Tukatae fedheha kuwa taifa linaloruhusu watoto kuolewa

NAKUMBUKA kumwona Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi siku chache zilizopita akitoa maelezo ya utetezi bungeni kuhusu kigugumizi cha serikali kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Utetezi ule wa Profesa Kabudi ulijengwa katika kile kilichoonekana kama ni kulinda au kuenzi mila na desturi za baadhi ya makabila nchini pamoja na sheria za kimila (customary laws) ambazo zinaruhusu mambinti kuolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18.

Sikutaka kuamini kile alichokuwa akikitetea Profesa Kabudi na kusindikizwa na makofi ya baadhi ya wabunge. Tangu wakati ule, nilitafakari sana lakini ukweli ni kwamba sikuwahi kupata majawabu.

Niliwaza kwamba watu wazima, wasomi ambao wameaminiwa na wananchi wenzao kwamba wanaweza kuwatetea na kuwasemea, ijakuwaje leo wanashabikia jambo ambalo lina athari kwa sehemu moja ya jamii?

Itakumbukwa kwamba Januari 2016, Mahakama Kuu ya Tanzania ilivitaja vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya ndoa kuwa kinyume na Katiba na kuiagiza serikali ivifanyie marekebisho kwa kuongeza umri unaofaa kwa ndoa kuwa miaka 18 kwa wanaume na wanawake.

Hata hivyo serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyokuwa imeipa ushindi taasisi isiyo ya kiserikali ya Msichana Initiative inayojishughulisha na utetezi wa haki za watoto wa kike, ambayo ilifungua kesi hiyo.

Kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya ndoa kinaruhusu ndoa kufungwa kwa taratibu za kidini na za kimila, hali ambayo inaweza kuwa fursa ya ukandamizaji kwa watoto wa kike katika jamii zenye mila zisizozingatia usawa wa kijinsia.

Hiki ndicho Profesa Kabudi alichokuwa akikipigania bungeni huku akipigiwa makofi na baadhi wa wabunge na tangu hapo mpaka leo hakuna mwendelezo wowote wa kuondokana na fedheha hii.

Nilitafakari sheria nyingine nyingi ambazo serikali imezipeleka bungeni kwa lengo la kuzuia ukatili wa kijinsia na ukandamizaji wa mwanamke. Halafu leo hii ni watu walewale ambao wanapata kigugumizi kubadili sheria ya ndoa. Hakika sikuwaelewa, sijawaelewa na sitawaelewa.

Tafiti mbalimbali za kitaalamu zimekuwa zikiikosoa Tanzania kwamba licha ya kusaini itifaki na maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu vita dhidi ya ndoa za utotoni, sheria zake bado zinalinda vitendo hivyo.

Miongoni mwa maazimio ambayo Tanzania imesaini ni lile la Afrika kuhusu haki na ustawi wa mtoto linaloweka mkazo katika vita dhidi ya unyanyasaji wa mtoto wa kike likisisitiza kutungwa kwa sheria zinazotaja miaka 18 kama umri wa kuoa au kuolewa.

Hata hivyo, Sheria ya ndoa ya 1971 ambayo inasimamia masuala yote ya ndoa na familia, inaruhusu wasichana kuolewa wakiwa na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi au miaka 14 kwa ridhaa ya Mahakama.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ndoa ni muunganiko wa hiari wa watu wawili mwanaume na mwanamke ambao wamekubaliana kuishi pamoja.

Uchambuzi wa kisheria uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya masuala ya sheria ya Velma (Velma Law) mwaka 2016, unabainisha kuwa suala la uhiari katika sheria hiyo halina uhalisia kwani mwanamke anayetajwa katika sheria anaweza kuwa mtoto asiyeweza kufanya uamuzi.

Mwaka 1994, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (TLRC) ilipendekeza sheria ya ndoa ifanyiwe marekebisho kwa kuongeza umri wa ndoa hadi miaka 21 kwa wanaume na wanawake, lakini suala hilo mpaka sasa halijafanyiwa uamuzi.

Nje ya sheria, ziko ripoti na tafiti nyingi za kitaifa na kimataifa ambazo zimeukosoa jambo hili, huku matokeo ya tafiti yakionyesha kuwa suala la ndoa za utotoni ni moja ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya mtoto wa kike.

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu la Human Rights Watch ya 2017, inaeleza kuwa kati ya watoto wa kike watano, wawili wameolewa kabla ya miaka 18 nchini.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Februari mwaka jana inataja ndoa za utotoni kuwa moja ya vikwazo vikuu kwa watoto wa kike wa Tanzania kupata elimu, huku taarifa ya Benki ya Dunia ya Januari 2016 ikiitaja Tanzania kuwa inashika nafasi ya tatu kwa ndoa za utotoni barani Afrika.

Taarifa kama hizi na nyinginezi ndizo zilizoisukuma serikali kupeleka bungeni sheria za kuwalinda watoto wa kike. Sheria hizi ni ile ya Makosa ya Kujamiiana ya 1998 na Sheria ya Mtoto ya 2009 ambazo zinamtambua mtu mwenye miaka chini ya 18 kuwa ni mtoto ambaye hawezi kufanya uamuzi kwa kijitegemea. Kwa maana hiyo, ni kinyume cha sheria kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.

Katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba mbili ya 2016, Bunge liliridhia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa mwanaume atakayethibitika kujamiiana na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18 akiwemo mwanafunzi, lengo likiwa ni kumlinda mtoto wa kike.

Jitihada hizi zimefanywa na serikali yetu na Bunge letu. Sheria zimepitishwa kumlinda mtoto wa kike kwa kiwango kikubwa, lakini inapofika kwenye suala la umri wa kuolewa, watu walewale na vyombo vilevile vinasita. Kuna nini katika hili jamani?

Kwa maoni yangu upo umuhimu wa kuacha kukaza shingo. Kama kweli tunataka kuongeza ulinzi kwa mtoto wa kike lazima sheria ibadilishwe na mabadiliko hayo yasimamiwe. Tunapokataza mtu kumuoa mwanafunzi au mtu kufanya mapenzi na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18, huku tukiruhusu ndoa za chini ya umri huo tena kwa wigo wa miaka mitatu, tunakuwa watu wa ajabu.

Lazima tutambue kwamba watoto wetu wa kike hawako salama. Iwe wale walioko shuleni au nje ya shule kwani wanafunzi wasichana wanaoacha shule kwa sasabu ya mimba pia ni kubwa katika mtazamo wa kitaifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma Julai 5, 2017 alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015, wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na tatizo hilo.

Kadhalika takwimu za utafiti wa Demografia na Afya nchini (TDHS) za 2016 zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana hupata ujauzito wakiwa na umri chini ya miaka 18.

Kanuni namba 4 ya Kanuni za Elimu toleo la 2002 inaelekeza kufukuzwa shule kwa mwanafunzi yeyote ya kike na/au wa kiume ambaye anajihusisha na vitendo vya ngono. Mimba imekuwa ikitumika kama uthibitisho kwamba mwanafunzi husika amejihusiaha na vitendo hivyo.

Waraka wa kanuni hizo unavitaja vitendo vingine vinavyoweza kusababisha mwanafunzi kufukuzwa shule kuwa ni pamoja na wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro.

Hapa tukumbuke kuwa hata zile harakati za kuwarejesha watoto wenye ujauzito shuleni haziwezi kuzaa matunda kwani Rais John Magufuli alikwishaweka msimamo wa serikali yake wazi kwamba hilo haliwezekani aslani.

Jamani tuchukue hatua sasa. Baada ya kuziba mianya mingine, na hilo la ndoa tumalizane nalo ili tuone jinsi ya kusonga mbele.

 

Mwandishi ni Neville Meena – Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), nevilletz@gmail.com; +255 787 675555

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *