JAMII ya wapenda muziki wa Tanzania imekuwa ikiaminishwa kwamba bendi ya DDC Mlimani Park Orchestre, Sikinde Ngoma ya Ukae, imekwisha kabisa siku hizi.
Dhana hiyo imekuwa ikijengwa na vyombo mbalimbali vya habari, hasa redio. Cha kusikitisha ni kwamba hata mtu anayeheshimika sana katika fani ya muziki nchini, Kamanda Muhidin Maalim Gurumo alisema hivyo mwaka huu kwenye mahojianao ya televisheni.
Dhana hiyo ingebaki ienezwe na wengine lakini si mtu mwenye hadhi ya Muhidin Maalim Gurumo.
Ukiitazama dhana hii ni kama kesi dhidi ya Sikinde ambapo wanaoieneza wameitia hatiani bendi hiyo kubwa na maarufu bila kuusikiliza utetezi wake.
Utetezi huo ni upi? Ni nyimbo zake inazotunga na kurekodi. Utetezi huo unakosekana kwa redio zetu nyingi kutopenda kupiga au kurusha nyimbo mpya za bendi hiyo. Zinazorushwa zaidi ni zile za enzi hizo.
Hali hiyo haina maelezo yoyote zaidi ya kwamba ni jitihada ya kuonyesha kuwa bendi hiyo sasa imedorora tofauti na ilivyokuwa zamani. Naomba nitoe mifano ya wazi wa juhudi hizo zisizokuwa na tija.
Wakati wa kipindi cha kushuka chini kwa muziki wa dansi wa nchi hii kufuatia ushabiki wa muziki kutoka DRC na ujio wa Redio za FM zilizoupuuza muziki huo, bendi hiyo, mwaka 1996, ilitoa wimbo uitwao "Kitendawili".
Ni wimbo ambao tangu nilipousikia kwa mara ya kwanza, niliuona kuwa mzuri sana. Ndani yake, kama kawaida ya bendi hiyo, kuna sauti za magitaa manne zilichanganyika kwa kupishana vizuri ambapo pia kuna vipande walivyoachiana kuimba mtunzi Hussein Jumbe, Shaaban Dede na Marehemu Ramadhani Mwinyikondo ambavyo viliimbwa kwa umahiri mkubwa.
Wimbo huo haukupata umaarufu kabisa wakati huo lakini leo mwanamuziki Hussein Jumbe wa Msondo Ngoma Music Band alipourudia ukiwa na upungufu kidogo wa vitu vilivyokuwamo kwenye ule wimbo asilia, (wimbo huo) umekuwa haukauki redioni, siku zote na saa zote kwa sababu sasa ni wa Hussein Jumbe na si wa Sikinde!
Miaka hiyo hiyo ya bendi zetu za muziki wa dansi nyingi kutoweka na zilizobaki kuwa chini kimuziki, isipokuwa OTTU Jazz Band (sasa Msondo Ngoma Music Band), Wana Sikinde walirekodi wimbo mmoja uitwao "Flora" ambao ulikuwa mzuri kweli kweli kwa mapigo yake yaliyotulia, hadithi yake ya kusisimua na uimbaji wa hisia kali hasa pale Dede alipolalamikia kitendo cha "Flora", Bi Harusi mtarajiwa, cha kuingia gizani baada ya kwenda Ulaya kufanya "shopping" ya Harusi.
Dede aliimba hivi huku wenzake wakichombeza kwa kutaja jina la mtarajiwa huyo: "... umechelewa ndege huko Amsterdam (Flora), au nimezidiwa ujanja ee (Flora), sijui umetekwa nyara bibi ee (Flora), mapigo ya moyoo oo oo presha..."
Wimbo huo wa mwaka 1994 ulikuwa mzuri kupita maelezo lakini haukupata mapokezi uliyostahili. Nitafurahi sana kama mtu fulani ataanza kuurusha leo kwenye redio yoyote ili ukweli wa maelezo yangu udhihirike kabla ya mtunzi wake hajaurudia kivyake ambapo ni wazi utakuwa mali ya thamani kubwa kwa sababu hautakuwa wa Sikinde bali wa mtunzi huyo!
Kudororeshwa huku kwa Sikinde hakuna msingi wowote zaidi ya juhudi za kuleta ‘Uyanga’ na ‘Usimba’ kwenye muziki.
Wanaofanya juhudi hizo wanataka ionekane kuwa Msondo sasa haina mpinzani, jambo ambalo ni la hatari si kwa muziki wetu wa dansi wa Kitanzania tu bali hata kwa Msondo yenyewe kwani kwa kuaminishwa kwamba wako pekee, hawataumiza vichwa sana kufanya vitu vikubwa.
Haipendezi kabisa kuleta siasa za Yanga na Simba kwenye muziki wetu kwa sababu huko hakuna kufungana mabao pamoja na Jumhuri ‘Julio’ Kihwelo kuwa shabiki wa Msondo na Hamisi Kinye na Juma Pondamali kuwa mashabiki wa Sikinde.
Kwa kawaida mimi ni mpenzi wa jumla wa muziki wowote mzuri wa aina yoyote uliopigwa na yeyote wa nchi yoyote ile. Ndiyo maana ninapenda kusikiliza mapigo ya wimbo kama "In da club" wa 50 cent kama ninavyoyapenda mapigo ya "This is how we do" wa "The Game" usiochuja kwangu kama vilevile ninavyofurahi kuusikiliza wimbo wa "Dar Mpaka Moro" wa Wanaume Family.
Lakini, bila kuzungusha maneno, napenda zaidi kusikiliza muziki wa The Kilimanjaro Band, Inafrika Band, Msondo Ngoma Discipline, Sikinde Ngoma Kubwa na Saga Rhumba. Kila ninaposikiliza muziki wa Sikinde, nashangaa kwa wanaoupuuza!
Baada ya bendi hiyo kupata nguvu mpya ya kina Hassan Rehani Bitchuka na marehemu Suleiman Mwanyiro, ilipanda juu tena kama ilivyokuwa miaka ya 1990 kurudi nyuma.
Walianza na albamu ya "Onyo" yenye nyimbo kama "Onyo" wenyewe, "Zumbukuku", "Isaya Mrithi Wangu", "Rehema K", "Milimo" na "Kumbuka Fadhila". Wakati huo, walishatoa wimbo mzuri wa"Nachechemea".
Nikizisikiliza nyimbo hizo, sioni kazi yoyote mbaya ya Sikinde inayohalalilsha maneno kwamba bendi hiyo sasa imekwisha. Ni nyimbo nzuri sana kwa kila kitu.
Baada ya albamu hiyo, ikaja nyingine ya "Huruma Kwa Wagonjwa" iliyokuwa na nyimbo za hadhi ya kimataifa ambazo ni "Huruma Kwa Wagonjwa", "Teddy Mwana Zanzibar", "Binamu", "Mkataa Pema", "Furaha" na nyingine.
Kwa wadau wa muziki wanaotenda haki, nyingi ya nyimbo hizo zinastahili kuwa za chati ya juu mno katika muziki wa dansi wa nchi yetu lakini cha kushangaza zilipotoka tu, hadithi ikabaki ile ile ya "Sikinde siku hizi haina kitu kabisa"!
Albamu iliyofuata nayo ya "Maneno maneno" haikusaidia kurejesha heshima ya bendi hiyo pamoja na kuwamo wimbo uliopangiliwa vizuri wa "Tende Halua" ambao wanamuziki wachanga wangeutumia kama kifaa cha kujifunzia upangaji mzuri wa muziki.
Nyimbo nyingine humo, ambazo ni nzuri pia, ni "Maneno Maneno", "SACCOS", "Kelele za Paka" na nyingine.
Kwenye albamu iliyofuata ya "Full Squad", kuna nyimbo kama "Full Squad", "Nani Amewadanganya", "Nipeni Pole", "Chozi la Huba", "Mbio za Sakafuni" na kadhalika.
Katika albamu hiyo, nyimbo kama "Nani Amewadanganya", "Nipeni Pole","Chozi la Huba" na "Mbio za Sakafuni" zinaweza kuuzwa kama njugu popote pale muziki wa aina ya wa kwetu unapokubalika lakini katu nyimbo hizo hazikupata umaarufu, lengo likiwa jamii iaminishwe kwamba Sikinde sasa iko hoi!
Kwenye wimbo "Chozi la Huba" kwa mfano, ambamo mume anasononeka mkewe kufanyiwa visa na watu wengine, lugha iliyotumika, mpangilio wa maneno na sauti, ukiongezwa na mpangilio mzuri wa vyombo vinafanya wimbo huo ustahili kuwa wimbo bora mfululizo kwa miezi kadhaa lakini hamna kitu, ingetokea hivyo ingeonekana kuwa Sikinde bado iko imara, jambo lisilokubalika na wanaoifanyia njama ionekane imekwisha.
Nimeshazisikia baadhi ya nyimbo zao za albamu inayokuja ambazo ni "Hamnazo", "King Fish" na "Heshima". Siuoni ubaya wake lakini sidhani kama albamu hiyo itathaminiwa kutokana na sababu za kibinafsi.
Kwa sababu Sikinde inatiwa hatiani kwamba imekwisha kimuziki, basi ipewe nafasi ya kusikilizwa kwa muziki wake kupigwa redioni vya kutosha kama zinavyopewa nafasi bendi nyingine. Si haki kuitia hatiani kwa kuisha kimuziki wakati sisi wasikilizaji wa pembeni tunaiona bado iko juu.
Kwa upande mwingine, uongozi wa bendi hiyo nao, pamoja na Sikinde Family ya akina Hamis Kinye, inabidi ujiulize kwa nini wao wanafanyiwa tofauti na bendi nyingine.
Kama wenzao wanatumia mbinu za ziada kuhakikisha muziki wao unapigwa hapa na hapa redioni, nao watumie mbinu hizo kama ni za halali kwa sababu kutangazwa kwa biashara ya muziki, zaidi hufanywa kwa nyimbo kusikika redioni na kuonekana kwenye televisheni.
Haiwasaidii chochote kukaa tu na kutarajia kubebwa na uzuri wa tungo zao zilizoshindwa kufanya hivyo licha ya uzuri wake.
Inasikitisha sana kwa maneno mazito ya kuenziana, ya kiutu uzima na yenye mantiki kubwa kama "msimsakamee yeye mke wangu, yeyee ndiye ubavu wangu wa pili, ooo huliaa chozi la huba" ya wimbo "Chozi la Huba" au maneno yaliyoimbwa kwa sauti isiyochuja ya Bitchuka: "Enyi ndugu zangu, jaribu kufikiria, ni nanii anayewadanganya... Nashangaa, mnavyonisakama, eti kwa nini sikumzuia eee. Yaonyesha mawazo yenu ni duuni, sitaki uhasamaa ni uamuzi wakee..." ya wimbo uliochangamka sana wa "Nani Amewadanganya" yawe yanasikika tu Old Trafford (Ukumbi wa DDC Kariakoo) Dar es Salaam wakati nyimbo hizo na nyingine za Sikinde ziko kwenye redio zote nchini zikitandwa na buibui au vumbi!
Naomba Sikinde ihukumiwe kwamba imekwisha baada ya watu Tanzania nzima kupewa nafasi ya kuzisikiliza nyimbo zao za sasa kwani wao ndiyo waamuzi kama bendi imekwisha au bado wamo.
Vinginevyo, bendi hiyo isitiwe hatiani kwamba imekwisha kimuziki bila kusikilizwa.
Wiki ijayo:- Licha ya Wasanii kujua kwamba Watanzania tumekuwa tukijivunia amani tunayoichezea sana sasa, wengi wao hawatimizi wajibu wa kuliweka sawa Taifa kuilinda amani hiyo.
<
Toa maoni yako