Krismasi imewadia. Na mwaka nao tunakaribia kuumaliza. Ni kipindi cha kushehereka na kutafakari. Maana nchi yetu nayo imetimiza nusu karne.
Tunaumaliza mwaka huku hali ya uchumi wa dunia ikiwa tete. Na sisi kama nchi tunaathirika zaidi kiuchumi. Kuathirika huku kiuchumi kunatokana na sababu za nje na za ndani.
Sababu za nje hatuwezi kuwa na uwezo nazo. Lakini za ndani zinatutaka sisi wenyewe tufanye jitihada za kurekebisha mapungufu yetu.
Mfumuko wa bei umepanda sana wakati huu tukielekea mwisho wa mwaka. Bei za vyakula zimepanda sana. Hali ya mwananchi wa kawaida imekuwa ngumu zaidi kiuchumi. Tumeona pia, kuwa matokeo ya mitihani ya darasa la saba yamewaacha karibu nusu ya watoto wetu bila hakika ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Tumeona pia kuwa vijana wengi wanaomaliza elimu ya sekondari hawapati nafasi katika soko la ajira. Hizi zote ni baadhi ya changamoto zinazotukabili kama Taifa. Zinahitaji juhudi za pamoja katika kukabiliana nazo, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi.
Na mapungufu ya ndani yanachangiwa na baadhi ya tuliowapa dhamana za ongozi kukosa mioyo ya uzalendo. Ni watu wenye kutanguliza ubinafsi zaidi. Hali hii imesababisha kuwafanya Watanzania wengi kukata tamaa.
Kuna wakati nilipata kupokea barua kutoka kwa Mtanzania anayeishi Ujerumani. Barua hii ilinigusa sana. Nitaweka hapa mwanzo tu wa barua husika, kisha nitayasema yangu.
Namnukuu mwandishi wa barua;
“Salaam!
Kaka yangu Mjengwa,
Tangu kuelewa kwangu ubovu huu wa serikali ya Tanzania nimekuwa nikilia kila siku ingawa mtu mzima machozi ni ngumu kutoka. Najipa moyo haya matatizo yataisha siku moja lakini naona sasa nakata tamaa. Hakuna uafadhali na kila siku zikienda ndio kwanza ufisadi unaimarika na mafisadi wanazaliwa pia.
Najiuliza kuna mwisho wa haya? Au natakiwa nifanyeje niache kulia? Niko Germany lakini huwa naona aibu nikiulizwa unatoka wapi?”
Kwanza kabisa, mwandishi wa barua na sisi sote, hatupaswi kuliona hili katika sura ya Serikali tu. Inahusu matendo yetu na wajibu wetu kama raia tuliozaliwa katika nchi hii.
Naamini, kuwa nchi yetu ni tajiri sana, lakini watu wake ndio masikini sana. Ni wachache tu ndio wenye kunufaika na utajiri wa nchi yetu. Na jambo hilo hatupaswi tukaliacha liendelee. Leo kuna watu wana muda wa kucheza densi wakati kuna watoto wetu kule Songosongo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha huku eneo wanaloishi kuna wawekezaji wenye kuvuna gesi yetu na kujitengenezea faida kubwa, tena kwa kukwepa kulipa kodi.
Na mkataba wao wa kuvuna gesi? Ni miaka 25! Robo karne nzima. Hao Watanzania wenzetu walioshiriki kuingia mikataba hii ya kifisadi huenda hawatakuwepo duniani baada ya robo karne ya wawekezaji kuchota na kukwangua gesi yetu asilia.
Rasilimali zetu tumeacha zisimamiwe na baadhi ya Watanzania wenzetu wenye hulka za mbweha. Ni watu wabinafsi na wasio na huruma kwa Watanzania wenzao.
Ndiyo maana tunasikia kila kukicha kashfa zinazofuatana; Rada, Richmond, IPTL, EPA, Meremeta na nyinginezo nyingi. Ni kashfa zinazowafanya wachache wameremete huku wengi wakifubaa kwenye lindi la umasikini.
Ndio, msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu. Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao.
Watanzania wengi sasa wanapoteza moyo wa uzalendo kwa nchi yao. Kuna hata wenye kufikia kutamka; 'Nchi hii ina wenyewe'. Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali. Hizi si dalili njema kwa Taifa.
Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa. Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao. Ni hatari.
Tuna lazima ya kuwa na ujasiri wa kupigania maslahi ya nchi yetu. Nimepata kuandika, kuwa ni heri kufa kwa kupigwa risasi kuliko fedheha ya kufa kwa kuumwa na mbu wa malaria katika nchi ambayo ina rasilimali za kutuwezesha kujenga uwezo wa kuangamiza malaria. Lakini, tunakubali wachache miongoni mwetu wahujumu rasilimali zetu.
Nimepata kuandika huko nyuma (Juni 16, 2004) kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini?
Ndiyo, kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbalimbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. Idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.
Hii ni kama mechi ya mpira isiyofuata taratibu. Ni mechi iliyojaa rafu. Haipendezi kuiangalia. Watanzania tuna lazima ya kuisimamisha mechi hii.
Na hizi ni salamu zangu za Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya kwenu nyote wasomaji wa safu hii.
Maoni ya Wasomaji
Watanzania ambao tunao ni
Watanzania ambao tunao ni wale waliokabidhiwa dhamana ya kulinda mali ya nchi lakini wameamua kufuata SIASA za WATU>Nchi yetu ina Polisi wapelelezi, ina uslama wa taifa, lakini kwa kuwa UFISADI unafanywa na wakubwa hawa watanzania au kwa mapezi yao waliingia kazi hizi kwa kiapo cha kulinda TANZANIA lakini wamesahau na wanaona kila leo kunaibuliwa makosa chungu mbovu,lakini cha ajabu mtu akiwashauri kwamba wawe WATANZANIA wanampeleka mahakamani kana kwamba wao wanajua kila kitu.
Kamati za bunge zinapofanya kazi na kuibua uozo ,mimi nilifikiri kuwa POLISI kwa dhamana iliyopewa wanaposikia taarifa fulani ya kuhujumu nchi wangechomoka kufanya pelelezi na wanapoona sheria imepindishwa basi wanawafungulia mashitaka wahusika
watu wamepewa kazi ya kufanya hivi kweli inakuja akilini tena ungojee yule aliyekupa kazi akwambie fanya hiki au kile? majukumu mtu unapewa unapo anza kazi . Polisi na vyombo vyake vimeshindwa kulinda mali ya taifa.hadi wanyama wa porini wanasafirishwa nje ya nchi . mbele yao .ukweli ni aibu tupu na fedheha kwa hao walopewa dhamana ya kuwa WATANZANIA lakini wamekuwaWAKIMATAIFA.MUNGU IHURUMIE TANGANYIKA.