LEO ninaanza safu hii kwa utabiri. Ninajaribu kutumia udadisi wa kawaida tu kueleza Afrika ninayoiona miaka 30 kutoka sasa. Na utabiri wangu hautokani na kile ambacho baadhi yetu wamekuwa wakidhani ni mawazo hasi au kutokuwa tayari kubadilika. Mtiririko wa matukio tangu miaka ya 1960 nchi zetu zilipopata uhuru wa bendera hadi hii leo unayo maelezo mengi yanayohitimisha utabiri ninaoutoa hapa.
Kama leo hatukuchukua tahadhari. Kama hatutakuwa tayari kuchukulia kwa uzito haya ninayoyadadisi sasa, upo uwezekano mkubwa kwamba miaka 30 kutoka sasa yafuatayo yakatukuta:
Kwanza upo uwezekano wa nchi zetu kuendeshwa na wawekezaji wakubwa kutoka nje. Kitakachotokea ni hivi: Watakuja wawekezaji wakubwa katika madini, ardhi (kilimo cha kisasa), mafuta na viwanda ambao watakuwa na utajiri mkubwa sana utokanao na faida kubwa wanayochuma. Katika mazingira haya ya vyama vingi na soko gulio, wale wawekezaji watakuwa na uwezo wa kuamua ni nani agombee urais, ubunge na hata udiwani. Wao kwa vile pesa itakuwa haisumbui watalipa tu.
Na wakishapata kuanzia rais, wabunge na hata madiwani basi watakuwa na uhakika kwamba sera, sheria na mifumo wanayoitaka ndiyo inayopitishwa na serikali iliyo madarakani hata kama inawaathiri wananchi kiasi gani. Mwekezaji katika wakati huo atakuwa na jeuri ya kukaa kwenye jakuzi katika nyumba yake iliyo shambani kwake au mgodini kwake huko Sumbawanga au Buzwagi lakini akampigia rais wa nchi na kumpa amri achukue ndege amfuate haraka sana kule shambani (au mgodini) kwake kwani kuna taarifa ya habari imemuudhi sana binti yake.
Katika mazingira hayo tunakopelekwa atakayekuwa anaamua ni nani awe waziri wa nini na nani awe jaji wa mahakama ipi ni yule aliyewaweka viongozi madarakani na si ninyi wananchi. Ninyi mtakuwa mnaamka asubuhi na kadi zenu za kupigia kura baada ya miaka mitano kwenda kucheza makida makida katika foleni huku anayewawekea viongozi madarakani ni mwingine kabisa.
Pili: Kwa vile sasa hivi mataifa yanayogombea rasilimali chache za dunia yameongezeka kwa kasi na kusababisha ushindani miongoni mwao basi upo uwezekano wa ama wakubwa wale kutwangana ili wakamate maeneo ya kuchuma hapa Afrika au kukaa na kuelewana jinsi ya kugawana kwa amani. Kama wataamua kutwangana kwa ajili ya rasilimali za Afrika basi matokeo yake ni kwamba atakayeshinda katika vita atakamata ama kukalia kabisa kijeshi maeneo aliyokuwa akiyapigania. Uwezekano huu si mkubwa sana endapo gharama zake hazitalingana na maslahi yanayotafutwa ya muda mrefu.
Kama wataamua kukubaliana kugawana tena basi watagawana kwa amani na watakuwa wanaungana mkono katika kila uamuzi wanaochukua kuhusu jinsi ya kuendelea kukalia kibiashara na kunyonya nchi zetu.
Tatu: Kuna uwezekano mkubwa kabisa kwamba ifikapo miaka ya 2040 wazungu watakuwa wamefikia kile kinachoitwa donor fatique (wamekwishafikia hapo, wamechoka). Wataamua kuwatolea uvivu viongozi wa Afrika ambao kazi yao wakiwa madarakani ni kufikia namna ya kujitajirisha wao binafsi na idadi ndogo ya ndugu au mashabiki wao kutumia fedha za wafadhili na rasilimali za nchi zao. Wazungu wataona aibu kwamba wakati wao wanahubiri demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, ushirikishwaji na mengine kama hayo na wakati ni wao wanaotoa fedha (ufadhili) kuendesha serikali hizi bado wananchi wengi katika Bara la Afrika wanaishi katika ukandamizwaji, hawapati haki, wanabaguliwa au kuachwa pembezoni, na kuzidi kuwa masikini.
Kitakachofanya wazungu wachukue hatua, nitakayoieleza hivi punde, ni aibu ya ubinadamu kwamba sasa ifike wakati waache kuangalia maslahi yao tu ya kujiendeleza na kujistawisha kiasi cha kuwaacha binadamu wengine kule Afrika wakidhalilika chini ya tawala dhalimu na zisizoweza kuendesha taifa la kisasa (modern state) kwa ufanisi kama wao.
Litapelekwa pendekezo katika Umoja mpya wa Mataifa kwamba nchi zilizoendelea ziruhusiwe tena kuja kuzikalia nchi za Afrika ili wale walioendelea watumie vizuri kodi za watu wao na rasilimali zilizo Afrika katika kuleta maendeleo ya watu wa bara hili. Hoja itakayojengwa wakati huo ni hii hii inayojengwa sasa baada ya ujio wa uliberali mamboleo kwamba tunaita wawekezaji kutoka nje kwa sababu: Mosi, wataleta mitaji. Pili, wataleta utaalamu (mitambo na wataalamu). Tatu watasaidia kutafuta masoko. Nne watatengeneza ajira. Tano watalipa kodi. Itajengwa hoja Umoja wa Mataifa kwamba lakini endapo hizo faida za wawekezaji wa nje zimekosekana katika nchi huru kwa kipindi cha zaidi ya nusu karne inawezekanaje sifa hizo zikapatikana katika uongozi wa nchi hizi? Na litatolewa wazo kwamba kufanyike referendam (kura ya maoni) ili wananchi waamue: Je, waendelee kutawaliwa na hawa hawa viongozi wao au wachague wawekezaji, tena wazungu ndo waje kuendesha nchi zao? Jibu hapa liko wazi.
Kwanza watatoa hoja ya kuja kutawala moja kwa moja lakini ikishindikana watatoa hoja kwamba uongozi wa nchi za Afrika ubinafsishwe kwa wawekezaji ili wao waendeshe nchi hizi kwa ufanisi zaidi. Na wataandika michanganuo kuonyesha jinsi nchi kama Tanzania inavyoweza kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 10 tu atakachokabidhiwa mwekezaji.
Tukiachana na utabiri huu turejee tena katika kile tulichokikusudia baada ya uhuru ili tuone tulipojikwaa. Mathalani tuchukulie mfano wa Tanzania. Siku zile wakoloni walipokuwa wakifunga virago, Rais wa kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwaomba Waingereza wale kurejea Tanganyika baada ya miaka kumi ili wajionee jinsi tutakavyokuwa tumepiga hatua kimaendeleo.
Na miaka ile baada ya uhuru maana moja kubwa ya maendeleo ilikuwa ni kurejesha utu, heshima na hadhi ya mtu mweusi ambaye alikuwa wa mwisho katika ‘gredi’ za binadamu kipindi chote kabla ya uhuru. Hili nitaendelea kulisisitiza kwa sababu maalumu. Leo watoto wetu na vijana wetu wengi huenda hawajui kwamba wazazi wao walipata kibali cha kuonja hadhi ya binadamu kamili baada tu ya uhuru.
Baada ya uhuru falsafa ya maendeleo ilisisitiza sana kujitegemea, japo huenda haikufanikiwa kama ilivyotarajiwa. Na kwa mtazamo wa kiudadisi zaidi moja ya makosa makubwa – japo lilifanyika kwa nia njema – baada ya uhuru ilikuwa pale waasisi wa taifa letu walipojenga dhana kwamba serikali ingeliwapelekea maendeleo wananchi. Na ndiyo maana hata oparesheni ya vijiji vya ujamaa iliendeshwa na serikali kibabe – japo kwa nia njema – kulazimisha watu waishi pamoja ili serikali iwapelekee maendeleo kule kirahisi.
Na moja ya viashiria vya maendeleo wakati ule vilikuwa na taswira ya usasa, kwa mfano kujenga zahanati vijijini (ili kuondoa adui maradhi); kujenga shule vijijini (ili kuondoa adui ujinga) na kujenga barabara na kupeleka huduma za maji (kusaidia kupunguza umasikini). Japokuwa ni kweli serikali ilijitahidi sana kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za umma za maendeleo bado staili iliyotumika ilijenga dhana kwamba serikali ndiyo iliyokuwa ikifikiri kwa niaba ya wananchi kuhusu njia bora za kufikia maendeleo.
Pamoja na nia njema ya Serikali ya Kijamaa ya wakati ule ya kuondoa umasikini, ujinga na maradhi ilishindikana kufanikiwa kwa namna ya kudumu kwa sababu nayo pia ilitazama suala la maendeleo kwa wananchi wake kwa jicho la usasa zaidi. Kwamba maendeleo yananyesha kama mvua au yanaletwa katika maboksi. Wiki ijayo nitajaribu kuanza kuhitimisha mjadala huu kwa kujenga hoja kwamba maendeleo ya kweli hayaletwi katika maboksi au makontena bali hutokana na fikra, mitazamo, maarifa, ujuzi na juhudi za wananchi wenyewe ambavyo ni matunda ya utamaduni wao unaozingatia asili yao.
Inaendelea
Maoni ya Wasomaji
Utabiri! Huu wala sio utabiri
Utabiri! Huu wala sio utabiri ndiyo yanayotokea sasa tena hapa Tanzania,Wawekezaji are the final decision makers,The government/Parliament are ruber stamps! Watapiga kelele nyingi mwisho wataunga hoja kwa asilimia mia, Hapo kuna logic yoyote ni usanii TUU wa kuombea kura za wajinga ndio waliwao.