Tanzania inakabiliwa na uhaba wa mbegu

TANZANIA inakabiliwa na uhaba wa mbegu bora za mazao ya nafaka katika msimu huu wa kilimo wa kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa mbegu bora katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa mbegu leo mjini Arusha Mkurugenzi mazao katika Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Twahir Said alisema hali hiyo imetokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kukosekana kwa mvua za kutosha katika baadhi ya maeneo.

“Uzalishaji wa  mbegu umeshuka kutoka tani 21,000 kwa msimu wa kilimo wa 2015/2016  hadi kufikia tani 15,000 na hii imechangiwa na mabadiliko ya tabia nchi na kutegemea mvua katika uzalishaji wa mbegu”alisema Mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi hiyo mahitaji halisi ya mbegu bora kwa Tanzania ni tani 212,274 na upatikanaji wake kwa sasa ni tani 36,000 ambazo kati ya hizo tani 21,000 huzalishwa nchini na tani 15,000 huingizwa kutoka nje.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuboresha mifumo yake ya uzalishaji,upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora na kuwahamisisha wakulima namna ya kuzitumia ili kuwa na kilimo chenye tija nchini.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Wizara yake imetoa waraka wa kuidhinisha matumizi ya mbegu za serikali zenye haki miliki kwa sekta binafsi.

“Lengo kuu ni kutoa kwa sekta binafsi kuweza kupata mbegu husika kutoka vituo vyetu vya utafiti moja kwa moja na kupunguza urasimu uliokuwepo hapo awali wa upatikanaji wa mbegu hizo kupitia wakala wa Taifa wa mbegu (ASA)”alisema.

Aliongeza:”Hali hiyo itayawezesha baadhi ya makampuni ya mbegu kutumia fursa hiyo na kuongeza chachu ya uzalishaji wa mbeguna upatikanaji wake hapa nchini”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wazalishaji na Wasambazaji wa Mbegu nchini (TASTA) Bob Shuma,alisema kuwa malengo makubwa  ya chama chake kwasasa ni kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu hadi kufikia tani 60,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

TASTA ambayo imetimiza miaka 15 tangu  kuanzishwa kwake Januari 10 mwaka 2002 imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa inaunganisha serikali, wakulima na sekta binafsi katika sekta ya kilimo.

“Pamoja na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu bora pia tutaendelea kuwahamisisha na kuwaelimisha wakulima wetu kuepuka matumizi ya mbegu zisizo bora(feki)  katika kilimo”alisema Shuma.

Aidha Mkuu wa Idara ya Mbegu katika Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Canuth Komba alisema kuwa Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo lakini hadi ni hekta milioni 24 ndizo zinazotumika kwa shughuli za kilimo.

“Kiasi kilichobakia bado ni mapori ambayo hayatumiki, na wakulima wetu bado wana fursa lukuki za kuendeleza shughuli za kilimo kwa  kuwa tuna ardhi ya kutosha”aliongeza.

Alisema kwa uapnde wa mbegu bora matumizi yake bado ni kidogo kwa kuwa asilimia 75 ya wakulima bado wanatumia mbegu za asili au zile wanazozalisha wenyewe hivyo  kufanya uzalishaji wa mazao hasa ya chakula kuwa kidogo sana.

“Mbegu bora ni tija katika kilimo, kwa mfano kwa kilimo cha mahindi tuna hekta milioni 4 ambazo zinahitaji tani 82,000 lakini uzalishaji wa mbegu za mahindi ni tani 15,000 tu”alisema.

Aliwataka Wazalishaji na Wafanyabiashara wa mbegu bora kutumia fursa iliyopo ya soko na ukubwa wa ardhi ya kilimo kuoneza kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuondoa kabisa upungufu wa chakula nchini.

Mkutano huo wa wadau wa mbegu  unawahusisha wataalamu wa mbegu na wadau wa sekta ya kilimo kutoka serikakalini, sekta binafsi na umefadhiliwa na mashirika ya US-AID na East Africa Trade.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *