SAFU hii iliwahi kuchambua kwa mfululizo ikihoji ni “Nani anamshauri Rais Jakaya Kikwete?”.
Ilijikita katika kuchambua makundi mbalimbali yenye nafasi ya kumshauri Rais na kuonyesha ugumu wa kufanya hivyo kwa sababu kadhaa zilizobainishwa wakati ule.
Kundi mojawapo nililosema wakati ule kuwa ina wajibu wa kumshauri Rais lakini hawezi kulisikiliza ni kundi la wana habari.
Mpaka ninapoandika makala hii, hakuna kundi hata moja linaweza kukiri kuwa limeweza kumshauri Rais ipasavyo namna ya kuinusuru nchi hii na machafuko ya kijamii. Marafiki wameshindwa, viongozi wa dini wameshindwa, Bunge limeshindwa na hivi sasa limefungwa mdomo lisifurukute, na hatimaye hata wana habari wamewekwa kitanzini.
Ni kutokana na uzoefu huu, nalazimika kujadili hali hii kwa namna nyingine. Badala ya kuendelea kulalamika kwa kuhoji ni nani mshauri wa rasi na serikali, sasa nahoji ni nani anampotosha rais na serikali?
Serikali imejiingiza katika vita na makundi mbalimbali kwa wakati mmoja. Ingedhaniwa kuwa kwa vile watu wengi wanahoji weredi wa kamanda katika kuongoza mapambano haya, ingekuwa bora wakapigana vita moja moja badala ya vita nyingi kwa wakati mmoja.
Mgogoro ulioibuliwa na mgomo wa madaktari haujaisha na hautarajiwi kwisha karibuni kwa sababu serikali imelifunga Bunge mdomo lisiujadili. Mgomo wa walimu umeanza kwa kishindo nchi nzima na viongozi wengi wanaficha vichwa vyao mchangani kama mbuni afanyavyo.
Kuushughulikia mgomo wa walimu ni kibarua kizito hata kama walimu wenyewe wamegawanyika katika makundi ya kimaslahi na kiitikadi. Unyonge wa walimu kimkakati una nafuu kuliko udhaifu wa serikali wanayopambana nayo. Kuteka na kutesa havitasaidia kama ambavyo havikusaidia katika mgogoro wa madaktari.
Zimwi la rushwa limechoka kufichwa ndani ya makabati ya Bunge. Safari hii limeibuka kwenye ukumbi wa Bunge. Rushwa imechafua hali ya hewa na Bunge halitawaliki.
Serikali ilipohonga kwa kutumia mkono wa David Jairo, haikuwa tabu sana kwa sababu rushwa ilifichwa ndani ya sahihi za kupokea rushwa hiyo (posho). Na kwa kuwa wakubwa kwa wadogo walipokea, rushwa hiyo ilitakaswa na kuitwa posho ya kuwezesha kabla msaliti mmoja hajapiga kelele na kutibua mpango mzima.
Ripoti ya tume maalumu iliyochunguza sakata hilo haijashughulikiwa mpaka leo na ni kana kwamba Spika hakumbuki ni kina nani walisaini kupokea posho/rushwa hiyo!
Rushwa ya safari hii inapigiwa kelele sana kwa sababu aliyehonga si mtu wa serikali bali ni makampuni ya mafuta. Kosa la pili, makampuni hayakuwapa wote, yaliwapa wale wanaojua kupiga kelele sana na kutoa machozi ya mamba. Waliokosa wamepiga kelele na bungeni hakuna amani tena. Hivi sasa ni mwendo wa miongozo na taarifa.
Ule msitari mzito uliowatenga wapinzani na watawala umefutika maana kama ulivyo ukimwi, rushwa ya bungeni haibagui gamba wala gwanda. Serikali iko vitani na maadui wa ndani wakati kamanda ni dhaifu.
Kana kwamba hilo halitoshi, wiki hii serikali imelifungia gazeti chokonozi la kila wiki linaloitwa MwanaHalisi. Kisa? Linachochea chuki kati ya wananchi na serikali yao pendwa. Ebu tuazimane akili kidogo hapa.
Dk. Steven Ulimboka alitekwa na kuteswa lakini hakufa kama nabii fulani. Rais akakana kuwa serikali haihusiki na akampa pole na kumtakia uponyaji wa haraka. Waziri Mkuu akafuatia na kukana mchana kweupe kuwa serikali haihusiki. Jeshi la polisi likakana askari wake kuhusika katika mchezo huo mchafu.
Wakanaji wa polisi wakasema hata kama polisi imekuwa ikijikuta kuhusika na mambo machafu, lakini si katika hili suala. Idara nyeti ya usalama wa taifa ikakana kuwa haihusiki na haina sababu ya kuhusika. Lakini, Dk. Ulimboka alitekwa usiku, akateswa vibaya sana, na hilo halina ubishi.
Kwa hiyo kwa kuwa serikali haikumteka, polisi hawakumteka na idara ya usalama wa taifa haikumteka, lakini alitekwa, basi kuna mtekaji asiyejulikana. Polisi ikaunda tume isiyofahamika lakini wananchi wakaipigia kelele kuwa hawana imani nayo.
Muda si mrefu akaibuka Kamanda Kova akisema ana mtekaji kutoka Kenya. Ilipobainika ni kichaa asiyejua asemalo, na pale Mchungaji wa Kanisa moja kusimama hadharani akisema hakuhusika na suala hilo kama alivyosema Kamanda Kova – suala la mtekaji huyo likaisha kama lilivyoanza.
Gazeti la MwanaHalisi, ama kwa unaoitwa “uchochezi”, uzalendo na uchokonozi likaziba mwanya wa kiuchunguzi na kuibua mambo mazito yanayoitwa uchochezi.
Ikumbukwe aliyetekwa si jasusi, si mbuzi, si kibaka wala mhaini. Ni mwanadamu mwenye haki zake za msingi. Haiwezekani, tuna serikali iliyoapa kulinda haki za raia wake inaamua kukaa kimya pale rais wake anapofanyiwa unyama kama aliofanyiwa Dk. Ulimboka. Kutokuhusika kwa serikali katika utekaji si kibali cha serikali kutokuonekana inashughulikia utekaji huo.
Ndiyo maana hata pale Polisi wanapoua jambazi, suala hilo haliishii hapo. Lazima uchunguzi ufanyike na ukweli ufahamike. Ninaamini gazeti la MwanaHalisi lilifanya kazi ya kuziba huo mwanya. Haiingii akilini kuwa mtu mwenye akili timamu atafungia gazeti hilo! Haiingii akilini kuwa kiongozi yeyote aliyeapa kwa katiba na msahafu anaweza kukubali unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka upite bila kuchukua hatua hasa kama yeye binafsi hahusiki.
Kwa hili, damu ya Dk. Ulimboka na damu ya MwanaHalisi itajitetea mbele ya Mungu wa haki, asiyevaa gwanda wala gamba.
Narudia tena kuhoji: Ni nani anaipotosha serikali yetu na rais wetu kuingia vitani na madaktari, walimu, na wana habari? Ni nani anaipotosha serikali kuchezea suala la rushwa bungeni? Vita hizi nne kwa wakati mmoja hazina tija na zinapungukiwa na weredi wa kimkakati kwa upande wa serikali.
Zama hizi za ukweli na uwazi, migogoro inaisha kwa kuikabili kwa hoja na si vitisho na utekaji. Hoja za MwanaHalisi na unaoitwa uchochezi wake, zinahitaji maelezo ya wazi ili kubainisha uchochezi wake.
Kulifungia gazeti na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari na kuwachochea wazitafute kwa njia ambazo hazitakuwa rahisi kuzifungia.
Kama nilivyowahi kudokeza wiki chache zilizopita, kuna mgomo wa washauri wa rais na serikali. Washauri wameingia kwenye mgomo na wapotoshaji ndio wako kazini.
Hebu tujaribu kuukabili ukweli mchungu. Kufungia gazeti kutaleta nafuu yoyote katika makali ya maisha yanayowakabili Watanzania wengi kwa sasa? Kufungia gazeti kutarejesha uadilifu ndani ya vyombo nyeti vya dola vinavyovujisha siri za serikali kwa Mwanahalisi?
Kufungia gazeti kutaongeza fedha katika hazina ya serikali ili iweze kuwalipa watumishi haki zao stahiki ili wasigome? Mbona serikali hiyo hiyo inayoimba wimbo wa utawala wa sheria na matumizi ya mahakama, isiende mahakamani kulishtaki gazeti hilo?
Nihitimishe: Mwanahalisi kwa Watanzania walio wengi ni zaidi ya gazeti. MwanaHalisi ni kiumbe hai ndani ya mioyo ya Watanzania walio wengi na hasa waliokosa matumaini.
Kufungia gazeti hili ni sawa na kuzima mashine ya oksijeni ya mgonjwa aliye mahututi. Mgonjwa huyo atakufa. Mbele ya wapenda demokrasia ndani na nje ya nchi, MwanaHalisi ni tochi yenye kurunzi mpya kila wakati. Inamulika na kuwahakikishia wajomba zetu kuwa fedha zao wanazotupa zinatumika kwa uadilifu. MwanaHalisi ni kimbilio la hata hao wanaolifungia.
Wanaponyanyasana na kukandamizana, huwa ni MwanaHalisi inayohabarisha na magazeti mengine yenye uthubutu. Mbinu ya kufungia uhuru wa habari inachochea maasi katika nchi hata kama mbinu hiyo imeigwa kutoka katika baadhi ya nchi.
Kitendo hiki kilaaniwe kwa nguvu zote na wapenda amani katika Taifa. Ni serikali inayopungukiwa na uadilifu tu inayoweza kufungia magazeti. Uchochezi wa magazeti hukomeshwa kwa kuacha yale yanayolalamikiwa au kubainisha uchochezi wa magazeti hayo.
Maoni ya Wasomaji
well said
well said
<p>Kwa Nini Mheshimiwa Raisi
Kwanini magazeti yamelifumbia
Kwanini magazeti yamelifumbia macho suala la sensa ambapo waislam wamegomea kushiriki,hakuna chombo chochote kilichoonesha madai ya waislam na udhaifu au ubora wa hoja zao!kumekuwa na tabia ya vyombo vya habari kukaa kimya kila mara ambapo jambo linahusu dhulma dhidi ya waislam katika tanzania na ulimwenguni kote,je ukombozi huu utafanikiwa kama jamii moja ikionewa ni sawa na nyingine ikiguswa tu basi kila mtu atapiga kelele?inashangaza sana.tuache ubaguzi haki za raia ni kwa wote na si kwa baadhi ya makundi tu!
nawasilisha
wako katika uadilifu wa jamii nzima.