Sadio Mane, Mungu anakuona

SADlO Mane, fundi wa mpira kutoka Afrika anaendelea kuweka heshima katika Jiji la Merseysde, Liverpool.

 Mane mkimya kama alivyo, asiye na maneno mengi na mara nyingi katika mahojiano yake na waandishi wa habari hutazama chini kwa kuona haya.

 Huyo ndio Mane aliyeamua kuwazima Senegal na kuwawasha Tottenham Hotspour katika uwanja wa Anfield mwishoni mwa wiki. Liverpool ilishinda mabao mawili. Mabao yote aliyafunga yeye.

Baada ya mchezo ule kumalizika Mane alimfuata kocha wake, Jurgen Klopp kukumbatiana naye na kukimbilia katika vyumba vya kubadilishia nguo akiwaacha wenzake wakiendelea na sherehe uwanjani hapo.

Moja ya jukwaa la mashabiki waandamizi wa Liverpool linaitwa The Kops’. Jukwaa hili linakutanisha wale mashabiki wenye mioyo ya chuma iliyowahi kumshangaza Simao Sabrosa ambaye alitembelea uwanjani hapo akiwa na kikosi chake cha Atletico Madrid.

Sabrosa aliwashangaa mashabiki hao vichaa wa kushangilia muda wote wa mchezo licha ya Liverpool kufungwa mabao 3-0. Unakuwaje nyuma kwa mabao 3-0 na timu yako ikizidi kushambuliwa uwanjani, huku wewe kwenye jukwaa ukizidi kushangilia?

 Haitokei kwa mashabiki wengi wanaoweza kuhamasisha timu yao kwenye nyakati zote nzuri na mbaya kama hawa.

Wiki kadhaa zilizopita tulikuwa kwetu Afrika tukimshuhudia Mane ‘fake’ kwenye michuano ya Mataifa Afrika (Afcon) ambayo bingwa wake ni Cameroon. Mane tuliyekuwa naye Afcon sio huyu tunayemshuhudia kwenye jezi za Liverpool akiutumikia vyema mshahara wake mnono.

 Angewezaje kuingiza mguu kuwania mpira sehemu ambayo inaweza kumsababishia matatizo? Ni ngumu kuliona hili wakati huu ambao Mane alikuja Afrika akiongozana na mmoja ya madaktari kutoka Liverpool.

Mpira wa Afrika ndiyo umefikia hapa. Hakuna tena uzalendo. Ni jambo la kawaida kushuhudia mchezaji wa Afrika anayetamba ulaya akikataa kuja Afrika kushiriki michuano ya Afcon kwa sababu za kuogopa kupoteza nafasi yake ulaya.

 Hizi sio nyakati za mchezaji wa kiafrika kujisikia fahari kuvaa jezi ya timu yake ya taifa na kuzipigania. Wazungu wametuharibia mpira ambao siku moja gwiji wa Nigeria, Nwanko Kanu aliwahi kutamka kuwa mchezaji kushiriki Afcon ni raha iliyoje maana michuano hii inaonyesha vipaji halisi vya wachezaji wa Afrika tofauti na wanavyokuwa ulaya ambako wanacheza mpira wa mbinu zaidi.

Rejea kuitazama penati ya Mane aliyompa mkononi mlinda mlango wa Cameroon, Fabrice Ondoa iliyoiondoa Senegal kwenye michuano ya Afcon mwanzoni mwa mwaka huu na Mane akitoa chozi la ‘kutuzuga’ katika uwanja wa Stade de Franceville.

 Mane aliilia na kujifanya ameshindwa hadi kutembea kwa uchungu na kufanya baadhi ya maofisa wa Senegal kuingia uwanjani na kumtoa kwa kumburuza. Huyu ndiyo Mane aliyeamua kutuzuga watu wazima wenye akili zetu timamu mbele ya luninga.

Wakati Mane akibeba mpira kwapani kwake kwa ajili ya kuutenga kisha kupiga penati ile wachezaji wawili wa Senegal nyuma ya kamera walionekana kunong’onezana.

Hatujui walichokuwa wakinong’onezana, lakini si vibaya nikitabili kile walichokuwa wakinong’onezana ndicho kilichotokea kwa Mane kupiga penati laini iliyodakwa na Ondoa. Mane aliingia kwenye mchezo ule mashabiki wa Liverpool mitandaoni wakifanya sala maalum ya kuiombea Senegal ifanye vibaya na staa wao arejee kwenye timu haraka.

Haikuchukua saa 24 tangu Mane amkabidhi penati ile Ondoa, alikuwa tayari ameshafika jiji la Merseyside ambako alitumiwa ndege maalum ‘private jet’ kuwahi mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Chelsea na hakutaka hata kuongozana na kikosi na kurudi Senegal kukutana na wananchi wenzao walisimama nyuma yao muda wote wa michuano mpaka wanatolewa.

 Fedha za wazungu zimetoa mioyo ya uzalendo kwa wachezaji wetu ambao wanaifikiria zaidi mishahara yao kuliko kuzipigania timu zao za taifa. Wachezaji wetu ndiyo wamefikia hatua hii ambayo tunawashangaa, nao wakitushangaa. Hakuna uzalendo tena. Tumebaki kushangaana.

Alichokifanya Mane ni sehemu ya kawaida kwa mastaa wengi wa Afrika wanaotamba ulaya kila kinapofika kipindi cha michuano hii inayofanyika kila baada ya miaka miwili.

 Kama staa akiamua kuja kuichezea timu yake ya taifa hajitoi kisawa sawa. Akiamua kuja kushiriki, ushiriki wake unakuwa wa kiwango cha chini kana kwamba ni majeruhi au mwisho wa siku akiamua kushiriki ndiyo anafanya kama alivyofanya Mane.

Kuna mastaa wengine wao ndiyo wanatoa sababu za kutotaka kuwa sehemu ya vikosi wakisema wana majeraha. Michael Essien aliwahi kuigomea Ghana kwa ajili ya Chelsea na muda wote wa michuano akisema ana majeraha, lakini baada ya Ghana kutolewa kwenye michuano alirudi uwanjani na nguvu kubwa. Aibu ilioje hii.

Didier Drogba mara zote alizokuwa akija Afrika kushiriki Afcon alionekana mshambuliaji goigoi aliyekuwa anazuiwa hata na mabeki wa kiwango cha chini. Lakini Drogba huyu alikuwa mshambuliaji hatari mara zote alizokuwa na jezi za kikosi cha Chelsea barani ulaya.

Kiungo mshambuliaji wa Ghana, Kelvin Prince Boateng kila akimaliza kushiriki michuano ya Kombe la Dunia na kikosi hicho cha ‘Black Stars’ hutangaza kustaafu timu hiyo na kukwepa kushiriki kwenye michuano ya Afcon, lakini nchi inapoanza harakati za kutafuta nafasi ya kushiriki kombe la dunia hujitokeza na kusema amejifikiria na familia yake na ameona arejee timu ya taifa. Alifanya hivi kwenye Kombe la Dunia mwaka 2010 (Afrika Kusini) na akarudia 2014 (Brazil) na sasa tumsubili kuelekea 2018 (Urusi). Haya ndiyo maisha ya Boateng kwenye kikosi cha Ghana.

Alichokifanya Mane ni muendelezo wa mastaa wa Afrika wanaotamba na waliowahi kutamba ulaya. Si kitu kipya machoni na masikioni mwa mashabiki wa soka Afrika.

 Wakati huu tunaokaa kumshangaa Mane tubakishe maneno kwa mastaa wapya wa Cameroon ambao wanacheza kwenye timu za kawaida sehemu mbalimbali barani ulaya.

Hawa mastaa wa Cameroon tuwasubili wakija kusajiliwa na timu kubwa ambazo zitawapa jeuri ya kufanya hiki walichokifanya wenzao.

Kama mchezaji bora wa michuano yenyewe Cristian Bassagog anacheza timu ya Aab ya Dernmark isiyoshiriki hata michuano mikubwa ya barani ulaya, mchezaji huyu anakuwaje mkaidi akiitwa kuichezea Cameroon? Kwa vyovyote vile atakuja tena mapema sana.

Lakini alichokifanya Mane hakihitaji ushuhuda mwingine kuona jinsi gani soka letu lilivyomezwa na mishahara minono ya wazungu ambao wanawapangia wachezaji hadi jinsi ya kucheza na wasijitoe kwa mioyo yao yote. Kwa kile alichokifanya Mane katika ardhi ya Gabon, si vibaya tukimwambia Mungu amemuona.

One thought on “Sadio Mane, Mungu anakuona”

  1. Esther Mollel says:

    Mnamwonea Mane, wachezaji wangapi bora wa dunia wanakosa penalt? Ronaldo na hata Messi wanakosa itakua Mane? acha kabisa. Katika mchezo wowote mkubwa, kuna kushinda na kushindwa. Sasa wewe ulitaka nani afungwe badala ya Senegal? maneno yako yanakuwa kama ya mzazi matokeo ya mtoto wake yakitoka vibaya anatoa maneno "yaani hata mtoto wa fulani amekushinda?" sasa wewe mzazi, unataka mtoto wa nani afeli?. Je, wewe ungefunga ile penalt?Acha kucheza mpira kwa macho na luninga yako. Jiweke badala ya Sadio uone shutuma zisizo kweli zinavyoumiza.. Tumtie moyo Mane ili aweze kuja kuwa mchezaji bora Afrika miaka ya baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *