Makala
Tafakuri Jadidi
Somo hili maridadi kutoka kwa jirani - Kenya!
Johnson Mbwambo
Toleo la 186
18 May 2011

KATIKA kipindi cha wiki mbili zilizopita, majirani zetu – Kenya, wameandika historia. Kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo lijipatie uhuru wake, wanasheria 24 walijitokeza kuhojiwa na jopo la wanataaluma baada ya kutuma barua rasmi za kuomba kazi ya ujaji mkuu na unaibu jaji mkuu. Chini ya Katiba mpya ya Kenya, Jaji Mkuu huyo ndiye atakayeongoza Mahakama Kuu, na ndiye pia atakayeongoza vikao vya Tume ya Huduma za Mahakama (Judiciary Service Commission –JSC).

Huko nyuma, nafasi ya jaji mkuu ilikuwa ni ‘mali’ ya mkuu wa nchi (rais); yaani yeye ndiye aliyekuwa akiteua yeyote anayemtaka na kumpenda. Aliteua kwa vigezo na sifa zake mwenyewe anazozijua. Na kwa sababu hiyo, tangu uhuru wa Kenya, uteuzi wa nafasi hiyo umekuwa ukilalamikiwa kwamba unaongozwa zaidi na ukabila na siasa za makundi kuliko uwezo na uadilifu wa mhusika.

Sasa Kenya imesema ‘yatosha’kwa uteuzi wa namna hiyo. Baada ya mafanikio makubwa ya kuwa na Katiba mpya, sasa imeanza kusonga mbele kutekeleza matakwa ya Katiba hiyo mpya ambapo mahojiano hayo ya kutafuta watu wawili wa kujaza nafasi hizo, ni mwanzo tu wa safari mpya ya Kenya mpya.

Mchakato huo wa kuwapata jaji mkuu na naibu jaji mkuu ambao unaratibiwa na tume hiyo ulianza kwa nafasi hizo kutangazwa rasmi katika vyombo vya habari. Tangazo hilo la kazi liliweka bayana sifa ambazo waombaji walitakiwa kuwa nazo. Baada ya kupokea barua nyingi za kuomba nafasi hizo, JSC ilifanya upembuzi wake na kubakia na majina 24 (akiwemo Mghana mmoja) ambao ndio walioitwa kuhojiwa na jopo hilo kati ya Mei 3 na Mei 12.

Lakini katika mchakato huo huo, Kenya iliweza kuweka historia nyingine ya aina yake. Kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake,  mahojiano hayo ya kazi (job interview) ya kutafuta watu wawili wa kujaza nafasi hizo mbili nyeti katika ustawi wa Kenya, yalirushwa moja kwa moja na televisheni.

Na ni kwa sababu hiyo niliweza kuyafuatilia kupitia televisheni ya Citizen ya Kenya. Nasema hiyo nayo ni kuandika historia; kwa sababu jopo lile lingeweza kabisa kuendesha mahojiano yale kwa siri, na kisha baadaye likaibuka na majina hayo mawili na kuyatangaza; lakini sivyo lilivyofanya; kwani liliamua kuweka mambo yote ‘hadharani’ likitekeleza kikweli kweli dhana ya ukweli na uwazi.

Mara kadhaa niliyafuatilia mahojiano hayo ya kazi kupitia televisheni ya Citizen kwa kuwa yalinisisimua. Nilisisimshwa na jinsi makamishna wanaounda tume ile walivyokuwa wakiwarushia maswali mazito baadhi ya wanasheria magwiji wa Kenya waliiomba kazi hiyo akiwemo yule ambaye Rais Kibaki alitaka kumpa nafasi hiyo ‘kinyemela’, Jaji Alanshir Vishram.

Nilishuhudia baadhi yao wakitokwa na jasho kwa namna walivyokuwa wakirushiwa maswali magumu na makamishna wa JSC -maswali yaliyogusa kila kitu kuanzia kwenye kupima uelewa wa taaluma yenyewe ya sheria ikiwa ni pamoja na kukumbushwa hata kesi fulani fulani za zamani walizopata kuzitolea hukumu zenye utata (mmoja alishangaa kuhojiwa kuhusu kesi aliyoisikiliza miaka 20 iliyopita).

Walihojiwa pia kuhusu  masuala yao binafsi,  uadilifu, masuala ya haki za binadamu, mikakati mipya waliyonayo ya kuboresha mahakama za Kenya, namna watakavyohakikisha haki inatendeka katika kesi zinazofikishwa mahakamani, na hata mikakati yao kuhusu milundikano ya kesi iliyopo katika mahakama za Kenya.

Hakika, mahojiano yalisisimsha. Kuna walioonekana kutojiamini kabisa, na hivyo kubabaika mno katika kujieleza. Kuna wakati mahojiano yalipandisha jazba, na hata kusababisha kurushiana maneno makali kati ya wasailiwa (waomba kazi) na wasaili (wana-jopo).

Nakumbuka, kwa mfano, kuna wakati Jaji Samuel Bosire wa Mahakama ya Rufaa alikuja juu na kumtuhumu mwana-jopo,  Ahmednasir Abdullahi, kwamba ana kiburi, na kwamba maswali aliyokuwa akimuuliza yalihusu zaidi mambo yake binafsi kuliko kazi hiyo anayoiomba ya ujaji mkuu. Ilibidi Mwenyekiti wa jopo hilo, Profesa Christine Mango aingilie kati kuwatuliza wawili hao.

Nasema nilisisimshwa kuangalia mahojiano hayo, na ninaamini kabisa fursa hiyo ya pekee ambayo Wakenya waliipata inawaweka katika mazingira mazuri ya kutarajia kupata jaji mkuu bora kabisa na naibu jaji mkuu bora kabisa. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu jopo lile haliwezi kuibua ‘washindi’ wababaishaji ambao Kenya nzima iliona kwenye televisheni jinsi walivyokuwa wanaboronga.

Hata mimi ambaye ni Mtanzania na si mwanasheria, nitashangaa kama jina la jaji mkuu litakalopelekwa kwa Rais Kibaki kwa uteuzi rasmi lililotokana na mahoajino hayo, litakuwa ni la mmoja wa wale niliowaona kwenye televisheni wakibabaika kujibu maswali waliyoulizwa!

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba Wakenya waliyafuatilia mahojiano hayo kwenye televisheni, na hivyo nina hakika wanajua ni nani wanaostahili kupata nafasi hizo mbili kati ya wale 24 waliohojiwa. Wanawajua walioboronga kwenye mahojiano hayo na waliofanya vizuri. Wanawajua waliodanganya na waliosema ukweli!

Kwa maneno mengine, hakuna jinsi ambavyo jopo hilo la JSC linaweza kucheza ‘usanii’ na kuibuka na mshindi feki. Pengine hilo lingewezekana kama mahojiano hayo yasingekuwa yanaonyeshwa moja kwa moja na televisheni za Kenya, na pengine kama waandishi wa habari wasingekuwa wamehudhuria!

Ndugu zangu, nikiri kwamba wakati nafuatilia mahojiano hayo ya kihistoria ya waomba kazi ya ujaji mkuu na unaibu jaji mkuu, nilikuwa naionea ‘gere’ Kenya kwa hatua ya demokrasia ambayo wameifikia. Niliionea ‘gere’ Kenya; hasa nikikumbuka mahali ambapo Tanzania bado tupo.

Sina hakika kama baadhi yetu tutaishi na kushuhudia mchakato wa kumpata Jaji Mkuu wetu au Mwanasheria Mkuu wetu wa Serikali kwa namna ile ile ambayo tumeshuhudia Kenya wakiwapata Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu wao.

Nasema sina hakika kama baadhi yetu tutaishi hadi kuyashuhudia hayo ya Kenya; kwa sababu bado naona kuna ‘usanii’ mwingi hapa kwetu Tanzania katika kuifikia demokrasia ya kweli, na mfano mmoja ni suala hili la Katiba mpya.

Sioni kama kuna dhamira ya kweli kwa Rais Kikwete na Serikali yake ya CCM kuiwezesha Tanzania kuwa na Katiba mpya tunayoistahili Watanzania – Katiba ambayo tumekuwa tukiililia kwa miaka mingi – Katiba ambayo itatuvusha kwenye changamoto za  miaka 100 ijayo!

Ukiangalia hapa Tanzania kilichotokea na kinachotokea kuhusu suala hilo la Katiba utaona kuna ‘usanii’ mwingi tu unaochezwa, na kwamba dhamira ya kweli haipo. Angalia, kwa mfano, suala la mchakato wenyewe wa kuipata hiyo katiba mpya ambao bado Watanzania hatujakubaliana nao kabisa, lakini Rais Kikwete na Serikali yake ya CCM wanataka kuliburuza hilo. Tafakari jinsi wasivyotaka masuala ya Muungano na Madaraka ya Rais yajadiliwe, na kisha niambie kama kweli wana dhamira ya kweli ya kuipa nchi Katiba mpya tunayoitaka sote Watanzania.

Nadhani analolitaka Kikwete ni lile tu la kusifiwa kwamba ameanzisha mchakato wa kuwa na Katiba mpya, basi. Ni mchakato upi huo, na je; unaafikiwa na Watanzania wengi? Ni Katiba ya namna gani Watanzania wanayoitaka? Maswali hayo yeye kwake si muhimu.

Anachotaka yeye ni akikutana na wahisani huko nje ya nchi au hata hapa Dar wakimuuliza kuhusu kilio cha Watanzania cha kuwa na Katiba mpya awajibu kwa tabasamu: “Ndiyo, tumeshaanza mchakato”.

Nina hakika huko mbele ya safari kelele za wanaharakati zitakapoongezeka kuhusu mchakato aliouchagua yeye wa kuipata hiyo Katiba atakuja kusema: “Walitaka Katiba mpya, tayari tumeshaanza mchakato; sasa wanataka nini zaidi?

Narudia tena kusema kwamba kwake yeye, mchakato na namna tunavyoweza kuwashirikisha wananchi kuipata Katiba bora itakayotuvusha kwenye changamoto za  miaka 100 ijayo, yeye hayo hayamnyimi usingizi; maana anaoucheza ni ‘usanii’ wa aina fulani tu lakini dhamira ya kweli haipo!

Ninaweza kusema kwamba ni kwa sababu tu kuna upepo wa kudai Katiba mpya unaovuma barani Afrika, na hata katika nchi za Kiarabu, na ni lazima aende nao kihiari badala ya kusubiri kuzolewa nao, ndiyo maana amekubali. Kama ingekuwa ni kwa mapenzi yake, Kikwete angeendelea na Katiba hii hii hadi anaondoka madarakani 2015.

Ndugu zangu, kwa kutumia Kiswahili cha mitaani, Kenya tayari wametupiga bao jingine. Wametutangulia katika suala la kuwa na Katiba mpya, na sasa wametutangulia pia kwa kuanzisha mpango wa kuwahoji hadharani na mbele ya kamera za televisheni wale wote wanaoomba nafasi nyeti za kitaifa kama tulivyoshuhudia majuzi kwenye hiyo ya ujaji mkuu na unaibu jaji mkuu!

Kila ninapoisoma sura ya pili ya Katiba yetu ya sasa, sehemu ya kwanza inayozungumzia Rais; hususan mamlaka makubwa aliyopewa ya kuwateua watu wa kushika nafasi za madaraka; huwa najiuliza kama kuna mantiki yoyote ya kukasimu kwa mtu mmoja tu uteuzi wa nafasi zote hizo nyeti  za uongozi.

Na baada ya kuyaona hayo ya majuzi ya Kenya, huwa najiuliza kama si vyema pia kwetu (Tanzania) nafasi hizo nazo zikaombwa na wanaozitaka ili nao wahojiwe na jopo mbele ya kamera za televisheni kama walivyofanya wenzetu Kenya. Maana; katika Uafrika wetu huu, unahitaji kuwa na Rais mwadilifu kwelikweli kuweza kuvishinda vishawishi vya kumteua Mkristo au Mwislamu mwenzake katika nafasi hizo au mjomba au shangazi au nduguye au hata Mkwere au Mpare mwenzake, au hata mwanamtandao mwenzake!

Lakini tunaweza kuwaepusha marais wetu wajao na vishawishi hivyo kwa kuifuata njia hiyo ya Kenya ya kuzitangaza baadhi ya nafasi nyeti magazetini ili watu wenye kujiona wana sifa zinazotakiwa waombe kwa barua rasmi, na waitwe kuhojiwa na jopo la wataalamu.

 Lakini hatuwezi kuwa na utaratibu huo kama hautabainishwa wazi kwenye katiba; kwa hiyo mahali pa kuanzia ni kwenye harakati hizi za kutaka Katiba mpya maridhawa. Natupambane, basi,  tuwe na Katiba mpya nzuri kama ile ya Ghana ya mwaka 1992 ambayo naambiwa ndiyo bora kuliko zote barani Afrika.

Nihitimishe kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kuukataa ‘usanii’ huu unaochezwa hivi sasa katika suala hili la Katiba. ‘Usanii’ huu ulishapitwa na wakati; maana ulishazolewa na upepo (gone with the wind); kwa maana halisi ya maudhui ya filamu ile ya kale ya Marekani ya mrembo Greta Garbo.

Mobutu alijaribu kuucheza ‘usanii’ huo lakini mwishowe haukumsaidia kitu; kwani hatimaye naye alibebwa na upepo. Baada ya kushutumiwa kuiendesha nchi kidikteta akaruhusu kuanzishwa kwa utitiri wa vyama vya siasa (vingine akitoa pesa yeye mwenyewe vianzishwe) ili eti aonekane kuwa ni mwana demokrasia kweli kweli kwa kuiwezesha Zaire kuwa na vyama vingi vya upinzani!

Vyama hivyo vikawa vinakorogana vyenyewe, na hivyo kumpa nafasi ya kuendelea kutawala bila jasho; huku akivikejeli (kama hapa nchini) kwamba si lolote wala chochote. Kwa ufupi, Mobutu hakuwa na dhamira ya kweli ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa Zaire. Aliukubali mfumo huo shingo upande, kwa sababu tu ya shinikizo alilokuwa akilipata kutoka kwa jumuiya za kimataifa kuhusu udikteta wake. 

Hata hivyo, kwa ‘usanii’ huo, Mobutu aliweza kuwaghilibu watu wachache na kwa muda mfupi tu; kwani kilichomsibu sote tunakijua – alibebwa kwa kasi na upepo wa mageuzi barani Afrika! Ni hoja yangu kwamba watawala wetu Tanzania wasisubiri nao kuzolewa na upepo wa mageuzi barani Afrika unaotaka uwepo wa Katiba mpya!

Kuna somo zuri tumelipata kutoka nchi jirani ya Kenya. Kenya sasa wana Katiba mpya, na kwayo tunashuhudia mambo mapya. Kenya wametuonyesha njia, na tuifuate kwa dhamira ya kweli ya kujenga demokrasia ya kweli nchini mwetu. Tuache ‘usanii’.

Tafakari.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Johnson Mbwambo
mbwambojohnson@yahoo.com

Toa maoni yako