
UJUMBE maalumu umewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kutoka kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambao kwa pamoja wamekiri kuwa baadhi ya mawaziri wana uwezo mdogo wa kukabili changamoto za hoja za wabunge na wamependekeza uteuzi mpya uzingatie zaidi umakini na uwezo binafsi wa mtu, sambamba na uadilifu, Raia Mwema, limeelezwa.
Kwa upande mwingine katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni Rais Kikwete kukubaliana na ujumbe huo na ushauri wa wabunge, pamoja na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, kwa mara ya kwanza tangu wito wa kuwawajibisha mawaziri utolewe, ameweka wazi kuwa atachukua hatua.
Kikwete aliweka bayana msimamo wake huo wakati wa hotuba yake ya Mei Mosi, mjini Tanga, Jumanne wiki hii, akikumbusha kuwa yeye ndiye aliyeruhusu ripoti za ufisadi zinazotokana na ukaguzi wa hesabu za Serikali zijadiliwe kwa uwazi bungeni na sasa, ni wakati wa kuwachukulia hatua kwa watu aliowaita “mchwa.”
Kwa mujibu wa Kikwete, hatua kali zitawagusa watendaji waliohusika na wizi ulioripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hata hivyo, hakufafanua ni hatua zipi zikazochukuliwa dhidi ya wahusika ingawa pia alieleza kufadhaishwa na ufisadi huo.
Kikwete anaungana na kauli iliyowahi kutolewa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwamba, mjadala mkali miongoni mwa wabunge kuhusu ripoti za CAG kutaja ufisadi kila mwaka zitakuwa zinabeba sasa heshima na uzito unaostahili.
Kwa upande mwingine, taarifa kuhusu ujumbe wa Makinda na Pinda waliouwasilisha kwa Kikwete unatajwa kutolewa kwa kuzingatia uwezo mdogo walioonyesha baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri, kiasi cha kuzidisha malalamiko ya wabunge wanaodai maswali yao bungeni kutojibiwa ipasavyo.
Mifano kadhaa imetolewa, ambayo ni pamoja na baadhi ya wabunge kuwahi kulalamika kwa maandishi kwa Spika wakieleza maswali yao kwa baadhi ya mawaziri kujibiwa kwa misingi ya ubabaishaji.
Katika kuwasilisha ujumbe huo kwa Rais Kikwete, Spika na Waziri Mkuu Pinda wamekaririwa kumweleza Kikwete kwamba wapo mawaziri ambao ni butu katika kujibu maswali bungeni au kukabili hoja zenye changamoto zinazopaswa kupata majawabu kutoka kwenye wizara zao, wakitaja mawaziri kadhaa.
Kutokana na ushauri huo maalumu kwa Kikwete, Spika na Pinda wametaka mawaziri wapya wateuliwe kwa kigezo cha umakini wao, sambamba na vigezo vingine, huku vyanzo vyetu vya habari vikieleza kuwa Kikwete ameahidi kuzingatia ushauri huo.
“Kuna ujumbe maalumu amepewa Rais Kikwete na viongozi waandamizi. Ni ushauri ambao unazingatia hali halisi na changamoto zinazoikumba Serikali ndani ya Bunge. Wameeleza kusikitishwa na mwenendo wa baadhi ya mawaziri na kwa kweli wamewataja kwa majina na kutoa mifano ya vitendo vyao ndani ya Bunge vinavyoashiria ama kuwa na uwezo mdogo katika kujibu hoja zinazoonekana kuishambulia Serikali au si wafuatiliaji wa masuala yanayohusu sekta zao.
“Spika ndiye kiongozi wa Bunge na Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, wanayo nafasi kubwa sana ya kuwapima mawaziri na naibu mawaziri, mapendekezo au ushauri wao ni muhimu sana na Rais ameonyesha kukubaliana nao,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Lakini wakati Spika na Pinda wakiwasilisha ujumbe huo maalumu kwa Rais Kikwete, vyanzo mbalimbali vya habari kutoka CCM vinabainisha kuwa, wito wa kuvunja baraza la mawaziri umemsaidia kwa kiasi kikubwa Kikwete ambaye anatajwa awali kuwa katika namna ya kutafuta njia ya kufanya mabadiliko hayo.
“Rais alikuwa na mpango wa kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa ni kama vile shinikizo hili limesaidia kufanikisha nia yake bila lawama kutoka kwa mtu yeyote wakiwamo hao mawaziri watakaoenguliwa,” anaeleza mtoa habari wetu.
Shinikizo la mabadiliko ya Baraza la Mawaziri msingi wake ni pamoja na ufisadi mkubwa kufichuliwa na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) wa Hesabu za Serikali, ufisadi ambao umekuwa ukijirudia karibu kila mwaka sasa.
Ni ufisadi huo kujirudia kila mwaka ndiko kulikomfanya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kabwe Zitto, kutoa wito kwa wabunge kutia saini fomu kwa ajili ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Zitto alifanikiwa kupata saini za wabunge 73 waliokuwa tayari kutaka Waziri Mkuu apigiwe kura ya kutokuwa na imani, hata hivyo, baadaye Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM ilikutana na kuazimia baadhi ya mawaziri kujiuzulu kutokana na kile kinachoelezwa kuwa mwenendo usioridhisha kiutendaji.
Baadaye Kamati Kuu ya CCM ilikutana na kuridhia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambayo yanatarajiwa kufanywa na Rais Kikwete wakati wowote.
Ni katika baraza hilo jipya, kumekuwa na wito wa kutaka ukubwa wake uzidi kupunguzwa kutoka idadi ya sasa ya mawaziri 31 pamoja na Waziri Mkuu.
Maoni ya Wasomaji
Kikwete haonyeki....
Kikwete haonyeki.....tusitegemee chochote kizuri toka kwake make kwa miaka hii mitatu alobakiza anaona ka ana cha kupoteza.....
kIKWETE NI CHAGUO LA MUNGU.......somo gumu kuelewaka lakini MUNGU alilzimisha tusome somo hili ifikapo wakati wa uchaguzi tutumie akili zetu vizuri kuchagua viongozi bora na si bora viongozi
Rais anayo mamlaka kamili ya
Rais anayo mamlaka kamili ya kuwajibisha au kuteua waziri wakati wowote atakapo dhibitisha ni sahihi kufanya hivyo,si kusubiri wabunge,wananchi au taasisi mbalimbali kupiga kelele.rais kusema kelele za wabunge zimemsaidia kukubali kuwawajibisha baadhi ya mawaziri intia shaka,inamaanisha kwamba bila kelele,shinikizo na kukejeliwa rais awezi kutumia mamlaka yake ya katibu,inatia shaka, swahiba mmoja amewahi kusema tuwe tayari kujukua maamuzi magumu.
Nakumbuka mara tu Mhe.
Tunawashukuru wabunge wetu
Tunawashukuru wabunge wetu kwa kupinga ufisadi uliokithiri kwa watendaji wakuu wa wizara na serikali za mitaa. Pia tunawapongeza kwa kukubali kutokuwa mafisadi kwa kujipatia posho kubwa. Tunawaomba wabunge wetu watumie busara zao kupigania tofauti ya kipato cha watanzania, manake kinatisha na muda si mrefu hali hii ikiendelea, italeta machafuko na kukosekana amani.
Kuwaondoa MCHWA na kuwatupa porini sio suluhisho, kwa sababu wataendelea kutafuna mazao waliyojilimbikizia na kwa kutumia nguvu ya pesa, kuendelea kuishi kama peponi. Tunaomba vyombo vya dola (kama vinafuatilia na kutekeleza majukumu yao), viwachukulie hatua za kuwashitaki na ikiwezekana kwa kuwafilisi mali zao kufidia ufisadi. Pahala salama zaidi kwao ni KEKO au SEGEREA.
Kama mfanyakazi (waziri
Kama mfanyakazi (waziri/mkurugenzi) katika duka lako (wizara/idara) ataanzisha duka kubwa (miradi binafsi, pesa nyingi BANK) kwa kukuibia wewe kwa ujanja na kufisha ushahidi wa kumhusisha moja kwa moja, je sio haki (polisi/TAKUKURUU) kumshitaki kwa kuwa amejipatia mali isivyo halali?
huyo moja kwa moja anapaswa
huyo moja kwa moja anapaswa kuchukuliwa sheria kali, tatizo la watanzania wengi tunafanya mambo kimasihala.Uchaguzi wa viongozi na hata upigaji kura wote umejaa masihala
when the rightous person is
when the rightous person is in authority people rejoice and the opposite is true