SAYANSI bila dini ni ulemavu. Dini bila sayansi ni upofu
Si tu aliyeshiba hamjui mwenye njaa, bali anataka wengine wasipate kabisa
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
LO, mwenzangu, usiumwe jamani. Ingawa najua sisi tusio na cheo wala chuo tunaponea kwa kudra za Mwenyezi Mungu, maana gharama za kwenda kwenye zahanati isiyo na dawa hatuimudu, lakini kwa sasa kaa chonjo. Kwa hiyo, ninapokuuliza u-mzima, ubaki mzima mpenzi.
Lakini baada ya kusema hivyo, mimi mwenyewe naumwa kichwa na nazidi kuumwa kichwa maana sielewi dunia hii hata kidogo. Yaani hao wanaodai miposho mikuuuuubwa ndio hao hao wanaowatukana na kuwadhalilisha na kuwafukuza wanaodai posho ya kawaida na mazingira mazuri ya kazi. Yaani nawaelewa kwa nini wanadai miposho mikubwa maana binadamu tulivyo nani anaridhika? Lakini sielewi unafiki huo wa kutaka kuwamaliza wengine wakati huo huo. Kama kweli wanaona madaktari hawastahili mazingira mazuri ya kazi, basi wakane kwanza madai yao, ndipo hapo watapata uhalali wa kuwasema wengine.
Hayo niliona moja kwa moja nyumbani kama kawaida maana bosi alirudi anafokafoka ovyo.
‘Unaona sasa. Hawa madaktari hawana hata chembe ya huruma. Yaani wako tayari kuwaacha watu wafe eti hawajalipwa stahili yao.’ Bosi alivyoiva nilifikiri Binti Bosi ataamua kumezea lakini kila siku najifunza kwamba hawezi.
‘Lakini baba, haya madai ni stahili yao au si stahili.’ ‘Hiyo si hoja. Udaktari ni kazi ya wito, ni kazi ya kuwatumikia watu na asiyefanya hivyo hastahili kuwa daktari kabisa, achilia mbali kupata stahili yake.’
‘Mbona unaniambia kila siku kwamba siasa ni wito lakini hamwachi kudai miposho zaidi na zaidi.’ ‘Hii ni tofauti. Watu wanawategemea madaktari ili wapone, lakini wanatutegemea sisi tuwagawie pesa ndiyo maana tunahitaji posho zaidi.’
BB alimwangalia baba yake kama vile pua imeenda upande. ‘Yaani baba kweli unaweza kuniambia hivi? Yaani nyinyi mnahitaji posho zaidi kwa ajili ya kuhongea nafasi zenu wakati madaktari wanatakiwa kufanya kazi bila malipo?’
‘Wewe kwa kweli unataka kuelewa mambo kwa namna tofauti kila siku. Hakuna kuhonga, tunachangia maendeleo ya majimbo yetu.’ ‘Lakini kuna mfuko wa jimbo ….’
‘Haitoshi.’ ‘Lakini sijasikia baba mahali ambapo watu wanatakiwa kuchangia fedha zao binafsi …’ Bosi akatabasamu, tabasamu ya kifedhuli kabisa.
‘Ndio wito wetu mwanangu.’
Lakini BB alikuwa hajamaliza.
‘Kwa hiyo, ili utekeleze wito wenu, inabidi uongezewe pesa za walipa kodi?
‘Sawa kabisa. Utagawaje fedha kama mfuko hauna kitu?’
‘Kwa hiyo wito wa madaktari ni vile vile. Lazima ulainishwe na fedha wanazostahili?’
Bosi kaona ametegwa vibaya sana.
‘Toka hapa mtoto wa ibilisi wewe ….’
Na kweli BB aliamka na kama nilisikia vizuri alisema kichinichini
‘Kama mimi ni mwanaibilisi, ibilisi ndiye nani?’
Bosi naye ni kama alisikia lakini hakuwa na uhakika.
‘Ulisemaje? Ulisemaje?’
BB hakujibu.
‘Ulisema nini? Hebu sema kwa sauti tusikie upumbavu wako.’
BB alisimama karibu na ngazi.
‘Nasema hivi baba. Si tu aliyeshiba hamjui mwenye njaa … aliyeshiba anataka kushiba peke yake na kuwanyima watu wote wengine wasipate chakula.’
Bosi alimrukia mwanaye na kumzaba kibao.
‘Huna adabu wewe. Mimi nahangaika kukupatia maisha mazuri, kumbe ujira wangu ni matusi.’
BB akalia kwa sauti huku akimkimbia baba ambaye alijaribu kumfikia ili amzabe vibao tena.
‘Kama maisha mazuri yanategemea hayo mimi sitaki. Bora nisome shule ya kata huku najivunia uadilifu wa baba kuliko kutukanwa kila siku shuleni eti baba na wenzie ni genge la wahuni tu.’
Lo! Baba alizidi kukasirika na kumkimbiza mwanaye kwa nguvu zote.
‘Ngoja nikupate. Ngoja, utatanitambua leo. Nitakuonyesha …’
Lakini wakati anajaribu kumfikia, akateleza na kuanguka chini. Kibaya zaidi akagonga kichwa kwenye meza na kuzimia. Ikabidi mama bosi aje mbio mbio na kumwangalia, pamoja na BB. Bosi alipata ufahamu kidogo hadi alikuwa analalamika bila kujijua.
‘Nitamwonyesha. Nitamwonyesha. Hatuwezi anguka sisi… hatu … angu … ka.’
Kisha akazimia tena. Ikabidi akimbizwe hospitali haraka haraka. Angekuwa akina hohe hahe kama sisi angehaha kweli na mgomo huo anaoutukana lakini bosi ni bosi. Anaweza kutukana hivyo maana anajua kwamba hatatibiwa na hao anaowatukana. Akapelekwa kwenye hospitali ya Wazungu tu, asipate kukutana na Mbongo mwenye hasira. Na baadaye akarudishwa na bandeji kichwani utadhani amepigwa na vibaka. Baada ya kumpeleka kitandani MB sasa akaamua kumvaa mwanaye.
‘Unaona sasa mwanangu, kazi ya kumchokoza baba yako kila siku. Angekufa ungefanya nini?’
BB kwa kweli ilikuwa kama ameloa.
‘Samahani mama haikuwa nia yangu. Lakini baba mara nyingine ananipa maisha magumu. Si rahisi kwenda shule kila siku huku wenzio wanakukejeli.’
‘Basi shule hiyo haifai. Sisi tulidhani uko na watu wenye hadhi ya juu, hali ya juu na hivyo uelewa wa juu.’
‘Siyo hivyo mama. Wanaweza kuwa ya hali ya juu lakini kila mtu anaona mkinzano uliopo. Na hata kama watu wanatoka kwenye familia zenye uwezo, si lazima waunge mkono unafiki wa aina hiyo.’
‘Sio unafiki mwanangu!’
‘Ni unafiki mama! Posho kwao tu, wengine wakitaka pesa za kuweza kufanya kazi nzuri ni kosa la jinai? Kwani wanasiasa ni miungu tofauti na binadamu?’
‘Na wewe nawe mwanangu. Sijui unapata wapi haya maneno.’
‘Si ndiyo maneno ya watu shuleni. Hakuna anayeunga mkono linalofanyika kwa sasa. Hata watoto wa waheshimiwa wengine nao wanapata shida na wana mawazo kama mimi.’
MB akatingisha kichwa.
‘Lakini hata mimi najaribu kumshauri baba yako wakati mwingine. Lakini sijui kwa nini ukiwa mheshimiwa unajaza pamba masikioni.’
BB akafurahi.
‘Unaona mama. Watu wanasema vibaya sana. Wameona watu wanaiba pesa za mikopo ya wanafunzi. Wanafunzi wakidai haki yao wanapigwa na al Shabaab na wengine wanafukuzwa lakini kumbe wamekosa mikopo kwa sababu ya wizi. Kuna wizi mara ngapi unafanyika lakini wanaoumia ni waathirika wa wizi si wezi wenyewe.’
‘Mbona wanakamatwa?’
‘Lakini mama wanasema kwamba hata hizi posho ni wizi pia. Waheshimiwa wezi …’
Lo hata MB naye alikunja uso hadi BB akanyamaza. Lakini mimi nashangaa. Watu wamechoka, wanaonyesha kuchoka lakini wenyewe wanaendelea kujitetea hadi wanaanguka na kuumia. Makubwa!
Akupendaye mpenzi wangu … na moyo wote
Hidaya
Add new comment