Makala
Tafakuri Jadidi
Tumebweteka, twasubiri ‘huruma’ ya Wazungu?
Johnson Mbwambo
Toleo la 239
16 May 2012

TOLEO lililopita niliandika kueleza jinsi mwenye hisa mkuu wa kampuni inayoongoza duniani kwa uchimbaji wa dhahabu, Barrick, alivyojaribu kuitumia Tanzania kuonyesha ‘huruma’ ya kampuni hiyo katika nchi ambako imewekeza.

Mmiliki huyo, Peter Munk, aliuambia mkutano wa mwaka wa wanahisa huko Toronto, Canada, kwamba Barrick imetoa misaada mingi ya hiari katika nchi za Tanzania, Chile, Papua New Guinea na nchi kadhaa nyingine na kwamba, si kweli kuwa kampuni yake  haisaidii lolote katika nchi ilikowekeza.

Nilieleza kuwa alichokieleza Munk katika mkutano huo si ukweli wote; maana katika Tanzania sote tunajua kuwa si tu kuwa uwekezaji wake ni wa kinyonyaji; bali pia ni wa kinyama; huku  nikitoa mfano wa unyama wake katika maeneo ambako ina migodi ya dhahabu.

Katika aya ya tatu kutoka mwisho wa makala hiyo, nilieleza kimakosa kuwa Barrick ilihusika na wale wananchi wa Geita ambao sasa wanaishi kwenye mahema kwenye kambi  iliyopachikwa jina la Darfur baada ya kuwa wamefukuzwa kwenye maeneo yao ya asili kumpisha mwekezaji huyo. Ukweli ni kwamba kampuni iliyohusika ni AngloGold Ashanti na si Barrick.

Japo hulka za uwekezaji wa kampuni hizo za madini za kigeni katika nchi yetu zinafanana, lakini kosa ni kosa tu, na hivyo naomba radhi kwa kosa hilo la kuitaja Barrick badala ya  AngloGold Ashanti. Hata hivyo, suala la sumu iliyowaathiri wanavijiji wa North Mara linaendelea kubaki kuwa ni la Barrick tu.

Baada ya kumradhi hiyo, naomba tuendelee kutafakari zaidi suala la uwekezaji wa kampuni hizo za kigeni za madini katika nchi masikini za Afrika ikiwemo Tanzania yetu.

Wasomaji wangu kadhaa walinitumia ujumbe wa sms na e-mail na kueleza kwamba sikupaswa kumlaumu Bilionea Peter Munk kwa uwekezaji huo wa kinyonyaji na usiozingatia haki za binadamu katika nchi yetu; bali ningewalaumu watawala wetu walioukaribisha uwekezaji huo.

Mmoja alikwenda mbali zaidi na kuniambia kwamba ana uhakika kama Bilionea Peter Munk angeitembelea Tanzania, angelipokelewa na Rais Kikwete kwa kutandikiwa zulia jekundu uwanja wa ndege siku anawasili, na kwamba angealikwa Ikulu kula chakula na Bwana Mkubwa!

Anachokisema huyo bwana ni kwamba, ni watawala wetu wenyewe ambao hujipeleka wenyewe kwa wawekezaji hao wa sampuli ya Peter Munk. Ni sawa na mbwa aendavyo mwenyewe kwa masikitiko kwa Chatu ili akamezwe!

Kimsingi, nakubaliana na hoja ya msomaji wangu huyo. Naamini kabisa kuwa kama watawala wetu wangedhamiria kuukomesha uwekezaji huo wa kinyonyaji wa kina Peter Munk, wangefanikiwa kutuwezesha kuwa na mikataba bora zaidi yenye maslahi makubwa zaidi kwa taifa.

Lakini mara nyingi watawala wetu wamekuwa wakitudanganya kuwa tukidai sana mikataba minono inayotutendea haki katika sekta ya madini, eti hatutapata wawekezaji wakubwa katika sekta hiyo. Eti kwamba, kwa mfano,  tukidai mirahaba ya asilimia 20 au tukidai umiliki wa 50-50 kwenye miradi hiyo ya migodi, hatutapata wawekezaji!

Huo ni uongo unaopikwa na kampuni za kimataifa za kibeberu (MNC) ili kuwatia woga watawala wetu. Ni uongo ambao Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliukataa , na ndio sababu aliamua kuyalinda madini yetu ili tuwe na uwezo wa kutosha wa kifedha na ki-teknolijia tuyachimbe wenyewe.

Kwa bahati mbaya, watawala wetu waliofuatia hawakuwa na subira hiyo ya Nyerere. Hawa ni watawala wanaoangalia miaka 10 tu ya urais wao, baada ya hapo hawajali sana kitakachotokea baadaye. Hawaangalii miaka 50 au 100 mbele.

Ukweli ni kwamba madini si kama hewa tunayovuta ambayo haiishi au kupungua. Madini huisha na yakabakia tu mashimo makubwa ya iliyokuwa migodi.

Na yanapokwisha, kampuni hizi za kibeberu huhamia katika nchi nyingine zilikogunduliwa na kuuendeleza unyonyaji huo huo. Lakini sasa, nchi ambazo bado zina madini hayo ni chache mno, na ndiyo maana hizi kampuni za kibeberu zikibanwa kikwelikweli, hulazimika kukubali masharti ya nchi zenye madini hayo; maana hawana pa kukimbilia.

Kwa hiyo, hoja hizi za watawala wetu kwamba tukidai mirahaba mikubwa zaidi au hata tukidai serikali imilikishwe hisa nyingi kwenye miradi hiyo ya uwekezaji wa kigeni katika sekta ya madini tutakimbiwa, si ya kweli. Ni hofu tu iliyojazwa katika vichwa vya watawala wetu na propaganda za mabeberu.

Na ndio maana, hivi karibuni,  tuliporekebisha sheria yetu ya madini na kudai maslahi zaidi, hatukuwaona kina Barrick na kina AngloGold Ashanti wakisusa na kufungasha virago. Bado wapo, na ni business as usual.

Nina hakika hata tukidai maslahi makubwa zaidi hawawezi kuondoka. Waende wapi wakati kwingineko dhahabu zinakauka kwa kasi? Waende wapi wakati tanzanite duniani inapatikana Tanzania pekee?

Kwa hiyo, tunachohitaji ni ujasiri tu wa watawala wetu kuwachachamalia hawa akina Peter Munk  -  ujasiri ambao, kwa mtazamo wangu, siuoni kwa chama tawala CCM na serikali yake. Ni aina ya  ujasiri ambao naona viongozi wa CHADEMA wanao; hususan Katibu Mkuu wao, Dk. Slaa.
 
Nirudie tena kusisitiza kwamba watawala wetu wakichachamaa, hawa kina Barrick hawana pa kukimbilia. Labda nitoe mfano. Wakati wa kampeni ya urais ya 2010 ya Guinea, mgombea urais, Alpha Conde, aliahidi kuwa akiutwaa urais atahakikisha serikali inamiliki hisa katika kampuni za kigeni za madini.

Kauli yake hiyo ilipokewa kwa vitisho vingi na kampuni hizo za kigeni za madini; huku nyingine zikitisha kwamba zitafungasha virago na kuondoka Guinea kama Alpha Conde atashinda urais!

Alpha Conde aliposhinda urais alihakikisha kuwa ndani ya mwaka mmoja tu wa urais wake, serikali, kwa kuanzia,  inatwaa asilimia 15 ya hisa katika kampuni za migodi za kigeni. Cha kushangaza,  wananchi wa Guinea hawakuona kampuni hata moja ikifungasha virago na kuondoka Guinea!

Kwa nini hawakukimbia kama walivyotishia wakati wa kampeni? Ni kwa sababu kampuni hizi za kigeni katika sekta ya madini barani Afrika hazina pa kukimbilia; maana madini yanazidi kuadimika duniani baada ya kuchimbwa kwa miaka mingi.

Nihitimishe tafakuri yangu ya leo kwa kusema kuwa, tunachohitaji Tanzania kujiokoa dhidi ya uwekezaji huu wa kinyonyaji wa kampuni za kigeni katika sekta ya madini, ni ujasiri tu wa viongozi wetu na si “huruma” ya kina Peter Munk.

Na linapokuja suala la “huruma”, naikumbuka hii nyingine ya wiki iliyopita iliyoonyeshwa na wabunge wa Uingereza kwa maliasili za nchi ya DR Congo – nchi ambayo ni tajiri mno kwa maliasili lakini wananchi wake ni miongoni mwa masikini wa kutupwa duniani.

Nazungumzia hatua ya wiki iliyopita ya kamati maalumu ya wabunge wa Uingereza kuwaita watendaji wakuu karibu 100 wa kampuni  za nchi hiyo zinazofanya biashara ya madini huko DR Congo. Kamati hiyo ya wabunge 11 imewaita ili kuwahoji kuhusu uwekezaji wao kwenye sekta ya madini katika nchi hiyo unaotia shaka.

Uchunguzi huo unatokana na kuibuliwa kwa habari kuwa kampuni ya Kiingereza ya Glencore iliuziwa na Serikali ya DR Congo migodi ya Kansuki na Mutanda (Jimbo la Katanga) kwa bei ya kutupa; yaani isiyoendana na viwango vya bei vya kimataifa.

Kampuni hizo za Uingereza pia zinatuhumiwa kutumia ujanja kukwepa kulipa viwango vya kodi vinavyostahili kwa DR Congo. Tuhuma hizo zilithibitishwa na Waziri wa Madini wa DR Congo, Martin Kaswilulu ambaye alisema kuwa, kwenye mauzo ya mwaka jana ya shaba, kampuni hizo zilipata dola bilioni 5, lakini DR Congo iliambulia asilimia 2 tu ya mapato hayo!

Kashfa hiyo inayoiandama kampuni ya Glencore iliibuliwa na asasi ya wanaharakati inayoitwa Global Witness. Asasi hiyo imeibana Glencore iweke hadharani dili zake za madini nchini DR Congo.

Global Witness inadai kuwa ndani ya mwaka mmoja tu watendaji wakuu sita wa kampuni hiyo wamekuwa mabilionea kutokana na madini ya DR Congo; ilhali mamilioni ya  Wakongo wanaendelea kuteseka kwa umasikini ikiwa ni pamoja na kukosa huduma muhimu za jamii.

Kwa mujibu wa Global Witness, baadhi ya Wazungu wanaonufaika na dili za madini ya DR Congo wameyaficha mapesa yao katika akaunti za siri katika visiwa vya British Virgins. Inadaiwa kuwa, hao ni pamoja na mfanyabiashara wa Israel, Dan Getler ambaye ni “rafiki mkubwa” wa Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa wabunge wa Uingereza wanaounda kamati hiyo, Pauline Latham, alisema ya kuwa wakati sasa umefika kwa pesa zinazotokana na dili za madini nchini DR Congo zibakie huko huko kuiendeleza nchi hiyo badala ya kuishia kwenye akaunti hizo za Ughaibuni.

“If the money from mining deals stayed in the country and was used for the benefit of the people, they would not need aid money from us, and they could be much better off,” ndivyo Latham alivyoliambia gazeti la Guardian la nchi hiyo wiki iliyopita.

Kimsingi, anachosema mama huyo ni kwamba; kama fedha zinazotokana na maliasili za DR Congo zitazungushwa huko huko, nchi za Ulaya hazitalazimika kutoa misaada ya fedha kwa nchi hiyo.

Nina hakika Peter Munk wa Barrick atakuwa amekasirishwa na mtazamo huo wa wabunge wa Uingereza wa kutaka fedha za madini za DR Congo zibakishwe huko huko.

Vyovyote vile, naiombea kwa Mungu  “huruma” hii ya wabunge wa Uingereza kwa DR Congo ifikie mwisho mwema; maana inaweza pia kuifikia Tanzania yetu siku moja! Lakini je; tusubiri mpaka tuonewe “huruma” na Wazungu?

Tafakari.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Johnson Mbwambo
mbwambojohnson@yahoo.com

Toa maoni yako