Spika atikisa kiberiti

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema si dhambi kwa taifa kutazama upya sifa za mtu kuchaguliwa kuwa mbunge; lakini mtangulizi wake, Pius Msekwa, anaamini kabla ya kufika huko ni muhimu kujiuliza kama taifa limepata tatizo lolote kwa kuwa na wabunge wanaojua kusoma na kuandika tu, Raia Mwema linafahamu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mojawapo ya sifa ya mtu kuwa mbunge ni kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika lugha za Kiingereza au Kiswahili; lakini katika siku za karibuni kumekuwa na hoja kwamba sifa hizo pekee hazitoshi katika dunia ya sasa.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dodoma wiki hii, Ndugai alisema kuna sababu za kihistoria zilizochangia kuwepo kwa kigezo cha kujua kusoma na kuandika pekee kwenye miaka ya nyuma, lakini pengine umefika wakati wa kuangalia upya sifa hizo kulingana na mahitaji ya sasa.

Kwanza ni bahati nzuri mimi najua sababu za kwa nini sifa hiyo iliwekwa kwa enzi hizo. Wanaozungumza leo inawezekana hawajui hasa sababu zilizosababisha kuwepo kwa sifa ya namna hiyo wakati huo.

“Msingi wa kuwapo kwa sifa hiyo ni kutoa nafasi pana ya demokrasia sawa kwa kila Mtanzania mwenye uwezo kuchangia ujenzi wa taifa bila kubaguliwa.

“Sifa hiyo ililenga zaidi watu masikini ambao walikuwa na uwezo mkubwa kuwatumikia wananchi lakini hawakubahatika kusoma sana kutokana na mazingira upatikanaji wa elimu kwa wakati huo,” alisema Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma.

Ndugai aliyezungumza na gazeti hili ofisini kwake bungeni mjini Dodoma, alisema hata wakati masharti hayo yakiwekwa, Bunge lilikuwa na wasomi wa viwango vya juu lakini lengo lilikuwa ni kuweka usawa.

Hata hivyo, alisema kwa sasa mazingira ya hapa Tanzania na duniani kwa ujumla yamebadilika na kusema hata baadhi ya nchi washirika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeanza kuweka masharti mapya kwa wabunge wake na ni muhimu kwenda kwa kasi sawa na wenzetu hao.

“Nilitaka tu kuweka sawa kwa kuwaondoa hofu watu ambao hawakujua kiini cha sifa hiyo kwa wakati huo wasije wakatafsiri vibaya bila kujua ilikuwa nia njema sana, na nikiri kwamba imetusaidia sana hadi hatua hii maana usipojua historia yako vizuri utapotosha kila kitu na huwezi kujua unakoelekea.

“Kwa kweli kwa maoni yangu kama Spika sasa ni wakati mwafaka kwa wahusika kuangalia upya sifa hii kulingana na wakati wa sasa. Wenzetu wa nchi nyingine katika jumuiya yetu walikwishatoka huko zamani. Wengine sifa ni kuanzia diploma na wengine shahada. Nadhani ni wakati muafaka kwa wahusika kuangalia hilo ili twende na wakati.

“Lakini ni kiwango gani na namna gani siwezi kuwasemea lakini ni muda mwafaka ili pia kuondoa hayo maneno au malalamiko yasiyo na tija wakati waheshimiwa wabunge walio wengi ni wasomi waliobobea.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania toleo la mwaka 1977, Ibara ya 67  (1) inasema;  “Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza..”.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake na gazeti hili juzi Jumatatu, Msekwa alisema kabla ya kufikiria kwenda na wakati au kufanya mabadiliko yoyote, ni muhimu kwanza wahusika wakajiuliza kama masharti ya sasa yamewahi kutupa shida yoyote kama taifa.

Msekwa ambaye alishiriki katika Bunge la Tanzania katika namna tofauti kwa zaidi ya miaka 30, alinukuu msemo wa lugha ya Kiingereza usemao; Don’t trouble the trouble before it troubles you ( Mwana kuyataka, mwana kuyapata), akisema kama hakuna tatizo, hakuna sababu ya kubadilisha kitu.

“ Mimi nimekuwa bungeni kwa muda wa mrefu hadi sasa nimestaafu. Katika wakati wangu, Bunge halijawahi kupata tatizo kwa sababu ya masharti haya. Kumekuwepo na wabunge waliosoma sana na wengine ambao hawakusoma sana.

“ Hata kabla ya Uhuru masharti haya yalikuwepo katika Baraza la Kutunga Sheria. Wajumbe wa Tanzania waliochaguliwa katika Baraza la mwaka 1960 ambalo lilileta Uhuru wengine hawakuwa wasomi sana lakini mchango wao tunauheshimu.

“ Mtu kama Bibi Titi Mohamed alifanya kazi kubwa sana kwenye baraza hilo hata kama hakuwa anafahamu sana lugha ya Kiingereza. Ndiyo maana, naamini kwamba jambo la kwanza kujiuliza ni endapo kama taifa tumepata shida yoyote na mfumo huu wa sasa,” alisema Msekwa.

Maelezo hayo ya Msekwa yaliungwa mkono na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliyesema Bunge linatakiwa kuwa Baraza la Wananchi na vigezo vya kielimu havina maana.

Alisema Bunge linatakiwa kuwakilisha aina ya wananchi waliopo na kwamba Tanzania si nchi ambayo wananchi wake wote wameelimika sana na hivyo Baraza lao (Bunge) linatakiwa kuwa na taswira hiyo pia.

“ Tukianza kuweka vigezo vya digrii na mengineyo kuna hatari ya kutengeneza Bunge ambalo ni elitist (la wasomi) lililo mbali na watu wake. Mtazamo wangu ni kwamba Bunge linapaswa kuwa Baraza la Wananchi na haya masharti ya kitaaluma yasipewe nafasi sana. Wananchi wapewe nafasi ya kuwachagua watu wanaowataka,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (NCCR-Mageuzi) ambaye sasa amehamia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila, alisema kwa maoni yake, mbunge anatakiwa kuwa na kiwango cha elimu cha shahada moja au kinacholingana na hicho.

Alisema kazi ya mbunge ya kutunga sheria na kuisimamia serikali inahitaji kufanyika kwa uchakataji mkubwa wa maoni ya wananchi huku ukipambana na timu ya serikali yenye wataalamu wengi.

Alisema katika nchi zilizoendelea, mbunge ni taasisi kwa vile anapewa wasaidizi wanaomsaidia katika mambo mbalimbali na hivyo hata kama yeye hana uelewa mkubwa, watu wa kumsaidia wapo –tofauti na hali ya Tanzania.

“ Hapa Tanzania mbunge analipiwa msaidizi ambaye mshahara wake hauzidi shilingi laki tatu kwa mwezi. Sasa utampata mtu gani wa kukuchambulia mambo na kukufanya uwe na mchango mkubwa bungeni ambaye mshahara wake ni laki tatu kwa mwezi?

“ Mbunge kwa hapa kwetu ni mtu binafsi. Wewe ndiyo utafute hoja, ushiriki katika kutunga sheria, kuisaidia serikali na kutengeneza hoja binafsi. Kama huna elimu ya kutosha, ni wazi haya majukumu yatakushinda,” alisema Kafulila.

One thought on “Spika atikisa kiberiti”

  1. Apolinary says:

    Na muunga mkono mheshimiwa kafulila kama taifa ni bora kubadilisha mfumo nakuendena na wakati kwenye kila nyanja kama tu ilivyo sasa serikali inayo fikiriwa na mheshimiwa raisi ya viwanda ni moja wapo ya mabadiliko maana tuna amini Tanzania inaelekea kua ya wasomi tuu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *