Serikali kujenga magereza maeneo yaliyo ‘bize’ kwa kilimo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amewaeleza wabunge kwamba serikali inalenga kujenga magereza katika maeneo ambayo uzalishaji kwa njia ya kilimo ni mkubwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mwigulu, hatua hiyo itasaidia kuwatumia wafungwa katika shughuli za uzalishaji kwa njia ya kilimo katika maeneo husika.

Mwigulu alitoa maelezo hayo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Vitimaalumu kutoka Mkoa wa Morogoro, Devotha Minja.

 “Magereza hayo yatajengwa katika maeneo yenye kilimo na yatakuwa kwa ajili ya watu waliokwisha hukumiwa huku yale magereza ya mijini yakiachwa kwa ajili ya mahabusu tu ili wawe karibu na mahakama,”alisema Mwigulu.                   

 Alisema mkakati huo wa serikali ni wa muda mrefu na wanahitaji kufanya hivyo ili kuharakisha shughuli za maendeleo zinazofanywa na wafungwa na pia kupunguza msongamano wa wafungwa katika magereza.

Alifafanua kuwa uamuzi huo pia unazingatia tamko la Rais Dk. John Magufuli alilowahi kulitoa hivi karibuni kwamba wafungwa wako katika kutumikia adhabu hivyo wanatakiwa kufanya kazi hasa za kilimo ili kujipatia chakula na si kukaa tu bure na kusubiri kila kitu wafanyiwe na serikali.

Mwigulu alisema serikali ina mkakati wa kutumia bajeti inayotengwa na nguvu kazi wanayoipata kutoka kwa wataalamu walionao kwa upande wa askari magereza na wafungwa ili kukarabati magereza chakavu na kujenga nyumba za askari.

Alibainisha kuwa suala la kukatwa kwa huduma ya umeme katika magereza, nyumba za askari, pamoja na maeneo mengine ya kambi za Jeshi la Polisi na Magereza limekwishafanyiwa kazi na serikali kupitia hazina imekwishatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *