Shemeji Unatuachaje Vs Ualimu Unalipa

WIKI iliyopita, matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne yalitokana kulikuwa na matokeo ambayo kwa upande wangu hayakuwa ya kushangaza.

Shule ambazo zilitakiwa kuongoza kwa ufaulu, zimeongoza kwa ufaulu. Shule ambazo zilitakiwa kuwa na wanafunzi wengi waliofeli, zimepata idadi kubwa ya waliofeli.

Kulinganisha matokeo kati ya Shule ya Feza ya Mikocheni na ile ya Manelomango iliyopo Kisarawe nikichekesho. Hizi ni shule mbili tofauti. Kinachofanana pekee ni kwamba zilifanya mtihani mmoja.

Hakunamashindanokatiyapakana samba. Hakunamashindanokatiya mamba nakenge. Hakunamashindanokatiyachanguna papa. KulinganishaFezanaKantalambaSekondariyaRukwanikulinganishapakanasimba.

Nimesoma elimu ya msingi na sekondari hapa nchini. Katika wakati wangu, na wala si zamani sana kutoka wakati huu, kulikuwa na shule za sekondari za vipaji maalumu.

Ukisikia mtu kachaguliwa kwenda Ilboru, Mzumbe au Kibaha ujue huyo uwezo wake kitaaluma ni mkubwa. Ukweli ni kwamba, wengi wa waliokuwa wakienda huko walikuwa na uwezo mkubwa.

Inawezekana kwamba kuna waliostahili kwenda huko lakini hawakwenda kwa sababu tu nafasi zilikuwa chache. Lakini, walau waliokwenda walikuwa watu wa kweli kweli.

Kwa bahati nzuri, kulikuwa na usawa katika mafunzo ya shule ya msingi. Aliyesoma Njombe na aliyesoma Moshi walikuwa wanafundishwa kituki moja katika ngazi ya shule ya msingi.

Kuna shule zilikuwa zinatoa walau uji kwa watoto wanafunzi. Hii maana yake ni kwamba hata mtoto wa masikini alikuwa anaweza kupata chochote akiwa shuleni.

Ni kweli kwamba wanafunzi waliosoma mijini walikuwa na faida kuliko wale waliosoma vijijini. Kulikuwa na walimu wengi, umeme, usafiri na faida nyingine za kimazingira.

Lakini, walau katika muda wao wa masomo, walikuwa wanasoma kituki moja na mtihani uliwakilisha sura ya kitaifa.

Leo kuna dunia mbili tofauti katika nchi moja. Kuna wanafunzi wanaosoma shule za msingi na kulipa shilingi milioni tatu kwa mwaka. Wengine wanasoma kwa kulipa shilingi elfu 40 kwa mwaka.

Ukienda katika shule za gharama za juu, utakuta walimu wa kutosha wa takribani masomo yote unayoyafahamu. Kuanzia Sayansi, Sanaa, Muziki na Michezo.

Kwenye shule za umma, walimu hawatoshi, idadi ikitosha, mara nyingi utakuta upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu.

Kwenye sekta ya umma, kuna walimu wanakaa miezi mitatu bila mshahara kwa sababu serikali inaendelea na uhakiki wa wafanyakazi hewa.

Kwenye shule za binafsi, walimu siku hizi wanaingia shuleni na magari wanayoendesha mwenyewe. Wiki moja iliyopita, rafiki yangu mmoja ambaye ni mwalimu, kaweka picha kwenye akaunti yake ya facebook akiendesha gari na kuweka maneno; “Ualimu Unalipa”.

Kwenye maandamano ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka juzi, walimu –wengi wao wakiwa wa serikali, walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa; “ Unatuachaje Shemeji?”.

Matokeo ya NECTA yaliyotangazwa wiki iliyopita yalikuwa baina  yashule mbili tu; Shule ya Shemeji Unatuacha je na Ualimu Unalipa.

Na ndiyo sababu, siamini kwamba mwanafunzi bora wa Tanzania ni yule aliyekuwa wa kwanza kwenye mitihani iliyofanyika. Kama mimi ningekuwa nagawa alama, mshindi angekuwa mwanafunzi aliyepata alama nzuri katika shule na mazingira magumu.

Mimi nina mfano mzuri wa hali ilivyo. Nilifaulu vizuri kuingia kidato cha kwanza. Nilipata daraja la kwanza. Kuna mwanafunzi nikakutana naye kidato cha tano ambaye alipata daraja la pili la mwisho mwisho.

Yeye alichaguliwa akitokea katika mojawapo ya shule za vijijini kabisa. Yalipotoka matokeo  ya kidato cha sita, yeye alifaulu kuliko wanafunzi wengine wote wa shule yetu.

Sababu ilikuwa kwamba kwenye shule mpya, hakuwa anafanya kazi asubuhi kabla ya kuja shuleni, alikuwa na uhakika wa milo mitatu kwa siku kwenye shule ya serikali, alikuwa na umeme wa kujisomea usiku na kusoma kwake na wanafunzi kutoka familia tajiri, ilimaanisha alipata baadhi ya vitini ambavyo asingevipata vijijini.

Ukiniuliza mimi, nitasema mwanafunzi bora katika mitihani ambayo matokeo yake yametangazwa, ni yule aliyepata matokeo mazuri katika shule yenye walimu pungufu, hakuna umeme, hakuna maabara na bado amefanya mtihani na kufaulu.

Huyu, kwa namna yoyote ile, siwezi kumlinganisha na mtoto aliyesomeshwa Feza, St Francis, Tusiime, Kifungilo na Baobab.

Tumewatangaza washindi na tumezitangaza shule zilizofanya vizuri. Lakini, kwangu mimi, hatujamtangaza mwanafunzi wala shule iliofanya vizuri.

Kwangu mimi, shule iliofanya vizuri ni ile ambayo ina mazingira magumu kwa namna zote lakini juhudi binafsi za walimu na wanafunzi zimeleta matokeo ya siyotarajiwa.

Hawa ndiyo mashujaa wangu.

One thought on “Shemeji Unatuachaje Vs Ualimu Unalipa”

  1. Shadrick kyamba says:

    Kamwaga umesema kweli lakini umesahau changamoto kubwa sana ambayo ni mlundikano wa wanafunzi darasani kwenye shule za kata na mbaya zaidi wakitokea eneo moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *