AWALI napenda nikiri huwa nafurahia makala za Privatus Karugendo kwani huwa anachambua masuala kwa kina.
Hivyo basi makala yangu hii haikusudii kumdhihaki wala kumdhalilisha kwa kiwango chochote kile. Ninaamini alitoa mawazo yake kwa nia njema kabisa.
Hata hivyo, nia njema pekee haimhakikishii mwanadamu kwenda peponi au paradiso. Lazima pia atende matendo mema, apime athari zinazoweza kutokea kutokana na kauli au matendo yake hata akiwa ameyatoa au kuyatenda kwa nia njema kabisa.
Katika toleo la Raia Mwema la wiki mbili zilizopita Privatus aliongelea suala la mashoga lakini hoja yake kuu ni kwamba suala hili linaweza kuongeleka katika jamii ya Kitanzania.
Kuna hoja nyingine alizotoa ambazo ni pamoja na kuwalaumu wale wanaowashambulia waliotoa jukwaa kwa mashoga kujitambulisha na kutoa madai yao. Pia aliwashangaa wale wanaoupinga ushoga kwa madai kwamba baadhi wakiwamo na viongozi ni wateja wa biashara hiyo.
Kabla sijajikita katika kujadili athari zitokanazo na kauli za kuchochea ushoga na matendo kama hayo ningepende kuonyesha udhaifu wa hoja za Privatus.
Kwamba suala hili linaweza kuongeleka na jamii ya Kitanzania: yeye mwenyewe ni shahidi ya kuwa jamii ya Kitanzania haipo tayari kujadili masuala haya. Ndiyo maana anajaribu kuishawishi jamii ibadilike.
Nimpe mfano huu: hivi hao wakurugenzi wa TNGP wanaotajwa wanaweza kwenda maeneo ya kwao wakaitisha mkutano na hoja yao ikawa HAKI ZA MASHOGA? Kama hawawezi (na mimi naamini hawawezi) basi ni ushahidi tosha jamii ya Kitanzania haiko tayari kujadili ushoga.
Mfano wa pili: hebu fikiria kama CHADEMA, CUF au CCM wangekwenda Igunga na ilani ya uchaguzi inayotoa ahadi ya kuboresha maslahi na haki ya mashoga! Nahisi hata uchaguzi wenyewe usingefanyika! Kama suala la mtandio limefanywa ni hijab, watu wakanyimana kura, wakaitana majina mabaya na wakatoana ngeu, ingekuwa vipi kama mmoja angekuja na ilani ya aina hii?
Kutokuwa huku tayari kwa jamii si kosa wala si ulimbukeni au kutokwenda na wakati. Hii ni haki ya msingi ya kila jamii tokea dunia iumbwe. Ni kosa na ulimbukeni mkubwa kulazimisha jamii ijadili suala ambalo jamii hiyo haipo tayari kulijadili hasa ikiwa jamii husika inafanya hivyo ili kulinda mila nzuri, desturi nzuri na imani bora.
Hoja kwamba TNGP wasilaumiwe nayo haina mashiko kutokana na sababu nilizoeleza hapo juu; hebu fikiria wanakijiji wameitisha mkutano kujadili ukame unavyoathiri mazao yao shambani, halafu anafika kiongozi au mwanaharakati anawaomba baada ya kikao wabakie kumsikiliza kwa kuwa ana mada muhimu ya kuwaeleza.
Wanakijiji wanakubaliana naye; mwanaharakati au kiongozi yule anaanza kwa kuwaeleza amekuja kutafuta wasichana warembo wa kushiriki Miss Tanzania!
Wanakijiji wanakuja juu na kumlaumu mwenyekiti wao kwa kumpa nafasi kiongozi au mwanaharakati yule kupoteza muda wao kujadili jambo lisilokubalika pale kijijni.
Halafu anapita jamaa mmoja anawaambia wasimlaumu mwenyekiti kwani suala la urembo linajadilika! Nani hana uelewa (nasita kusema hana akili kwa kuwa na mheshimu Privatus) kati ya hawa? TGNP wanastahili kulaumiwa tena kwa nguvu zote; uanaharakati wa haki za binadamu isiwe tiketi ya kutuletea mijadala ya hovyo kama hii.
Hoja kwamba tusikemee ushoga kwa kuwa viongozi ni wateja wa biashara hii ni dhaifu mno; kwanza usahihi wa takwimu au hoja hii haujulikani. Pili, hata kama ni kweli hadi viongozi wakuu wa nchi, dini na vyama vya siasa ni wateja (mimi siamini hivyo) hii haiwezi kuwa sababu ya sisi wengine kukubali ushoga na tabia kama hizo.
Ikiwa hivyo akili ya kawaida itatutuma kutowachagua, kuwanya’ng’anya madaraka, kuhama vyama vyao vya siasa au nyumba zao za ibada (si dini). Hivi hatuna viongozi wazinzi? Wezi? Waliolewa madaraka? Waliotelekeza familia zao? Waliotelekeza watoto waliozaa nje ya ndoa? Wasema uongo? Wavunja sheria za nchi? Kama wapo (na mimi naamini wamejaa tele) basi nasi tulazimishwe kukubali uongo, wizi, kuzaa nje ya ndoa, ulevi wa madaraka, uzinzi na tabia kama hizo eti kwa kuwa kuna viongozi wanashiriki?!
Sasa nirejee kwenye athari za maneno na matendo japo nia njema. Kwanza ni muhimu tukaelewa mapana na marefu ya suala hili. Ushoga na usagaji si wawakilishi pekee wa makundi ya aina hii. Kuna watu waliobadili maumbile (transgender) pia.
Yaani wale ambao waliumbwa na Mwenyezi kuwa jinsi ya kiume au ya kike, lakini wakatamani jinsi isiyokuwa yao na wakaenda kufanyiwa operesheni kuwabadili jinsi waliyozaliwa (na mara nyingi kukulia) nayo!
Huwezi kukubali haki za mashoga ukaacha haki za makundi haya mengine. Ukikubali moja lazima ukubali yote, hakuna nusu nusu! Hawa wote (pamoja madada poa) siku hizi wanatambulika kama vulnerable groups. Kwenye makongamano ya kimataifa hasa ya kuhusu UKIMWI au Haki za Binadamu wanashirikishwa sana siku hizi.
Wenzetu wa Ulaya, Marekani na Amerika ya Kusini wameyatambua makundi haya kiasi kwamba ni nadra kuhudhuria mkutano ulio chini ya ufadhili wao bila kuwakuta wawakilishi wa makundi haya. Tena wanapewa kipaumbele kuliko makundi mengine! Wanatoa ushuhuda wanavyonyanyaswa na wanavyonyimwa haki zao hata kwenye nchi walizotambulika kisheria!
Kwa hiyo unapodai haki au kutambulika au mjadala juu ya mashoga ni vyema ukatambua haitaishia hapo; kuna makundi yataibuka na kudai ’na sisi’ je? Usipotambua ukweli huo kesho TNGP au wengine wataitisha ’jukwaa’ la transgenders au madada poa, watu watapinga na watu wazima wenye akili zao, waafrika weusi (kama au kupita sisi) watadai ’linajadilika’!
Tukiwamaliza hao wengine wataibuka (na wako wengi), kwa mfano, kuna kikundi Marekani kinaamini kujamiiana ni haki isiyopaswa kuzuiwa na mahusiano ya kifamilia! Eti kuwa binti hakumzuii baba kuzini na bintiye au kuwa kijana wa kiume si kipingamizi cha kutembea na mama mzazi! Hawa nao wakijitokeza hapa kwetu tutasemaje? Tuingize haki zao kwenye katiba? Hii si itakuwa katiba ya kiwendawazimu? Lazima tupime maneno na hoja zetu za sasa na athari zake za baadaye. Nia inaweza kuwa njema lakini matokeo yakawa mabaya kupindukia. Lets us not open the pandoras box!
Lakini twende mbele zaidi ya mijadala; tuangalie athari zinazoweza kutunyemelea huko mbele ya safari kama tutajiingiza katika harakati za kupigania haki za mashoga, wasagaji, transgender, madada poa na wengineo.
Nitatoa mfano: una binti yako, amekuja jamaa mwanaume kuposa. Kavaa suruali na shati na kaja na heshima tele na kwa kufuata mila zote za jamii (kwa mfano kule kwa watani zangu Wachagga anakuja na mkungu wa kupika machalari).
Mnamtazama yeye na ujumbe wake mnakubali posa. Hayawi hayawi mtoto anaolewa kwa harusi kubwa kwa kuwa michango imekusanywa mwaka mzima. Haooo, wanaondoka na binti yenu. Wanawazalia wajukuu wazuri; mara bwana anaingia kichwa kichwa tabia za Ulaya!
Anasema yeye tokea utoto alikuwa anajisikia kama msichana! Kwa kuwa ana pesa anaenda London anabadilishwa kuwa mwanamke! Mwanamke hasa hadi maumbile! Anaanza kuvaa kike akiwa huko huko!
Je, siku anarudi mtakwenda kumpokea mkwe? Je, huyu hajakiuka haki za mkewe, wakwe zake na jamii? Alipokuja kuposa mlimkubali kwa kuwa ni dume; sasa kabadilika! Si atakuwa si tu amepora haki yenu kama wazazi bali haki ya mke wake (mtoto wenu) na watoto zake (wajukuu zenu)? Kama alikuwa anajua yeye anatamani kuwa mwanamke mbona hakusema hivyo alipokuja kuposa? Yaani yeye ana haki ya kujibadili lakini sisi wengine hatuna ya kuendelea kuwa na mkwe au mume au baba mwanaume?
Mwisho kabisa ndugu Karugendo kumbuka haki yako wewe, mimi, yule na yeyote mwingine inakoma pale inapoathiri haki ya mwingine (bora haki hiyo iwe inakubalika na wengi).
Sisi kama jamii tunayo haki ya kuishi katika jamii isiyokuwa na vibaka, wezi, wabakaji, wasema uongo, walevi wa madaraka, watoa matusi, wavivu, mafisadi, wezi wa kura, majambazi, mashoga, wasagaji, transgender, madada na makaka poa, n.k.
Ni haki yetu kama jamii kwa utamaduni, mila, desturi na imani zetu zimetufanya wengi tuamini hivyo. Si haki kwa kundi dogo lilioamua kwenda kinyume cha haki hizi kulazimisha wengi wawatambue au wajadili maslahi yao.
Tafadhali zingatia kuwa nimetumia suala la haki ‘kukubalika na wengi’; hili ndilo la msingi. Ndiyo maana kule Afghanistan pamoja na kuwa uzalishaji wa madawa ya kulevya ni jambo lisilokubalika sehemu nyingi duniani, wao na serikali yao walibobea kwa miaka mingi kwenye kilimo cha ‘poppy’.
Juhudi zote za majeshi ya kigeni kuharibu zao hili zimegonga mwamba! Matokeo wanajamii wanagombana na kuuana kutokana na kutuhumiana kwamba jirani zao ndio wanaowataarifu maadui kuhusu kilimo hicho. Pia tunaelewa Waafrika wengi wanapenda kufuga; watafuga hata kama ni mjini, nyumba ya serikali, hata kama mifugo inaharibu nyumba zao na mazingira na hata kama sheria inakataza.
Wanafanya hivyo kwa kuwa jamii ya Kiafrika imekubali ufugaji. Kwa kawaida jamii haiwezi kuacha tabia au jambo lilokubalika na kutumika miaka dahari.
Lakini Mswahili huyo akihamia London halafu eti pale eneo la Picadilly akaanza kufuga bata, mbuzi, nguruwe, ng’ombe, n.k. jamii pale haitakubali si tu kwamba sheria za Uingereza zinakataza bali si utamaduni wao.
Akifuga mbwa na paka angalau watamwelewa kwa kuwa jamii yao inaamini mbwa na paka wanafugika mjini.
Mswahili huyo huyo akilazimishwa kufuga paka au mbwa pale Picaddily basi mbwa au paka huyo atakufa kwa njaa! Jamii anayotoka imeamua mbwa na paka lazima watembee kutafuta chakula!
Kwa mantiki hiyo hiyo, Mzaramo nae hawezi kuhamia Paris halafu akaanza kuvanga mdundiko mtaa mmoja hadi mwingine! Wafaransa watakataa na kumfungashia virago! Jamii yao haikubali mdundiko wala tabia ya kuzunguka mitaani ukipuliza bomba na kupiga vigoma!
Huku kwetu mdundiko umekubalika hadi tunapoteza watoto! Kule Bagamoyo, Kibiti na kwingineko wazazi wakiona fahari binti kuolewa na mpuliza bomba! Jamii imekubali!
Nahitimisha kwa kusema suala hapa si uzuri wa hoja au tabia bali ni kukubalika hoja au tabia hiyo katika jamii husika. Jamii yetu haijakubali hoja, isilazimishwe au kuaminishwa kuwa hoja hii inajadilika.
Aidha, wenye mawazo kwamba linajadilika watafakari madhara ya maneno na matendo yao kwa wengine na hasa vizazi vijavyo! Kwenye mchakato wa kujadili mkataba wa Shirika la Kazi la Dunia (ILO) kuhusu UKIMWI sehemu za kazi (ILO Recommendation 200 on HIV and AIDS and the World of Work) ni nchi mmoja tu ya Afrika ilisimama kidete kutetea makundi haya yaingizwe kwenye mkataba.
Nilipata fursa ya kumhoji mwakilishi wa Afrika Kusini (rafiki yangu wa siku nyingi); nilimwuliza ‘Komredi nyumbani kwako una mtoto wa kiume shoga au wa kike msagaji au aliyejibadili jinsi? Akaniambia hana! Nikamwambia ‘ungekuwa naye ndio ungejua madhara ya kuwa na mtoto kama huyo katika familia’! Alitahayari akapunguza munkari kwenye majadiliano!
Leo ningependa kuwauliza ndugu zangu wa TNGP, Ndani ya majumba yenu mnao watoto wa aina hii? Ndugu zenu wa karibu wanao watoto wa aina hii? Jirani zenu wanao? Nasubiri jibu!
Ni vyema watanzania wakatambua kuwa kuna makundi hasa NGOs za nchi za Magharibi yanajaribu kupenyeza utamaduni huu kwenye nchi changa.
Nyingi ya NGO hizi zinafanya hivyo kama njia ya kupata fedha kutoka serikali zao au mifuko ya hisani. Hawa wanaanzisha uhusiano na NGO za kwetu (si zote) ambazo nazo kwao hela ni hela! Wote hawa wanachumia tumbo!
Lakini zipo NGO mbaya zaidi huko kwa wenzetu; hizi nia yao haswa ni kuvuruga mila na tamaduni za wenzao! Wanajua, jamii isiyo na mila na desturi ni rahisi kuimiliki. Ukiwaambia wavae kaptura watavaa! Leo vaeni suruali zenye viraka watavaa! Kesho vaeni sidiria zilizotumika, watavaa! Wengine wanaufaika kiuchumi lakini baadhi yao nia ni kuharibu tamaduni za wengine, ndiyo starehe yao!
NGO zetu nazo zisifuate mkumbo. Hatari ni kwamba zitadharaulika hata pale watakapokuwa na hoja nzuri jamii itawapuuza.
Utamsikilizaje mtu au taaisi inayotetea mmomonyoko wa maadili? Hujui lini atageuka na kukutaka uunge hoja uozo huu; salama ni kuwa naye / nayo mbali iwe kwa jambo jema au baya.
Huwezi kuambatana kwenda msikitini na jambazi aliyefunga swaumu kwani hujui ataanza kuiba lini na wapi? Wala huwezi tabiri wanaowaona mkiwa pamoja njiani wanajua mnaelekea msikitini kusali au kama jamaa kafunga! Pia hauwezi kumshirikisha mzinifu kwenye kwaya ya Kanisa eti kwa kuwa Krismasi imekaribia! Kwaya ina mabinti na wake za watu na wazazi au waume zao hawatakuwa na uhakika na usalama wao!
Mungu akinijaalia nitafanya utafiti kidogo kwa kuwa nina taarifa kuna kikundi cha NGO ya Uholanzi mwaka 2010 wamemhamishia mhamasishaji wao mmoja nchini Tanzania.
Huyu ni mwanamama mwenye asili ya Afrika Kusini. Nitajaribu kujua hapo Dar es Salaam ofisi yao iko wapi na wanashirikiana na taasisi gani. Nikifanikiwa nitawaelimisha.
Kwa ndugu yangu Privatus, naheshimu sana uhuru wako wa kutoa mawazo, natumaini nawe utaheshimu uhuru wangu wa kutoa mawazo na nakushukuru kwa kuchochea mimi kuandika makala hii. Mungu atubariki na awaondolee wote mawazo na matendo yasiyokubalika katika jamii.
Mwandishi wa makala hii, Yahaya Msangi, anapatikana kwa emaili ya yahya.msangi@ituc-africa.org
Toa maoni yako