Makala
Tumejiruhusu kuwa mateka wa wageni
Yahya Msangi
Lome, Togo
Toleo la 190
15 Jun 2011

NAREJEA habari zilizochapishwa na Raia Mwema wiki karibu tatu zilizopita kuhusu kutoroshwa wanyama nje ya nchi. Habari hizo zilinigusa sana.

Kwanza, zimenikumbusha mambo niliyoshuhudia nilipokuwa nafanya kazi katika Sekta ya Maliasili. Pili, nimesoma kwenye mtandao kwamba wahusika waliotajwa wamefikishwa mahakamani. Tatu ni taswira ya tukio hili inayoonyesha kuota mizizi kwa dharau dhidi ya sisi kama Taifa. Nne ni udhaifu wa usalama wa mali na rasilimali tulizokabidhi kwa wawekezaji. Tano, ni jinsi uzalendo ulivyoenda likizo au ulivyoacha kazi nchini mwetu. Nitachambua hoja hizi moja baada ya nyingine.

Hebu tuanze na niliyoshuhudia enzi hizo katika Sekta ya Maliasili. Mwaka 1998 – 2001 Serikali ya Marekani, kupitia Shirika lake la Misaada la USAID, lilibuni mradi wa kutathmini na kufuatilia (assessment and monitoring) idadi ya maliasili na idadi inayovunwa kihalali na kiharamu katika pori moja la hifadhi.

Nilipata fursa ya kuwa Ofisa Mpango (Programme Officer) wa mradi huo. Jukumu langu lilikuwa kuweka mpango wa kisayansi utakaowezesha kuhesabu maliasili kama wanyama, samaki, mimea, wadudu na ndege katika pori hilo la hifadhi.

Nilikuwa pia na jukumu la kuandaa kikosi cha kuzuia ujangili, kukipa taarifa za kisayansi na vifaa vya kisasa vya mawasiliano ili kuzuia ujangili katika hifadhi hiyo. Matarajio ilikuwa kwamba mradi ukifanikiwa uweze kuigwa katika mbuga za hifadhi Tanzania na eneo la Kusini mwa Afrika.

Hapo ndipo nilipojua ya kuwa kuna u-Mafia katika mali asili zetu. ‘Sinema’ yenyewe inaanza hivi: Mhusika mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori (chini ya yule jamaa ambaye baadaye aliingia katika uongozi wa soka). Mara Wizara ikaona kumbe wanaofaidi ni Mkurugenzi na maofisa wake, kwa nini?

Likaanza zogo, ugawaji vitalu ukahamishiwa wizarani chini ya Waziri! Pesa haina bosi bwana, soni inatupwa kando, watu wanavaa uso wa chuma! Hapo ndipo kukatokea kuumbuana, mara fulani anamiliki vitalu, mara wamegawa vitalu kwa wageni nk!

Ikawa sasa kila kambi ina watu wake ambao ni mameneja wa hifadhi! Mara wameruhusu Waarabu kuwinda! Hapo ndipo mameneja na watumishi wa mbuga wakaanza kujipangia mishahara na marupurupu ya kufuru! Nani wa kuwauliza? Hawa jamaa simba wamewakuta, mito wameikuta, lakini wanaona ni stahili yao kujipangia marupurupu ya ajabu!

Wagawaji wote wawili wa vitalu (Idara na Wizara) hawakuupenda mradi hata kidogo! Hawakutaka mahesabu yajulikane! Kwa nini? Hapo kale kulikuwa na retention scheme ambayo kila hifadhi ilikuwa na mgao wake utokanao na mapato na fedha zinazobaki zinaenda kwao. Sikumbuki vizuri lakini nafikiri kila hifadhi ilistahili 7% kwa miaka ile (sijui siku hizi).

Tatizo maharamia wale wa Idara na Wizara hawakutaka mapato halisi yajulikane ili waweze kutia ndani sehemu ya mgao wao. Mameneja wa hifadhi nao hawakupenda idadi ya mapato ijulikane ili nao washibishe matumbo yao. Wanatoa taarifa za uongo kwa Idara na Idara inatoa taarifa za uongo kwa Wizara na hatimaye Hazina inapokea taarifa za uongo!

Yaani ulikuwa ni msururu wa wezi, mwizi anamwibia mwizi na wote wanaiibia Serikali! Kama kuna waandishi watafiti hebu kaulizeni orodha ya wenye vitalu, wanawinda wanyama wangapi na wa aina gani? Ombeni orodha ya watalii, wawindaji, watafiti na watu waliotumia mbuga zetu uone kama watu watakusikiliza!

Uliza mgawanyo wa mapato utokanao na maliasili? Hiyo ni sawa na kumuuliza shetani kama moto wa jehenamu upo?

Hawakutaka pia idadi ya wanyama ijulikane. Si wataulizwa kama simba ni 500 mbona unatoa kibali cha kuua simba 50 kwa mwaka? Si watakwisha? Wanataka ugawaji usiozingatia takwimu; kwani simba, chui, fisi wakiisha kuna ubaya gani kwao? Si watasafiri kwenda Ulaya au Uarabuni kuwaonyesha watoto na wajukuu wao wanyama hao!

Idadi wanayoruhusu iwindwe ikifahamika si watakosa kisingizio kwamba majangili na wanaoishi jirani na mbuga zetu ndio wanaomaliza wanyama wetu? Eti wanaomaliza wanyama wetu ni Wamasai kwa ajili ya mifugo na si wao!

Lakini chuki dhidi ya mradi haikutoka kwa hawa jamaa zetu peke yao. Kuna jamaa wanaitwa PF (professional hunters). Hawa wanakodishwa na makampuni au watu binafsi Ulaya, Marekani, Japan na kwingineko kuwaletea wanyama au viungo vyao.

Hii mi-PF hata kwa hulka yao tu ni mijitu roho ngumu! Wengi ni katili ile mbaya; japo Wazungu! Wanaingia na kutoka Idara ya Wanyamapori na Wizarani utafikiri bafuni kwao! Ina mahusiano makubwa pia na makampuni yaliyopewa vitalu. Siku ikiingia utafikiri the eagles have landed !

Bunduki za kila aina, misuruali na mikofia ya kaki! Hawa huwa wanakuja na maombi ya idadi ya wanyama wanaowataka kufuatana na oda za wateja. Mara nyingi oda ni kubwa sana na ni za wanyama mbalimbali au viungo vyao. Kupitia wamiliki wa vitalu wanapewa idadi (quota) lakini mara nyingi haikidhi mahitaji ya wateja wao.

Hapo ndipo dili inachezwa; tunakupa simba dume wawili lakini unaweza kuua kumi au jike, au jike mwenye mimba au simba mtoto; hivyo toa ten percent kwanza. Hadithi ya ngoja niwinde kwanza haipo!

Naye huyu PF akifika mbugani ana kikwazo ambacho lazima atatue. Si kuna meneja wa hifadhi, kikosi cha kuzuia ujangili na wahudumu (guides)? Hawa lazima wawekwe sawa ili wafumbe macho na washiriki kuwinda zaidi ya kibali!

Nilishuhudia jioni moja hawa guides wakipewa 1000 USD wagawane! Furaha tupu porini! Risasi zinapigwa juu hewani utafikiri Mizrata, Baghdad au Sanaa! Pesa uongo, sabuni ya roho! Basi baada ya sherehe uwindaji halali na haramu unaanza! Nina uhakika hata ufisadi huu uliofichuliwa na Raia Mwema uliendeshwa kwa mtindo huu. Tusubiri matokeo ya kesi!

Lakini cha msingi hapa ni kufumua mfumo uliopo. Ikibidi uwindaji usitishwe kwa miaka 10 (Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusitisha) ili kutoa fursa kwa wanyama kuzaliana na kuweka mfumo mzuri usioruhusu hujuma za aina hii. Tusipobadili mfumo tusishangae siku moja tukawa kama nchi ambazo hata mjusi hazina!

Sasa tuzungumzie suala la pili – kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa. Hili limenigusa kwa kuwa wamefikishwa mahakamani baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa umma na gazeti la Raia Mwema! Yamkini shinikizo hilo pia limetoka kwa vyombo vya kimataifa vyenye wajibu juu ya maliasili.

Mara nyingi serikali zetu hizi za Kiafrika zinapochukuwa hatua ya namna hii matokeo huwa kinyume na matarajio ya wengi. Niseme tu, tusishangae mashtaka ya hovyo yakaandaliwa (kwa makusudi) na jamaa wakaachiwa huru. Muda utakuwa mwalimu mzuri.

Lakini cha msingi hapa tulazimishe serikali hiyo ya Kiarabu irudishe wanyama wetu kwa gharama zao wenyewe. Kuna sheria za kimataifa kuhusu hili. Masikini nembo yetu ya Taifa, Twiga! Imeibwa au imetolewa kirahisi? Masikini Tanzania na watu wake! Mungu atatubariki vipi kama tunauza au tunaruhusu nembo ya Taifa itoroshwe? Twiga Stars kaeni chonjo msije nanyi mkauzwa au kutoroshwa!

Sasa, jambo la tatu lililonikuna - inasikitisha eti hata jirani zetu wametudharau kiasi cha kuuza wanyama wetu! Hebu fikiria kuna mtu angethubutu kuuza wanyama wa Nairobi Game Reserve au Masai Mara? Yaani jirani yako achukue paka, mbwa, mbuzi, kuku na ng’ombe wako halafu amshirikishe mwanao na mgeni aliyeomba hifadhi nyumbani kwako kuwauza kijiji cha jirani? Hii ni dharau ambayo kwa bahati mbaya tumejitakia.

Hii inatokana na tabia na hulka yetu ya kuthamini vya wageni (hata wageni malofa kutuzidi). Angalia kwenye elimu ya watoto wetu ndio utatambua uzuzu wetu; kwenye shule zetu wenyewe tumewakabidhi wao! Kisa? Wanajua Kingereza! Jamani hiki Kingereza chenye lafidhi mbaya ndicho kinatuzuzua hadi tujidhalilishe hivyo?

Mbona dunia inapenda Kingereza cha Watanzania zaidi! Lafidhi yetu ya Kingereza haina harufu ya kabila lolote wala hatuigi lafidhi ya wenye lugha yao. Kumbukeni Kingereza cha Mwalimu Nyerere au hata cha Ben Mkapa mtatambua tunu tuliyonayo, lakini hatuitambui!

Kingereza chetu saafi! Wengi wanatuheshimu kwa kutukuza lugha yetu ya Kiswahili, hili nalo hatulitambui kutokana na uzuzu wetu! Msahau kwao ni mtumwa!

Nakumbuka 1997 – 98 nilikuwa Katibu wa Watanzania waishio Ireland. Tuliandaa sherehe mwaka 1998 kuwakaribisha Watanzania waliofika kwa masomo na kujiandaa kwa ujio wa Mwalimu Nyerere Ireland. Nakumbuka matangazo ya wenyeji wake kwenye kuta na vyombo vya habari; Come and See the Pride of Africa, the Special One’.

Na sisi katika kumuenzi Mwalimu Nyerere tulialika wageni wa mataifa mbalimbali na sherehe ilianza kwa Watanzania kujitambulisha kwa kueleza majina, mkoa wanaotoka nyumbani, wanavyoipenda nchi yao na tofauti kati ya Tanzania ya Mwalimu Nyerere na nchi nyingine za Afrika.

Wote walieleza uzuri wa Tanzania – lugha, haki, fursa sawa kwa wote, umoja, undugu, n.k. Ikafika zamu ya vibinti viwili (tena watoto wa wanasiasa wanawake). Acha watutie aibu! Kamoja kakaanza kwa kusema ‘mtanisamehe kwa lafidhi yangu kwa kuwa naongea Kingereza kama Wamarekani! Ka pili kakasema I hate Tanzania and I don’t want to go back because there are no opportunities like those which are available here!

Mama yangu! Kama mkuu wa shughuli nilitamani ardhi ichimbike nipotee! Lakini, uzuri wa waridi hauharibiwi na mbolea ya kinyesi cha kiti moto! Bila subira, alisimama mama wa Kizungu akatoa macho na kumwambia wa kwanza kwa Kiswahili fasaha: ‘Wewe Kingereza chako ni kibovu mno kufananisha na Kingereza cha Wamarekani ambacho nacho ni kibovu mno kufananisha na cha Waingereza’! Na hata ungeweza kuongea Kingereza cha Wamerakani kamwe hutakuwa Mmarekani’. Hapa Ireland tunaongea Kingereza na bado wajinga wengi’.

Na Yule wa pili akamwambia: ‘Mimi nilizaliwa hapa na sikuona hizo fursa unazoziona wewe ambaye una wiki moja tu toka ufike hapa’. Fursa yangu ya kwanza na nafikiri ya mwisho niliipata Tanzania kama Volunteer !

Wote tuliokuwepo tulilipuka kwa shangwe! Vibinti vile vilinywea kama pimbi! Sikuwaona siku ya mkutano wala cocktail ya Mwalimu Nyerere. Nimesema hili kwa urefu kuonyesha tunavyoweza kujidharau wenyewe na pia jinsi kile tunachodharau kinavyoheshimiwa na wengine!

Hakika sisi ndio tungepaswa kudharau majirani wetu; wanakuja kutafuta kazi kwetu, wanakuja kutafuta hifadhi kwetu na wanapogombana tunawalisha kutokana na kilimo chetu. Watanzania wenzetu watoa huduma na wafanyabiashara waonyeshe uzalendo, watoe ajira kwa Watanzania.

Serikali nayo iwakataze makampuni ya kigeni kuajiri wageni; mbona kwao wanakotoka kuna sheria kali kuhusu hili? Tuache kujidhalilisha wenyewe kwani itakuwa rahisi majirani kutudharau.

Suala la nne: Usalama wetu. Tukio hili linapaswa kutushtua kama Taifa kuhusu usalama wa mali na watu wetu. Kama katika uwanja wetu wa Kimataifa watu wameweza kupakia mnyama mkubwa na mrefu kama twiga bila kukamatwa, ndege ya jeshi la nchi nyingine imetua na kuruka bila kuzuiwa na vikosi vyetu vya usalama (ambao taarifa za kiintilijensia kwao si tatizo) na kama wananchi wetu na vyombo vyetu vya usalama vimeweza kushiriki katika uhalifu huu (haiwezekani jeshi la nchi nyingine lifike nchini bila jeshi letu na vyombo vya usalama kujua) basi hatuko salama kiulinzi.

Ni madudu gani yanayohatarisha usalama wetu na wa mali zetu unaotokea kwenye migodi? Mbuga zetu nyingine?, mabenki yetu?, mashirika yetu? Makambi yetu ya kijeshi? Hivi kweli tukivamiwa leo na nduli mwingine (na si kwamba nia hii haipo) tutamudu? Nikitembelea na kuongea na baadhi ya Waganda napata hisia kuna dukuduku na hasira dhidi yetu! Wanaona tuliwadhalilisha wakati wa vita ya Kagera, wanaona tuliharibu taifa lao na kama vile wanasema ngoja, ipo siku!

Nani leo atajua adui kaingia kama wamefika KIA na kuondoka na ushindi? Nani leo atawashawishi Watanzania adui aliyetuvamia ni adui yetu sote? Nani leo atawashawishi Watanzania watoe ng’ombe na mali zao kwa hiari kumkabili adui? Si tumeanza kupigana wenyewe? Si tumeanza kugeuza usalama wa Taifa letu suala la masihara na dili? Si tumeshatengeneza maadui na uadui miongoni mwetu?

Vyombo vya dola vilivyoheshimika na raia vimeanza kujenga uadui wa kutisha kati yake na raia? Si vyombo hivi vimeanza kuua raia potelea mbali hata kama raia hao wana makosa? Nchi ikiingia vitani hata wafungwa wanapewa msamaha ili washiriki kulinda Taifa au sio? Ee Mola tuepushe asije nduli mmoja akafikiria kutuvamia sasa! Atatukuta tumegawanyika na kuhasimiana kiasi wengi watakula ngumu au hata kumsaidia adui!

Haya suala la tano na la mwisho lililonikuna! Hivi ule uzalendo wetu umeingia pori gani? Yaani kwa pishi ya mchele na kibaba cha dona tumesaidia nembo ya Taifa iibiwe? Kwani twiga mchezo? Lazima mijibaba ya nguvu ilijitolea toka huko mbugani. Huenda wengine waliumia katika kazi hiyo au walinyewa na wanyama hao!

Katika kuwasafirisha lazima walivuka vizuizi vingi vya polisi barabarani, trafiki na polisi uzalendo mliacha depo? Vibaya hivyo! Ili ndege iruhusiwe kutua lazima kuna watu waliiongoza au siyo? Pale uwanjani kuna Watanzania wengi tu wanafanya kazi ingekuwaje kama wote wangetoka na kusema tunaomba vibali vya wanyama hawa? Kwa nini mnapakia wanyama usiku? Dili lingekwama! Jeshi letu ni kweli halikujua kuna ndege ya jeshi la kigeni ipo KIA? Mbona wakati wa uchaguzi wa mwaka jana tuliwaona makamanda wakiwa sharp namna ile? Vipi mkuu? Je Ikulu haikujua mali ya mfalme ipo nchini? Yaani waje tu bila kubisha hodi kama nyumba haina mwenyewe? Hata mochuari tunabisha hodi jamani pamoja na kuwa tumefiwa! Wazee wa intelijensia je? Mbona wamejaa pale KIA na jirani Mererani kibao? Au mnamlinda AFGEM basi! Hivi kweli tumeichoka Tanzania yetu kiasi hicho?

Viongozi onyesheni uzalendo na raia watawaiga! Wabunge onyesheni uzalendo kwa nchi si chama na mtakuwa mmetoa somo zuri kwa raia. Askari onyesheni uzalendo kwa Taifa na si watawala nanyi mtabarikiwa milele! Serikali rudisheni masomo yenye kuibua uzalendo na mtakuwa mmeliokoa Taifa!

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Yahya Msangi
+255-0816529
yahya.msangi@ituc-africa.org

Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa muda mrefu wa gazeti hili la Raia Mwema na mchangiaji mada mbalimbali gazetini humu. Ni Mtanzania anayeishi Mji wa Lome, nchini Togo, akiwa anafanyakazi katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (Organisation Re'gionale Africaine de la Confe'de'ration Syndicale Internationale (CSI - Afrique)

Toa maoni yako