Shule ya St. Juddy Arusha matatani kwa kufukuza wanafunzi

UONGOZI wa shule ya binafsi ya St. Juddy, mkoani Arusha umeingia matatani baada ya ‘kuchongewa’ kwa Mkuu  wa Mkoa huo, Mrisho Gambo, kwa tuhuma za kuwafukuza shule wanafunzi saba wenye umri kati ya miaka sita na 12, kwa sababu mbalimbali za kinidhamu.

St. Juddy ni kati ya shule binafsi maarufu mkoani Arusha ikiwa na mtandao wa shule ya msingi na sekondari na hutumia mtaala wa masomo ya lugha ya Kiingereza.

Wanafunzi hao walifukuzwa shule Novemba 29 mwaka huu, wakidaiwa kuwa ni ‘wadokozi’ wa vitu mbalimbali shuleni hapo ikiwemo cocoa, biskuti, milo, kahawa, papai na fedha taslimu  shilingi 1,000.

Kwa mujibu wa barua ya mmoja wa wanafunzi waliofukuzwa ambayo Raia Mwema inayo nakala yake, wanafunzi hao wanadaiwa kudokoa vitu vilivyotajwa kwa nyakati tofauti shuleni hapo.

 Moja ya barua hizo kwenda kwa mazazi inasomeka: “Ninakufahamisha kuwa kamati ya shule katika kikao chake cha tarehe 15 Novemba 2016 kiliafiki kufukuzwa kwa mwanafunzi (jina linahifadhiwa) kwa kosa la wizi….vitu vilivyoibwa na mwanafunzi ni pamoja na mapapai, milo, cocoa, biskuti, kahawa na shilingi 1,000”

Barua  hiyo imesainiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Elizabeth  Thobias na Katibu wa kamati hiyo, George Stephen, kisha nakala ya barua kutumwa kwa Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Afisa Elimu Jiji la Arusha na Mratibu wa Elimu, Kata ya Mwivaro.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka shuleni hapo wanafunzi waliofukuzwa ni wa darasa la pili (mmoja), darasa la nne (watatu) na darasa la sita (watatu) na wote wametoka kaya masikini.

Aidha kwa mujibu  wa maelezo ya wazazi, uongozi wa shule hiyo hutoa msaada kwa familia masikini kwa kuwatafutia wafadhili kutoka nje ambao hulipa gharama za masomo kwa wanafunzi hao ambao huchukuliwa kutoka katika shule za serikali kwa kuzingatia viwango vya kufaulu.

“Huwa wanakwenda shule za serikali za msingi na kuwachagua wanafunzi bora wanaoshika nafasi za juu kuanzia wa kwanza hadi wa tano na kuwahamishia katika shule zao na kuwapatia ufadhili wa masomo,” alisema mmoja wa wazazi hao, Luttu Ikondo, ambaye mtoto wake ni miongoni mwa waliofukuzwa shule.

Shule hiyo pia hutumiwa na watu wengi wenye uwezo wa kifedha kuwapeleka watoto wao kupata elimu. 

Malalamiko kwa RC

Katika barua yao ya malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wazazi hao wamepinga hatua ya uongozi wa shule hiyo kuwafukuza watoto wao kwa makosa hayo.

“Tunapinga hatua ya uongozi wa Shule ya St.Juddy kuwafukuza  watoto wetu kwa sababu sisi kama wazazi hatukuwahi kuitwa shuleni kuelezwa matatizo ya kinidhamu ya watoto wetu,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Wazazi hao wameongeza: “Hasa ikizingatiwa kuwa watoto hao muda mwingi huwa mikononi mwa uongozi wa shule kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa wanaporejeshwa nyumbani kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa wiki.”

Wazazi hao wameongeza kuwa sababu kubwa ya kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ni kutokana na mazungumzo ya ‘kidiplomasia’ na uongozi wa shule ya St.Juddy kugonga mwamba.

“Pamoja na hayo pia watoto hawawezi kurudi tena shule za serikali kutokana sababu kubwa mbili, kwanza ni lugha kutokana na msingi kuwa kule walikuwa wanajifunza kwa Kiingereza masomo yote, na shule za serikali zinafundisha kwa Kiswahili,” iliendelea kueleza barua hiyo yenye malalamiko ya wazazi kwenda kwa RC Gambo.

Akizungumza na Raia Mwema juzi mmoja wa wazazi hao, Rehema Joseph, alieleza kuwa kutokana na uwezo wake duni kiuchumi hawezi kumpeleka shule binafsi nyingine mtoto wake aliyefukuzwa.

“Inawezekana watoto wamefanya makosa kwa kuvunja sheria za shule lakini watoto hawa ni wadogo sana hivyo adhabu tu ingetosha, kuwafukuza shule ni kuwafanyia ukatili na kuwaharibia maisha yao ya baadaye,” alilalamika mama huyo.

Mzazi huyo aliongeza kuwa adhabu ya kufukuzwa shule ni kali sana na ni ukatili dhidi ya watoto na pia hata uongozi wa shule unao wajibu wa kuwalea na una nafasi sawa na wazazi katika malezi na makuzi ya watoto.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kuhusu kuzungumzia barua hiyo hazikuweza kufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika wilaya za Longido na Arumeru, ziara ambayo hata hivyo, imekwishakamilika.

Sheria za shule

Kwa mujibu wa sheria na kanuni namba nane ya shule hiyo ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, hairuhusiwi kwa mwanafunzi kumiliki vitu vinavyokatazwa kama vile simu, redio, CDs, VCD, kamera na vifaa vya kompyuta.

“Ni marufufuku kuleta aina yoyote ya chakula au vitu vya kutafuna shuleni, chakula kitaandaliwa na kuliwa kwenye bwalo la chakula hakuna chakula kitakachoruhusiwa kuliwa nje ya bwalo,” inaeleza kanuni hiyo.

Lakini  wazazi ambao wanalalamika watoto wao kufukuzwa na wanapinga sheria na na kanuni za shule hiyo kuwa hazikidhi mahitaji ya elimu katika dunia ya sasa.

Kiongozi wa kundi la wazazi ambao watoto wao wamefukuzwa shule Luttu Ikondo aliliambia Raia Mwema kuwa sheria na kanuni hizo haziwezi kuwa sababu ya watoto wao kufukuzwa shule.

“Hivi inawezekanaje mtoto wa darasa la pili afukuzwe shule kwa sababu tu ‘amedokoa’ kitu shuleni? Watoto kwa kawaida sheria inawalinda nimeshangazwa na sheria za shule hii na ningejua kabla, wasingemchukua mtoto wangu,” alisema Ikondo.

Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo Elizabeth Thobias ambaye  ametia saini barua zote za wanafunzi hao kufukuzwa shule aliliambia Raia Mwema kwa njia ya ujumbe wa simu kuwa yuko safarini kuelekea mkoani Mbeya na hana nafasi ya kuzungumzia jambo hilo.

Juhudi za gazeti hili kuwapata wamiliki wa shule hiyo ambao  wametajwa kuwa ni raia wa Australia hazikuweza kufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa wote wako likizo na malalamiko ya wazazi hao yatajibiwa wakati muhula mpya wa masomo utakapoanza mwezi Januari  mwaka 2017.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *