Michezo
Sasa tuziheshimu filamu za Kitanzania
Ezekiel Kamwaga
Toleo la 234
11 Apr 2012
Jeneza la Steven Kanumba mazishini

MAJIRA ya saa 10 alfajiri Jumamosi iliyopita nikiwa katika usingizi mzito jijini Setif, Algeria, ulitumwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yangu ya mkononi kuniarifu kuhusu kifo cha msanii mahiri wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba.

Nikiri mapema hapa kwamba sikuwa na mahusiano yoyote binafsi na msanii huyu. Tulikuwa tukifahamiana tu kwa sababu ya aina ya shughuli tunazofanya. Mnasalimiana, mnatakiana heri na kila mmoja anaendelea na ustaarabu wake.

Kwa bahati mbaya, nimekuwa nikipata shida sana na baadhi ya rafiki zangu ambao kwao filamu za Kitanzania ni upuuzi mtupu. Wanapoziangalia wanazifananisha na filamu za akina Tom Cruise wa Marekani.

Hata hivyo, mimi nina ushahidi wa wazi wa namna filamu za Kitanzania zilivyoweza kututangaza nje ya nchi. Mwaka jana, mwezi wa saba, nilikwenda nchini Ghana na wenyeji wangu waliniomba niende na filamu mpya za Kitanzania.

Miezi miwili iliyopita, rafiki zangu wa Kinyarwanda waliofikiri kwamba nitakwenda Rwanda kuangalia mechi ya Simba na Kiyovu, walinituma mapema kwenda nchini kwao na filamu hizihizi za akina Kanumba.

Miaka mitatu iliyopita, nilistaajabu kuona filamu feki za Kitanzania zikiuzwa jijini Addis Ababa, Ethiopia. Naomba nikumbushe kuwa ni filamu hizihizi ambazo mara nyingi huwa zinapondwa na wasomi washaufu wa Kitanzania!

Kwa maoni yangu, Kanumba, pengine kuliko mwingine yeyote, ndiye alikuwa msanii mbunifu zaidi na mwenye maono ya mbali zaidi (vision) kuliko mwingine yeyote hapa nchini.

Yeye ndiye mtangulizi kwenye kuweka majina ya Kiingereza kwenye filamu za Kitanzania, yeye ndiye mtangulizi kwenye kutafsiri kwa Kingereza filamu za Kiswahili na yeye ndiye msanii wa kwanza kuigiza na msanii wa nje wa kiwango cha Ramsey Nouah hapa nchini.

Ramsey Nouah, pengine msanii maarufu zaidi wa kiume wa Nigeria amekuja nchini kwenye msiba wa Kanumba. Kanumba huyuhuyu ambaye Watanzania wengi, haswa wasomi, wamekuwa wakimponda kwamba filamu zake si lolote si chochote!

Utafiti wangu umebaini kwamba watu wanaochukia filamu zetu hizi wanafanya hivyo kwa sababu eti zina majina mabaya, zina Kingereza kibovu na zinaiga maisha ambayo si ya Kitanzania.

Lakini kimsingi, haya ni mambo madogo kwa wananchi wa kawaida. Kwanza Watanzania walio wengi hawaangalii tafsiri kwa sababu wao wanasikiliza kinachozungumzwa moja kwa moja. Pili jina la filamu si kitu muhimu zaidi ya kilichomo. Watu wanaipenda filamu si kwa sababu imeitwa Fake Pastor lakini kwa sababu ya kile kilichomo ndani ya stori.

Ninakubali kwamba bado kuna kazi kubwa inahitajika kufanyika kuboresha filamu za Kitanzania lakini ninaamini kwamba kwa sasa filamu zetu zinaelekea katika njia nyofu kila kukicha.

Filamu za Kitanzania leo hii ni tofauti na zile za miaka minne iliyopita. Zimebadilika kuanzia mwonekano wa waigizaji, mtiririko wa matukio na hata vionjo vya ki-graphic na uhalisia wa uigizaji.

Filamu za Tanzania zikianza kupata faida inayotakiwa, wataajiriwa wafasiri wazuri zaidi na kutakuwa pia hakuna haja ya filamu kuchezwa Part One na Part Two kwa vile kazi moja tu itatosha kumpa msanii faida.

Kanumba ameliliwa kuliko wanasiasa na wanamichezo maarufu ambao walifariki dunia katika siku za karibuni. Tanzania imepoteza majenerali wa majeshi, wanamuziki, wabunge, mawaziri wakuu na watu wengine maarufu lakini sijaona ambaye amefikia kiwango cha kugusa watu kama hiki cha Kanumba.

Hii maana yake ni kuwa tasnia ya filamu inafanya makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania. Watu hawafahamu tu lakini hawa akina Kanumba na Ray ni wageni majumbani kwetu karibu kila siku usiku.

Jambo jingine muhimu ambalo wengi wetu tunashindwa kuliona linatokana na ajira ambayo sekta ya filamu imetoa kwa wananchi wa kawaida. Kuna watu ambao bila ya kuwa waigizaji wangekuwa pengine ni wauza dawa za kulevya au mateja, vibaka, makahaba, majambazi au wangekuwa wamepoteza maisha tayari.

Kanumba, anatajwa kuwa miongoni mwa watu ambao wamefanikiwa kuwaingiza watu wengi kwenye tasnia hii. Watu hao sasa wamepata ajira ya kuwapa mapato halali. Baadhi yao, vipato vyao vimewapa uwezo wa kufungua miradi ambayo imeajiri watu wengine.

Kama kuna Watanzania wanaochapa kazi kwelikweli ukiondoa wakulima basi ni waigiza filamu hapa nchini na nadhani hakuna aliyekuwa bize kuliko marehemu Kanumba.

Wanaandaa stori, wanatengeneza script, wanapiga picha, wanaongoza filamu, wanacheza filamu na wanafanya shughuli za masoko (marketing) ya kazi zao. Wanafanya wenyewe kwa vile wale ambao wangeweza kuwasaidia kufanya hivyo wanaona wanafanya upuuzi.

Hata hivyo, wanasonga mbele. Na kwa picha ambayo nimeipata tangu kutokea kwa msiba wa Kanumba, wananchi wengi pia wako nyuma yao. Wanajua kuwa wacheza filamu wa Kitanzania si mafisadi na chochote kile wanachokipata, wanakipata kwa jasho lao.

Nilikuwa nikifurahia sana ushindani wa Ray na Kanumba kwenye filamu. Hawa walikuwa washindani wa kweli na katika hali ya kawaida, ushindani unasaidia sana kukuza soko.

Kwa vile Kanumba kaondoka, ni muhimu kwa wasanii wengine kama vile JB, Richie, Sajuki, Cheni na wengine kuongeza juhudi ili kuendeleza ushindani wa kutoa filamu kali. Na ni muhimu kwa Ray kutobweteka kwa vile mshindani wake namba moja hayupo nasi.

Lakini, kubwa zaidi ni kwa jamii ya Watanzania kuzibuka masikio sasa na kufahamu ni kwa jinsi gani filamu za Kitanzania zinawagusa wananchi wetu kwa kiasi gani. Filamu hizi zinaonyesha tabia zetu kwa wageni wanaozitazama.

Filamu hizi zinatoa ajira kwa watu. Filamu hizi zinaokoa maisha ya watu. Filamu hizi zinasomesha watoto na kuweka chakula mezani kwa mamia ya Watanzania.

Kifo cha Kanumba kituzindue kwamba badala ya kuziponda na kuzilaumu, ni muhimu kwetu kutafuta namna ya kuzifanya ziwe nzuri zaidi, ziajiri watu wengi zaidi, ziingize mapesa zaidi na zilitangaze zaidi Taifa letu.

Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Kanumba, bila shaka. Kumpenda maana yake ni kuitimiza ili huko aliko aishi kwa amani akijua waliobaki walimtendea haki.

Buriani Steven Charles Kanumba…. Tunalia kwamba hatutakuona tena lakini tunafurahi kwa sababu umelifanyia Taifa lako makubwa.

Mola na akuweke mahali pema peponi.

Amen.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ezekiel Kamwaga
ezepolka@yahoo.com
+255-718814875

Mwandishi ni msomaji wa Raia Mwema, vilevile ni Msemaji wa Timu ya Soka ya Simba

Toa maoni yako