
UZITO wa kauli za Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika utawala wa Bunge na hata mbele ya jamii unaweza kuwa umeanza ‘kupwaya’ baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuweka bayana kuwa, hakuna posho mpya kinyume cha kauli ya Makinda kwamba posho hizo zipo zikiwa zimepanda kutoka Sh. 70,000 hadi 200,000.
Hatua hiyo ya Ndugai inazingatia taarifa ya Ikulu kwamba, Rais Jakaya Kikwete hajatoa kibali cha kuidhinisha malipo ya posho hizo na kwa hiyo, hakuna malipo ya posho mpya, kama ambavyo iliwahi kuelezwa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Bunge.
Tayari Rais Kikwete katika kikao chake na wabunge wa CCM kilichofanyika Jumatatu, wiki hii mjini Dodoma, akiwa ametokea Mwanza katika maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM, anakaririwa kurejea msimamo wake kwamba si wakati muafaka kwa wabunge kuongezewa posho.
Katika kikao hicho na wabunge wa CCM, Kikwete anadaiwa kuwaeleza wabunge hao kuwa mazingira halisi hayaruhusu ongezeko hilo kwa sasa, kauli inayotafsiriwa na baadhi ya wabunge kuwa inawezekana kuwapo kwa ongezeko hilo katika bajeti ijayo.
“Ametueleza hili suala si wakati wake sasa, anatambua mantiki ya nyongeza ya posho hizo kwa wabunge lakini anasema tatizo ni mazingira yaliyopo, na akasisitiza katika suala hili pia tumechafuana wenyewe kwa wenyewe (wabunge),” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka katika mkutano wa Kikwete na kundi maalumu la wabunge hao.
Kwa upande wake, Ndugai amezungumzia kutokuwapo kwa ongezeko hilo akisema hakuna nyongeza ya posho hizo na pia jamii haina haja ya kuendelea na mjadala ambao kiini chake hakipo tena.
Kuhusu viongozi wakuu wa mhimili huo wa taifa viongozi wake kupishana kauli, Ndugai anaamini hilo si jambo kubwa, akisisitiza utaratibu ni posho kutolewa baada ya kupata kibali cha Rais-Ikulu ambacho taarifa ya Ikulu inaeleza hakuna kibali hicho.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge mjini Dodoma wamekuwa hawataki kuthibitisha kama malipo ya posho zao ipo nyongeza hiyo au wanaendelea kulipwa posho ya zamani kinyume cha uthibitisho wa Spika Makinda kwamba wameanza kulipwa muda mrefu posho hizo.
Wapo wabunge ambao wanasema wanaendelea kulipwa posho za zamani lakini wengine wakigoma kuthibitisha suala hilo huku kukiwa na taarifa kuwa, Kambi ya Upinzani, imejadili suala hilo na kutetea posho mpya katika kikao chake cha ndani kilichofanyika Jumatatu,
Mbunge mmoja machachari ambaye pia ni mwanasheria maarufu, ambaye alishiriki kikao hicho cha kambi ya upinzani anakaririwa kueleza kuwa; “Hakuchaguliwa mbunge ili awe masikini.”
Uchunguzi umebaini kuwa katika kambi hiyo ya upinzani, mbunge pekee anayepinga ongezeko la posho ni Kabwe Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, wakati kutoka kambi ya CCM, Mbunge anayepinga ongezeko hilo ni Januari Makamba wa Jimbo la Bumbuli, Tanga.
Hadi sasa rekodi zinawapandisha hadhi ya kisiasa wabunge hao vijana ambao walikuwa tayari kupinga ongezeko hilo la posho hadharani na katika vikao rasmi vya Bunge, ingawa huko wamekuwa wakikumbwa na mashambulizi makali kutoka kwa wenzao.
Mara baada ya kuwapo kwa taarifa za ongezeko la posho na hasa kupishana kwa kauli kati ya Spika na Katibu wa Bunge, gazeti hili lilifanya utafiti kubaini kama kweli nyongeza ya posho ilikuwapo au la.
Uchunguzi wetu ulibaini kuwa posho hizo hazikuwa zikilipwa tofauti na kauli aliyopata kusema Spika, hali ambayo sasa inathibitishwa na Naibu Spika, Ndugai kama ilivyokuwa kwa Katibu wa Bunge, lakini pia, taarifa ya Ikulu kutotoa kibali inazidi kuipa uzito habari hiyo tuliyowahi kuichapisha katika moja ya matoleo ya gazeti hili.
Maoni ya Wasomaji
Tunza hadhi yako jiuzuru.
Tunza hadhi yako jiuzuru. Muda hauendani na utendaji. Umetumikia tayari. usikubali kupakazwa kinyesi.