Shiza Kichuya sasa anachanganya

TAKWIMU za Shiza Kichuya hazimoseki vizuri wakati huu. Hazisomeki kwenye chati ya ufungaji wala kuhusika katika kutengeneza mabao.

Huyu sio Kichuya aliyetoka Morogoro, mji uliokuwa chimbuko la wanasoka wengi hodari nchini kuja Dar es Salaam kujiunga na timu za Dar es Salaam. Amebadilika kidogo.

Kichuya aliyefunga mabao tisa katika michezo ya Ligi Kuu Bara sawa na washambuliaji wa Yanga, Simon Msuva na Ammis Tambwe, amekuwa na wakati mgumu tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Bao lake la kusawazisha dhidi ya Yanga Oktoba Mosi, 2016 ni miongoni mwa vitu vizuri vinavyokumbukwa na wapenzi wengi wa soka nchini.

Lakini sasa, Kichuya aliyefunga bao lake la mwisho Novemba 2, 2016 kwenye mchezo wa timu yake dhidi ya Stand United, hajafunga tena mpaka wakati huu ambao timu yake imekuwa na uhaba wa mabao klabuni.

Baada ya kuona kiwango cha kiungo huyo kimefikia hatua hii, Raia Mwema, iliwatafuta baadhi ya makocha na wachezaji wa zamani na kuzungumzia juu ya kiwango cha kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.

Wakizungumza kwa wakati tofauti juu ya kiwango cha kiungo huyo, watu hao wamesema Kichuya anahitaji kuzungumza na watu wa kumjenga kisaikolojia ili arejeshe makali yake.

Ofisa Maendeleo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jemedali Said, amesema nyota huyo hakupotea kama inavyodhaniwa na wengi isipokuwa anavyocheza sasa ndiyo uwezo wake wa kila siku tangu yuko Mtibwa Sugar.

Jemedali aliongeza kuwa anavyocheza Kichuya hivi sasa ndiyo alivyokuwa akicheza hata Mtibwa Sugar, lakini kutokufunga ndiyo shida inakoanzia.

“Kichuya hajashuka kiwango kama inavyodhaniwa, lakini wengi wanamtazama kwenye chati ya ufungaji kitu ambacho wanakosea.

Simba walimsajili Kichuya kwa maana ya kutengeneza mabao na sio kufunga, licha ya kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye mzunguko wa kwanza.

“Hali aliyonayo sasa inatokea kwa wachezaji wengi wanapoanza msimu, katikati ya msimu na mwisho wa msimu. Lakini kikubwa ni watu wake wa karibu kuzungumza naye vyema maana wao ndiyo watakuwa wanajua matatizo aliyonayo tofauti na sisi ambao tunaishia kumtazama tu akiwa uwanjani.

“Kuishi katika presha ya timu kubwa kunahitaji mchezaji aliye timilifu. Timu kubwa kuna presha inayotokea kila upande na kuna msukumo mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo mara nyingi huwatoa kwenye reli wachezaji wengi. Kichuya alivyokuwa Mtibwa Sugar hakuwa katika hali hii ya kuandikwa na kuzungumzwa kila siku, sasa anavyokuja timu kubwa atarajie haya yanayomtokea na ayachukue kama changamoto na aanze kucheza kitimu na asitake kucheza kibinafsi ili afunge na kulifanya jina lake liendelee kuwa juu.

Umri wake mdogo unahitaji utulivu wa ziada ili aweze kuikubali hali hii,’’ alisema Jemedali.

Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ kocha aliyewahi kuzinoa klabu mbalimbali nchini amesema watu wanamtazama Kichuya kama mfungaji ndiyo maana wanamuona amepoteza, lakini Kichuya ni mtengenezaji mzuri zaidi wa mabao.

“Wasichokijua watu wengi kuhusu huyu Kichuya tangu anashiriki michuano ya Copa Coca Cola alikuwa mtengenezaji mahiri wa mabao na sio mfungaji mahiri wa mabao. Alivyokuwa akifunga ni kama ilikuwa bahati yake tu, lakini muda mrefu tangu nimjue Kichuya ni mtengenezaji wa mabao. Kichuya hawezi kuwa Tambwe wala Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ambao ni wafungaji mahiri.

“Kama mwalimu namuona anafanya vyema kazi yake ndani ya uwanja, lakini ukija kumtazama kishabiki utaona ni kama mchezaji anayecheza bila malengo uwanjani,” alisema Mzazi’.

Mshambuliaji aliyeacha rekodi ya kufunga mabao mengi katika mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara wakati huo mpaka hivi sasa, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ amesema kinachomfanya Kichuya afikie katika hali hii ni kutukuzwa katika vyombo vya habari.

Mmachinga aliyewahi kufunga mabao 26 msimu wa 1994/1995, amesema vyombo vya habari vilimuweka juu na mchezaji hawezi kucheza vizuri kwenye kila mchezo, hivyo inakuwa ngumu kwa mchezaji mdogo kuimudu presha ya namna hii.

“Nimecheza mpira katika kiwango kikubwa sana. Nawafahamu mlivyo nyinyi (waandishi) mkiona mchezaji anafanya vizuri kidogo tu huwa mnamkuza mpaka mnamtoa mchezoni na kujiona yeye ni mkubwa wa kila kitu, sasa kitu hiki ndicho kilichopunguza kasi yake wakati huu ambao hafungi mara kwa mara kama ilivyokuwa kwenye mzunguko wa kwanza. Ukomavu wa mchezaji huanzia kwenye mazingira ya namna hii sasa anahitaji kutuliza munkari na ajengwe upya kisaikolojia na iko siku atarudi katika makali yake maana ana kipaji kizuri cha soka,” alisema Mmachinga.

Kiungo wa zamani wa timu ya taifa Tanzania (Taifa Stars), na klabu za Simba na Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ amemtaka nyota huyo aimarishe upya kiwango chake na ikiwezekana ajiulize ilikuwaje mzunguko wa kwanza alifunga idadi kubwa ya mabao na mzunguko wa pili anaonyesha kiwango duni uwanjani.

“Kuna baadhi ya vitu Kichuya anatakiwa kuvifanya wakati huu, kimojawapo ni kujiuliza ilikuwaje wakati ule anafunga mabao na hivi sasa hafungi tena, hiki ni kitu anachotakiwa kujiuliza na akishapata majibu yake nadhani tutaendelea kumuona Kichuya wa mzunguko wa kwanza,” alisema Chuji.

Chuji aliendelea kusema kuwa kuja na kupotea kwa wachezaji wengi wanaosajiliwa timu kubwa ni kushindwa kujilinda na mambo ya mjini ambayo wengi huwazidi wachezaji.

Chuji alifafanua kuwa anafahamu Kichuya anakamiwa na walinzi wa timu pinzani ambao inaweza kuwa sababu ya yeye kushindwa kufanya vyema na kuongeza kuwa hali ya kukamiwa iko duniani kote na ndiyo inayompa mchezaji ujasiri wa kupambana na kuonyesha kiwango chake bora.

“Unadhani mtu kama Tambwe yule wa Yanga hakamiwi? alihoji Chuji. Wachezaji wengi wanakamiwa lakini ukikamiwa ndiyo unatakiwa kuonyesha kiwango, haina maana ya kukamiwa ndiyo unashindwa kabisa kucheza hata mpira wenyewe,” alisema.

Chuji alimaliza kwa kumtaka Kichuya afahamu mpaka sasa hajapata majeraha ambayo anaweza kusema yamepunguza kasi yake, hivyo hana tatizo lolote mwilini mwake sasa anatakiwa kuonyesha kiwango kwenye mazingira yoyote yale.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *