Makala
Sitta angesita kusema
Ncheme Nchicheme?
Toleo la 014
30 Jan 2008

KATIKA sakata linalohusu kashfa ya wizi wa mabilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) usingetaraji kwamba Spika wa Bunge, Mheshimiwa Sam Sitta, naye angetoa sauti yake kujaribu kukisafisha chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) .

Mwanzoni kabisa sakata hili lilikuwa bungeni, wakati Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa alipoibua masuala kadhaa kuhusu ufisadi na utendaji mbovu ndani ya BoT, lakini kwa kutumia mbinu ambazo ziliwashangaza baadhi ya watu hoja ya Slaa ikazimwa.

Sitta alihusika moja kwa moja na jitihada za kumzuia Slaa asiendeleze hoja yake bungeni, na wakati mmoja akatishia kwamba nyaraka alizokuwa ameleta Slaa ni ‘za ajabu’ na kwamba angezipeleka Polisi. Baadaye akatoa tamko kwamba Bunge haliwezi kuendekeza vijitaarifa vinavyosambazwa kwenye internet kuhusu ufisadi wa baadhi ya watawala na watendaji.

Lakini, taratibu, taarifa ambazo Sitta hakutaka zijadiliwe kwa kina bungeni zikatangazwa na wabunge wa Upinzani katika mikutano ya hadhara, zikatandaa katika internet, zikaandikwa katika magazeti, zikasomwa na Watanzania wengi, zikajadiliwa kwenye televisheni na redio, zikakataa kufa hadi Rais Jakaya Kikwete alipotangaza kuunda kamati ya kuchunguzza sakata hilo.

Sasa wananchi wengi wanashuku kwamba sehemu ya fedha hizo nyingi kupita kiasi zilitumiwa na CCM katika kampeni. Hili linaweza kuwa kweli au la.

Bila shaka kamati ya Rais itatuambia, lakini Sitta angekaa kimya kwa sababu hajakuwa na nia njema na hoja hii tangu ilipokuwa bungeni. Hakika, kwa kuizima hoja ya Slaa kiujanja alilinyima Bunge fursa ya kufanya kazi yake ya usimamizi wa shughuli za serikali na asasi zake.

Badala yake ikawa ni Rais ndiye anachukua hatua ya kutaka kujua ukweli.

Ungetaraji kwamba Sitta angetoa tamko la kujutia kutoisikiliza hoja ya Slaa bungeni, kwa sababu sasa imedhihirika kwamba Slaa alikuwa anajua anachokisema na Sitta hakujua anachokisema. Sasa anasema chama chake hakihusiki. Ikibainika kilihusika?

Sitta angelisaidia Bunge, angekisaidia chama chake, angewasaidia Watanzania kama angepigania haki ya Bunge kujadili kila kitu bila mipaka, hasa pale Wabunge, wawe wa chama tawala au wa Upinzani, wanapoonyesha ari ya kuibana Serikali isitende mambo hovyo hovyo, badala ya kujifanya ni sehemu ya Serikali. Kwa sasa Sitta asite kusema,   

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako