Siri imefichuka, tumegawanyika!

MCHAKATO wa kuelekea kuandika Katiba mpya ya taifa letu umefichua siri kubwa ya Watanzania: Tumegawanyika! Hatuiangalii Katiba mpya kwa jicho moja la utaifa, bali tunaiangalia kisiasa, kidini na kijamii. Vyama vya siasa vinataka kuhakikisha Katiba inalinda maslahi, sera, malengo na matumaini ya vyama vyao; tumeshuhudia hivi karibuni vyama vya siasa vikipigana vikumbo Ikulu kuwasilisha maoni juu ya mchakato wa Katiba mpya kana kwamba Tanzania haina Bunge na vyombo vingine vya uwakilishi.

Viongozi wa dini nao hawako nyuma, Waislamu wanataka Katiba mpya izungumze wazi juu ya Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) na Mahakama ya Kadhi na mambo mengine muhimu zaidi kwa waumini wa dini hiyo. Wakristu nao wanataka Katiba mpya ‘inahakikisha’ hakuna ndoa za mashoga na kwamba suala la Mahakama ya Kadhi lisiingizwe kwenye Katiba hiyo; wanapenda kuona Katiba mpya inabeba maadili ya dini yao.

Makundi yanayopigania haki za binadamu na usawa wa jinsia wanataka Katiba mpya kuzingatia haki za makundi mbalimbali. Mchakato wa kuitafuta Katiba mpya umeifichua siri hii kubwa ya ufa mkubwa katika umoja wa taifa letu.

Kama miaka 15 iliyopita niliandika sana juu ya hekalu. Kwamba Watanzania tunahitaji hekalu. Kwamba tunahitaji kitu cha kutuunganisha kama taifa. Kwamba tunahitaji kitu ambacho kila Mtanzania atalazimika kupiga magoti na kunyenyekea kwa uaminifu na kutoa moyo wake, akili zake, nguvu zake na kila kitu chake kwa heshima na utukufu wa hekalu letu. Kwamba hekalu hili lisiwe na dini, madhehebu wala makabila. Hekalu la Watanzania wote. Wakati nikiandika haya, kuna watu walifikiri nimechanganyikiwa, kuna watu walifikiri nataka watu wote wawe Wakristu.

Wakati ule baadhi ya watu walikuwa na upofu wa kutoona mbali, maana tulikuwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kwa kipaji chake, hekima na busara, aliweza kuzima kwa nguvu zote zinazoashiria dalili mbaya za kuligawa taifa letu. Daima alikuwa mkali kama pilipili, pale mtu, watu au kikundi cha watu kilipoonyesha dalili yoyote ya kutaka kuleta mgawanyiko.

Tunakumbuka kundi maalumu la wabunge, marufu kwa jina la G-55, tunakumbuka matukio yaliyomlazimisha Mwalimu kuandika kitabu  juu ya hatima ya taifa letu, tunakumbuka jinsi Mwalimu alivyokemea kwa nguvu zote Uzanzibari na Uzanzibara, tunakumbuka jinsi Mwalimu alivyotaifisha shule za kidini ili watoto wote wa Tanzania, wapate elimu bila ya ubaguzi.

Kwa vile Mwalimu, aliyazima, watu walifikiri tunaweza kuendelea hivyo milele. Mbaya zaidi ni kwamba “upofu” huu unaendelea hadi leo hii.

Hoja yangu kubwa wakati nikisisitiza umuhimu wa hekalu ilikuwa kwamba hatuwezi kuendelea bila kuwa na kitu  cha kutuunganisha. Kwamba, hatuwezi kuendelea bila ya kuwa na kitu cha kujenga uzalendo wetu na kuchochea mshikamano miongoni mwetu. Ingawa Mwalimu, aliweza kutuunganisha, tulihitaji kitu fulani cha kudumisha mshikamano wetu hata baada ya kifo chake; kitu  cha kuweza kutukumbusha daima kwamba ni lazima kutanguliza Utanzania wetu zaidi ya kitu kingine kile.

Mbali na Muungano wetu kuyumba baada ya kifo cha Mwalimu, matukio mengine ya kidini kama vile OIC na Mahakama ya Kadhi, yanayochomoza kwa nguvu zote wakati huu wa mchakato wa Katiba mpya, yameonyesha kwamba mshikamano wetu kama taifa umejengwa mchangani. Msingi si imara!

Wakati mjadala wa Mahakama ya Kadhi ukijadiliwa bungeni, jambo hili la mgawanyiko lilijionyesha wazi. Wabunge Wakristu, walitupitilia mbali tofauti zao za vyama vya siasa na kushikamana kupinga hoja ya Mahakama ya Kadhi.

Wabunge Waislamu nao walitupilia mbali tofauti zao za vyama vya siasa na kushikamana kutetea hoja ya Mahakama ya Kadhi. Hakuna mbunge, mbali ya Zitto Kabwe, aliyeonyesha kuwa na msimamo wa kati kimjadala, na kujadili hoja hizo “Kitanzania”.

Kinachoshangaza na kusikitisha ni kwamba hoja hizi zinajadiliwa kwa misingi ya kidini. Hazijadiliwi kwa misingi ya “utaifa” kwa misingi ya “Utanzania”. Tunajigawa kwenye makundi mawili ya Waislamu na Wakristu na kuwaacha nje Watanzania ambao wanamwabudu Mungu kwa dini zao za jadi. Ingawa, mara nyingi kuna kiburi cha “udini” kwa maana ya dini hizi za kigeni, kuna Watanzania waliobaki na dini zao za jadi. Hawa nao ni Watanzania, ni lazima wawe na haki zote za kikatiba kama Watanzania wengine. Kuwatupa nje ya mjadala huu, ambao baadaye utamgusa kila Mtanzania, ni makosa makubwa!

Wakristu wanashindwa kuelewa ni kwa nini Mahakama ya Kadhi, iendeshwe kwa fedha za Serikali, fedha za walipa kodi ambao ni Waislamu, Wakristu na wale wanaoamini kwa dini za jadi. Waislamu nao wanashikilia hoja ya kwamba hospitali teule kwenye wilaya mbalimbali ni za Wakristu na zinaendeshwa kwa fedha za Serikali. Zinaendeshwa kwa fedha ya walipa kodi ambao ni Waislamu ,Wakristu na wale wanaoabudu kwa dini za jadi.

Tunaweza kujiuliza: Je, hospitali hizi teule zinawatibu Wakristu peke yao? Je, hospitali hizi  teule zinaajiri Wakristu peke yao? Kwa nini tusiangalie huduma zinazotolewa kwa Watanzania wote? Je, mtu anapokwenda kutibiwa anaulizwa dini yake?

Kuna malalamiko kutoka kwa Waislamu kwamba Serikali imejaa Wakristu. Na kuna malalamiko mengine kwamba Rais Jakaya Kikwete, amewajaza Waislamu serikalini. Nina shaka kama hili ni kweli. Lakini hata hivyo, kwa nini tuangalie dini ya mtu badala ya kuangalia utendaji wake. Je, Wakristu na Waislamu hao waliojazwa serikalini wana sifa? Je, wanafanya kazi kwa moyo wa kizalendo? Je, wanatoa huduma kwa kuangalia kwanza dini ya mtu?

Kuna malalamiko kwamba vyuo vikuu vinachukua namba kubwa ya Wakristu. Hili kweli? Na kama ni kweli, je, Wakristu hawa wana sifa au wanaingizwa bila sifa? Na kama wana sifa, kwa nini tusiwaangalie kama Watanzania badala ya kuwaangalia kama Wakristu. Na wasomi hawa wanapohitimu je, wakifanya kazi, wanatoa huduma kwa Wakristu peke yao au wanatoa huduma kwa Watanzania wote?

Kuna hatari ya kufikiri kwamba Mwislamu wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na nchi nyingine, ni muhimu zaidi kwa Mwislamu wa Tanzania, kwa sababu ya dini – kuzidi Mkristu wa Tanzania. Vile vile kwa upande mwingine Mkristu wa Tanzania, atakuwa na undugu wa karibu na Mkristu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na nchi nyingine, kwa sababu ya dini – kuliko Mwislamu wa Tanzania. Maana tunapotanguliza dini, hakuna mipaka; kama ni kutanguliza dini, yeyote mwenye imani kama yako, ni muhimu kuliko jirani yako mwenye dini tofauti na ya kwako. Hatari hii ni sawa na kifo kwa utaifa wetu.

Ni kipi kinatufanya kuwa Watanzania? Ni dini zetu za kigeni tulizozipokea zaidi ya miaka 100 iliyopita, au ni  “uzawa” wetu unaokwenda nyuma maelfu ya miaka? Ni kipi kinachotangulia? Ni dini zetu za kigeni au ni utaifa wetu? Tukijibu maswali haya, hatuwezi tena kuwa na dukuduku na masuala ya kidini kama vile OIC na Mahakama ya Kadhi.

Kwenye maandishi yangu ya nyuma, nilishadokeza kwamba dini hizi za kigeni ziliingia na kupokewa ‘kiushabiki’. Nikimaanisha theolojia ya dini hizi haikufundishwa kwa waumini. Viongozi wa dini hizi waliifanya theolojia, kuwa ni siri. Masuala mazito ya dini yanabaki kuwa wazi kwa viongozi na kuwaacha waumini walei katika giza nene. Matokeo yake zinapoibuka hoja nzito za kidini kama hizi za OIC, Mahakama ya Kadhi, Ubalozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania – na mambo mengine magumu kama Utatu mtakatifu, Ubikira wa Maria Mama wa Yesu, Roho Mtakatifu na Maisha ya useja, mijadala inatawaliwa na ushabiki kama ule wa kwenye viwanja vya mpira. Hakuna hoja za kitheolojia zinazotolewa na waumini walei.

Mfano, Wakristu wote wanaikataa OIC na Mahakama ya Kadhi, lakini hakuna anayeweza kutoa sababu za kitheolojia kutetea msimamo huo. Wanakataa kwa kufikiri kwamba tukiikubali OIC, sote tutalazimishwa kuwa Waislamu. Wanakataa Mahakama ya Kadhi, kwa kufikiri kwamba italeta sharia kama ile ya Somalia na Nigeria.

Hoja ninayoijenga ni kwamba, ni lazima tuwe na kitu cha kutuuganisha kama taifa. Tusitangulize dini zetu, bali tutangulize utaifa wetu. Mtanzania Mwislamu, akiwa serikalini au akiwa anafanya kazi yoyote ya kitaifa, tuamini kwamba anaifanya kazi hiyo kama Mtanzania na wala si kama Mwislamu. Mkristu Mtanzania, akifanya kazi au akiongoza Serikali tuamini kwamba anafanya kazi hiyo kama Mtanzania na wala si kama Mkristu.

Tukiendekeza udini tunaweza kufikia hatua ya kuligawanya taifa vipande viwili, kama zilivyofanya nchi nyingine za kiafrika. Tunahitaji hekima na busara za viongozi wetu wa dini (dini zote hata na zile za jadi) na viongozi wetu wa Serikali.

Tukishapata kitu cha kutuunganisha kama taifa, ni lazima tuwe na vipaumbele vya taifa. Kila Mtanzania hata na mwendawazimu afahamu kwamba kitu fulani ni kipaumbele cha taifa. Hadi sasa inatia shaka kama kweli kuna vipaumbele vya taifa. Ukiangalia jinsi tunavyoshughulikia kilimo chetu, huwezi kusema kwamba hiki ni kipaumbele cha taifa. Bado tunatumia jembe la mkono na kumsubiri Mwenyezi Mungu, atuletee mvua. Hatupanui mashamba yetu, kule Kagera, mibuni na migomba iliyopandwa na Babu zetu ndiyo hiyo hiyo hadi leo hii. Ukiangalia afya, miundombinu, nishati, elimu na mengine, huwezi kusema kitu fulani ni kipaumbele cha taifa.

Nchi ya Cuba iliweka elimu, kilimo, afya na nishati kama vipaumbele vya taifa. Leo hii Cuba inabadilishana madaktari kwa mafuta. Inatoa madaktari, inapata mafuta. Sukari, inayozalishwa Cuba inaweza kuendesha bajeti ya Serikali. Leo hii Cuba wana uwezo wa kuwa na daktari kila kijiji, wamesambaza umeme na maji karibu asilimia 90 ya nchi nzima.

Nimetoa mfano wa Cuba, lakini kuna nchi kama India, ambazo zimefanya elimu kuwa kipaumbele cha kwanza – na zimewekeza kwenye elimu, kiasi kwamba sasa India, iko mstari wa mbele kwa mambo ya teknolojia.

Juzi, pale eneo la Tabata relini Dar es Saalm, nilishuhudia kwa macho watoto wanne wa shule wakisukumwa kwenye daladala na kuanguka na kuumia vibaya. Tatizo hili la kuwasukuma watoto wa shule kwenye daladala ni la miaka mingi. Limezungumzwa, limejadiliwa bungeni, limetangazwa na kuandikwa kwenye vyombo vya habari. Hakuna kinachofanyika. Watoto wanasukumwa, wanaumizwa, wanakufa, wanaachwa kwenye vituo vya daladala. Kwa vile Serikali yetu ni masikini, ndiyo maana tatizo hili halishughulikiwi au ni kwa vile elimu na watoto wetu si kati ya vipaumbele vya taifa letu?

Mikopo ya elimu ya juu imekuwa ni tatizo. Lakini kama elimu, ingekuwa ni kipaumbele cha taifa tungekubali kuchangia mikopo hii kwa kuongeza senti hamsini kwenye soda, bia, sigara na mafuta. Kila mkulima angekubali kukatwa senti hamsini kwa kila kilo ya zao analouza.

Wafugaji nao wangekubali kukatwa senti hamsini kwa kila mfugo wanaouza. Na hili lisingefanyika kila mara, maana mikopo ya elimu inazunguka – wanaomaliza wanalipa. Kwa njia hii tungeweza kuwapatia wanafunzi wote mkopo wa elimu kwa asilimia 100.

Wimbo kwamba Serikali haina fedha, hauna kikomo. Hakuna siku itakayotokea Srikali ikawa na fedha. Kazi ya kufanya kama kuna vipaumbele ni Serikali kubuni vyanzo vya mapato. Serikali yenye uwezo wa kuwashawishi watu wake kwamba ni masikini, ikibuni vyanzo vya mapato ni lazima wananchi waikubalie.

Tatizo la Tanzania, pamoja na ukweli kwamba vipaumbele vyetu haviko wazi ni kwamba Serikali yetu imeshindwa kuwashawishi wananchi wake kwamba ni masikini. Kama watu wawili wanaweza kuisababishia Serikali hasara ya bilioni 11 na wengine wakajichotea zaidi ya Sh. bilioni 123 Benki Kuu, na wengine kwa ujanja wakawa wanalipwa zaidi ya Sh. milioni 152 kwa siku, ni kiasi gani Serikali hii ni masikini?

Ingawa haikuandikwa popote, kwa kuangalia tu, mtu unaweza kusema kwamba kipaumbele namba moja katika taifa letu ni kuboresha maisha ya viongozi. Kuhakikisha wana usafiri mzuri, wana majumba mazuri, wana ulinzi wa kutosha, familia zao zinatunzwa vizuri, wanasafiri daraja la kwanza kwenye ndege na kutibiwa nchi za nje kila wanapokuwa na matatizo kiafya.

Umakini, fedha, juhudi zinazotumika kuhakikisha viongozi wetu wanaishi maisha mazuri – vingeelekezwa kwenye elimu, kilimo na nishati – taifa letu lingepiga hatua kubwa ya maendeleo. Kuna haja ya kutafuta kitu cha kutuunganisha kama taifa, na kuna kazi ya ziada ya kukaa chini na kupanga vipaumbele vya taifa. Mchakato wa kuandika Katiba mpya utuelekeze huko; kujenga  taifa moja lenye mshikamano na si kuendelea kutugawanya kwenye makundi ya kisiasa, kidini na kijamii.

Comments

No comment Father Priva..Ila umenivunja mbavu kweli na haya makala yako ya wiki hii na hasa  sana  'paragraph' ya pili kutoka mwisho!!!!!!!!!

da bravo,lakini hawa viongozi wanasoma hizi makala kweli au wanakesha wakihangaika kupitia bronchua za mahoteli ya ughaibuni na ndio maana kila siku wako hewani utadhani ni mbayuwayu

Nchi yetu sasa ni gulio kila mtu anatangaza bidhaa zake na anataka auze wengine na apate kuliko wengine wanunuzi wanataka vinavyouzwa vidode ( maana yake watu wanaangalia maslahi binafsi, wabunge wanataka posho bila kuangalia kama maisha yamekuwa aghali kwa watumishi wote wa umma. hao ndo wanaoponda wa kuongezwa kima cha chini ndo wanaosema maisha kwa wabunge ni magumu- uhuni tu 

Father Karugendo, hongera sana kwa makala nzuri yenye kutanabaisha mambo mengi ya msingi kuhusu mustakabali wa "Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa Moyo wote!"
Upendo huu wa moyo wote unajengeka kwenye nguzo moja kuu - Utaifa (ukijumuisha uzalendo ndani yake).  Nadhani hili ndio lina mapungufu.  Yoote mengine, Udini, ukabila, hali ya kipato (wenye/wasio nacho), yanazungukia kwenye hili.  Na ndio katika hili nakubaliana nawe asilimia MIA MOJA na haja ya kujenga "HEKALU"
KATIBA ambayo umeipa taswira ya HEKALU, au pengine ingependeza ukaaita "MAZABAHU" (mimbari), katika zama hizi za upeo na uelewa wa kila mtu kwa namna na itikadi yake (hakuna stereo type ya uelewa kwa kufuata kanuni; Elimu Guni?), inabaki na option moja tu: SIO TU KUWA YENYE KUWEKA USAWA KWA KILA RAIA WA TANZANIA, LAKINI ZAIDI KUUTENGENEZA USAWA HUO KWA MAKUSUDI. BASI!!
Ninachojaribu kuongeza katika hoja yako, ni kuwa na katiba ambayo inavuka mipaka ya fikra za kidni, kikabila, kijimbo n.k. na kuangalia jinsi yoyote ya kuinua ama kundi, jamii au hata familia/mtu mmoja mmoja ili asogee kwenye fursa asizo nazo, ambazo zimesababishwa na historia au legacy nyingine yoyote. KATIBA IWE NA VIPENGELE VYA KULETA KWA MAKUSUDI "AFFIRMATIVE ACTION" ambayo itapelekea kusogeza walio chini ya fursa kuzisogelea.
Hili limefanyika kwenye nchi nyingi, na hata nchini mwetu liliwahi kutokea, mfano kusogeza fursa za wanawake.  Ili hili liweze kufanikiwa, lazima tupitukie silka za mwamba ngoma kuvutia kwake.  Basi katiba iweke wazi sana kwamba sio kosa kulivuta kundi lilokosa fursa ili japo lisogee kwenye fursa za kitaifa zilizopo (basic opportunities).  Hili litaleta mambo mawili makuu: KWANZA - imani kwa kila mtu, hususan kundi kubwa (majority) ambalo liko chini ya mstari wa fursa (below poverty line).  Mara ukifanikiwa kuleta hali hii, basi bila shaka yoyote utapata utaifa wa hali ya juu kabisa.  Mwl. Nyerere alipoweka utaratibu wa kila mtu apate elimu mpaka hatua yoyote ilmradi anao uwezo kiakili kufanya hivyo, utaifa wetu ulikuwa kweli kweli, na kila mtu aliona kwamba kusonga mbele ni juhudi zako mwenyewe.  leo hali hiyo imetoweka, na fursa zipo kwa makundi fulani tu, na bahati mbaya zipo hata hisia ni kwa ajili ya dini fulani.  Unategemea nini katika hali hiyo?  MGAWANYIKO HAUEPUKIKI!
PILI - ni mantiki ya MAENDELEO YA UCHUMI: Katiba ikizingatia kusogeza makundi yote ya jamii kwenye fursa, itakuwa inakidhi hoja na ukweli kwamba, hakuna nchi inayoweza kuendelea na kusonga mbele kwa matambo makubwa - huku sehemu kubwa ya jamii ya nchi hiyo imo kwenye ULOFA.  HAIWEZEKANI.  Labda Bwana Mapesa Cheyo alikuwa namaanisha hili alipokuja na Sera ya Kujaza Pesa mifukoni mwa watu/wananchi.  Kanuni nyepesi ya Uchumi (Economics) ni kwamba huwezi kuwa na SOKO la wamaskini.  Uchumi imara ni ule wenye jumuia yenye uwezo wa kununua.  Kwa maaana hiyo, moja ya nguzo muhimu za "HEKALU" letu ni kuwapa watawala jukumu mahsusi la kubadilisha hali ya uchumi na kipato cha wananchi.  Kipimo kiwe ni kiwango cha KUWATOA KWENYE UMASKINI WATANZANIA KWA NGUVU ZOTE, NA KUELEKEZA RASLIMALI ZA NCHI KWENYE KUTEKELEZA KIPAUMBELE HICHO.
Ukiweka jukumu hilo kwenye KATIBA, hawezi kutokea mwendawazimu akasema inunuliwe "yatch" ya kumpatia upepo wa bahari mkubwa au watawala, kabla hujahakikisha zipo njia za kukuza ajira na hivyo vipato vya wananchi.  Au dege la fahari.
TUFIKE MAHALA TUKUBALI KUWA NA ROLL CALL, SIO YA WENYE NACHO ILI TUWANYANGANYE - BALI KINYUME CHAKE - TUWE NA ILE YA WASIONACHO, IKIBIDI KWA MAJINA - NA TUJIPE JUKUMU LA KUWATOA WALIPO KWA MUDA MAALUM, AMBAO PIA NDIO UWE UKOMO WA AWAMU ZA UONGOZI.  HUJAWEZA JUKUMU HILO ONDOKA!!!

acha unafki priva unasema ni sawa kwa hospitali za kikristu kupata msaada kutoka serikalini eti kwakuwa tu muislam akija kuhudumiwa haulizwi  dini yake au ajira haijali dini ya mtu? usawa uko wapi hapa wakati mmoja anamiliki asset na mwingine anapata huduma itolewayo na asset husika,ukitaka usawa kwa maana ya usawa useme kuwa kama serikali inatoa msaada kwa hospitali ya kikristu na muisalam anakwenda kupata huduma bila kuulizwa jina lake basi na kuwepo hospitali ya kiisalam ambayo mkristu atakwenda kuhudumiwa bila kuulizwa dini yake,huu ndio usawa wa kweli lakn sio mmoja kumiliki full assset yaani jengo na vilivyomo na mwingine akapata huduma tu then ukasema tatizo liko wapi ,what if ikiamuliwa kuwa hospitali hii inauzwa au kubinafsishwa muislam atagawiwa nini hapo? usawa kwenye asset yoyote ni kumilikiwa ile asset na wahusika kwa usawa,kwahiyo kwa mtqzamo wangu mm ni sawa kwa waislam kudai mahakam ya kadhi kuwezeshwa na serikali hapa ndo kutakuwa na usawa kwamba waislam wanapata kutoka serikalini ktk organization yao ya kidini kama ambavyo wakristu nao wanavyoapata kutoka serikalini ktk organization yao ya kidini then utoaji huduma sasa iwe kwa hiayari ya anaetaka kwamba hata wewe ukitaka huduma katika mahakama ya kadhi uruhusiwe tu kama ambavyo muislam anavyoruhusiwa kupata huduma katika hospitali ya kikristu,andika makala zilizo newtral priva usijisahau kwa dini yako kuwa kama zitto alivyozungumza kuhusu mahakama ya kadhi bungeni,pamoja na uislam ake aliweka utanzania mbele,jitahidi uwe hivi,wasomaji wa makala hizi ni wa dini tofauti kaka.

Mimi nadhani badala ya kuwa na ubishi usiotusaidia, nikushauri tu kwamba. Na waislamu wajenge Mahospitali kama wakristu, wajenge mashule kama wakristu then serikali ikikataa kutoa ruzuku, wote tutaandamana. Lakini kulinganisha Mahakama ya kadhi na Hospitali na kulinganisha kifo na usingizi

Padre mada zako ni nzuri na zenye ukweli mwingi kiasi cha mtu muovu kutaabika kuzipinga au kuzikosoa. Kwa mafano ndugu hapo juu alieandika kuwa "acha unafiki" ameshindwa kuthibitisha upi ndo unafiki wako. Amejaribu kuzungumzia Asset zinazomilikiwa na Wakristo ktk hospitali za wakriso kwa kuzilinganisha na mahakama ya kadhi! kwa mtizamo wangu hv ni vitu viwili tofauti sababu hospitali hizi zinaendeshwa kwa (generally accepted proffessional procedures and ethics-uuguzi wa binadamu) na wala si kwa utashi wa kidini wala kwa desturi za dini ya kikristo. Namaanisha mgonjwa muslamu aendapo hospitali hizo kama ana shida ya malaria atapata huduma sawa na ambayo ngepata angeenda Muhimbili au pengine ambapo sio pa wakristu. Kinyume na mahakam ya kadhi itakuwa inaongozwa na desturi na sheria za dini ya kiislamu hivyo mkristo hana nafasi ya shida zake za kisheria kutatuliwa ktk mahakam hii. Maoni yangu ni kwamba waislamu km wanataka usawa basi wajitahidi na wao kuanzisha kitu cha kufanana na hicho wanachozidiwa na wakristu mfano na wao kuanzisha hospitali zao wakitegemea msaada toka serikalini kama ambavyo wakristu wanapata na si vinginevyo. Ndugu kaza ubongo fungua akili na moyo wako elimu ipenye ukombolewe.

Napata Mashaka na makala yako
Hivi Tanzania kama nchi ya kisekula inakuwaje inaingia mkataba na makanisa kuyapa mabilioni ya fedha kwa ajili ya uendeshaji wa hizo taasisi zao kama hospitali, shule na vyuo. Je huoni hapa ni kuimarisha ukristo dhidi ya uislamu? Waislamu si wajinga wanapolalamikia hili suala. Kama serikali ina uadilifu basi izipe taasisi zote za dini hayo mabilioni la sivyo serikali ijitosheleze kwa kuwa na hospitali za kutosha. Ubia huu wa serikali na makanisa ni hatari sana kwa mustakbali wa nchi yetu.
Pia serikali imekuwa ikidharau maslahi wa waislamu, kwa hakika hili ni bomu hatari sana. Tangu wakati wa Nyerere waislam wamekuwa na madai mbalimbali lkn yakipuuzwa. Pia kwa muda mrefu serikali imekuwa ikidhibiti harakati za waislam ima kwa kuitumia BAKWATA, kupitisha sheria mbovu kama ya ugaidi n.k. Kwa kuwa waislamu madai yao ni ya msingi wataendelea kudai tu, na hicho unachosema tuweke utanzania mbele, utanzania gani wakati kundi moja linadhulumiwa haki zake?
 
 
 

Fr. Karugendo, kwanza hongera sana kwa kuwa na fikra za juu kiasi hiki.
Mimi najiuliza swali moja tu ambalo pengine wahusika wangenisaidia kujibu.
UKRISTO na UISLAM zote ni dini, na Serilali yetu haina dini, ila ninachojua tu ni kuwa serikali yetu mara nyingi inashirikiana na dini hizi katika kuendesha miradi mbalimbali, sasa swali langu ni kwa , ENDAPO WAKRISTO WANAJENGA MAHOSPITALI AU MASHULE NA HATIMAYE SERIKALI KUINGIA UBIA NAO KUYAENDESHA, JE,NI KITU GANI KINAWAFANYA WAISLAMU KUSHINDWA KUJENGA MASHULE NA MAHOSPITALI NA HATIMAYE KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTOA HUDUMA KWA RAIA WOTE KAMA WANAVYOFANYA WENZAO WAKRISTO?
 
Ni ufinyu wa mawazo kama tutaishia kuwa watu wa kulalamika bila kujishughulisha.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.