Tugange yajayo

TUMEINGIA  mwaka 2017. Maisha binafsi na ya Tanzania lazima yasonge mbele.

Ni kwa kutekeleza kwa vitendo yale tuliyoazimia, kwa nafsi zetu na kama taifa.

Wanadamu tuna ya kujifunza kutoka maisha ya tembo. Msafara wa tembo huwa na kawaida ya kutorudi nyuma. Ndiyo maana porini huzioni nyayo za tembo zenye kwenda mbele na kurudi nyuma.

Ni ukweli kuwa tembo ni mnyama mkubwa na ndiye mfalme wa pori. Lakini, hufika mahali tembo akasumbuliwa na siafu kiasi cha kuweweseka na hata kutamani kulihama pori.

Ni kwa kosa la tembo kukanyaga kichuguu cha siafu. Naam, siafu 500 ni wengi kuliko tembo mmoja, pamoja na ukubwa wa tembo.

Adili ya jambo hili ni ukweli kuwa duniani mkubwa anapaswa kumheshimu mdogo, na mdogo pia kumheshimu mkubwa. Hivyo, wanadamu tunapaswa kuheshimiana.

Kwenye ngazi ya taifa tuwe na mtazamo wa timu ya mpira. Timu bora ni ile yenye uwezo wa kushindana. Maana, timu inaweza kushindana ikiwa haina uwezo wa kushindana kuweza kushinda na kupata inachokitaka. Duniani kuna tofauti ya kushiriki kushindana na kuwa na uwezo wa kushindana.

Ndiyo maana kwenye FIFA kila nchi mwanachama hupewa nafasi ya kushindania kucheza fainali za Kombe la Dunia. Hata hivyo, ni timu zile zenye uwezo wa kushindana ndizo hufika hatua za mbali kwenye kushindania kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia. Nyingi hupukutikia hatua za mwanzoni tu za mtoano.

Tanzania ni nchi yetu. Tuna wajibu bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kimitazamo. Bila kujali ni serikali ya chama gani iko madarakani, kufanya yote kuhakikisha tunaisadia serikali iliyo madarakani ifanikiwe katika kuifanya nchi yetu kuwa yenye uwezo wa kiushindani kwenye dunia ya ushindani.

Huko ni kutimiza wajibu wetu wa kizalendo kwa nchi tuliyozaliwa na tunayoipenda.

Na hakika,  uchumi wetu bado ni duni. Wananchi wengi bado wanataabika kwa umasikini.  Mwaka huu mpya wa 2017  uwe ni mwaka wa kuelekeza pia juhudi zetu kwenye kujenga na kuimarisha uchumi wetu.

Tukumbuke pia, katika nchi yeyote yenye dhamira ya kweli ya kwenda mbele kimaendeleo, usalama na amani ni vitu viwili muhimu kuwepo.

Bila usalama na amani hakuna maendeleo. Na katika mazingira yenye kuruhusu kushamiri kwa rushwa, kubwa na ndogo, basi, haki na usawa katika nchi hiyo hukosekana. Na pasipo na haki na usawa, hakuna amani na usalama.

Unaweza kuwa na amani katika nchi lakini ukakosa usalama kwa maana ya kuwa, ingawa nchi haimo vitani, lakini wananchi kwa
kiwango kikubwa hawana hakika ya usalama wa maisha na mali zao.

Hawana hakika ya maisha yao ya kila siku, chakula chao, afya yao, elimu yao na ya watoto wao. Nchi inaweza kuwa na amani lakini  haina usalama kwa maana ya pili niliyoielezea. Na hilo la kukosekana kwa usalama husababisha kuvunjika kwa amani.

Kuwapo kwa amani na usalama katika nchi hujengeka katika misingi ya haki na usawa, misingi ya kuaminiana. Misingi ya kuheshimu haki na uhuru wa raia kutoa mawazo yao. Ni muhimu kuwapo  misingi imara ya demokrasia.

Ni vema wananchi wakawaamini viongozi wao, na viongozi pia ni vizuri wakawaamini wananchi wao. Na hili viongozi waaminike ni lazima wawe wakweli na wawazi. Wawe waadilifu.

Wanadamu hatuna budi kufahamu, kuwa uaminifu ni biashara nzuri, ni biashara yenye tija. Tusipoaminiana na kibaya zaidi, tusipoaminiwa kama watu binafsi, tusipoaminiwa na wengine ndani na nje ya mipaka yetu. Hayo ni mambo ya msingi kabisa kuyatafakari tunapouanza mwaka huu mpya wa 2017. 

Tuendelee kutekeleza yaliyo  kwenye wajibu wetu wa kizalendo, kwa mwaka huu wa 2017 na inayokuja.

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.

0754 678 252, http://www.mjengwablog.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *