Makala
ITIKADI YA CCM KIZAZI KIMOJA BAADAYE
Sheria za Tanzania bado zina mianya inayoruhusu kujengeka kwa udikteta
Deusdedit Jovin
Toleo la 011
9 Jan 2008

MWAKA 2005 wakati wa kampeni za kuwania urais, Jakaya Kikwete akiongozwa na ibara za 69 na 99 katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2005); ibara za 84, 85 na 86 katika kijitabu cha Mwelekeo wa Sera za CCM (2000-2010); na ibara za 5(5) na 5(8) katika katiba ya CCM (1977), alizunguka nchi nzima akifafanua kwamba "CCM ni muumini thabiti wa dhana za demokrasia na utawala bora".

Aliahidi kwamba "CCM itahakikisha" kwamba jitihada za makusudi zinafanywa ili "kuendeleza na kuimarisha mazingira yenye kuthibitisha kwamba, wananchi ndio wenye madaraka ya kuongoza Serikali". 

Kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo, alisisitiza kwamba Serikali atakayopewa ridhaa ya kuiunda itaimarisha "utawala wa sheria na kuzipitia upya sheria zinazogongana kwa lengo la kuiondoa migongano hiyo".

Aidha, alisema kwamba "mambo ambayo yamekuwa yakifanywa kwa maagizo" yatawekewa "mfumo wa sheria" ambao hautaacha "mianya ya kujengeka kwa udikteta wa aina yoyote". 

Hivyo basi, kwa kuzingatia kwamba hivi sasa tunaelekea katika uchaguzi wa mwaka 2010, makala hii inachunguza maana na maudhui ya dhana ya "utawala wa sheria" ili kubainisha vizuri ninachofikiri alikisema Kikwete kama ahadi yake kwetu wapiga kura hapo mwaka 2005.

Kimsingi, nitaonyesha kwamba bado mfumo wa sheria za Tanzania umeendelea kuacha "mianya ya kujengeka kwa udikteta" na hivyo kupuuzia misingi mikuu ya "utawala wa sheria".  Ninazo sababu kadhaa za kunifanya niamini hivyo.

Sababu ya kwanza inayonifanya kuamini kuwa sheria za Tanzania zina mianya inayoruhusu kujengeka kwa udikteta ni kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya 1977, ibara ya 7(2), Serikali imepewa haki ya kuishi juu ya paa la nyumba ya sheria.

Ibara hii inasema kwamba hakuna mahakama nchini yenye mamlaka ya kuchunguza ikiwa Serikali imetekeleza au haikutekeleza majukumu yake katika jambo lolote linalohusu malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za nchi.

Lakini katika dola inayoongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, raia na serikali kwa pamoja hulazimika kuishi chini ya paa la nyumba moja ya sheria kwa sababu utimamu wa akili ya binadamu hautabiriki.

Katika ujumla wake, utawala wa sheria ni utawala unaohakikisha kwamba haki zote za binadamu zimeingizwa katika zizi la sheria za dola na kuwekwa chini ya ulinzi endelevu wa mahakimu wanaolinda zizi hilo.

Yaani, utawala wa sheria ni utawala unaohakikisha kwamba ikiwa kuna mdai aitwaye 'A' akiwa na haki ya kudai kitu kiitwacho 'B' kutoka kwa mdaiwa aitwaye 'C' ambapo mdaiwa 'C' anao wajibu wa kutimiza madai kwa sababu ya maelezo ambayo hapa tuyaite 'D', basi pia kuna msuluhishi aitwaye 'E' akiwa na jukumu rasmi kisheria la kusuluhisha ugomvi kati ya mdai na mdaiwa, iwapo hawa wawili watatofautiana.

Kuna uhusiano wa haki na majukumu kati ya serikali ya dola na raia. Hivyo, mara zote, katika dola inayoongozwa kwa kufuata kanuni sahihi za utawala wa sheria, msuluhishi aitwaye 'E' huwa ni mahakama yenye mamlaka ya kutafsiri sheria husika ili kuona matendo yapi ni ya kifisadi na yapi siyo ili hatimaye haki ichukue mkondo wake.

Hivyo basi, inaweza kuhitimishwa kwamba, ibara ya 7(2) katika Katiba ya Tanzania (1977) haikubaliki kwa sababu ni ibara inayotoa mwanya wa kujengeka kwa udikteta wa Serikali dhidi ya raia.

Sababu ya pili inayonifanya kuamini kuwa sheria za Tanzania zina mianya inayoruhusu kujengeka kwa `udikteta ni kwamba, si Katiba wala Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini (2004) inayoeleza chochote kuhusu 'sifa za kazi' (compensable factors) zinazoweza kutumika katika kutengeneza mifumo ya mishahara ya haki kazini (equitable salary structures).

Kutajwa kwa sifa hizo kungeweka mizani huru ya kitaifa kwa waajiri wote pale wanapotengeneza mifumo yao ya mishahara. Mifumo ya mishahara iliyotengenezwa kwa kuzingatia 'sifa za kazi' huonyesha vizuri viwango vya malipo ya waajiriwa na fomula zitakazotumika katika kuamua mwajiriwa fulani alipwe kiasi gani.

Bila hilo kufanyika mishahara inaweza kulipwa, si kwa kuangalia 'sifa za kazi' inayofanywa, bali kwa kuangalia sura, dini, kabila, mbari (race), na kadhalika.

Lakini katika dola inayoongozwa kwa kufuata utawala wa sheria raia lazima waishi chini ya paa la nyumba ya sheria iliyoandikwa ili binadamu wote waweze kutendewa kwa usawa mbele ya sheria hiyo.

Katika Tanzania ya leo, kadiri mifumo ya mishahara inavyohusika, ni wazi kwamba kunaweza kuwapo na mifumo tofauti ya mishahara kwa kila tabaka linaloweza kufikirika duniani, hata kama ni ndani ya kampuni ile ile moja!

Hii ni kweli kwa sababu, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini (2004), mbali na kutaja katika ibara ya 15 kwamba mwajiri anawajibika kumwambia mwajiriwa fomula iliyotumika katika kuamua malipo ya mishahara, haitoi mwongozo wowote kwa mwajiri huyo kuhusu namna ya kutengeneza fomula hiyo!

Hii ni dosari kubwa kwa sababu, unyumbulifu wa tabia ya binadamu umeruhusiwa kutawala na hivyo kutoa mwanya wa udikteta katika zoezi zima la kuamua ujira.

Naamini ni kwa sababu hii, katika makampuni mengi na katika idara nyingi za Serikali, kuna bonde la ufa kati ya mishahara ya waajiriwa wa ngazi za juu kabisa kwa upande mmoja na mishahara ya waajiriwa wa ngazi za chini kabisa kwa upande mwingine!

Ninakubali kwamba usawa mbele ya sheria haumaanishi kuwa waajiriwa wote wapewe ujira sawa hata kama wanafanya kazi zenye sifa tofauti. Lakini lazima wote wahukumiwe kwa mujibu wa mfumo mmoja wa mishahara japo mfumo huu waweza na unapaswa kuwa na ngazi tofauti za malipo zilizohalalishwa na kuwekwa wazi kulingana na 'sifa za kazi' zinazofanywa (equality in kind coupled with diversity of difference in degrees).

Lakini tofauti tajwa haziwezi kuwekwa kwa kutumia vigezo nasibu (arbitrary criteria) kama vile rangi ya ngozi, jinsia, dini, ukanda, cheo kama vile mkuu wa mkoa au mbunge, urafiki, nasaba na vigogo, au vigezo vingine ambavyo binadamu hakuvichagua yeye. Hii ndiyo maana ya usawa mbele ya sheria!

Ni maoni yangu kwamba, kwa lengo la kuziba bonde hilo sheria za ajira lazima ziboreshwe kwa kuweka bayana mfumo wa mishahara wa kitaifa. Mfumo huu utawaongoza waajiri katika kuandaa mifumo yao ya mishahara ambayo watalazimika kuioanisha na mfumo wa mishahara kitaifa. 

Ni kwa njia hii pekee tunaweza kuongelea usawa mbele ya sheria ya ajira. Hivi sasa usawa huo haupo na hii ndiyo sababu tunaaendelea kupiga kelele kuhusu bonde la ufa wa kipato kati ya matabaka ya juu kabisa na matabaka ya chini kabisa katika sekta mbalimbali za jamii.

Sababu ya tatu inayonifanya kuamini kuwa sheria za Tanzania zina mianya inayoruhusu kujengeka kwa udikteta ni kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika viitwavyo Saccos (2003) katika ibara ya 26(2) Msajili wa Saccos akikataa kuisajili kwa sababu yoyote ile rufaa inapaswa kuandikwa kwa Waziri wa Ushirika ambaye uamuzi wake ni wa mwisho!

Katika hili, Waziri wa Ushirika amepewa mamlaka ya kufanya kazi za mahakimu na wabunge. Lakini kanuni za utawala wa sheria zinaelekeza kwamba lazima uwepo utenganisho wa kofia za madaraka ya kiofisi kadiri kazi za kutunga sheria, kutafsiri sheria na kusimamia utekelezaji wa sheria zinavyohusika. Binadamu si malaika kwa maana kwamba akili yake haitabiriki.

Na, kwa kweli, maumivu yamekwishaanza kujitokeza kwa sababu ya mwanya huu wa udikteta katika sheria ya Saccos. Kuna baadhi ya Saccos zinaendeshwa kama maduka ya kaya kama si miradi ya nyumba ndogo za marafiki zao maafisa ushirika! Sheria ya Saccos lazima iboreshwe kuondoa mwanya huu wa udikteta.

Ninayo mifano mingi kuonyesha mianya ya udikteta katika sheria za Tanzania lakini ukurasa hautoshi. Hivyo naishia hapa kwa leo.

Lakini hapa itoshe tu kusema kwamba sheria za dola ni taratibu halali zinazomega uhuru wa raia katika kufikiri, kuamua na kutenda na hivyo kulazimisha utii wao kwa mamlaka husika kwa lengo la kuzuia ufisadi na hivyo kuongoza matendo yao katika namna ambayo itafanikisha matilaba ya pamoja (common goods), taratibu hizi zikiwa zimetungwa na mamlaka halali baada ya mchujo timamu wa kiakili, na kisha kutangazwa kwa wanajumuiya wote kabla ya kuanza kutumika, ambapo mamlaka hii huwa na kibali cha kusimamia utekelezaji wake hii ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu dhahiri kwa wale watakaothibitika kuzikaidi.

Lakini je, ni halali kutunga sheria kwa lengo la kumega uhuru wa binadamu katika kufikiri, kuamua na kutenda? Tutalijibu swali hili katika makala ijayo.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Deusdedit Jovin
deus.jovin@gmail.com
+255-0758341483, +255-0684175182

Toa maoni yako