Tanga jamani, itarudisha heshima yake ya soka?

TANGA ni miongoni mwa mikoa yenye historia kubwa na soka la Tanzania. Ni ngumu kuizungumza historia ya soka la Tanzania, bila kuutaja mkoa wa Tanga ambako waliwahi kupita wachezaji wakubwa na kucheza hadi timu ya timu ya taifa Tanzania (Taifa Stars).

Pia wachezaji kadhaa wa mkoa huo kuchezea  klabu kongwe za Simba, Yanga za Dar es Salaam  baada ya kuwika katika klabu zao za Tanga za African Sports na Coastal Union.

Historia yetu ya soka haijawaacha Tanga, japo wana Tanga wenyewe wanaonekana kutojali na hali waliyonayo sasa kwenye medani ya soka.

Taifa Stars ya mwisho kushiriki fainali za  Mataifa Afrika ilikuwa mwaka 1980 nchini Nigeria na  Tanga ikitoa mchango wake kupitia kwa Mohamed Salim na Salim Amir katika timu hiyo.

Na hata nyota wa wakati wote wa Stars, Peter Tino ‘Samjo’ alishiriki fainali hizo akitokea kwenye klabu ya Tanga ya African Sports.

Historia ya soka letu inawabeba Tanga kuliko mikoa mingi hivi sasa ambayo inafanya vyema katika medani ya soka.

Licha ya historia kuwa upande wao, lakini ni hali ya kawaida hivi sasa kutoona hata timu moja ya mkoa huu ikishiriki michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mapumziko yangu ya Sikukuu ya Pasaka nilikuwa mkoani hapa na nilitumia muda huo kuwatafuta mashabiki, wadau na viongozi wa soka kuzungumza nao ni kwanini soka la Tanga limekuwa na sura hii iliyonayo sasa.

Asilimia kubwa ya wadau hao walisema Tanga watu hawapendani ndiyo maana hali hiyo imejitokeza, hivyo si kweli kwamba mkoa huo hauna vipaji.

Mmoja ya wadau, Athuman Juma alisema ndani ya mkoa wao, soka limekuwa halipendwi kutokana na chuki zilizoko kwa kila mmoja dhidi ya mwenzake na hicho ndicho kinachofanya mpira wa mkoa wao kushindwa kupiga hatua.

“Ndugu mwandishi, sisi tunapenda sana mpira wa miguu, lakini kubwa ni sisi wenyewe kutopendana baina yetu na hali hii imesababisha hata mpira wenyewe kuchukiwa na kutokuwa na hamasa kama ilivyokuwa zamani.

“Tunahitaji kuungana pamoja kama mkoa ili kurudisha heshima yetu, lakini mnaweza kukubaliana hivi kwa sauti moja mkiwa ndani ya vikao, ila kuna watu wakitoka nje  ya kikao hicho wanasema mengine, sasa hiki si kitu kizuri na ndiyo kinauua mpira wenyewe,” alisema Juma.

Mmoja wa mdau aliyeonekana kuwa wa zamani katika soka la Tanga, Usi Mohamed alisema hamasa imeshuka kwa kiwango kikubwa ndani ya mkoa wao kutokana na ubinfasi wa hali ya juu uliotawala.

Alisema hivi sasa haoni hata raha ya kwenda uwanjani kutazama mpira kutokana na kukosa ladha nyingi ambazo zamani zilikuwepo.

“Hapa (Tanga) kwanza ukisikia mechi ya African Sports na Coastal Union kunakuwa na mpira mwingi unaochezwa na wachezaji wa pande zote mbili na vituko vya kila aina vilivyokuwa vinachangamsha na kuleta hamasa kubwa ya soka letu.

"Sasa hiyo ladha ambayo tulikuwa tukiipata zamani mpira ulipokuwa kwa watu wenye weledi, lakini hivi sasa ubinafsi na ujuaji umetawala kwa kiwango kikubwa na hiki ndicho kilichoufanya mpira wa Tanga ufikie hapa ulipo,” alisema Mohamed.

Mdau mwingine Bi Ashura Issa, alisema hajui kama hata Tanga kwenyewe kama kuna mpira siku hizi. Bibi huyo aliyekuwa akizungumza kwa tahadhari alisema wao waliozaliwa zamani wameona mafanikio ya Tanga kwenye soka, lakini vijana wa kisasa ndiyo wamechagia mpira wa Tanga kushuka kwa kiwango kikubwa.

“Zamani hakukuwa na masuala ya usomi kama ilivyo sasa na mafanikio yalikuwepo tofauti na sasa watu wanaleta masuala ya usomi kwenye soka. Mimi kwanza siku hizi sijui hata kama kuna mpira wenyewe ambao unachezwa. Nilishaacha kwenda uiwanjani siku nyingi tu baada ya kuona hakuna mwendelezo mzuri wa mkoa wetu.

“Enzi zetu tulishuhudia mafanikio ya soka la Tanga, lakini vijana wa sasa wanashuhudia mifarakano ya soka la Tanga. Ukitaka kuamini soka letu lina matatizo tazama tumeshusha timu zetu tatu kwa wakati mmoja katika mikimikimiki ya Ligi Kuu Bara, sasa ukishaona vitu kama hivyo hapo lazima kuwe na tatizo hapo,” alisema bibi huyo aliyekuwa akizungumza kwa uchungu.

Baada ya kuzungumza na wadau hao mbalimbali, Raia Mwema ilimtafuta Mwenyekiti wa soka Mkoa wa Tanga, Said Soud kuzungumza naye juu ya hali hiyo na mambo mengine aliyopanga kufanya ndani ya uongozi wake kuhakikisha heshima ya Tanga katika medani ya soka inarejea upya.

Soud alisema peke yake kama (kiongozi) hawezi kuufanya mpira wa Tanga uweze kupiga hatua na kusema juhudi za watu wote wa Tanga zinahitajika. Aliendelea kusema kuwa mpira ni mchezo wa kushikamana pamoja ndiyo mnaweza kusonga, sasa kikubwa wanachotakiwa kuwa nacho watu wa Tanga ni kushikamana pamoja na hiyo ndiyo kipaumbele chao.

“Kikubwa hapa ni kushikana pamoja na kuachana makundi makundi ambayo ndiyo yamechangia mpira wetu kuwa hivi. Binafsi kama Soud siwezi kuwa na maajabu kama nitakosa ushirikiano wa wakazi wa mkoa. Tunahitaji kujiunga pamoja ili tukifanikiwa tufanikiwe pamoja na tukishindwa tushindwe pamoja, lakini sio kila kitu aachiwe Soud peke yake,” alisema kiongozi huyo.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa ndani ya mkoa kulikuwa na makundi ambayo ameyataka kuwa pamoja na waujenge mpira wa Tanga. Sitaki kuamini kama Tanga hakuna vipaji vya soka. Hivi sasa tuna wachezaji kama Hamad Juma  (anayechezea Simba) na Juma Mahadhi (Yanga). Sasa unaweza kuona tuna vipaji, lakini tunaangushwa na makundi yetu ambayo hivi sasa yavunjike na tuujenge mpira wetu kwa pamoja.

“Kama tukishakuwa pamoja sidhani kama tutashindwa kufanya kitu kizuri cha kumpendeza kila mwana Tanga na kila Mtanzania anayependa mpira wa miguu,” alifafanua Soud.

Soud alikwenda mbali na kusema licha ya majukumu makubwa waliyonayo kama viongozi wa soka Tanga, lakini wanahitaji nguvu ya serikali ya mkoa kuwaunga mkono kwenye mambo mbalimbali.

Alieleza mikakati yao kama uongozi ni kuungwa mkono na serikali katika kuuinua upya mpira wa Tanga na kama hilo likifanikiwa haitachukua muda mrefu watarudi kwenye kilele cha mafanikio kwa nguvu kubwa. “Mipango yetu ni kuwa na timu nyingi za vijana kuanzia umri wa chini kabisa ndiyo maana hapa tunaihitaji na nguvu ya serikali kwenye soka.

“Tunawahitaji kwenye masuala ya uwanja na wachezaji wenyewe ambao wengi watakuwa ni wanafunzi. Mipango yetu kama uongozi ni kuwa na timu za soka la vijana kuanzia miaka 12-17, 17-20 ambako wachezaji hawa lazima watoke huko mashuleni.

”Ukishamkuza mchezaji huyu kuanzia chini mpaka juu ni rahisi kuwa na mchezaji aliye tayari kupambana na akishakuwa na ubora mkubwa unamuuza kwa ajili ya kuja kuwaanda wachezaji wengine ambao watakuwa wakichipukia.

“Kama kila kitu kikienda vizuri, sioni sababu ya soka la Tanga kutofanya vizuri, lakini kubwa na la kusisitiza ni kuhitaji kuungana pamoja kwa wakazi wote wa Tanga,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *