Saccos ya idara ya kilimo Moshi washitukia ufisadi

MOSHI

WANACHAMA wa Ushirika wa Mema na Mabaya unaoundwa na watumishi wa Idara ya Kilimo na Mifugo katika Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wameulalamikia uongozi wa chama hicho kwa kushindwa kuwahudumia kwa mujibu wa katiba yao.

Ushirika huo ulianzishwa mwaka 1998 na watumishi wa Idara hiyo kwa malengo ya kusaidiana katika masuala mbalimbali ya kijamii kama misiba, ugonjwa na hata pale mtumishi anapostaafu kazi.

Chama hicho kina wanachama zaidi ya 200 na kila mwanachama wa ushirika huo hukatwa shilingi 5,000 kama mchango wake kila mwezi katika mshahara wake.

Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho mwanachama hupewa shilingi 500,000 iwapo atafiwa na ndugu wa karibu kama mume, mke, wazazi, mtoto ili fedha hizo zisaidie katika shughuli za mazishi.

Aidha pia kila mwanachama hupewa shilingi 50,000 pale atakapokuwa mgonjwa na kulazwa hospitali na shilingi 500,000, kila mwanachama anapostaafu kazi.

Hata hivyo pamoja na makubaliano hayo kikatiba taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kuanzia mwaka jana viongozi wa chama hicho walisitisha utoaji fedha kwa wanachama wake bila kutoa maelezo ya kuridhisha.

Wakizungumza na Raia Mwema huku wakiomba majina yao yahifadhiwe kwa sasa wanachama hao wanadai kuwa hawajaelezwa sababu za msingi za kutopewa fedha pale wanapopata matatizo.

“Katika kipindi chote kuna wanachama wamepata matizo ya kufiwa na watu wao wa karibu, kulazwa na wengine wamestaafu lakini chama hakikuwapatia fedha kama tulivyokubaliana katika katiba yetu,” alieleza mmoja wa wanachama hao.

Wanachama hao walikuwa na mchanguno wa malipo ya mishahara yao  (salary slip) zinazoonesha kuwa waajiri wao ambao ni Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini kwa muda wote walikata shilingi 5,000 na kulipa fedha hizo kwa ushirika huo.

“Kila tulipowahoji sababu za kutotoa fedha pale mwanachama anapokuwa na matatizo viongozi wetu wamekuwa wakitueleza sababu ambazo hazina msingi kwamba fedha zimechukuliwa na hazina. Sisi tunajiuliza hivi hazina wanahusika vipi kuingilia na kuchukua fedha kutoka chama hiari?” alihoji mwanachama huyo

Waliongeza kuwa viongozi wao pia wameshindwa kuitisha mkutano mkuu wa chama ambao kwa kawaida hufanyika Januari ya kila mwaka, hivyo kushindwa kupata fursa ya kujadili suala hilo.

Wanachama hao wanahofia kuwa huenda fedha zao zimetumika kifisadi na viongozi. Juhudi za kumpata mwenyekiti wa chama hicho, Joyce Kessy, hazikuweza kufanikiwa na mweka hazina wake, Kanza Niwael, alikataa kuzungumzia malalamiko ya wanachama hao akidai kuwa yeye si msemaji wa chama.

Taarifa ambazo Raia Mwema imezipata kutoka ndani ya vyama hiari na vile vya ushirika wa akiba ya kuweka na kukopa, Saccos, katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro zinaonesha kuwa kumekuwapo ufujaji mkubwa wa fedha anaofanywa na baadhi ya viongozi hali ambayo imefanya wanachama wengi kukosa fedha za mikopo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *