- Ulipigwa ukunga, wanakijiji wakajitokeza na mapanga
- Kisa hawataki kuondoka kwenye ardhioevu
- Kama si ulinzi wa polisi, damu ingemwagika
KATIKA miaka yangu takriban 30 ya uandishi wa habari, sikupata kufikiria kwamba kuna siku ningelazimika kutimua mbio eneo la tukio kuokoa maisha yangu, lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa Jumatano ya wiki iliyopita, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Nilikuwa naongoza msafara wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) uliojuimuisha waandishi kutoka Tanzania, Kenya na Uganda kutembelea maeneo ya Mlima Kilimanjaro kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea huko.
Chanzo cha ziara hiyo ni hatua ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama ya kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Ushauri la Mkoa huo (RCC), kujadili hali hiyo ya kutisha ya uharibifu wa mazingira katika vijiji vinavyouzunguka Mlima Kilimanjaro.
Ziara yetu ilianza vyema asubuhi ya Jumanne ya Machi 20, kwa kukutana na Kaimu Mkuu wa Mkoa, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Musa Samizi, aliyetupa maelezo ya jumla kuhusu uharibifu huo wa mazingira.
Baadaye ujumbe huo wa waandishi wa habari saba uliweza kutembelea Ofisi ya Maji ya Bonde la Mto Pangani (PBWO), kwa mazungumzo zaidi juu ya hali ya vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro kabla ya mchana kukutana na gwiji la masuala ya mabadiliko ya tabia nchi (climate change), Profesa Willy Makundi.
Siku iliyofuata, asubuhi, ratiba yetu ilituelekeza Kata ya Machame Mashariki, ambako ujumbe huo wa JET ulikutana na diwani (CCM) wa kata hiyo, Rajab Nkya, aliyetutembeza katika moja ya misitu inayouzunguka Mlima Kilimanjaro ambako tulijionea ushahidi wa kuwepo biashara ya magogo (ukataji miti) ndani ya msitu huo.
Mchana wa siku hiyo ya Jumatano ratiba yetu ilitupeleka kwenye tindiga (ardhioevu) la Boloti, lililoko karibu na Bomang’ombe, nje kidogo ya mji wa Moshi.
Ni katika tindiga hilo ambako tuliponea chupuchupu kukatwa mapanga na wananchi wa Kijiji cha Kyuu, wenye hasira wanaopinga kuzuiwa kulima na kufuga ndani ya tindiga hilo.
Wenyeji wetu katika ziara hii walikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Watumiaji Maji cha Sanya Kware, Frank Kimaro na Katibu wake, Goodchance Johanne Moshi. Hawa tuliungana nao katika mji mdogo wa Bomang’ombe tayari kwa kulitembelea tindiga hilo la Boloti.
Mshituko wa kwanza niliupata tukiwa hapo hapo Bomang’ombe wakati mwenyekiti wa umoja huo wa watumiaji maji aliponiita pembeni na kuniambia kwamba ni lazima tupite kwanza kituo cha polisi cha Bomang’ombe ili tupate polisi wa kuandamana na sisi.
Nilimwambia kwa kujiamini kabisa kwamba JET hatuna kawaida ya kuandamana na polisi wakati tunapotembelea vyanzo vya maji, lakini Mwenyekiti huyo, Frank Kimaro, akaniambia kwamba tunahitaji ulinzi wa polisi kwa sababu wanavijiji wanaoishi karibu na tindiga hilo ni wakorofi.
Nilikubali wazo la kuandamana na polisi kwa shingo upande. Na hata tulipofika kituo cha polisi cha Bomang’ombe kuomba polisi wa kuandamana nasi, na kujikuta tunasubiri muda mrefu bila kupewa polisi huyo, nusura nimwambie mwenyeji wetu kwamba twende tu bila kuwa na polisi. Hakika, lingekuwa kosa kubwa!
Baadaye, sote tuliduwaa tulipoona kuwa tumepewa si polisi mmoja; bali wawili, na tena kila mmoja akiwa amebeba SMG. Tuliuliza kulikoni na tukaambiwa kuwa ni kwa usalama wetu.
Baadhi yetu tuliupuuza ulinzi huo na tulidhani suala la ukorofi wa wanavijiji hao linatiwa chumvi tu na mwenyekiti huyo na katibu wake. Tukaondoka kuelekea tindiga la Boloti tukiwa hatuna hofu yoyote.
Tulipokaribia tindiga hilo tukaona mamia ya ngo’mbe wakila nyasi za kijani pembezoni kabisa mwa tindiga hilo. Gari letu likasimama na tukateremka kwa ajili ya kupiga picha za mifugo hiyo; huku vijana waliokuwa wakichunga ng’ombe hao wakisonya na kututolea macho kwa hasira.
Tulirejea katika gari na kwenda ndani kabisa ya tindiga hilo kujionea jinsi wanavijiji walivyopanda mahindi na magimbi ndani kabisa ya tindiga kinyume cha sheria, na huko ndiko masahibu haya ninayoyasimulia yalikotukuta.
Tuliacha gari kwa mbali kidogo na kuliendea eneo hilo la tindiga kwa miguu. Tulielekea chini kidogo ambako mazao hayo yamepandwa.
Tulipolifikia eneo hilo, tulisimama na kuwazunguka wenyeji wetu hao wawili wakati wanatupa maelezo kuhusu tindiga hilo. Wakati wote huo, polisi wale wawili walikuwa mbali kidogo na sisi wakielekeza macho yao maeneo ya juu vilipo vijiji hivyo.
Ghafla, alijitokeza mwanakijiji mmoja akiwa na ndoo ya maji ambaye alitusogelea kabisa tulipo akijaribu kusikiliza mazungumzo yetu. Polisi alipomwendea na kumwamuru aondoke pale, alimjibu kwa jeuri na kejeli; licha kwamba polisi yule alikuwa na SMG.
Kwa majibu yale ya kichokozi, ilikuwa ni dhahiri kwetu sote kwamba mwanakijiji yule hakuwa na nia ya kwenda kuchota maji; bali alitumwa kutukaribia ili asikilize kile tulichokuwa tunazungumza.
Dakika 15 baada ya kijana yule kuamriwa na polisi kuondoka, ghafla zikaja pikipiki nne zinazoendeshwa na vijana na zikasimama karibu na tulipo. Vijana wale walituangalia kwa mbali wakiwa bado kwenye pikipiki zao, na kisha wakaondoka kwa kasi na kwa mbwembwe!
Tulikuja kugundua baadaye kuwa vijana wale walitumwa kuchunguza polisi tuliokuwanao walibeba silaha nzito kiasi gani!
Mara baada ya vijana wale wa pikipiki kuondoka, kilichofuatia ni sauti za ukunga za uuuwiiiiiiii…..uuuwiiiiii…… uuuwiiiii zikitokea sehemu za juu wanakoishi wanavijiji. Niliwatazama wenzangu na nikaona wote wamepoteza hamu ya mazungumzo na wameshikwa na hofu.
Hofu hiyo iliongezeka pale polisi wetu wawili walipoanza kushikilia SMG zao katika hali ya utayari wa kufyatua risasi; huku wakitazama maeneo ya juu yalikokuwa yakitokea mayowe hayo.
Binafsi, hofu ilikuwa kubwa kwa sababu (nikiwa Mpare) nafahamu kuwa, kwa Wapare na Wachaga, ukipigwa ukunga wa uuuwiiiii; maana yake ni kilio cha hatari ya kutisha iliyo mbeleni, na kwamba kinapotolewa kilio hicho kila mtu hupaswa kuacha anachokifanya na kuchukua silaha yoyote – panga, nondo, upinde, bunduki kuelekea chanzo cha mayowe hayo ‘kumkabili adui’.
Na hivyo ndivyo pia ilivyokuwa Boliti; maana tulipotazama maeneo ya juu tuliona umati wa wanavijiji waliobeba mapanga, mikuki na mawe wakiteremka kilima kwa kasi kuelekea tulipo; huku wakiendelea kupiga ukunga huo wa uuuwiiiii….uuuwiiii…. uuuwiiii!
Polisi mmoja kati ya wale wawili aliitathmini hali hiyo haraka na kutuamuru kukimbilia garini na kuingia ndani haraka ili tuondoke eneo hilo kabla umati huo wa wanavijiji haujatufikia. Tulifanya hivyo kwa kasi kubwa, na hivyo tulifanikiwa kuondoka tindiga la Boloti kabla wanavijiji hao waliokuwa wakiendelea kuitana kwa kupiga ukunga, hawajatufikia.
Mmoja, ambaye ni mwanamke, tayari alishafikia eneo tulikosimama awali na aliendelea kulikimbilia gari letu kwa mita kadhaa huku akiendelea kupinga kwa nguvu ukunga wa uuuwiiii!
Tukiwa ndani ya gari tulitazamana tukitweta kwa jasho, na ilituchukua muda kidogo kuanza kusemeshana na kusimuliana jinsi tulivyoepuka chupuchupu kukatwa mapanga na wanavijiji wale wenye hasira.
Ilitutisha sote kwamba licha ya wanavijiji wale kufahamu wazi kwamba polisi wetu wawili walikuwa na SMG, hawakuziogopa; kwani waliendelea kutukimbilia wakiwa na mapanga huku wakipiga ukunga huo kwa nguvu. Ni dhahiri walikuwa wameamua lolote liwalo liwe!
Ni dhahiri vilevile kwamba kama wanavijiji wale wangetukaribia kabisa, polisi wetu wangelazimika kufyatua risasi, na hatujui kama risasi zingewazuia kutufikia na kutukata mapanga. Hakika, aliyesema vita ijayo itakuwa ya kugombea vyanzo vya maji hakukosea!
Akizungumzia tukio hilo, mwandishi wa siku nyingi wa masuala ya mazingira nchini, Deo Mfugale, alisema kuwa hiyo kwake ni mara ya kwanza kutokea. “Tukio hili lina sehemu mbili. Kwanza ni mara ya kwanza waandishi wa habari za mazingira nchini kufanya kazi zao wakiwa chini ya ulinzi wa polisi. Kwa nchi zenye vita, hiyo ni hali ya kawaida; lakini kwa Tanzania, tukio hili ni jipya”
“Ukiondoa tukio la Karamoja nchini Uganda, mwaka 2005, ambako tulipata msukosuko kidogo kutoka kwa wananchi, tukio hili la Boloti wilayani Hai, ni la kwanza kwangu kunikuta,” anasema Mfugale.
Sura ya pili ya tukio hilo ambayo Mfugale aliizungumzia ni ile hali ya waandishi wa habari za mazingiraTanzania kuzuiwa na wananchi kufanya kazi yao.
“Hili nalo ni mara ya kwanza kutokea hapa Tanzania. Tumeyashuhudia hayo kwenye siasa, lakini sasa tunayaona kwenye masuala ya mazingira. Waandishi wanahamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji kwa ajili ya manufaa ya wanavijiji wenyewe, lakini wanavijiji hao hao wanataka kuwaua waandishi hao. Huu, hakika, ni ukurasa mpya,” anasema Mfugale.
Je, alihofia kupoteza maisha wakati wa tukio hilo? Mfugale analijibu swali hilo hivi: “Hata baada ya uzoefu wa Karamoja kule Uganda, bado tukio hili la Boloti lilinitisha mno. Hofu ya kukatwa mapanga ilikuwa kubwa mno.”
Naye mwandishi kutoka Kenya, Nicholas Begisen, alisema hivi kuhusu tukio hilo la Boloti: “Nimewahi kuandamana na wanajeshi katika operesheni maalumu ya kuwaondoa waasi waliokimbilia Mlima Elgon kule Kenya, lakini sikuingiwa na hofu ya kufa kama iliyoniingia Boloti.”
“Mayowe yale yalinitisha sana, na nilipoona wanatujia mbio wakiwa na mapanga, nilijua kwamba huo ndio mwisho wetu. Japo sisi ni waandishi na hatupaswi kukimbia eneo la tukio, lakini ulikuwa ni uamuzi sahihi kwetu tulipokimbia Boloti. Maisha kwanza, habari baadaye”, alisema mwandishi huyo wa habari kutoka Kenya.
Na inapozungumzwa suala la waandishi wa habari kukimbia eneo la tukio kuokoa maisha yao, namkumnbuka Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, ambaye wakati wa ziara hiyo ndiye aliyekuwa mpigapicha wetu mkuu.
Ulipopigwa ukunga wa uuuwiiii…. uuuwiiiii.. uuuwiii; huku wanavijiji wenye mapanga wakitujia kwa kasi, Chikomo alikuwa mstari wa mbele kukimbilia Landcruiser yetu (Hardtop). Alisahau kabisa wajibu wake wa kuwapiga picha wanavijiji wale wenye mapanga, na hivyo kutufanya sote tukose picha za kihistoria za tukio hilo.
Nilipomuuliza baadaye ni kwa nini alisahau kupiga picha za tukio hilo na kuikimbia “story”, Chikomo alijibu hivi: “Nilikimbia kwa ajili ya kuokoa uhai wangu. Sikuweza kupiga picha. Walikuwa wanatujia kwa kasi kama vile wanakwenda vitani. Nasikitika nilishindwa kukamilisha kazi yangu ya kupata picha za tukio hilo, lakini ilibidi nikimbie.”
Naye Adam Mussa – mwandishi kutoka Uganda, alizungumzia hivi tukio hilo la Boloti; “Nilitishika na kuingiwa na hofu. Japo Waganda tumezoea mambo ya Joseph Kony, lakini hili la Boloti lilinitisha, na sikuamini kwamba kitu kama hicho kinaweza kutokea Tanzania.”
Tukio hilo lililotusibu waandishi wa JET liliripotiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, na habari tulizozipata wakati tukirejea Dar es salaam zilisema kwamba watu sita (wahamasishaji wakuu) tayari walishakamatwa na kufikishwa mahakamani ambako walinyimwa dhamana.
Nimelizungumzia kwa kirefu tukio hili la aina yake lililotusibu katika ardhioevu ya Boloti, wilayani Hai, kwani, kimsingi, ndio chanzo cha tatizo kubwa la uharibifu mkubwa wa mazingira mkoani Kilimanjaro. Namaanisha ukaidi na ukali wa wanavijiji wa Mkoa wa Kilimanjaro wanapoamriwa kuondoka kwenye vyanzo vya maji.
Kwa mfano; katika suala hilo la tindiga la Boloti, sisi si watu wa kwanza kutimuliwa eneo hilo na wanavijiji. Kwa mujibu wa simulizi ya Mwenyekiti wa Chama cha Watumiaji Maji cha Sanya Kware, Frank Kimaro, walipata kutimuliwa eneo hilo kwa mawe.
Na si hivyo tu; kwani pia waliponea chupuchupu kumwagiwa unga wa pilipili wakati walipoitisha mkutano eneo hilo ili kuwaelemisha wanavijiji umuhimu wa kulitunza tindiga hilo ambalo wote wanalitegemea kwa maji ya kunywa.
Tindiga hilo lililokuwa na ukubwa wa kilomita sita za mraba sasa limesinyaa kabisa na kubaki eneo dogo tu kutokana na kuharibiwa vibaya na mamia ya ng’ombe yanaoingizwa humo kwa malisho, na pia shughuli za kilimo ndani ya tindiga.
Ni dhahiri muda si mrefu tindiga hilo ambalo ni tegemeo kuu la maji la vijiji vitatu vya Kyuu, Kware na Mungushi wilayani Hai, litakauka kabisa na wanavijiji wale hawatakuwa na sehemu nyingine ya kuchotea maji kwa matumizi yao ya nyumbani.
Lakini wapo wanavijiji ambao bado hawajakata tamaa na ambao wako tayari kupoteza maisha yao katika harakati ya kuliokoa tindiga la Boloti. Frank Kimaro ni mmojawao.
“Najua mimi ndiye ninayetafutwa kuuawa kuliko wengine wote. Mimi ndiye adui yao nambari moja. Wamenitisha kuniua na wanaendelea kunitisha, lakini sitarudi nyuma. Nimepania kuliokoa tindiga la Boloti hata kama kwa kufanya hivyo nitapoteza uhai wangu,” alisema mwanamazingira huyo ambaye ni baba wa watoto watatu.
Kimaro, ambaye tayari, mara mbili, ameshafungua RB kwenye kituo cha polisi cha Bomang’ombe, alisema kwamba wameanza kusakamwa tangu Novemba 2010, na kwamba ingawa mpaka sasa wameitisha mikutano sita ya kuwaelemisha wanavijiji juu ya umuhimu wa kulitunza tindiga hilo, bado wanavijiji wameiweka mioyo yao migumu kiasi hata cha kutisha kuua.
“Katika mkutano wa mwisho tulikubaliana kuwa tarehe ya mwisho ya kuendesha shughuli ndani ya tindiga ni Januari mosi, 2012. Tuliwapa muda wa kutosha ili kuvuna mazao yao waliyopanda.
“Lakini ilipofika tarehe hiyo bado shughuli zilikuwa zinaendelea ndani ya tindiga, na ilisikitisha kuwa miongoni mwa waliokamatwa wakilima ndani ya tindiga ni mwenyekiti wa kijiji na diwani wa zamani.”
Frank anamshutumu diwani huyo wa zamani wa CCM, ambaye tayari ana kesi ya kulima ndani ya tindiga hilo, kuwa ndiye mhamasishaji mkuu wa wanavijiji kuwashambulia watu wanaokwenda katika tindiga hilo wakiwa katika harakati zinazolenga kuwaondoa eneo hilo.
Simulizi za ukali wa wanavijiji kiasi cha kutishia kuua pale wanapoambiwa kuondoka katika vyanzo vya maji pia tulizipata wakati tulipotembelea Bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga.
Kuna simulizi katika maeneo ya Bwawa la Nyumba ya Mungu ya ofisa uvuvi aliyevunjwa mkono na wavuvi kutokana na ‘kimbelembele chake’ cha kuwakamata wanavijiji wanaolima pembezoni kabisa mwa bwawa hilo na wanaovua kwa kutumia nyavu ndogo au vyandarua. Bwawa hilo nalo linasinyaa kwa kasi na ukubwa wake unazidi kupungua mwaka hadi mwaka.
Kuna pia simulizi huko huko Nyumba ya Mungu ya katibu mtendaji mmoja ambaye ni mwanamke aliyenusurika kubakwa na wavuvi hao kwa kuokolewa na wafugaji wa kimasai. Baada ya kupona chupuchupu kubakwa, mama huyo aliyeendesha mapambano ya kulilinda bwawa hilo alisalimu amri na kuomba uhamisho.
Kwa ufupi, mapambano ya kuokoa mazingira ya Mkoa wa Kimanjaro ni magumu, na yanawahitaji akina Frank Kimaro wengi ambao wako tayari kufa kuyaokoa mazingira ya mkoa huo, na pia yanawahitaji viongozi wa sampuli ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama ambaye ameamua kupambana kuuokoa mkoa huo usiteketezwe na waharibifu wa mazingira.
Tayari Leonidas Gama ameanza kunyooshewa kidole na baadhi ya wananchi wa mkoa huo wakiwemo viongozi wenzake kwamba ni ‘mkora’, na kwamba watahakikisha anahamishwa haraka kama walivyohamishwa haraka baadhi ya ma-RC waliopelekwa Kilimanjaro na wakaamua kulipigia debe suala hilo la utunzaji mazingira.
Kwa wengi wao, vita hiyo ya utunzaji mazingira inamaanisha mwisho wa biashara yao haramu ya magogo na mwisho wa kulima na kufuga ng’ombe kwenye vyanzo vya maji. Na yaelekea hawako tayari kuacha kujishughulisha na uovu huo. Hakika, muda unayoyoma kwa Mkoa wa Kilimanjaro!
Toleo lijalo: Moshi yaonja mgao wake wa kwanza wa maji baada ya miaka 20, kulikoni?
Maoni ya Wasomaji
Tatizo ni ukosefu wa uchumi
Tatizo ni ukosefu wa uchumi mbadala kwa wenyeji. Badala ya kuwashawishi kuacha uchumi tegemezi waliouzoea, waelimishwe na kupewa mitaji waanzishe biashara mbadala.