MIONGONI mwa mambo yanayochukiza kuhusu wapenzi wa michezo wa Uingereza ni unazi wao uliokitihiri.
Japo unazi kwenye michezo ni kitu cha kawaida, hata kama umekithiri, lakini unazi usiozingatia hali halisi unaweza kuonekana kama wendawazimu.
Muda mfupi kabla ya kuandaa makala haya, nilikuwa naangalia kilichoitwa pambano la ndondi la kufungia mwaka kati ya Floyd Mayweather wa Marekani na Mwingereza Ricky Hatton.
Sijihesabu kama shabiki mzuri wa ndondi na mara nyingi huwa napendelea kusikia matokeo badala ya kuangalia pambano “live”. Pengine nami nasumbuliwa na unazi, japo wangu ni wa busara zaidi kuliko huo wa mashabiki wengi wa michezo wa Kiingereza. Takriban mwezi mzima kabla ya mapambano huo, Waingereza wengi walikuwa wakiamini kwamba bondia wao Hatton angeshinda.
Ni vizuri kumsapoti mwanamichezo anayewakilisha nchi yako lakini ni vizuri zaidi kuangalia uwezo wa mpinzani wake. Na hapo ndipo Waingereza, kama ilivyo kawaida yao, walipokataa kwa makusudi kuangalia na kuheshimu umahiri wa mpinzani wa Hatton.
Inaaminika, na imethibitika kwamba Mayweather ndiye bondia bora kabisa kwa sasa, ambapo kwa lugha ya mchezo huo wanamwita “the best ever pound-for-pound boxer in the world”.
Lakini pengine kwa vile Hatton ni kipenzi cha wengi, na alikuwa akiiwakilisha himaya ya malikia, Waingereza wengi walizifumbia macho sifa za Mayweather na kupiga kelele nyingi kwamba bondia wao atashinda na kuweka historia.
Kabla ya pambano hilo, mabondia hao wote wawili walikuwa hawajapoteza pambano lolote, na ukichanganya kwamba mmoja alikuwa mzungu mweupe na mwingine Mmarekani Mweusi, kulikuwa na kila aina ya mashamushamu yaliyochangiwa kwa namna flani na weupe na weusi wa mabondia hao (ubaguzi wa rangi).
Sijui na mie ni mbaguzi au la, lakini nilitaka Mayweather ashinde nikiamini kwamba hiyo ingekuwa zawadi yangu nzuri ya siku ya kuzaliwa kwangu.
Na kweli niliipata zawadi hiyo na kusahau machungu ya kulipia pauni takriban 15 kuangalia pambano hilo kwenye runinga ukiachilia mbali kukesha hadi alfajiri kutokana na tofauti ya saa kati ya Las Vegas na Aberdeen.
Pengine nilitaka Mayweather ashinde kwa vile ni Mweusi,na naamini baadhi ya Weupe waliotaka ashindwe walikuwa na sababu hiyo hiyo, lakini sababu kubwa zaidi ya kutaka Hatton ashindwe ni kelele za unazi wa Waingereza.
Ni unazi wa namna hii unaowafanya watu hawa wakurupuke na visingizio vya ajabu kabisa kila wanaposhindwa kwenye michezo. Majuzi walipotolewa kwenye kuwania nafasi ya fainali za michuano ya soka ya bara la Ulaya (Euro 2008) lawama kibao zilielekezwa kwa mastaa wa kigeni wanaocheza Ligi kuu ya nchi hii kwa madai kwamba kujazana kwao hapa kunadumaza vipaji vya wanasoka wa ndani na hivyo kuathiri maendeleo ya soka. Walipotolewa kwenye michuano iliyopita ya Kombe la Dunia walimlaumu kocha wa kigeni, Sven Eriksson.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa michezo wa hapa wameamua kuweka pembeni unazi (japo walikaa kimya kabla ya kipigo cha Hatton) na kukiri kwamba bondia wao ni mpiganaji (fighter) ilhali mpinzani wake ni bondia (boxer).
Na ni baada ya kipigo hicho ndipo nilipopatwa na huruma dhidi ya Hatton hasa baada ya kupata undani wa “background” yake. Huyu ni bondia anayetoka katika familia duni na ndondi ni sawa na ajira kwake. Kimsingi, mabondia wote wawili wanatoka katika familia duni na mafanikio yao katika ndondi imekuwa fursa yao pekee ya kuwa na maisha bora waliyonayo sasa. Ni watu waliotumia vipaji vyao kujiondoa kwenye tabaka la chini.
Unazi wa Waingereza naulinganisha kwa namna fulani na baadhi ya wanasiasa wetu huko nyumbani ambao kwao habari sahihi ni zile za kuwapongeza, kuwasifia na pengine kuwatukuza. Sijashangazwa na matokeo ya utafiti wa REDET kuhusu hali ya kisiasa huko nyumbani.
Lakini kilichonishangaza ni kauli za baadhi ya wanasiasa ambao hawaafikiani na matokeo ya utafiti huo pengine kwa vile hayaendani na matakwa yao. Hivi Spika anataka kutuambia nini anapopingana na matokeo yanayoonyesha kushuka kwa imani ya wananchi kwa Bunge kwa vile tu taasisi hiyo imefanya marekebisho kadhaa katika mfumo wa utendaji wake?
Je Bunge limeshafanya utafiti wowote kujua iwapo maboresho iliyofanya yamewapendeza wananchi? Busara ya kawaida tu inaweza kutuambia kwamba sio kila kinachoboreshwa kinakidhi matarajio ya wanaokitegemea. Ni ukweli usiopingika kwamba wapiga kura wengi wamekuwa wakililalamikia Bunge kwa ‘kukosa meno’ ya kutatua mengi ya matatizo yanayolikabili nchi yetu.
Chukulia mfano wa mjadala kuhusu sakata la kampuni ya Richmond na namna ulivyokuwa ukipigwa danadana bungeni. Hata maamuzi ya kuunda kamati ya kuchunguza sakata hilo unaonekana umechelewa, na binafsi sintoshangaa iwapo tume iliyoundwa na Spika isipopata matokeo yanayokusudiwa kutokana na kuchelewa kuundwa kwake.
Si ajabu wahusika watakuwa wameshaharibu ushahidi muhimu na pengine wengine wameshatokomea mbali ambako hata wakishitakiwa itakuwa vigumu kuwakuta na hatia.
Ugonjwa unakabiliwa pindi unapotokea na sio kwa kufukua makaburi ya waliofariki kwa ugonjwa huo.
Kuna wanaodai kwamba matokeo ya utafiti wa REDET hayawakilishi maoni ya Watanzania wote kwa vile idadi ya waliohojiwa ni ndogo. Kama mwanafunzi ninayefanya utafiti, kitu pekee nachoweza kuhitimisha kuhusu mawazo kama hayo ni kwamba pengine wanaopinga hawajui lolote kuhusu maana nzima ya utafiti.
Kwa kifupi, tafiti zinazohusisha kukusanya maoni hufanywa kwa kupata mawazo ya watu wachache tu wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii inayotafitiwa.
Ni vigumu sana kufanya utafiti unaoweza kukusanya mawazo ya Watanzania zaidi ya milioni thelathini, isipokuwa kwa kuwahoji idadi kadhaa ya watu wenye sifa zinazowakilisha makundi mbalimbali katika taifa letu.
Uwakilishi sio muhimu kwenye tafiti pekee bali hata kwenye maeneo mengine kwani hata tunapokubaliana kwamba Bunge ni taasisi inayowakilisha Watanzania haimaanishi kila Mtanzania anaingia ndani ya jengo hilo tukufu.
Binafsi nadhani upinzani dhidi matokeo ya utafiti huo hautokani na idadi ya waliohojiwa bali kasumba iliyotawala baadhi ya wanasiasa wetu wenye mawazo ya zama za mfumo wa chama kimoja ilhali tuko kwenye mfumo tofauti.
Katika mfumo wa chama kimoja, ni lazima mawazo ya wananchi yalingane na mawazo ya wanasiasa. Kinyume cha hapo ni uhaini, uchochezi au kupachikwa jina la kibaraka wa wasioipenda nchi.
Katika zama hizo ni dhambi isiyosameheka kumwambia kiongozi kuwa amesahau kufunga zipu ya suruali yake, na kwa vile kauli za kiongozi ni sahihi, basi hata akitukana ni lazima apigiwe makofi ya pongezi.
Sio kosa kwa mwanasiasa kutamani tabia za watu ziendelee kuwa kama zilivyolazimishwa wakati wa chama kimoja, kama ambavyo haikuwa kosa kwa wapenzi wa ndondi wa Uingereza kutamani Hatton angemshinda Mayweather licha ya hali halisi kuwa tofauti na matamanio hayo. Ila sio sahihi kulazimisha matamanio hayo yawe ndio hali halisi.
Badala ya kuona matokeo ya tafiti kama hiyo ya REDET kuwa hayawakilishi maoni ya watu wengi na pengine ni ya ‘kizushi’, wanaopinga wanapaswa kuona hiyo ni baraka iliyofichika (blessing in disguise) kwani inawapa changamoto ya kujipanga upya kuwapatia wananchi kile wanachotarajia kutoka kwa viongozi wao na taasisi wanazoongoza.
Toa maoni yako