Simba na Basena: Sheria inapogeuka punda kihongwe!

WAINGEREZA wana msemo: the law is an ass, wanaoutumia hasa pale sheria moja inapoweza kutumiwa kuamua masuala mawili tofauti kabisa kwa kutegemea tu uwezo wa hakimu ama wakili wa kunyumbulisha sheria husika na pengine kuzungusha maneno.

Kwa tafsiri njema ya Kiswahili tunaweza kuutafsiri msemo huo kama 'sheria ni punda kihongwe' pengine Waingereza wakijaribu kuoanisha sheria na punda ambaye hubeba mzigo wowote na kwenda popote unakotaka wewe aende.

Mzozo unaoendelea (japo kwa siku mbili tatu hizi umetulia kidogo) kati ya Klabu ya Soka ya Simba na kocha wake wa zamani, Mganda, Moses Basena, ni mfano mzuri wa jinsi sheria inavyoweza kuwa punda kihongwe ama makalio hata kama mzozo huo haujafika kwenye vyombo vya sheria.

Mzozo huo ulipoanza kuibuka klabu ya Simba ilidai kwamba ilikuwa haijamtimua kocha huyo bali ilikuwa inamtaka akafundishe timu ya pili ya Simba.

Kwa kuwa hatufahamu iwapo mkataba wa Simba na kocha huyo ulitamka vipi wazi kwamba anaweza kutakiwa na klabu hiyo kufundisha timu yoyote ya Simba hata ya maveterani ama ya wanawake, hatuwezi kuchangia sana katika hili.

Yatosha tu kusema kwamba baadaye Simba waligeuza kauli na kudai kwamba walikuwa wameamua kuvunja mkataba wake na kocha huyo kwa sababu alikuwa ameshindwa kuwasilisha kwao vyeti halisi vya taaluma yake.

Kocha Basena alipeleka malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, maadili na hadhi za wachezaji ya TFF, akitaka Shirikisho hilo kumsaidia kupata fedha anazostahili kutokana na Simba kuvunja mkataba baina yao.

TFF inasema; "TFF ilikataa maombi ya Simba kulitaka Shirikisho hilo kuiandikia barua idara ya Uhamiaji kuthibitisha barua ya kumuombea kibali cha kufanya kazi kocha Moses Basena baada ya kocha huyo kushindwa kuwasilisha vyeti vyake vya taaluma ndiyo maana tuliazimia kuwa angekuwepo mpaka sasa asingeongoza timu hiyo kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu".

Swali linalosumbua hapa ni je, TFF walisubiri hadi mgogoro huu utokee na Basena aombe msaada kwao ndipo watuambie kuwa walikuwa wanasubiri hadi mzunguko wa pili uanze ndipo wafanye vitu vyao vya kumsimamisha Basena?

Wakati Simba wakiendelea kushikilia msimamo wao kwamba kutokana na Basena kushindwa kuwakilisha vyeti vyake vya taaluma kwao basi mkataba waliowekeana unakuwa batili, kocha huyo ameendelea kusisitiza kuwa mkataba alioingia na Simba ni halali na Simba wanapaswa kumpa chake.

Dhana ya sheria kuonekana punda kihongwe ama eneo la binadamu kwa ajili ya kuchapwa viboko tu inaanzia hapa. Iwapo Simba waliingia mkataba na Basena bila kwanza kuona na kuhakiki vyeti vyake basi wanapaswa kuacha longolongo na kumpa Basena haki yake kwa kuvunja mkataba labda tu kama katika mkataba huo waliweka kifungu kinachotamka wazi kwamba mkataba wao utakuwa halali tu pale Basena atakapowasilisha vyeti vyake Simba na wakaviafiki.

Iwapo Simba walipitiwa ama kuendekeza ule ubabaishaji wetu wa siku zote na kushindwa kuweka wazi kifungu kama hicho kinachombana Basena kutakiwa kuwasilisha vyeti vyake vya kitaaluma kwao, basi imekula kwao.

Sana sana Simba wanapaswa kushikana mashati na kutafuta kiongozi mchawi aliyewaingiza mkenge kama huo wa kuingia mkataba na kocha bila hata kuhakiki vyeti vyake.

Lakini pia 'upunda kihongwe' wa sheria unakuja pale ambapo Simba wanaweza wakadai, na kushinda, kuwa waliingia mkataba na Basena kwa kuamini sifa ambazo kocha huyo alidai kuwa nazo na kwa maana hiyo pale inapothibitika kuwa sifa hizo hakuwa nazo basi mkataba huo unakufa 'automatiki'!

Kwa upande wao, TFF, limezidi kunogesha dhana hii ya sheria kuwa punda kihongwe pale wanapokiri kuwa Simba wana mkataba wa miaka miwili na Basena lakini mkataba huo hauwezi kufanya kazi kwa vile kocha huyo hakuwa na kibali cha kufanya kazi nchini, hatua inayoua nguvu ya mkataba huo.

Tunalazimika kujiuliza, kama mkataba wa Basena na Simba hauwezi kufanya kazi kwa kuwa kocha huyo hakuwa na kibali cha kufanya kazi nchini ambako kulitokana na kushindwa kwake kuwasilisha vyeti vake vya taaluma, kwa nini TFF tena wajisumbue hata kutamka tu kuwa Basena ana mkataba wa miaka miwili na Simba?

Tunalazimika pia kujiuliza; kati ya mkataba na kibali cha kufanya kazi nchini kinachotakiwa kutangulia ni nini? Kama ni kibali cha kazi, kwa nini Simba waliingia mkataba wa miaka miwili na Basena, unaofahamika na TFF, wakati hakuwa na kibali cha kazi?

Na kama ni mkataba ndio unaotangulia kama walivyofanya Simba, kwa nini linapokuja suala la kumpa Basena chake wadai kuwa ni mkataba wao na yeye ni batili kwa sababu hakuwa na kibali cha kazi wakati wanauandika kwa sababu hakuwakilisha vyeti vyake kazi kama ilivyotakiwa?

Naam, yale yale ya maji yazime moto, moto uichome fimbo na fimbo nayo imcharaze Kalumekenge ili aende shule!

The law is an ass na ndiyo maana mshiriki mmoja wa mkataba anavunja mkataba na kushinda kesi na kulipwa mamilioni licha ya kutokuwa na sifa alizodai kuwa nazo wakati akiingia mkataba na mshirika mwenzake katika nchi ile ile ambayo mshirika mwingine wa mkataba mwingine anaelekea kulaliwa haki zake kwa hoja hiyo hiyo ya kushukiwa kutokuwa na sifa alizodai kuwa nazo ni ushahidi kamili wa jinsi sheria inavyoweza kugeuzwa ni eneo la makalio la binadamu ambalo faida yake kuu ni kupokea viboko tu!

Kwa hakika, hatupaswi hata kuilaumu TFF pale wanapoamua kugeuka Liwali Pontio Pilato kwa kuitisha bakuli la maji na kunawa mikono kama ishara ya kujivua na kuwaachia wahusika, Simba na Basena, wayaangalie haya wao wenyewe! Hakika the Law is an ass.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.