Spika: Lijualikali bado mbunge

Mbunge Lijualikali (katikati) akiwa katika purukushani na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, anaendelea na wadhifa wake huo baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kufanya fujo.

Akizungumza na RAIA Mwema, Ndugai alisema kwa mujibu wa Katiba, Mbunge atakoma kuwa mbunge endapo atafungwa jela kwa muda wa zaidi ya miezi sita.

“ Ukisoma Katiba ya Tanzania Ibara ya 70 na 71, zikisomwa kwa pamoja na Ibara ya 67, utaona kwamba Lijualikali bado ni mbunge,”alisema Ndugai.

Lijualikali pamoja na dereva wake, John Kibasa, wamehukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero kwa kosa hilo lililofanyika wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema chama chake kitakata rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kilombero.

Alisema uamuzi huo ni mgumu kueleweka kwa sababu katika vurugu zilizotokea hakuna mtu aliyeumizwa na adhabbu hiyo ina harufu ya siasa.

Katika hatua nyingine, akizungumza na TBC jioni ya leo Januari 11, 2017, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, aliungana na Spika Ndugai kwa kueleza kuwa Lijualikali ataendelea kuwa mbunge kwa kuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita tu jela na si zaidi ya miezi sita kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyojieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *