zanzibar na wadau mbalimbali,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza: “Hadi sasa matumizi ambayo yamefanyika ni milioni 190 ambazo zimetumika kwa kila familia kupewa shilingi 3,850,000, pia fedha zimetumika kugharimia taratibu zote za mazishi, kama usafiri na posho ya madereva kupeleka miili ya waliofariki kunakohusika”

Hata hivyo juhudi za kumpata kutoa ufafanuzi wa kauli yake hiyo hazikuweza kufanikiwa kutokana na mkuu huyo wa mkoa kutopokea simu yake ya mkononi kila alipopigiwa.

Chadema waibua utata

Akizungumza Jumatatu wiki hii na waandishi wa habari Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema hawakubaliani na mchanganuo uliotolewa, kwa kuwa umeacha maswali mengi kuliko majibu.

  “Tunamtaka Gambo aje hadharani atueleze orodha ya wadau wote waliochangia kila moja na kiasi chake, atueleze kwa kuainisha kwa ushahidi jinsi fedha hizo zilivyotumika,” alisema Lazaro.

Meya huyo alisema lengo la kuhoji matumizi ya fedha hizo si kuwakumbusha wafiwa uchungu wa kuondokewa na wapendwa wao bali ni kuweka rekodi sawa ili kutowavunja moyo wasamaria wema waliotoa michango yao.

“Lakini pia sisi ni viongozi katika jamii, tumezungumza na wafiwa na wengi hawajapata hizo fedha, kama alivyokaririwa Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo kuwa wametoa kiasi cha shilingi 3,850,000 kwa kila familia,” alidai.

Meya huyo alidai kuwa hadi juzi Jumatatu idadi kubwa ya wafiwa walikuwa wamepokea kiasi kisichozidi shilingi milioni mbili hivyo kuwa na wasiwasi na kauli sambamba na mchanganuo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa.

“Mimi binafsi nimezungumza na mzazi mmoja wa wanafunzi (jina linahifadhiwa) ambaye ni mkazi wa kata yangu ya Sokon-One hadi Jumapili jioni alikuwa amepokea shilingi milioni moja ambazo alipewa siku ya mazishi na Jumapili hiyo alitumiwa 230,000 kwa njia ya M-Pesa na ushahidi upo wa kutosha,” alidai Meya huyo.

 Alisema kupitia kwa viongozi wa ngazi ya mitaa na madiwani wamezungumza na sehemu kubwa ya wafiwa na hadi Jumatatu mchana wiki hii, fedha anazodai Gambo zilikuwa hazijawafikia.

“Ukikokotoa hesabu vizuri malipo ya shilingi 3,850,000 kwa familia 32 ni shilingi milioni 123, katika milioni 215 ukitoa kiasi hicho kuna zaidi ya milioni 90 ambazo zinabaki. Je, fedha hizo ndizo zilizotumika kama gharama ya mazishi?” alihoji Meya Lazaro na kuongeza; “Katika hili lazima Gambo aje hadharani atueleze, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa hayo alikuwa nani? Wajumbe wake ni nani? Kwa nini amehodhi shughuli zote za msiba bila kuwashirikisha wadau muhimu kama wazazi na wamiliki wa shule?”

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye amekuwa akilumbana katika mitandao ya kijamii na Gambo alisema anatarajia kuzungumzia suala hilo katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ngarenaro.