Sheria ya Habari yapingwa mahakamani

ASASI za kiraia na wanaharakati nchini wamefungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) jijini Dar es Salaam kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari Tanzania.

Kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2016 imefunguliwa leo ambapo, pamoja na mambo mengine, inapinga sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5 mwaka huu.

Walalamikaji wakuu katika kesi hiyo ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  nchini(THRDC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, walalamikaji katika kesi hiyo wanaoziwakilisha taasisi zao ni pamoja na  wanasheria Fulgence Massawe, Donald Deya, Jenerali Ulimwengu, Jebra Kambole, Francis Stolla na Mpole Mpoki.

“Washirika wanataka baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ambavyo vinakandamiza uhuru wa habari  wa kujieleza vifutwe kwani vinakiuka matakwa ya Mkataba wa Jumuiya  ya Afrika Mashariki ambazo zinataka nchi mwanachama kuzingatia na kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye Ibara 6(d) na 7(2);

Ibara ya 6 (d) ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inahimiza umuhimu wa kufuata kanuni za utawala bora, utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi ,haki kwa wote, usawa wa kijinsia, kulinda na kuheshimu haki za binadamu.

Mukajanga alifafanua: “ Hali kadhalika, Ibara ya 7 (2) ya mkataba huo inaitaka nchi mwanachama kufuata na kuheshimu kanuni za utawala bora, ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni za demokrasia, utawala wa sheria na haki kwa wote”.

Kama ilivyo kwenye kifungu cha 8(1)(c), Tanzania inatakiwa kuchukua hatua za kuhakikisha haki zote zinazotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na kutekelezwa .

Kwa mujibu wa walalamikaji katika kesi hiyo, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari 2016 inafinya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari ambayo ni msingi wa demokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi na utawala wa bora ambayo Tanzania iliridhia mkataba huo Julai 7, 2000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *