Serikali yasita nini kuweka wazi ugonjwa wa Mwakyembe?

NAANDIKA makala hii kwa uangalifu mkubwa nikitambua kwamba ni mfano wa makala ambazo ukishaandika na kuchapishwa gazetini, kesho yake unaweza kufuatwa nyumbani na maofisa wa polisi au wa Usalama wa Taifa na kutakiwa utoe ushahidi wa uliyoyaandika.

Najihami mapema kwao kwamba hakuna jambo lolote jipya katika makala hii linaloweza kuwachochea kunifuata; maana yote yalishawekwa wazi kwenye vyombo vingi vya habari, na wala hayakupatwa kukanushwa.

Kwa hiyo, hakuna jipya hapa mbali ya hoja zangu ambazo naamini zinafikirisha. Kama bado watanifuata, basi, lengo lao litakuwa ni kunitisha (mimi na wengine) ili nisiandike tena kuhusu suala hili.

Ndugu zangu, suala ninalojaribu kuliandika kwa tahadhari kubwa hapa ni la masahibu yaliyomkuta Naibu Waziri wa Ujenzi, Mbunge wa Kyela na mmoja wa makamanda wa vita dhidi ya ufisadi nchini, Dk. Harrison Mwakyembe.

Ni karibu miezi miwili sasa tangu Dk. Mwakyembe arejee kutoka India alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa ambao mpaka sasa umma haujaelezwa rasmi jina lake.

Nimekuwa nikisita kwenda nyumbani kwake kumpa pole, kwa sababu mwenzetu wa Raia Mwema tuliyemtuma kwenda kumuona mara aliporejea kutoka India, alitupa simulizi ya kusikitisha juu ya hali yake. Na mimi kwa udhaifu wa moyo wangu, nahofia ‘presha’ inaweza kunipanda nikimuona, na pengine kuanguka hapo hapo nyumbani kwake.

Kusita kwangu kwenda kumuona na kumpa pole kuliimarishwa zaidi na habari niliyoisoma kwenye gazeti la Tanzania Daima, toleo la Januari 4, 2012, ukurasa wa kwanza, iliyobeba kichwa kinachosomeka “Dk. Mwakyembe ana siri nzito”.

Kwenye habari hiyo ilielezwa kwamba afya ya Mwakyembe inasikitisha; kwani licha ya kupata matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake si ya kuridhisha.

Kwa mujibu wa habari hizo, kucha za vidoleni na miguuni zimeoza na zina rangi nyeusi, miguu na mikono yake imepasuka mithili ya mtu mwenye magamba ambayo wakati mwingine hutoa damu.

Si hivyo tu. Tumeelezwa pia kwamba kichwani hana nywele; kwani zimepukutika zote ikiwa ni pamoja na nyusi za kope. Hali hii humfanya muda wote avae kofia kichwani na glovu mikononi na hata miguuni kuhifadhi viungo vyake hivyo.

Maelezo hayo ya hali ya Dk. Mwakyembe hayanipi mimi, mwenye moyo dhaifu, ujasiri wa kwenda kumuona, na naishia tu kumwombea kwa Mwenyenzi Mungu kwenye sala zangu. Niseme tu kwa Dk. Mwakyembe kupitia makala hii: Hang in there brother, pambana kuokoa maisha yako. Mungu atakusaidia.

Ukweli ni kwamba, kwa yaliyomsibu Dk. Mwakyembe; hata kama atapona kabisa, hawezi kuwa Mwakyembe yule yule tuliyemzoea.

Kwa hakika, atahitaji miaka mingi ya tiba ya kiroho (spiritual healing) na ushauri nasaha kutoka kwa mabingwa wa dunia wa fani hiyo kuweza kusahau yote yaliyomsibu na kuendelea na maisha yake kama kawaida. Huo ndio ukweli wa kipimo cha masahibu yaliyomkuta.

Nikitafakari masahibu hayo yaliyomkuta kamanda huyu wa vita dhidi ya ufisadi, nahisi kuna kitu hakiko sawa katika namna Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inavyolishughulikia suala la kiongozi huyo wa Serikali.

Hata hivyo, kabla sijakizungumzia kitu hicho, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa hatua aliyoichukua ya haraka ya kumpeleka India Dk. Mwakyembe siku alipomtembelea nyumbani kwake na kusononeshwa na hali aliyomkutanayo.

Habari za uhakika nilizonazo ni kwamba Rais Kikwete alihuzunishwa mno na hali ya Dk. Mwakyembe kiasi kwamba alianza hapo hapo sebuleni kwa Mwakyembe kumpigia simu Waziri Magufuli na Waziri wa Afya na kuwapa maelekezo kwamba anataka kuona Dk. Mwakyembe anapelekwa India kwa matibabu ndani ya kipindi cha saa 24! Na ndivyo ilivyokuwa.

Kwa mtazamo wangu; namna Kikwete alivyoishughulikia kwa haraka safari hiyo ya India ya Mwakyembe, ni uthibitisho wa kutosha kwamba Rais wetu ni mwenye huruma na upendo.

Kikwete anaweza akawa na udhaifu wake kiuongozi; lakini ukweli unabaki pale pale kwamba yu mwenye huruma na mpole, na hizo ni sifa zinazotunisha thawabu zake kwa Mungu!

Kuhusu suala la mushkeli ninaouona katika namna ambavyo Serikali yake inavyolishughulikia suala la Mwakyembe, napenda nikite kwenye huu ububu wa Serikali katika kuueleza umma nini hasa kilimsibu jemadari huyo wa vita dhidi ya ufisadi.

Kwa jinsi ninavyofahamu, Dk. Mwakyembe amerejea nchini na ripoti ndefu ya madaktari wa India waliomtibu ambayo inaeleza nini hasa chanzo cha kuzorota kwa hali yake ya afya, na ripoti hiyo ameiwasilisha serikalini; kwani ni Serikali ndiyo iliyompeleka India kwa matibabu. Hili halina ubishi.

Linaloweza kuwa na ubishi lakini unaojadilika, ni hili ambalo nimelijenga katika hisia. Hisia zangu ni kwamba Dk. Mwakyembe mwenyewe anapenda Serikali iweke hadharani ripoti hiyo ya madaktari wake aliyorejeanayo kutoka India. Kwa maneno mengine; Dk. Mwakyembe anataka umma uelezwe nini kilichomsibu.

Baadhi ya watu anaowaamini waliopata kumtembelea nyumbani kwake, si tu amewadokezea kilichomo kwenye ripoti hiyo, lakini pia amesema kwamba kama Serikali itaendelea na ububu wa kutoitoa hadharani, basi, yeye ataeleza umma siri iliyomo kwenye ripoti hiyo ya madaktari wa India.

Sasa kama nipo sahihi kwamba Dk. Mwakyembe mwenyewe anataka umma uelezwe kilichomo kwenye ripoti ya madaktari hao wa India, sielewi ni kwa nini Serikali inasita kufanya hivyo.

Majibu ambayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alilipa gazeti la Majira (toleo hilo la Januari 4); kwamba eti suala la ugonjwa wa Mwakyembe aulizwe mwenyewe Mwakyembe, hayaridhishi na hayana busara ndani yake.

Ni kweli kwamba ugonjwa wa mtu ni siri ya mgonjwa mwenyewe; lakini vipi kama mgonjwa mwenyewe anataka siri ya ugonjwa wake iwekwe hadharani? Na tunao mfano wa ridhaa ya Rais Kikwete kwa daktari wake kuelezea hali ya afya yake (ugonjwa) mbele ya waandishi wa habari. Uamuzi uliofuatia na tukio la yeye (Kikwete) kuanguka jukwaani, mkoani Mwanza.

Isitoshe; hapa hatuzungumzii mgonjwa wa kawaida. Hapa tunazungumzia mgonjwa ambaye ni Naibu Waziri, Mbunge, mwanaharakati wa haki za binadamu na mmoja wa makamanda wa vita dhidi ya ufisadi.

Isitoshe; hapa vilevile tunamzungumzia kiongozi wa ngazi ya waziri ambaye waziri mwingine mwandamizi serikalini, na ambaye ni mpambanaji mwenzake katika vita dhidi ya ufisadi (Samuel Sitta) tayari alishautangazia umma kwamba kinachomsibu Dk. Mwakyembe ni sumu.

Na Samuel Sitta si pekee kuutangazia umma hivyo kwenye kipindi cha Dakika 45 cha ITV; kwani Mwenyekiti wa Halmshauri ya Kyela naye alisema hivyo hivyo na kunukuliwa na magazeti siku alipomtembelea Mwakyembe nyumbani kwake aliporejea kutoka India.

Watu hawa wawili – Sitta na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela, ni watu walio karibu sana na Dk. Mwakyembe, na hivyo yawezekana kabisa dhana hiyo ya kupewa “sumu” imetoka kwa Mwakyembe mwenyewe (from the horse’s mouth).

Sasa, kama mazingira ni haya, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuiweka hadharani ripoti hiyo ya madaktari wa India ili ukweli rasmi ufahamike? Inaona ugumu gani kufanya hivyo?

Kama, kwa mfano, (narudia maneno ‘kwa mfano’ ) kilichomsibu ni kuwekewa sumu ya polonium 210 kama ile iliyotumika kumuua kachero wa Urusi, mjini London, Alexander Litvinenko, basi umma uambiwe; maana katika u-Mafia ambao tumeufikia hivi sasa hapa nchini kwetu, hilo nalo halitatushangaza sana.

Lakini kama pia kilichomsibu si sumu, ni logic (mantiki) umma ukatangaziwa ili fikra hizo kwamba Dk. Mwakyembe aliwekewa sumu ziondoke vichwani mwa Watanzania.

Hivi kuna tatizo gani Waziri wa Afya akaitisha mkutano na waandishi wa habari na akawaeleza, japo kwa ufupi, kilichomo kwenye ripoti hiyo ya madaktari wa India?

Hata kama ripoti inasema kuwa tatizo ni sumu aliyopewa, kuna hatari gani watu kufahamishwa hivyo; hasa kama jeshi la polisi nalo litasema kwamba linaanzisha uchunguzi kujua namna sumu hiyo ilivyompata Mwakyembe?

Nauliza maswali haya yote kwa sababu suala la Mwakyembe si la kawaida, na linaweza kuwa ni tukio la aina yake katika historia ya miaka 50 ya uhuru wetu.

Nasema hivyo kwa sababu, hata kabla hajakumbwa na masahibu haya ya sasa ya mwili kubabuka na kuota magamba; huku nywele na kope zikipukutika, Dk. Mwakyembe alishautangazia umma kwamba maisha yake yamo hatarini.

Huyu ni mbunge na naibu waziri ambaye ataingia katika vitabu vya kumbukumbu kwamba ni mbunge wa kwanza nchini kuandika rasmi barua kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) akilalamika kwamba kuna wauaji wa nje wamekodishwa kuja kumuua, na kisha akatoa maelezo zaidi jinsi walivyomfuatilia kwa gari alipokuwa safarini.

Sikumbuki kama katika historia ya Tanzania ya miaka 50 iliyopita kuna mbunge au waziri aliyemwandikia barua rasmi IGP akimtaarifu kuwa kuna wauaji wa kigeni wanamfuatilia kwa lengo la kumuua. Kama yupo, nikumbusheni.

Lakini japo IGP wetu alikiri kuipokea barua hiyo ya Mwakyembe, hakuna maelezo yaliyotolewa mpaka sasa kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na madai hayo ya Mwakyembe au hata kuuelezea tu umma upelelezi wa suala hilo ulipofikia.

Sasa wakati umma ukisubiri kuelezwa na IGP maendeleo ya uchunguzi wa malalamiko hayo yaliyowasilishwa na Mwakyembe juu ya watu wanaotaka kumuua, ghafla anakumbwa na ugonjwa huo wa ajabu na kukimbizwa India – ugonjwa ambao yeye mwenyewe anaamini chanzo chake ni sumu!

Sasa, katika hali hii, na katika mazingira haya ambapo bado hali ya afya ya Naibu Waziri huyo haijatengemaa; licha ya kupelekwa India kwa matibabu, Serikali haioni lojiki kuiweka sasa hadharani ripoti hiyo ya madaktari wa India waliomtibu ili ukweli ufahamike?

Nionavyo mimi, ni busara Serikali ikatoa tamko sasa kuhusu kilichomsibu Mwakyembe na kuweka hadharani chanzo cha ugonjwa unaomsumbua wakati Mwakyembe mwenyewe angali hai ili awe na fursa ya kukubaliana na hicho kitakachoelezwa na Serikali au kukikataa.

Mungu aepushie mbali, lakini kama Mwakyembe atafariki na kutangulia mbele ya haki, chochote ambacho Serikali itakitamka baada ya yeye kufa kuhusu kilichomuua, hakitaaminika kwa jamii.

Kwa maneno mengine; ni vyema Serikali itamke sasa kuhusu chanzo cha ugonjwa wa Mwakyembe; vinginevyo akifariki, itabidi ifunge mdomo milele!

Nimalizie makala yangu kwa kumwambia tena Dk. Mwakyembe: Hang in there brother, pambana kuokoa maisha yako. Mungu atakusaidia utapona. Watanzania wanakupenda kwa jinsi ulivyojitolea mhanga kuwatetea kwa kupambana na ufisadi.

Kwa upande wa Serikali yetu, nisisitize tena kwamba ina wajibu wa kuueleza umma wa Tanzania juu ya kilichomsibu Dk. Harrison Mwakyembe.

Tafakari.

28 thoughts on “Serikali yasita nini kuweka wazi ugonjwa wa Mwakyembe?”

 1. joe says:

  Kwanza nikupongeze sana kwa ujasiri wako mkubwa wa kuuelimisha umma juu ya ugonjwa wa shujaa wetu ,kiukweli binafsi imenigusa sana,na kama serikali yetu haina mkono wake juu ya ugonjwa wa mwakiembe wasimame na wauweleze umma kwamba nini hasa kinamsibu jemadari wetu,hatuoni sababu yeyote ya msingi serikali yetu kuficha angali muhusika kasema iwekwe hadharani.

  Hii inaonyesha wazi kwamba serikali yetu sio wazi na wapo baadhi ya viongozi mafisadi wanatunyonya na ndio chanzo cha maisha magumu hivi ambao wanajilimbikizia mimali na pindi wanapofichuliwa wanataka kuwauwa wasema ukweli,

  Kwa kifupi no one is above the lord,mwakiembe ni mtetezi wa watanzania na ni wazi kwamba mungu kamuacha mwakiembe hai mpaka sasa ili watanzania wajue ukweli juu ya mchezo mchafu unaofanyika,na ndio maana unasikia mara moja fulani kafariki ghafla kumbe ni wao wanaowamaliza.

  Hakika mungu wetu sio wa namna hiyo jinsi mfikiriavyo,na mtashindwa kwa jina la yesu,ngudu zetu waislamu na wakristo tuombe sana kwa mungu awaadhibu mafisadi na hao viongozi wanaootaka madaraka kwa ajili ya masilahi yao na hao wanaouwa viongozi wetu wema wanajali masilahi ya wananchi.

   

 2. Msomaji wetu says:

  Mimi ni miongoni mwa hao watakao ikataa taarifa yoyote ya serikali kuhusu kifo cha Dr Mwakyembe, ikitoka baada ya kifo chake..Ili serikali isije kuwa na kazi pevu ya kujieleza kwa matanzania. Ni vema kama wasema leo wakati Dr yu hai.

 3. raia says:

  We absolutely believe that God will heal Dr Mwakyembe, and  the WHOLE Tanzania will know that

  there is  a LIVING AND HEALING GOD… God is above ALL and His eyes are perfectly watching both the

  righteous and wicked. 

 4. John Maina says:

  ISAYA 5:22-23

  22. Ole wao walio na nguvu katika kunywa divai , na wanaume walio na nguvu za kuchanganya kileo. 23 wale wanao mtangaza mtu mwovu kuwa mwadilifu kwa kufikiria rushwa, na wanaomwondolea mwadilifu hata uadilifu wake.

 5. Mussa says:

  Nashukuru Mr. Mbwambo kwa uandishi huu. NImecheka jinsi ulivyo jitahidi kuwazuia POLISI wasije nyumbani kwako, lakini pia ukajitahidi kuyasema kwa uwazi yale ambayo kimsingi ndiyo yangewaleta nyumbani kwako kwa "mahojiano zaidi"…

   

  Nimevutiwa na JInsi ulivyomsifu Rais KIKWETE, ukam-'mponda' katibu wake wa Afya, zaidi SIO tu na taarifa zilizomo, bali UJASIRI wa kuziandika bila kuonesha hofu au wasiwasi. Nashukuru, na Mungu akulinde an wote wanaoweza kuwa wameudhiwa na makala hii…..

 6. Kiasi says:

  Jamani ni lini mtaacha kuvuatavuata serikali hata kwa personal issues?????????????????

 7. Kiasi says:

  Ni lini tutaacha kuzingizia vitu vyote kwa serikali bila hata kujali kuwa tunachokisema ni kweli? Kweli kwa sasa tumebaki kama watu tusiokuwa na imani na kuamini uchawi na uzadiki? Hivi watu hawana maadui wao binafsi ambao wanaweza kutumia nafasi hii kuwaumiza wengine kwa vile tu kuna watu wenye uwezo wa kutuisti maandiko na kuizingizia serikali? Haya ni maajabu ya kutosha.

 8. mwai says:

  mh mpaka machozi yananitoka katika makali hii mungu amlinde mnyakyusa mwenzetu maana mungu ndo ajuaye yote maana yeye ndiye aliyeanzisha safari yetu na ndiye ajuaye mwisho wake ka maana katika yote

   

 9. hakimu mwafongo says:

  nami nikupongeze kwa kuuarifu umma kwa kina juu ya matukio yaliyotokea kwa kiongozi, na mpiganaji juu ya kupinga ufisadi. Inashangaza juu ya ukimya huu juu ya ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe, wakati watanzania wanapenda kujua juu ya si maendeleo yake bali nini kinachomsumbua.

   

  Mwakyembe aliwahi kupata ajali mbaya ya gari alipokuwa akitokea mby kwenda jijini DSM. Baada ya ajali ile umati mkubwa ulijaa hospitalini kujua hatima ya kiongozi huyo wakati huo akliwa MB.

   

  Lakini pia nimefuatilia kwa kina juu ya taarifa zilizotolewa na yeye mwenyewe na viongozi wengine juu ya sumu. Ifike wakati serikali itoe taarifa juu ya nini kilichopo kwenye ripoti ili watanzania wapate ukweli.

   

  Mungu ni mweza wa yote.

   

   

 10. INAUMA SANA says:

  MATESO YA MWENYE HAKI NI MENGI ILA MUNGU HUMPONYA NAYO YOTE

 11. Ralph says:

  Binafsi sioni sababu ya kuilaumu serikali kwa kutotoa taarifa. Alaumiwe Dr. Mwakyembe mwenyewe kwa unafiki wake! Hilo ni pigo la pili wanamkosakosa! Alipopata pigo la kwanza la ajali, alisema kwamba anamwachia Mungu!! Safari hii amepata pigo la pili; wamemchua kwa mafuta ya kinyonga! Yote anamwachia Mungu! Anakaa kimya ili kukinusuru chama chake kinachotaka kumtoa roho! Huyu mtu, si wa kuonea huruma hata kidogo!! Angekuwa mwanamapinduzi wa kweli angekwishaweka mambo yote hadharani na kisha kuchukua msimamo na uamuzi wa dhati kuhusu hatima ya maisha yake!! Lakini Kwa mtindo huo wa kinafiki, asubiri tu pigo la tatu; hapo ndipo atakapomwachia Mungu yote kikwelikweli!!

 12. raia says:

  Mimi nashauri Dr Mwakyembe atambue kwamba mlinzi wa kwanza wa maisha yake ni yeye mwenyewe. Hivyo kama kweli kuna taarifa basi aiweke tu hadharani kwani ni taarifa juu ya ugonjwa wake, ana haki kuiweka wazi yeye mwenyewe. Kwa nini analazimisha serikali ndio iweke wazi wakati serikali inaonekana dhahiri haipo tayari kufanya hivyo? Atasubiri hadi lini? 

 13. Mambosasa says:

  Haki ya kuweka wazi ugonjwa ni ya Mwakyembe NA SIYO SERIKALI. Mwakyembe, ambaye ni mwanataaluma wa uandishi wa habari na sheria analielewa hili fika! Kama ni nia yake kutueleza Watanzania ugonjwa wake, basi afanye hima, atumie mwanasheria wake au yeye mwenyewe kutueleza yaliyomfika. Ni utaratibu duniani kote kutotoa hadharani ugonjwa wa mtu bila ridhaa yake na haki hii haihamishiki, hata kama mtu huyo ni kiongozi, LAZIMA ARIDHIE kwanza!

 14. Mashaka says:

  MLINZI WA KWANZA NI MUNGU

  Nadhani nianze kwa kuweka sawa hilo jambo hapo juu kwamba mlinzi wa kwanza wa maisha ya binadamu awaye yote ni Mungu Aliye Hai.

  Kwa hiyo anachokifanya Dr. Mwakyembe ni sahihi.

  Lakini mimi binafsi mpaka sasa ripoti yoyote itakayotolewa na serikali tayari nimeshaikaaa!

 15. Victor- Kenya says:

  Nimevutiwa sana na Kiswahili cha waTanzania kwenye ukurasa huu. Ningefurahi kama waKenya na wengine wa Afrika Mashariki wangezungumza kiswahili sanifu kama mnavyozungumza nyie waTanzania!

 16. Othman Mambosasa says:

  Kwanza nampa pole Mh. Mwakyembe kwa kuumwa. Bw. Mbwambo unataka wasomaji tuamini kuwa serikali inawajibika kutoa hadharani ugonjwa wa Mh. Mwakyembe, la hasha. Haki ya ku-disclose ugonjwa ni ya Mh. Mwakyembe mwenyewe na familia yake. Ugonjwa wa mtu ni kitu "very personal" Duniani kote suala la "disclosure" ni la binafsi. kamwe haliwezi kuhamishiwa kwa serikali au taasisi yoyote ile bila ya ridhaa ya mhusika. Namshauri Dr Mwakyembe, kama ni kweli anataka waTanzania tujue undani wa matatizo yake basi aseme yeye mwenyewe. Ataendeleaje kusubiri serikali itamke ilhali serkali hiyohiyo inaonekana kutokuwa tayari kufanya hivyo?

 17. Honolulu says:

  Hivi umri wa Mwakyembe ni chini ya miaka 18? Anahitaji mtu mwingine wa kumsaidia kujieleza? Anao mtindio wa ubongo kiasi kwamba hawezi kuongea? Ikumbukwe pia kwamba yeye ni waziri. Kwa maana hiyo, yeye ni serikali! Atoe tamko yeye mwenyewe kama waziri wa serikali! Ni serikali ipi tena unayoitaka itoe tamko? Mwakyembe ni mtu mzima na yeye ni serikali; mwacheni ajisimamie mwenyewe wala asituumize vichwa!

 18. Chris says:

  Namshukuru sana Mungu kwani hata sasa amemtunza ndugu yetu huyu mpambanaji halisi wa haki za wanyonge wa nchi hii. Lakini naomba kuthubutu kuandika kuwa Serikali inajua fika kilichomo ndani ya ripoti 'original' ya kutoka India kuhusu tatizo halisi linalomsibu Dr Mwakyembe. Nimesema 'original' kwa sababu mimi si mgeni wala Watanzania wenzangu,juu ya uchakachuaji wa kiwango cha laana wa mambo kadha wa kadha wa watendaji wengi wa nchi hii.

  Sitashangaa iwapo Dr Mwakyembe atatoa taarifa yake na kisha watendaji Wizara ya Afya wakaipinga na kutoa yao. Cha msingi ni kama Dr mwakyembe anayo nakala halisi,jambo ambalo naamini amelifanya.

  Katika hoja yangu kuhusu Serikali kujua uhalisi wa tatizo la afya ya Dr Mwakyembe,hapo ndipo penye tatizo. Kama kuna sumu,nani anahusika? Na ni nani katika Serikali hii au iliyopita? Ana uhusiano gani na utawala uliopo au uliopita? Nini athari za kuweka wazi tatizo la Dr Mwakyembe kisiasa,hasa mbio za urais 2015?  Kama ni kachero,je alitumwa na nani? Ni mkakati wa baadhi ya viongozi waliopo ama waliokuwepo madarakani ili kulinda chain yao ya kutawala? Hatuna sababu ya maana sana kwa ufuatiliaji kwa afya ya ndugu yetu kama mtu tu,hapa tunapenda kujua iwapo upo uhusika wa waandamizi wa serikali au waliopo ama waliopita katika kufanya umafia kama huu hapa nchini,na kama upo,basi iwe wazi kwa wote ili wenye kuutumia wautumie na wengine waseme sasa siasa basi. Maana isiwe mkuki kwa nguruwe tu,isiwe nafasi kwa wenye madaraka au fedha kuutumia kwa wanyonge au wapinzania wao,halafu wao wasiwekewe,no,na wao waonje joto yake ili tufike mahali tukubaliane na kuamua kwa dhati ya moyo kabisa kukomesha vitendo kama hivyo.

  Na hii nimesema,kama kweli ni sumu!

 19. Chris says:

  Sina personnal relation na Dr Mwakyembe,ila naumia sana kuona either of the two sides zinashindwa kuongelea issue yake,pengine ndugu yetu keshaona nguvu ya support ya wananchi kama akisema wazi ni ndogo,na ndio ukawa mwisho wake,au kapewa vitisho na wakubwa wake. Lakini kama ni vinginevyo basi kutakuwa na hitilafu ileile ya kutowataja na kuwawajibisha wezi wa pesa za EPA,Richmond,Meremeta nk. Ugonjwa huo ni mkubwa na hatari zaidi kuliko unaomkabili Dr Mwakyembe. Hapo je ni upole na huruma zilizopitiliza za Mh.Rais au ndio huo ugonjwa wa kuwaachia wahalifu wanaotuumiza kuliko ndugu yetu huyo?

 20. Fina says:

  jamani tusiumeze vichwa vyetu wa nyuma ya pazia kuna kundi la watu watatu,  IGUNGA YA MWAKA 47, MZEE WA VIJISENT NA MR RITCHMOND.

  sasa mwisho wa siku watakuja watuambie, hapo ndo watajua wakwamba WANYAKYUSA SI WATU WA KAWAIDA. BHAKOMILE PAMASO, IMILOSI IGHI, KIGUBHINDA NA PAMUSI, NA HAMTUWEZI KWA LOLOTE, kazi kushinda kanisani ili mchaguliwe urais, atakupa nani uraisi mwizi mkubwa wewe, matuse ga mwisukulogo.

 21. Da vinci says:

  Biiiiig up b rother kwa kuyaibua haya. BINAFSI NINASIKITISHWA NA UKIGUGUMIZI WA SERIKALI KWA JAMBO NYETI KAMA HILI. NASEMA KUWA SERIKALI INASUBIRI MWAKYEMBE AFE ILI IUDANGANYE UMMA KWA VILE SHAHIDI NA MOJA ATAKUWA AMEKUFA. PLEASE BROTHER NAOMBA UTAFUTE WANAHABARI WENZIO ILI MUENDE KWA MWAKYEMBE ILI AKAWAPE NAKALA YA RIPOTI HIYO NA MUICHAPE HADHARANI NA IINGIZWE KWENYE MTANDAO

 22. Msomaji wetu says:

  Mwakyembe toa Tamko piga CCM njoo CHADEMA ndiyo itakayotoa ripoti kwenye Kampeni za 2015,unakaa huko CCM kufanya nini Doctor wakati wameshakunyonyoa nywele,kope na kucha??

  Keep well Mwakyembe

 23. Jiniaaz says:

  Ndugu yetu hayathamini maisha yake. Ilibidi aanze mbele kitambo sana, haya yote yasingemkumba. Mbona wenzake walianza mbele na kuanzisha CCJ?

  Hakuna wa kumlaumu hapa, umechelewa kuchukua uamuzi. Tunakuombea Mungu akupunguzie machungu, na akupe ujasiri wa kuikabili hiyo hali mpya uliyomo kiafya katika maisha yako.

 24. WAKUMYITU says:
  • MUNGU NI MWEMA ATAKULINDA HATA KAMA WATAKUPA SUMU YA MAMBA
  • WATATANGULIA WAO WEWE UTABAKI TU BABANGU UKIMTUMAINIA YEYE UTASHINDA TU MPAKA KUCHA KUWA NYEUSI SIO MCHEZO HAYO MAFISADI NAYO YATAKUFA TU YATAENDA WAPI KAMA SIO JEHANAMU
 25. MWANAKIJIJI says:

  MIMI NAONA KWA SUALA HILI LA NDUGU YETU MWAKYEMBE; NI VYEMA MWENYEWE ATOE IZINI YA KUCHAPISHWA KATIKA MAGAZETI REPOTI YA UGONJWA UNAOMSUMBUA. VILE HUYO DCI MANUMBA KAMA REPOTI YAKE HAIFANANI NA HIYO YA HOSPITALI YA APOLO BASI AWAJIBIKE PAMOJA NA BOSI WAKE IGP. KWANI WANANCHI WATAKUWA HAWANA IMANI NAYE TENA. NAKUTAKIA MAISHA MAREFU NA AFYA NJEMA DR H. MWAKYEMBE. HAO WANAOCHANGISHA HELA KANISANI NA KUPIGA KAMPENI HUKU WATU WANAPATA TABU WASITEGEMEE URAISI 2015. WAGOMBEE UJUMBE WA NYUMBA KUMI

 26. Harson Njau says:

  Mambo ya hii nchi yanakera viongozi Wendi
  Kuingia kwenye utawala Kwa njia ya rushwa
  Uonevu nk.yote yana mwisho.

 27. Musemakweli says:

  Ukimya na uwoga  wa Watanzania ndiyo umefanya nchi  ikawa na hali mbaya.  Mwakyembe asinge kaa kimya angesema na kuwaeleza Watanzania wazi kitu gani kinamusumbua ili kuwasaidia Watanzania wengine wakae chonjo shida iliyompata iwe mufano wa kuepukana na watu waliyompa sumu. Uwoga wetu na Ukimya wetu Si  wa kawaida Bali ni Kama ulemavu. Kila kitu kikizidi kinaumiza.

 28. Godat Nzowa says:

  Ugonjwa wa mtu ni siri yake na daktari wake ndio maana madaktari huaga wanakula kiapo cha kutunza siri. Kwa hiyo serikali isibughuziwe mwenye shida saana akamuulize mheshiwa mwenyewe, maana serikali haijawahi kwenda kutibiwa Bara Hindi, sana sana huaga wanaenda kule watu binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *