Makala
Serikali iwadhibiti Vibwetere hawa
Aristariko Konga
Toleo la 025
16 Apr 2008

MACHI 17, 2000 zaidi ya waumini 500 wa Kanisa la African Movement for the Restoration of the Ten Commandmends (Kanisa la Kutunza Amri Kumi za Mungu), waliingia kwenye kanisa lao dogo, lililokuwa eneo la Kangungu, eneo la Magharibi ya Uganda.

Waliimba nyimbo kwa saa kadhaa kabla ya kanisa hilo lililojengwa kwa mbao tupu kuanza kuungua kwa moto ukitokea ndani.

Milango ilikuwa imefungwa na madirisha yalifungwa kwa kupigiliwa misumari. Kila aliyekuwamo ndani aliteketea kwa moto. Miili iliyoungua, ikiwamo ya watoto 11, baadaye ilikutwa na mamlaka husika.

Kulikuwa na mshituko mkubwa kutokana na tukio hilo, wakati polisi wa Uganda walipowakuta waumini zaidi wakiwa wameuawa kwa moto huo.

Kwa mujibu wa wataalam walioifanyia uchunguzi miili hiyo, baadhi walikuwa wamepewa sumu, wengine walikuwa wamenyongwa na wengi walikuwa na alama za kuchomwa na vitu vya ncha kali, au mafuvu yalikuwa yamepasuka.

Miili yao ilifichwa kwenye nyumba au kutupwa kwenye visima na vyoo vya mashimo. Idadi ya waliokufa baadaye iligundulika kufikia 780, ingawa ripoti nyingine zilikuwa zinataja hadi kufikia watu 1,000. 

Kanisa The Movement for the Restoration of the Ten Commandments lilianzishwa na Joseph Kibwetere katika miaka ya mwisho ya 1980, na wakati mmoja liliwahi kufikisha waumini 5,000. Askofu huyo (68) ambaye alijipa wadhifa huo, wakati mmoja alikuwa muumini maarufu wa Kanisa Katoliki, na mtu aliyekuwa akichangamkia siasa za Uganda.

Mwaka 1998 Kibwetere alilazwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa akili. Alidai kuwa alikuwa na maono na aliweza kuyasikia mazungumzo baina ya Yesu na Bikira Maria. Alidai kuwa Bikira Maria alikuwa akilalamikia jinsi ulimwengu ulivyoziacha Amri Kumi za Mungu. Mwishowe akadai kuwa aliamriwa kutangaza ujio wa kiyama na maafa mwaka 2000.

Kibwetere aliandika kitabu, kilichoelezea ujio wa maafa ambayo yangewateketeza sehemu kubwa ya watu duniani. Alisema ni wale tu ambao wangezitii Amri Kumi za Mungu na kumfuata yeye (Kibwetere), wangeweza kunusurika kupitia kanisa lake, aliloliita Safina.

Baadhi ya viongozi waliokuwa chini ya Kibwetere walihubiri kwamba mali binafsi ilikuwa ni dhambi, na waliwashawishi waumini kuuza kila walichonacho na kukabidhi mali zao kwao. Hatimaye viongozi hao wakawa matajiri, wakiwa wamelimbikiza mashamba, nyumba na magari.

Kibwetere na viongozi wake wakahakikisha kuwa waumini wao hawana mawasiliano na watu wengine ‘wenye dhambi’. Kila kunapokuwa na mawasiliano ya aina hiyo, kulikuwa na udhibiti wa hali ya juu.

Kitabu cha Kibwetere kilikuwa kimesambazwa kwa maelfu ya watu, kikiwa na kichwa cha habari: "A Timely Message From Heaven: The End of the Present Time." (Ujumbe wa wakati muafaka kutoka mbinguni: Mwisho wa Nyakati Hizi).

Kilieleza kuwa siku ya kiyama ingekuwa Desemba 31, 2000. Ilipopita tarehe hiyo na ahadi nyingine nyingi hewa, baadhi ya waumini wakataka kuondoka na wakaanza pia kudai mali zao walizowakabidhi viongozi wa kanisa. 

Machi 15, 2000 (siku mbili tu kabla ya moto kutokea kanisani) Kibwetere akatoa waraka wa ‘kuwaaga’ maofisa wa serikali. Waraka huo ulizungumzia mwisho wa kizazi hicho hapa duniani. Familia ya Joseph Kibwetere ilitangaza kwamba alikuwa amekufa.

Nimelazimika kurejea kisa hiki kutokana na taarifa za hivi karibuni, kwamba kuna waumini wa Kanisa la Wasabato wenye imani kali wilayani Kyela, waliyakimbia makazi yao na kuweka kambi porini kwa lengo la kujiandaa kumpokea Yesu.

Tukio hilo lilitokea siku chache kabla ya kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, na kwa vyovyote vile, ilikuwa ni rahisi kwao kushawishika na jambo lolote linalohusu imani yao.

Waumini hao walitangaza kuuza nyumba zao na kutelekeza jamaa zao waliokuwa wakiishi nao. Walikuwa wakiamini kuwa Yesu angerejea wakati wowote baada ya Machi 30, 2008.

Waumini hao walianza kuyaacha makazi yao baada ya ujio wa mchungaji mmoja kutoka mkoani Mara, aliyejitangaza kuwa nabii na kuwahamasisha wafanye maandalizi ya kumpokea Masiya.

Baadhi ya waumini walitangaza kuuza mali zao, zikiwamo nyumba, na kwenda kuishi katika pori kubwa lililopo katika Kijiji cha Tenende, Kyela, mkoani Mbeya, ambako kwa imani zao ndiko Masiya angetua akitokea mawinguni. Ni yale yale yaliyotokea kwenye kanisa la Kibwetere!

Kuna wakati kulikuwa na waumini katika mkoa huo huo wa Mbeya, ambao walikuwa wakiwakataa watoto wao wasiimbe Wimbo wa Taifa, kwa maelezo kwamba ilikuwa ni dhambi.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela alikiri kuwa na taarifa hizo. Polisi katika Mkoa wa Mbeya walikiri pia kuwa na taarifa hizo, na kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikaa na mchungaji huyo kutoka Mara, ambaye alikubali kuwarejesha waumini wote kwenye makazi yao.

Kwa mtazamo wangu, Polisi walipaswa kuchukua hatua kali zaidi kwa wahusika kwa kuwa walikuwa wakihatarisha usalama kwa kutelekeza ndugu zao na kuziyumbisha familia zao, na hivyo kuhatarisha maendeleo ya nchi.

Wakati tukio la Kijiji cha Tenende likijiri, waumini watatu wa Kanisa la Waadventista Asilia, walihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kuwazuia watoto wao kusoma kwa madai kuwa Yesu anakuja.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 17, 2008, katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara. Hakimu alitoa hukumu hiyo baada ya washitakiwa kukiri kosa kwa kusema kuwa hawaoni umuhimu wa watoto wao kusoma, kwa kuwa mwisho wa dunia ulikuwa umefika.

Mashitaka dhidi yao yalionyesha kuwa walitenda kosa hilo Machi 10, mwaka huu. Kwamba waumini hao waliwachukua wanafunzi hao na kuwapeleka katika Kijiji cha Kiagata, kwa madai kuwa waende kumsubiri Yesu, ambaye anatarajiwa kuja mwezi ujao, na kwamba Kijiji cha Kiagata ndicho kilichobarikiwa. 

Kwa maoni yangu, hatua iliyochukuliwa dhidi ya wahusika ilikuwa inastahili, na ndiyo iliyopaswa kuchukuliwa dhidi ya waumini mkoani Mbeya.

Haiingii akilini kuwa na watu ambao wanaghilibu akili za wenzao, kiasi cha kuuza mali zao na kudanganya umma.

Tukio la Kijiji cha Tenende lilisababishwa na mchungaji kutoka mkoani Mara. Tukio la Kijiji cha Kiagata pia linawahusisha waumini wa mkoa huo huo wa Mara. Hapa kuna nini? Pamoja na kwamba matukio ya hivi karibuni yanawahusisha waumini wa mkoa huo, basi kuna haja ya kuwa na wasiwasi na waumini wa sehemu nyingine.

Wafuasi wa Kibwetere walianza kama mchezo wa kuigiza kwa kurubuniwa na hatimaye uongo ulipodhihirika wakauawa na wenye kutengeneza uongo huo.

Sisi tumeshuhudia matukio kama haya, na tunayachukulia juu juu tu. Hii ni hatari.

Ni sawa kwamba Katiba inatoa fursa ya uhuru wa kuabudu lakini uhuru huo, kama zilivyo sheria nyingi, hauna budi kuwa ndani ya mipaka fulani. Kwa hiyo, Katiba inautwaa uhuru wa kupita kiasi kwa kuweka vifungu vya udhibiti wa uhuru huo.

Katiba inaeleza kwamba kila mtu ana uhuru wa imani na uchaguzi katika mambo ya dini na kutoa uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.

Katiba inaeleza kwamba kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa jambo huru na la hiari la mtu binafsi. Kwamba shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Lakini, pamoja na uhuru huo, ni kazi ya serikali kuhakikisha shughuli za kidini hazihatarishi usalama wa nchi na ustawi wa watu wake. Kwa hiyo, kuabudu dini kwa kikundi kimoja jamii kisiingilie uhuru, amani na utulivu wa kikundi kingine au jamii.

Vibwetere wanaoanza kuibuka nchini hivi sasa hawana tofauti na yule Kibwetere wa Uganda, aliyesababisha mamia kuteketea kutokana na imani za kudanganyana, hivyo ni wajibu wa serikali kupitia vyombo vyake, kuwapukutisha badala ya kuwafanya wastawi.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako