Makala
Tatizo ni Mwakyembe au kanuni za Bunge?
Godfrey Dilunga
Toleo la 074
25 Mar 2009

DHANA ya uwajibikaji bila shinikizo (best practice) ni dhana ya kiungwana. Ni dhana ambayo inaweza kutekelezwa kwa hiari ya mhusika au nguvu za kikanuni au sheria. Lakini ni vizuri zaidi dhana hii ikatekelezwa kwa hiari ya mhusika.

Hata hivyo, katika kutekeleza dhana hii ni lazima kuwapo na sababu zenye mantiki. Vinginevyo, kujitia uwendawazimu katika kutekeleza dhana hii bila sababu zenye mantiki ni wazi kuwa utaishangaza jamii ambayo itaweza hata kutilia shaka uwezo wako wa kupambanua mambo.

Awali, kabla ya kuibuka kwa mjadala kuhusu kampuni ya kufua umeme wa upepo ya Power Pool East Africa inayomilikiwa na Dk. Harrison Mwakyembe na wenzake, sikuweza kubaini changamoto za kiufundi ndani ya baadhi ya kanuni za Bunge.

Sasa changamoto katika baadhi ya kanuni za Bunge ni dhahiri, na hasa baada ya Dk. Mwakyembe, Mbunge wa Kyela, kutoa ufafanuzi wake kuhusu kile kinachodaiwa kuwa amegubikwa na mgogoro wa maslahi katika sekta ya umeme nchini.

Kabla ya haya, nilijiridhisha kanuni hizi ziko wazi, hazina mianya inayoweza kuzua mjadala mkali ndani yake. Mjadala unaoweza hata kugawa washiriki katika pande kuu mbili, kulingana na msimamo wa kila mhusika.

Nitajadili kanuni iliyoandikwa au kutajwa mara kadhaa katika vyombo vya habari nchini. Kanuni kutoka katika Kitabu cha Kanuni za Kudumu za Bunge. Kanuni zilizotungwa chini ya Ibara ya 89, fasili ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sura ya pili, toleo la mwaka 2002.

Ninukuu kanuni ya 61, kutoka katika sehemu ya tano ya kanuni za majadiliano bungeni. Kanuni hiyo ya 61, fasili ya kwanza inaeleza; ‘‘Wakati wa majadiliano bungeni au kwenye kamati yoyote ya Bunge, mbunge hataruhusiwa kuzungumzia jambo lolote ambalo yeye mwenyewe ana maslahi binafsi nalo ya kifedha, isipokuwa baada ya kusema jinsi anavyohusika nalo na kutaja kiwango cha maslahi hayo

‘‘ …na kwa sababu hiyo, itakuwa ni lazima kwa mbunge yeyote anayetaka kuzungumzia jambo hilo bungeni au kwenye kamati yoyote ya Bunge, kusema kwanza jinsi anavyohusika na jambo hilo na kutaja kiwango cha maslahi ya kifedha aliyonayo kuhusiana na jambo hilo kabla ya kuanza kulizungumzia.’’

Hapa zingatia maneno ‘‘kutaja maslahi ya kifedha.’’ Lakini pia, katika kitabu hicho, kanuni hiyo imewekewa msingi wa maneno yanayosisitiza kuwa; ‘‘Kutozungumzia jambo ambalo lina maslahi binafsi ya kifedha.’’ Hapa utaona neno fedha linavyosititizwa katika kanuni hii.

Lakini kwa upande mwingine, fasili ya pili ya kanuni hiyo ya 61, inaendelea kusisitiza suala la maslahi binafsi ya kifedha ikisema; ‘‘Kwa madhumuni ya kanuni hii, mbunge au mwananchi yeyote anaweza kumwarifu Spika, kwa maandishi, akitoa na ushahidi kuwa mbunge amezungumzia jambo ambalo ana maslahi binafsi nalo ya kifedha bila kusema jinsi anavyohusika nalo wala kutaja kiwango cha maslahi hayo.’’

Kama nilivyoeleza awali, pamoja na maudhui yote ya kanuni hii bado inatoa mwaliko wa kukosolewa. Inatoa mwanya wa kugawa watu katika makundi kimjadala. Hailazimishi watu wanaovutana kupata tafsiri moja, na hasa watu wanaotofautiana kimsimamo au mtazamo iwe kwa kigezo cha maslahi fulani au kinyume chake.

Tutanue zaidi upeo wetu wa kuchambua mambo katika mizani huru ya kifikra. Tujadili haya maelezo ya “maslahi binafsi ya kifedha.” Tutafakari huku tukijiuliza je, maslahi ya kifedha yanaanzia wakati gani hasa?

Je, wakati mhusika akiwa na wazo la kuanzisha taasisi au kampuni, au wakati mhusika akiwa katika hatua ya kujadiliana na wenzake namna ya kuanzisha kampuni? Au wakati tayari kampuni imeanza kuingiza fedha (faida)? Lakini pia tujiulize hivyo huku tukizingatia kuwa lengo la kuanzisha kampuni, taasisi au mradi ni kupata fedha.

Ukitafakari kwa kina unaweza kubaini kuwa maswali haya ndiyo yanayothibitisha mwanya uliopo katika kanuni hiyo ya Bunge. Nitafafanua.

Kanuni inazungumzia maslahi ya kifedha na bila shaka, fedha zinazotokana utendaji au uendeshaji wa kampuni husika. Ukweli ni kwamba, ili kampuni itoe faida (fedha) ni lazima iwe katika utendaji, iwe imeanza uzalishaji.

Lakini kwa kuwa kanuni inatamka wazi maslahi binafsi ya kifedha, ni wazi kuwa haijitoshelezi. Tunahitaji uwazi zaidi wa kikanuni ili tupate jibu kuwa maslahi hayo ya kifedha, yanaanzia wapi na wakati gani?

Tutafakari kwa kujiridhisha kuwa; Je, kanuni hizi za Bunge zinatusaidia kutambua bila shaka yoyote kuwa maslahi binafsi ya kifedha yanaanzia wakati gani?

Kwa hakika, majibu ya maswali haya hayajawekwa wazi na kanuni hiyo ya 61, na badala yake mwanya umeachwa kwa mtu yeyote kutafsiri anavyotaka. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba, kanuni hii inaweza kuzalisha hukumu iliyozingatia zaidi ushahidi wa kufikirika.

Kwa mfano, wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti wabunge mbalimbali wamekuwa wakichangia kuhusu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, lakini mara kwa mara sijawahi kusikia wakitangaza suala la maslahi binafsi.

Kwa nini wabunge hawa hawakuwahi kutangaza maslahi binafsi licha ya kusomesha watoto katika shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu vya umma? Wamekuwa wakilalamikia upungufu wa walimu au madawati bila kutaja mgogoro wa maslahi.

Je, jibu ni kwamba hawatangazi mgogoro wa kimaslahi katika mijadala yao kwa kuwa katika suala hilo hakuna maslahi ya kifedha kama kanuni inavyotamka? Kama hilo ndilo jibu, je, ni kwa nini kampuni ambayo haijaanza kutoa maslahi ya kifedha mmiliki wake atangaze mgogoro wa maslahi mapema? Tutanue fikra zetu zaidi.

Hebu tuendelee na mfano wa mbunge kusomesha mwanawe. Hapa, lengo la kusomesha linaweza kuwa ni kumwezesha kupata elimu kwa mtazamo mwingine. Mfano, mbunge anasomesha mwanawe ili awe meneja katika kampuni yake, hali ambayo hatimaye itaibua maslahi ya kifedha kwa mbunge mhusika baadaye.

Mfano huu wa mbunge kuwa na maslahi ya kifedha eti kwa kuwa amesomesha mwanae atakayekuwa meneja katika kampuni yake binafsi pindi atakapohitimu, unawiana na hoja kwamba maslahi binafsi ya kifedha yanaanzia pale linapokuwapo wazo la kuanzisha kampuni. Kwa tafsiri kuwa lengo la hatua hiyo ni kupata maslahi ya kifedha baadaye.

Lakini katika upande mwingine wa mjadala, hasa wale wanaopendekeza Kamati za Kudumu za Bunge zipanguliwe, tuwaulize hivi ni kweli inaingia akilini mbunge yeyote anayesomesha mwanafunzi shule ya msingi, sekondari au chuo kikuu hapaswi kuwamo katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, inayohusika na sekta ya elimu?

Na ni mbunge gani asiyesomesha mwanafunzi shule ya msingi, sekondari au hata chuo kikuu? Ukweli ni kwamba hata kama tukikubaliana na mawazo ya wabunge hawa, ni wazi kuwa majukumu ya msingi ya mbunge na Bunge kama yanavyotamkwa na Serikali yatakuwa katika mtikisiko. Na hiyo maana yake ni kwamba, hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazo kasoro, pengine kama ilivyo kwa kanuni hii ya 61 ya Bunge.

Tukubaliane kuwa kanuni hii ya 61 haiko wazi kiasi cha kutosha, ni kanuni inayoalika mvutano wa pande mbili na hasa ikizingatiwa kuwa inasisitiza mno kuhusu maslahi binafsi ya kifedha. Neno fedha lina maana kubwa hapa! Je, fedha inaanza kupatikana wakati gani, wakati wa uendeshaji au utendaji wa kampuni au wakati tu mtu anapoanza kuwa na ndoto ya kuanzisha kampuni?

Kanuni haiendi mbali zaidi nje ya wigo wa maslahi ya kifedha, na ndiyo maana nataka tutanue zaidi upeo wetu wa kuchambua mambo. Tujikokote mbele zaidi kifikra, tujiulize kama kinachozungumzwa hapa ni maslahi binafsi ya kifedha, kuna uhalali gani wa mtu kutangaza mgogoro kwa jambo ambalo bado hajaanza kuchuma hizo fedha?

Hapa kuna mambo mawili. Mosi, kama tunaona kuwa ni vema mtu akatangaza mgongano wa maslahi ya kifedha hata kwa kampuni ambayo haijaanza utendaji wala kuingiza fedha, basi tukubaliane kuwa kanuni hii inathibitisha kuwa na matundu ya kiufundi.

Lakini pili, kama tunaona kuwa si lazima mtu kutangaza mgongano wa maslahi wakati kampuni anayoanzisha ipo katika hatua za awali, basi, tukubaliane kuwa kanuni hii haina matundu ya kiufundi, ni kanuni iliyoshiba katika kusimamia malengo yake. Isipokuwa, kanuni binafsi ituongoze kwa kujieleza kinaga ubaga.

Nafahamu kwa upande mwingine, wapo watu wanaoweza kujitokeza na kuhoji je, maslahi binafsi ya kifedha yanaumbwa katika mwelekeo gani?

Watajenga hoja kwamba katika hali ya kawaida maslahi ya binafsi ya kifedha, kama yanavyotamkwa na kanuni ya 61 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaanza ‘kuumbwa’ katika wazo (dhamira) la mhusika au wahusika, yaani wazo la kuanzisha kampuni.

Kwamba kwa sababu tayari unalo wazo la kuanzisha kampuni, ni dhahiri kuwa utakuwa na mikakati ya kuhakikisha dhamira yako inafanikiwa. Na katika kutimiza mikakati hiyo ni lazima ufanye juhudi ili ndoto itimie. Bado, mtazamo huu unaweza kuwa sahihi ndani ya maudhui ya kanuni ya 61 ya Bunge. Ndiyo maana nasema, kanuni inagawa watu kimjadala, irekebishwe ili iwe wazi.

Nasisitiza kuwa kanuni ya 61 ya Bunge inafungua mjadala wa kukosolewa na hata kufanyiwa marekebisho zaidi.

Inafungua au kualika mjadala kwamba haijitoshelezi na hasa katika ubishani wa kiufundi tena ubishani unaohusisha wanasheria waliobobea, kama Dk. Harrison Mwakyembe.

Na bila shaka, wanasheria wanaweza kuwa katika nafasi nzuri mno ya kutambua ambiguity ndani ya kanuni hii ya 61 ya Bunge. Kwa bahati nzuri, Bunge linao wanasheria bingwa wa kutosha, akiwamo Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Lakini pia ni vema ikaeleweka kuwa upungufu huu ninaouona katika kanuni hii ya Bunge, upungufu ambao Dk. Harrison Mwakyembe amejitokeza ku-challenge na baadhi ya wabunge wenzake wachache wakijitokeza kumpinga, pengine kwa kukariri tu maneno yanayotamkwa na kanuni bila kutafakari kwa kina, unaakisi upungufu uliopo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nilivyoeleza awali.

Hivyo basi, kwa kuwa kanuni zimetungwa na wabunge ni busara zaidi mianya kama hii ya kikanuni ikaanza kutafutiwa ufumbuzi kwa malengo maalumu ya kufanikisha maudhui ya kanuni husika.

Matundu ndani ya kanuni za Bunge yazibwe, na kanuni iwe wazi kueleza wapi mwanzo wa maslahi binafsi ya kifedha kwa kuzingatia changamoto ya Dk. Harrison Mwakyembe.

Je, ni pale mhusika au wahusika wanapokuwa katika maandalizi ya kuanzisha kampuni au ni pale ambapo kampuni inapokuwa imekwishaanza uzalishaji na hivyo kuanza kuzalisha maslahi ya kifedha?

Ushauri wangu ni kwamba katika kuitafakari kanuni hii tuangalie namna kamati nyingine za kudumu za bunge zilivyoundwa na aina ya wajumbe wake na kile tunachoweza kukitafsiri kama mgongano wa maslahi ya kifedha. Tukumbuke kuwa Bunge linazo kamati za kudumu 16, zinazogusa sekta zinazoingiliana na maisha ya kila siku ya raia wa Tanzania.

Tutafakari, kama tunataka kanuni iaanze kuuma pale ambapo mradi unaanza kujadiliwa kwamba je, hali itakuwaje pale mradi unaposhindwa kutimia? Lakini je, kama mradi hautakuwa umetimia na mhusika atakuwa ametangaza mgogoro wa maslahi ya kifedha mapema bungeni je, ikibainika mradi au kampuni hiyo imeishia mfukoni kabla ya kuanza kuingiza maslahi ya kifedha atakuwa amedanganya bunge na akiadhibiwa atajitetea katika misingi ipi ya hoja?

Katika hili la Mwakyembe, nadhani kiini cha tatizo ni kanuni za Bunge, hususan kanuni ya 61, isiyoeleza mwanzo wa maslahi binafsi ya kifedha. Naamini, Mwakyembe bado analindwa na kanuni hiyo isiyomeza moja kwa moja dhana au maudhui ya kile tunachoweza kuita “best practice.” Nashukuru bado Dk. Mwakyembe anazidi kuwa chachu ya mabadiliko katika Bunge, kuanzia kashfa ya Richmond.

Tupanue mawazo yetu, huku tukiweka fikra zetu katika mzani huru. Tukubaliane kuwa kanuni ina upungufu, haisemi bayana maslahi ya kifedha yanaanzia wapi na wakati gani katika mchakato wa kuanzisha iwe kampuni au jambo jingine linaloweza kuibua maslahi ya kifedha.

Kanuni hii inajitenga na maudhui ya dhana ya “best practice” kwa kuwa kama kanuni ingekuwa imemeza dhana hii, ni wazi kuwa ingebeba ufafanuzi wa maslahi binafsi ya kifedha yanaanzia wapi na kwa wakati gani.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Godfrey Dilunga
gdilunga@raiamwema.co.tz
+255-787643151

Toa maoni yako