Serikali yawakumbuka Wahadzabe

Wahadzabe ni jamii ya Kitanzania inayoishi maisha ya kale wakitegemea mizizi, matunda na wanyamapori kwa ajili ya chakula.

JAMII ya wakusanya matunda na mizizi kutoka kabila la Wahadzabe ambayo iko hatarini kupotea katika uso wa dunia, hivi sasa ina jambo la kujivunia baada ya serikali kuikumbuka kupitia ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuwatembelea watu wa jamii hiyo.

Jamii ya watu hao wanaoishi wilayani Karatu, mkoani Arusha na Mbulu, mkoani Manyara, inakadiriwa kuwa na watu wasiozidi  400 katika Wilaya ya Karatu pekee kwa sababu ya mazingira magumu ya maisha yaliyotokana na wao kuporwa maeneo yao na jamii za wafugaji na wakulima.

Wahadzabe ambao hawana uwezo wa kujitetea wamejikuta wakisukumwa pembezoni na jamii zenye nguvu na kuwafanya kukosa mahitaji yao ya kimsingi kama wanyama, matunda, mizizi ya miti na asali na hivyo kuanza kupungua.

Waziri Lukuvi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametoa agizo la jamii hiyo kulindwa kwa gharama yoyote ili isije ikatoweka katika uso wa dunia.

Lukuvi pia alitumia ziara hiyo kuwataka viongozi wa vijiji na Wilaya ya Karatu kulinda ekari 700 za ardhi ya Wahadzabe 400 waliosalia wilayani humo isije kutwaliwa na wakulima pamoja na wafugaji.

“Ni ruksa kwa Mhadzabe anayetaka kuachana na mila zake ajiunge na Watanzania wengine kufaidi umeme na huduma nyingine za kijamii na kwingineko nchini lakini ni marufuku kwa jamii nyingine kupata ardhi katika eneo la Wahadzabe,” alionya.

Waziri Lukuvi aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano haiwezi kuvumilia kuona kuwa wananchi wake wanakosa haki zao za msingi kwa sababu kuna kundi la watendaji na wataalamu ambao hawana maadili ya kikazi.

“Na nikirudi hapa baada ya miaka mitano nataka nikute ardhi hii haijaguswa na idadi ya watu wa jamii hii imeongezeka maradufu,” alisema Lukuvi.

Shirika la UCRT

Shirika lisilokuwa la kiserikali la Ujamaa Community Resources Team (UCRT) ambalo limekuwa mstari wa mbele kupigania haki za ardhi kwa jamii za pembezoni, limeona umuhimu wa kuwasaidia Wahadzabe kupata hati miliki za ardhi ili kuokoa utamaduni wao usitoweke katika uso wa dunia.

“Tuliamua kuzisaidia jamii za pembezoni juu ya matumizi bora ya ardhi na kupata hati miliki za kimila ili kuhakikisha zinabaki katika uso wa dunia,” alisema Mkurugenzi wa UCRT, Makko Sinandei.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, shirika hilo limeandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa jamii ya Wahadzabe na Watatoga wa miaka kumi ijayo ili kulinda ardhi yao.

Wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao umewezesha jamii hizo kupata hati miliki za kimila, UCRT ilikabiliwa na chagamoto ya muingiliano wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 na sheria ya wanyamapori.

Sinandei aliiomba serikali kuangalia sheria hizo upya ili kusaidia jamii za pembezoni kutokupoteza haki zao za kumiliki ardhi siku za usoni.

“Changamoto ya uhusiano mbaya kati ya jamii za pembezoni na wawekezaji, ni kubwa sana hivyo naiomba serikali kutenga maeneo maalumu ambayo yatatenganisha shughuli za jamii na wawekezaji,” alisema.

Mwaka huu UCRT ilipata tuzo hiyo ya juu inayotolewa kwa mashujaa wa mazingira duniani ijulikanayo kama Goldman Environmental Prize award, kwa jitihada za kusaidia jamii za pembezoni kumiliki ardhi kisheria.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mratibu wa UCRT, Edward Loure, mwezi mwaka huu, nchini Marekani.

Kwa miongo miwili UCRT wamefanikiwa kusaidia jamii zilizoko pembezoni hasa kaskazini mwa Tanzania kumiliki takribani hekari nusu milioni kisheria katika jitihada zao za kulinda jamii hizo na tamaduni zao kutopotea katika uso wa dunia.

“Sitapumzika mpaka hapo jamii hizi za pembezoni zitakapomiliki ardhi zao kisheria …lengo letu ni kuongeza mara mbili ya ardhi itakayomilikiwa na jamii hizi kufikia mwaka 2020,” alisema Mratibu wa UCRT, Loure.

Shujaa huyo wa Mazingira, pamoja na mambo mengine, ametuzwa kwa kubuni mkakati wa amani unaowashirikisha serikali, jamii na washirika wa kimaendeleo kumilikisha jamii hizo ardhi kisheria.

Mfano halisi wa mkakati huo ni mafanikio ya kuwamilikisha jamii iliyoko katika hatari ya kutoweka, ya waokota matunda na mizizi, maarufu kama Wahadzabe, kumiliki ardhi yao ya Bonde la Eyasi wilayani Mbulu, mkoani Manyara.

Loure na wafanyakazi wenzake wa shirika la UCRT kama vile Makko Sinandei, Edward Lekaita na Dismas Partalala Meitaya, waliwezesha jamii hiyo kujiunga na mpango wa biashara ya hewa ukaa na sasa jamii hiyo imekwishapata dola za Marekani laki moja sawa na shilingi milioni mia mbili.    

“Ardhi ni uhai wa jamii zilizoko pembezoni… tunapaswa kuhakikisha jamii hizi zinamiliki, zinatumia na kunufaika na ardhi yao bila vitisho vya kuporwa na wenye nguvu,” Loure alisema.

Wahdazabe ni nani?

Wahadzabe ni jamii ya Kitanzania inayoishi maisha ya kale wakitegemea mizizi, matunda na wanyamapori kwa ajili ya chakula. 

Jamii hiyo hupatikana katika wilaya za Karatu mkoani Arusha, Mbulu mkoani Manyara, Meatu mkoani Shinyanga na Iramba mkoani Singida.

Wakati wanaume hutumia pinde na mishale kuwinda wanyama wa aina mbalimbali wakubwa kwa wadogo, wanawake hukusanya mizizi, matunda na asali kwa ajili ya chakula chao.

Katika dunia ya sasa iliyojaa technolojia unaweza kuwaonea huruma Wahadzabe kwa maisha yao ‘duni’, lakini wao hawayataki maendeleo yatakayodumaza mila, tamaduni na elimu yao ya asili hivyo kwa muda wote wamejikuta katika njia zao za asili kimaisha.

Hata hivyo Wahadzabe miaka ya hivi karibuni wamekabiliana na changamoto ya uvamizi wa ardhi yao unaofanywa hasa na wafugaji pamoja na wakulima kutoka wilaya jirani za mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Uvamizi huo unatishia siyo tu mila, tamaduni na elimu yao asilia, bali pia uhai wao kwani kilimo na ufugaji siyo rafiki kwa uoto wa asili na wanyama pori wanaowategemea kwa chakula.

Miaka 10 iliyopita kampuni ya United Arab Emirates Safiris Limited yenye uhusiano na Falme za Kiarabu, kwa mfano, walikaribia kupora ekari zaidi ya 2,000 za ardhi ya Wahadzabe ya Yaeda Chini na Bonde la Ziwa Eyasi.

Baadhi ya Wahadzabe wenyewe waliungana na wanaharakati pamoja na waandishi wa habari kuzuia jaribio la kubadilisha matumizi ya ardhi yao kuwa pori la uwindaji kwa ajili ya familia hiyo ya kifalme.

Kutokana na mahitaji yao ya msingi kuzidi kupungua, idadi ya Wahadzabe pia imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka na sasa wanakadiriwa kufikia 1,500 nchi nzima kutoka 5,000 miaka ya 1990.

Wahadzabe ni asilimia 6.3 tu ya wakazi wa Wilaya ya Karatu ambayo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ina wakazi 254,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *