NIANZE makala hii kwa kuwatakia wasomaji wangu heri ya Christmas na mwaka mpya wenye baraka tele. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuhusu kuendelea kuwepo; si kwa ubora wetu bali kwa neema zake.
Hivyo basi kwa vile tumejaliwa bure bila hata kustahili, tuelekeze nguvu zetu zote katika upendo, amani na kuwahudumia jirani zetu.
Sasa tuanze tafakuri ndefu juu swali ambalo limekuwa likinisumbua kwa miaka mingi: Yesu wa Nazareti au Yesu Mkristu? Lengo la tafakuri hii si la kiimani wala kihistoria. Kila mtu anakaribishwa kutafakari pamoja nami.
Kila mtu anakaribishwa kutafakari juu ya mtu huyu Yesu Kristo aliyeishi karne ya kwanza kule Palestina, na kujaribu kumwangalia kwa macho ya karne ya leo katika mazingira ya Mtanzania.
Shauku yangu kubwa ni kumwangalia mtu huyu kabla ya kutekwa nyara na kutumiwa kama chombo na imani ya kikristu.
Tafakuri yetu haitaanza na imani katika Kristo, ingawa nafikiri hitimisho litakuwa hilo. Wala tafakuri yangu haina lengo la kuutetea Ukristu, hii ni dini kongwe ambayo inaweza kujitetea yenyewe. Pia sina lengo la kumtetea na kumlinda Kristo, maana yeye ana uwezo wa kujitetea mwenyewe.
Hata hivyo, tunaambiwa na wanafalsafa wa zamani kwamba ukweli hujisimamia wenyewe. Yesu alipobanwa juu ya ukweli ni nini, alikaa kimya ikimaanisha kwamba ukweli ni yeye mwenyewe!
Lakini ikitokea baada ya tafakuri yetu mtu akaamua kumfuata Kristo, nitakuwa sikumshawishi, bali atakuwa amegundua mwenyewe kwamba Kristo ni njia ya wokovu. Maana tunasikia katika Injili ya Yohana kwamba Ukweli utatuweka huru: Yohana 8:32.
Katika tafakuri yetu tutajikita zaidi juu ya Yesu wa kihistoria. Lakini pia lengo letu kubwa si huyu Yesu wa kihistoria. Hatutafakari kutuliza kiu ya tafiti nyingi za kisomi zilizofanyika juu ya Yesu Kristo. Lengo kubwa la tafakuri hii ni mahitaji muhimu na ya haraka.
Ni mahitaji ya kutafuta mfumo wa kupambana na matatizo yanayomzunguka mwanadamu wa leo. Mamilioni ya watu wanaishi kwenye mateso kila siku ya Mungu. Kuna njaa, vita, umasikini, upweke, magonjwa, uonevu na ubaguzi. Hapa Tanzania, watu wanakufa kwa Ukimwi, Malaria na magonjwa mengine yanayotibika. Ujambazi, ufisadi, rushwa na kutowajibika vinasambaratisha uchumi wetu.
Idadi ya wajane na wagane inaongezeka kwa kasi, watoto yatima, watoto wa mitaani (japo baba zao si mitaa) na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi inaongezeka kwa kasi ya kutisha. Lengo na tafakuri hii ni tufanye nini kuondokana na mateso na mambo mengine yanayotishia uhai wa mwanadamu na hasa Mtanzania.
Mamilioni ya watu kwa miaka mingi wamekuwa wakilitaja jina la Yesu na kumwabudu, lakini wachache kati ya mamilioni ndiyo waliomuelewa Kristo na namba chache kabisa ndiyo waliofuata kile alichokitaka kitendeke.
Maneno ya Yesu Kristo, yamebadilishwa na kupindishwa ili yatekeleze kile watu wanachokitaka, na wakati mwingine maneno yake yamebadilishwa na kupindishwa yasimaanishe kitu chochote!
Jina la Yesu, limetumiwa kubariki maovu ya kila aina, kama wale waliokuwa wakiongoza vita na kuua watu huku wakitanguliza msalaba na Biblia Takatifu. Latini Amerika, mamilioni ya watu walipoteza maisha yao na sehemu nyingine kizazi kilifutika kabisa katika harakati za kueneza neno na mafundisho ya Yesu Kristo.
Lakini pia jina la Yesu, limetumiwa kuwashawishi na kuwaletea imani kubwa wanaume na wanawake wengi hata kufikia hatua ya kupumbazika na kufanya matendo ya kijinga, kama kujinyima chakula na kuitesa miili yao kufikia kiwango cha uwendawazimu.
Yesu amekuwa akitukuzwa na kuabudiwa kwa yale ambayo hakuyalenga, yale aliyoyapinga na kuyakemea kuliko yale aliyoyalenga, aliyoyahubiri, aliyoyatetea na kuyafia. Jambo la kushangaza ni kwamba mambo ambayo Yesu aliyapinga wakati wa uhai wake, yalifufuliwa, yalihubiriwa na kusambazwa dunia nzima kwa jina lake.
Hatuwezi kumuunganisha moja kwa moja Yesu wa Nazareti na hii dini kubwa ya kizungu, inayojulikana kama Ukristu. Yeye alikuwa mwanzilishi wa dini kubwa zaidi ya hii tunayoifahamu. Anasimama juu ya Ukristu na kutoa hukumu juu ya yale yote dini hii imeyafanya kwa jina lake.
Hata hivyo Ukristu, hauwezi kudai ni mmiliki wa Yesu Kristo, maana mtu huyu alikuwa ni wa binadamu wote.
Je, hii ina maana kwamba kila binadamu (Mkristu na asiyekuwa Mkristu) ana uhuru wa kumtafsiri Kristo katika maisha yake jinsi anavyotaka? Inawezekana kabisa kila mtu akamtumia Kristo anavyotaka kwa mabaya na mazuri?
Lakini yeye alikuwa ni mtu aliyekuwa na imani nzito ambayo alikuwa tayari kuifia. Je, hakuna namna ya watu, wenye imani na wasiokuwa na imani kumpatia nafasi katika maisha yao Yesu huyu wa Nazareti, akazungumza yeye mwenyewe kwenye mioyo yao? Je, hakuna namna ya watu kulinganisha matatizo yao, nyakati zao na zile za Yesu wa Nazareti?
Hivyo tafakuri yetu inaanza na matatizo mengi yanayoisumbua dunia ya leo. Tishio lililopo leo si la mtu binafsi, kabila, taifa au bara. Tishio ni la dunia nzima, ni tishio la ubinadamu. Tumefika mahali tunachanganyikiwa na kufikiri kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuzuia tishio la kuumaliza ulimwengu na binadamu.
Wapo vichaa kama Kibwetere na wajinga wengine wanaofikiri kwamba mwisho wa dunia na ubinadamu vinashuka kwa miujiza, kwamba tunaweza kulala na kuamka tunakuta dunia imekwisha. Huu ni ujinga mtupu! Mwisho wa dunia, unaletwa na matendo ya binadamu ya muda mrefu.
Matendo ya ubinafsi yasiyozingatia umuhimu wa binadamu na viumbe vingine, yanaweza kupelekea mwisho wa dunia. Hili si jambo la kutokea leo ama kesho, lakini mtu anayejali ni lazima kuhakikisha anarithisha dunia hii kwa vizazi vijavyo. Tunakata tamaa kwamba hakuna tena mfumo mzuri wa maisha unaowafaa binadamu wote. Mfumo wa kuweza kuangalia na kutengeneza maisha bora ya mwanadamu wa leo na kesho.
Siku za nyuma kidogo tulifikiri labda silaha za nyukilia zingeweza kutumika kuteketeza ulimwengu. Tumeanza kupunguza woga huu, lakini mambo mengine mengi kama vile uharibifu wa mazingira, uchimbaji ovyo wa madini, upungufu wa chakula na ardhi nzuri ya kustawisha chakula, hatari ya kupungua kwa maji na ongezeko la binadamu, ni vitisho vipya kwa uhai wetu na ulimwengu tunamoishi.
Ukweli kwamba binadamu wanaongeza kwa kiasi cha milioni 80 kwa mwaka, ni tishio kwamba kwa miaka michache ijayo, matumizi ya maji na chakula yatakuwa katika hali mbaya duniani kote. Ukweli kwamba magazeti, vitabu na utengenezaji wa karatasi za kuandikia unaitafuna misitu ni tishio la uharibifu wa mazingira katika enzi hizi tulizomo.
Kuna uharibifu mkubwa katika kila biashara zinazofanywa kwa lengo la kupata faida. Viwanda vingi vimekuwa vikiharibu mazingira kwa moshi unaotoka viwandani, lakini pia uchafu unaotiririshwa kutoka viwandani kwenda mitoni na kwenye maziwa na bahari umechangia uharibifu mkubwa wa viumbe katika maji. Ni wazi ili tupone, panahitajika mabadiliko makubwa. Swali ni je, nani atakubali hasara ya kusimamisha viwanda vyake?
Inakuwa vigumu kuwashawishi watu kubadili mtindo wa maisha, ili kurefusha maisha yao wenyewe, inakuwa vigumu zaidi kuwashawishi kufanya hivyo ili kuyarefusha maisha ya watu wengine. Inakuwa vigumu zaidi na zaidi kuwaambia kufanya hivyo kwa lengo la kunusuru maisha ya mabilioni ya watu ambao bado hawajazaliwa.
Kuna ukweli kwamba dunia hii ina baadhi ya watu, wake kwa waume wenye nia njema, na wanayaona matatizo yote hayo na wangependa kufanya chochote kuleta mabadiliko. Lakini wanaweza kufanya nini?
Mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache kinaweza kufanya nini kwenye matatizo haya ya ulimwengu wa kisasa? Kilicho mbele yetu ni kitu kikubwa, ni mifumo ya dunia hii iliyojikita na kustawi! Ni mifumo ya ubepari, soko huria na utandawazi. Mara ngapi tunasikia kilio cha watu kwamba mtu hawezi kupambana na mifumo?
Hili ndilo tatizo kubwa. Tumejijengea mifumo ya siasa na kiuchumi kwa kuzingatia mambo fulani fulani, ambapo sasa tunaanza kutambua kwamba mifumo hii italeta maafa kwa dunia nzima.
Ni kama tumefungwa mikono na miguu, kiasi tunashindwa kubadilisha mifumo na inafika mahali hakuna kinara katika kuisimamia na kuiendesha.
Jambo la kushangaza ni kwamba uharibifu wa mifumo hii hautambagua mtu yeyote. Mfano uharibifu wa mazingira unaoendelea kuongeza joto duniani, hautabagua matajiri na masikini, mataifa makubwa na madogo. Utatuangamiza sote!
Maoni ya Wasomaji
Zi wapi hekima za zama hizi
Zi wapi hekima za zama hizi?hakika hekima za wanadamu ni UPUMBAFU mbele Mungu muumba!!.