Tanzania twendapi?

WIKI hii, Ikulu imetangaza orodha ya mabalozi wapya watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali ulimwenguni. Hili ni jambo zuri kwa sababu baadhi ya vituo vilikuwa havina balozi kwa muda mrefu sasa.

Ni jambo la heri pia kwamba nchi yetu imetangaza kufungua balozi mpya katika nchi ambazo huko nyuma hatukuwa na balozi.

Huu ni uamuzi wa kupongezwa kwa sababu nchi ambako tumefungua balozi mpya ni zile ambazo zimeanza kuibua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi na nchi yetu.

Hata hivyo, kuna mambo mawili matatu ambayo ni lazima yasemwe mapema. Kwanza ni suala la kuwa na ubalozi nchini Israel; kinyume cha msimamo wetu kama taifa uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.

Tanzania haina ugomvi binafsi na Israel. Tatizo baina yetu ni la kimsimamo. Kwamba Israel inakalia kimabavu Wapalestina ambao wamekuwa rafiki zetu kwa muda mrefu.

Miaka takribani 40 baada ya Tanzania kufikia uamuzi huo, Israel bado inakalia kimabavu ardhi ya Wapalestina. Sasa hatua yetu ya kurejesha uhusiano wa kibalozi na Israel pasipo kutolewa maelezo ya kina unazua maswali mengi kuliko majibu.

Hatua ya kurejesha uhusiano na Israel imekuja siku chache baada ya kupata ugeni wa Mfalme Mohammed wa Morocco ambayo nayo inaikalia kimabavu Jamhuri ya Watu wa Sahrawi.

Tunafahamu mwelekeo wetu wa kinachoitwa Diplomasia ya Uchumi. Tunafahamu pia kwamba Tanzania haijawahi kuwa na sera ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Lakini, mabadiliko haya katika diplomasia yetu yameanza kututia wasiwasi. Je, diplomasia ya uchumi inamaanisha kwamba sasa taifa letu haliangalii chochote kile kingine zaidi ya manufaa ya kiuchumi.

Je, hii inamaanisha kwamba, kwa diplomasia hii, tungekuwa tayari kufanya biashara na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini na kuwatelekeza wapigania uhuru wa taifa hilo kwa sababu uchumi wetu ungepaa?

Vitabu vya dini zote vinaeleza kwamba binadamu hataishi kwa mkate tu lakini tunadhani mwelekeo wetu mpya sasa ni kutazama wapi tutapata mkate wetu wa kila siku kwanza.

Hatudhani kwamba huu ndiyo mwelekeo ambao waasisi wa taifa letu wangependa twende nao. Wakati tukisherekea maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyia, kuna swali moja kubwa la kujiuliza:

Twendapi?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *