Makala
TAKUKURU wanatuchezea akili na uchunguzi wao wakati wa uchaguzi
Lula wa Ndali Mwananzela
Toleo la 227
22 Feb 2012

SIJUI kwa nini wakati mwingine tunakuwa na matumaini sana na uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Kwamba watu wanaamini kuwa TAKUKURU inauwezo wa kupambana na rushwa zinazohusisha wagombea wa kisiasa. Tumesikia – kwa mara nyingine tena – kuwa taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa havitokei kwenye uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.

Wapo wenye kuamini kuwa kauli hiyo inamaanishwa na wakuu na watendaji wa taasisi hiyo.

Uchaguzi wa 2010

Kwa wale wanaokumbuka Uchaguzi Mkuu wa 2010, bila shaka wanakumbuka vizuri jinsi vitendo vya rushwa vilivyokuwa vimeshamiri sehemu mbalimbali nchini huku baadhi ya wanasiasa wakongwe wakihusishwa na vitendo hivyo.

 Wengine walitangazwa kabisa kuwa wamekutwa katika mazingira ambayo yalionesha kuwa wanapanga vitendo vya rushwa na kati yao walifanikiwa kushinda uchaguzi na wengine kuteuliwa kuwa mawaziri.

Siyo tu kwenye uchaguzi wenyewe lakini kwenye teuzi za vyama na katika kampeni kulikuwa na vitendo vingi ambavyo viliashiria ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uchaguzi lakini taasisi hiyo iliishia kuzungumza kwa ukali tu. Miaka miwili sasa baadaye hakuna mwanasiasa yeyote mkubwa au chama chochote kikubwa ambacho kimetajwa kuhusika na vitendo vya rushwa.

Hitimisho tulilonalo ni kuwa hakukuwa na vitendo vya rushwa na kama vilikuwepo havikuwa vikubwa hivyo vya kuweza kunaswa na makachero wa TAKUKURU.

Uchaguzi mdogo wa Igunga

Kama kuna wakati mwingine ambao watu walio na imani na Serikali wangedhania kuwa TAKUKURU ingeweza kufurukuta ni kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga. Hakuna uchaguzi uliofanywa katika mazingira ya hatari, ya kibaguzi na rushwa katika miaka ya karibuni kama uchaguzi wa Igunga.

Lakini kama kawaida taasisi hii ikaja na lugha yake ya vitisho na “mikwara mbuzi” huku wenye kuhofia wakiwa wao wenyewe na siyo wanasiasa.

Hata baada ya kundi la mabalozi wa CCM kudai rushwa kubwa imetumika, TAKUKURU hawakufanya lolote.

Tulishuhudia jinsi Waziri, Dk. John Magufuli akitumia nafasi yake ya kisiasa kwenda kupigia chama chake debe kinyume cha sheria ya uchaguzi. TAKUKURU hata uwezo wa kumuuliza au kumkaripia hawakuwanao! Tunakumbuka jinsi CHADEMA walivyoandika barua kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi (nakala kutumwa TAKUKURU) ikilalamikia vitendo vya mmoja wa viongozi wa CCM aliyekuwa akigawa fedha maeneo ya Igunga na kutuhumiwa rushwa lakini kama kawaida, TAKUKURU ilichezacheza patapotea na uchaguzi ukaenda kama kawaida!

TAKUKURU ni sehemu ya tatizo

Ndugu zangu, TAKUKURU ni sehemu ya tatizo la kupambana na rushwa nchini. Ni taasisi ambayo imekaa kisiasa zaidi kuliko kiweledi. Imeundwa ili kuwalinda watawala na watawala wananufaika nayo.

 Pamoja na mabadiliko yote ya sheria taasisi hii haina ubavu wala uthubutu wa kupambana na watu wanaochafua demokrasia nchini.

Watu ambao wanaharibu mchakato wa wananchi kutumia haki yao kujichagulia viongozi wanaowataka bila kurubuniwa na fedha au kuzuiwa na wenye fedha!

Ni taasisi ambayo ni tatizo kwa sababu bado inasimamiwa toka juu. Muundo wa taasisi hii ni mbaya katika mapambano ya rushwa.

Matokeo yake amri na maagizo yanaingiliwa sana na yanahitaji mnyororo mrefu wakusimamiwa huku madaraka makubwa yakiwa kwa mkurugenzi wa taasisi hiyo.

Matokeo yake makamanda walioko chini nao wanaangalia nafasi zao za kwenda juu.

Kutotumia teknolojia ya kisasa

Kati ya vitu vinavyoshangaza sana ni kuwa leo hii nchi yetu inashiriki katika matumizi ya teknolojia mbalimbali ambazo zingeweza kabisa kutumiwa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Inashangaza zaidi ni jinsi gain hakuna makachero wa siri (undercover agents) ambao wangeweza kupenya kwenye vyama hivi vya siasa na taasisi hizi kuweza kunasa wanaopanga na kutekeleza vitendo vya rushwa. Hadi leo hii TAKUKURU imeshindwa kutumia ushahidi wa mazungumzo ya simu au rekodi za video kuwanasa wanaotoa rushwa.

Kwa nini? Kwa sababu wakianza kutumia teknolojia ya namna hiyo watakamata wengi na hatua hiyo inaweza kutikisa Serikali. TAKUKURU imekataa kwa makusudi kutumia teknolojia hiyo kunasa mafisadi watoa rushwa kwa sababu inaogopa. Fikiria kama siku moja waziri au mkurugenzi anaonekana akikatiwa asilimia kumi yake au akibembeleza agawiwe gawio la ufisadi kama atapitisha mkataba fulani au kuwezesha jambo fulani lifanyike. TAKUKURU wanaogopa hili. Wangeweza kabisa kuwakamata wanaotumia rushwa kwenye uchaguzi kwani hawa ni rahisi sana kuwanasa kwa kutumia teknolojia – lakini itakuwaje kama wataonekana ndio vigogo wenyewe wa nchi?

Jibu ni rahisi. Wananchi waanze kutumia simu zao na kamera zao kuanza kuwanasa waharibifu hawa wa demokrasia na sisi kama waandishi na vyombo vya habari tutawafichua pasi na shaka.

 Nawasihi Watanzania waanze wao wenyewe kufanya kazi hii ya kupambana na watoa rushwa – wasiitegemee TAKUKURU kwani ni taasisi iliyoshindwa ambayo hatima yake ni kuvunjwa na wakuu wake wengine kufikishwa mahakamani! Ni taasisi mbovu, imeundwa na sheria mbovu na inafanya kazi kwa ubovu unaolindwa na watawala. Watanzania waanze kuchukua sheria mkononi kwa kuwafichua watoa rushwa!

Waandishi wa habari wana nafasi kubwa zaidi. Waandishi waache kuitegemea TAKUKURU. Kama waandishi wanataka kusaidia kujenga demokrasia ni jukumu lao kufichua ufisadi wakati wa uchaguzi. Waandishi waende chini kwa chini (undercover) katika vyama hivi na kunasa –kwa sauti, picha na video- wenye kutoa rushwa na kuwafichua kwenye vyombo vya habari na mitandao ya jamii. Kwa vile TAKUKURU imeshindwa basi vyombo vya habari ambavyo ndio wasimamizi wa watawala vinatakiwa kufanya kazi hiyo.

Lakini waandishi wakiwa wavivu na waoga kufanya hivyo vyama vya siasa vyenyewe vianze kufichua. Haitoshi tena kutuambia kuwa “kulikuwa na rushwa” wakati umefika wa kuwapiga picha, kuwa rekodi na kuwafichua watuhumiwa wa rushwa ili TAKUKURU ifanye kazi yake. Kama kuna watu wananunua shahada za uchaguzi waanze kukamatwa wakifanya hivyo. Tusipoanza kupambana na rushwa sisi wenyewe, hawa TAKUKURU wataendelea kutuchezea akili kwa maneno matamu na hadithi za hapa na pale.

Kwa ufupi, tusiiangalie taasisi hii katika kuzuia rushwa kwenye uchaguzi. Tayari tunajua hawawezi, wameshindwa na hawatoweza kwa sababu wenyewe, baadhi yao wanakula humo humo!

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Lula wa Ndali Mwananzela
lulawanzela@yahoo.co.uk

Toa maoni yako