- Tume ya Mkuu wa Mkoa Magesa yafichua uozo
SAKATA la Halmashauri ya Jiji la Arusha kutoa zabuni ya ukusanyaji wa ushuru wa maegesho ya magari katika mji wa Arusha kwa Kampuni ya Barack Printers Ltd, limechukua sura mpya kwa madudu mengi kubainishwa.
Zabuni hiyo ambayo imezua malalamiko kutoka kwa wadau Mbalimbali, ilitolewa kwa Kampuni ya Barack Printers Ltd, kwa shilingi 42,500,000, lakini hata hivyo, wamiliki wake na usajili wake umegubikwa na utata mkubwa.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa kampuni hiyo ama inamilikiwa “kwa mlango wa nyuma” au ina uhusiano wa karibu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Moris Makoi, akiwatumia baadhi ya watumishi wake na watu wake wa karibu.
Katika mahojiano yaliyofanyika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana, baina yake na Raia Mwema na habari hiyo kuchapishwa na gazeti hili, Makoi alikiri kuwa na uhusiano na kampuni hiyo akisema wanatekeleza kazi ya kukusanya ushuru huo baada ya kampuni yake, Mkomilo Trading, kuingia mkataba wa kibiashara na Barack Printers Ltd., ili kuwasaidia kazi hiyo kwa kuwa hawana uzoefu.
“Hawa Barack Printers wametu-sub contract sisi kampuni ya Mkomilo Trading ili tukusanye ushuru kwa niaba yao, lakini kazi hii wamepewa kihalali baada ya kushinda zabuni iliyotangazwa ila hawana uzoefu na kazi hiyo,” alieleza Makoi.
Hata hivyo, sheria za halmashauri zinazuia kampuni iliyopewa zabuni kuingia mkataba na kampuni nyingine kutekeleza kazi walizokubaliana na maelezo ya Makoi yaliongeza utata kuhusu uhalali wa zabuni hiyo ya ushuru wa maegesho.
Wakati bado kukiwa na “wingu jeusi” kuhusu uhalali wa kampuni hiyo tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, imefichua mengi yaliyokuwa yamefichwa nyuma ya pazia kuhusu kampuni hiyo.
Tume hiyo iliyoundwa na RC Mulongo kwa kuwahusisha wataalamu wawili kutoka Mamlaka ya Manunuzi na Ugavi (PPRA), ilichunguza mikataba kadhaa ya manunuzi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha inayodaiwa kugubikwa na vitendo vya ufisadi.
Taarifa za kiuchunguzi zilizokusanywa na Raia Mwema kutoka vyanzo kadhaa vya habari kuhusu sakata hilo zinabinisha kuwa tayari tume hiyo imekwishakumaliza kazi yake na imeshakabidhi ripoti ya uchunguzi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
Taarifa hizo za kiuchunguzi kuhusu sakata hilo zinabainisha kuwa tume hiyo imefichua upungufu mkubwa katika utoaji wa zabuni hiyo ambao awali ulielezwa kuwa umegubikwa na wingu la ufisadi.
Taarifa hizo zinafichua kuwa kampuni hiyo ya Barack Printers Ltd ilisajiliwa na msajili wa kampuni (chini ya sheria ya makampuni ya mwaka 2002) Aprili 20, mwaka 2011 na kupata hati ya usajili namba 82834, ikiwa ni siku 29 kabla ya kutangazwa kwa zabuni husika.
Zabuni hiyo ilitangazwa chini ya zabuni namba GA/003/2011/12/ACC/NC/002/LOT.3 katika magazeti mawili ya Mei 19 na 20, mwaka 2011 na mwisho wa kupokea zabuni ilikuwa Juni 18, mwaka 2011.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo ni mwendelezo wa habari tuliyopata kuichapisha katika matoleo yaliyopita ya gazeti hili, habari ambayo ilipingwa na Makoi ambaye aliwasilisha katika ofisi za gazeti hili hati ya madai kutoka kwa mawakili wake kwa lengo la kushitaki gazeti hili, imebainika kuwa, kampuni hiyo inamilikiwa na watu sita.
Watu hao sita ambao ni wakurugenzi na hisa zao kwenye mabano ni Petty Levi Kaduma (250), James Kitutu Saronga (200), Mohamed Abdalah Marumba (150), Himid Mansoor Ally (100), Veronika Thadeo Mwanyinga (100) na Mohamed Rajab Chobu (50).
Katika orodha hiyo imebainika kuwa Veronika Thadeo Mwanyinga ni Katibu Muhtasi katika ofisi binafsi ya Mwenyekiti huyo wa Halmashauri na Mohamed Rajab Chobu ambaye pia hufahamika kama Mohamed Kassim ni dereva wake.
Taarifa zaidi za kiuchunguzi kutoka ndani ya Halmashauri ya Jiji zinaeleza kuwa tume iliyoundwa na Mulongo imebaini kampuni hiyo haikukidhi vigezo kadhaa, hivyo haikuwa na haki ya kupewa zabuni ya ukusanyaji wa ushuru wa maegesho katika maeneo mbalimbali ya mji wa Arusha kwa mujibu wa ramani iliyotolewa na Halmashauri ya Jiji.
Kati ya upungufu huo ni kampuni hiyo kutokuwa na leseni sahihi kwa ajili ya zabuni waliyoomba na badala yake iliwasilisha leseni inayoonyesha ilitolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa ajili ya kuendesha shughuli za ukusanyaji mapato katika Mtaa wa Shekilango jijini Dar es Salaam na si Arusha.
Aidha, imebainika kuwa mzabuni huyo hakuwa hata na akaunti katika benki yoyote nchini wakati akipewa zabuni hiyo na hakuwasilisha taarifa ya kuweka na kutoa fedha benki (Bank Statement) na kampuni hiyo ilikiri upungufu huo kwa kuandika barua yenye kumbukumbu na: BPT/ARS/AMC/TD- CP/02/2011/2012, ya Juni 16, mwaka 2011.
Katika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, kampuni hiyo ilikiri kuwa haijafungua akaunti katika benki yoyote na kwamba ipo katika mchakato wa kufanya hivyo lakini hata hivyo, kamati ya tathmini ya halmashauri iliweka alama ya vema kwenye kigezo hicho kinyume cha sheria.
“Kigezo cha kuwa na akaunti katika benki na taarifa ya miezi sita ya kuingiza na kutoa fedha (bank statement) ni moja ya vigezo muhimu sana katika zabuni yoyote kwa mujibu wa sheria mpya za manunuzi, kwani hii inasadia kufahamu uwezo wa kampuni husika kifedha na katika kuendesha zabuni iliyopewa”alisema mtoa habari wetu.
Upungufu mwngine kwa mujibu wa uchunguzi ni hatua ya Barack Printers kuanza kazi ya kukusanya ushuru wa maegesho kuanzia Desemba Mosi, mwaka 2011 kabla ya kusaini mkataba kinyume cha sheria namba 21 ya ununuzi wa umma kifungu cha 55 (7) ya mwaka 2004, ambayo inaainisha kuwa kabla ya halmashauri yoyote kuingia mkataba na mzabuni lazima kwanza wasaini mkataba ambao ndio msingi wa makubaliano ya kibiashara.
“Pamoja na nia njema ya kuiingizia halmashauri mapato utekelezaji wa mkataba ulitakiwa kusubiri mpaka mkataba usainiwe (formal contract signing) na hii ni kwa sababu mkataba ndiyo unaoeleza haki na majukumu ya pande zote, taratibu za kufuatwa panapotokea mgogoro, masharti ya nini kifanyike na nini kisifanyike,utaratibu wa malipo na utaratibu wa kuvunja mkataba,” kilieleza chanzo chetu.
Upungufu mwingine uliotajwa na tume hiyo ni kampuni hiyo kutokuwa na uzoefu wa miaka mitatu katika kazi ya ukusanyaji mapato na pia mzabuni kuwa angalau awe amefanya kazi mbili inayolingana thamani ya fedha na zabuni aliyoomba na vigezo hivyo vyote viwili kampuni ya Barack haikuwa navyo.
“Pamoja na kuwa kampuni ya Barack Printers haikukidhi vigezo vya zabuni tajwa ilipendekezwa na kamati ya tathmini na kuridhiwa na PMU (timu ya wataalmu) kupewa kazi ya uwakala wa ukusanyaji mapato ni wazi kuwa kamati ya PMU waliipotosha Bodi ya Zabuni kwa kuipa taarifa isiyo sahihi kuwa Barack Printers amekidhi vigezo vya zabuni wakati wakifahamu fika kuwa si kweli”aliongeza mtoa taarifa wetu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo tume hiyo imebainisha zaidi kuwa kitengo cha manunuzi kilishindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kutoa taarifa za uongo kwa Bodi ya Zabuni kuhusu kampuni hiyo na pia Bodi ya Zabuni ilizembea majukumu yake na hivyo kupelekea kampuni hiyo kupewa zabuni kinyume na matakwa ya sheria za manunuzi ya umma na nyaraka za zabuni.
Taarifa zimesema tume hiyo ya wataalamu imehitimisha uchunguzi wao kwa kupendekeza kuwa zabuni hiyo isitishwe mara moja na mchakato wa kumpata wakala mwingine atakayetekeleza kazi hiyo uanze mara moja.
“Baada ya kupitia kwa kina mchakato wa zabuni ya ushuru wa maegesho ya magari imethibitika pasipo shaka kwamba kulikuwa na upendeleo wa waziwazi miongioni mwa watumishi wa Halmashauri waliohusika kuipa kampuni hiyo zabuni bila kufuata vigezo vilivyoanishwa,”anaeleza mtoa habari wetu.
Habari zaidi zinasema tume hiyo pia imeanisha majina ya watumishi (majina yao yanahifadhiwa kwa sasa) waliohusika katika uhujumu dhidi ya halmashauri hiyo na imependekeza hatua za kinidhamu zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yao.
Raia Mwema iliwasiliana na moja wanaotajwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Veronika Thadei Mwanyinga ambaye alikiri kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Barack Printers Ltd, lakini alikataa kuzungumza kwa maelezo kuwa yeye si msemaji huku mwenzake Mohamed Chobu pia akikataa kuzungumza kwa madai kuwa yuko barabarani akiendesha gari.
“Mimi si msemaji mkuu, nipe muda niwasiliane naye nitakujibu baadaye”alisema kwa kifupi huku akikataa kumtaja jina anayemwita kuwa ndiye msemaji wa kampuni hiyo. Hata hivyo alipopigiwa simu tena baada ya saa moja simu yake iliita bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Makoi alikataa kzungumzia suala hilo akihoji sababu za habari hiyo kufuatiliwa na gazeti hili, lakini baada ya muda mfupi alibadilisha kauli yake na kudai kuwa hakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia.
“Unataka kufahamu nini? Unafuatilia ili ujue kitu gani, ” alihoji Makoi. Lakini baada ya muda akaeleza: “ Siko katika nafasi ya kuzungumza. Niko maeneo ya KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro) na sikusikii vizuri naendesha gari na kuna upepo mkali”alisema na kukata simu yake.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomih Chang’a, hakupatikana kuelezea kuhusu taarifa hizo mpya za tume iliyoundwa, lakini Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alithibitisha kwa njia ya simu kuwa ni kweli wamepokea ripoti ya uchunguzi huo.
“Kwa sasa bado ripoti hii ni siri ya Serikali kwani tunaifanyia kazi.
Muda wa kuitoa hadharani bado. Wanahabari nawaomba mvute subira muda muafaka ukifika mtaelezwa kwa ufasaha,” alisema Mulongo.
Halmashauri ya Jiji la Arusha ni kati ya Halmashauri zinazolalamikiwa sana nchini kutokana na kushamiri wa vitendo vya ufisadi ambapo mwishoni mwa mwaka jana Serikali ililazimika kuwahamisha watumishi 19, wakiwemo wakuu wa idara sita, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kushamiri wa vitendo vya ufujaji wa fedha za miradi.
Halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati chafu kwa miaka zaidi ya mitano mfululizo baada ya hesabu zake kukaguliwa na mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa miradi mbalimbali kuonekana yamepotea kutokana na usimamizi duni wa watendaji.
Toa maoni yako