WIKI iliyopita niligusia mashinikizo matatu ambayo naamini ndiyo yalipelekea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.
Mashinikizo hayo ni mosi, wafadhili, pili, majemedari wa mageuzi, na tatu, Mwalimu Julius Nyerere. Nilitumia neno kurejeshwa kwa sababu vyama vingi vya siasa vilikuwapo kabla na baada ya uhuru. Ingawa TANU ndicho kilikuwa chama kikubwa kwa upande wa Tanganyika, lakini vilikuwapo vyama vingine kama UTP na ANC. Hata Zanzibar, vyama vikubwa vya siasa vilikuwa ZNP, ASP, na ZPPP.
Viongozi wengi walioongoza nchi za Afrika mara tu baada ya uhuru, waliviona vyama vingi vya siasa kama kielelezo cha kukosa umoja wa kitaifa. Hivyo, yaliwekwa mazingira ya kuvidhoofisha na mwishowe kuongoza chini ya chama kimoja.
Mfano, Rais Jomo Kenyatta wa chama cha KANU nchini Kenya, aliwaendesha puta na kuwanyamazisha viongozi wa chama pinzani cha KADU. Pia, Rais Kwame Nkrumah wa chama cha CPP cha Ghana, Rais Nyerere wa chama cha TANU, na wengineo, walifanya hivyo hivyo.
Binafsi sioni ushahidi wa dhana kwamba vyama vingi vya siasa vilikuwa ni kielelezo cha kukosa umoja wa kitaifa. Pia, sioni ushahidi kuwa mfumo wa chama kimoja pekee ndio ambao ungeleta umoja wa kitaifa katika nchi za Afrika.
Mfano, kwa Tanzania, nafikiri staili ya uongozi uliokuwa na maono yasiyo kifani, na ulioweka maslahi ya wananchi mbele kuliko ya watu wachache, ndio uliounganisha juhudi na matarajio ya Watanzania ili kuleta umoja wa kitaifa tunaojivunia. Mfumo wa chama kimoja chini ya staili za uongozi tulioshuhudia miongo ya karibuni, kamwe, usingeweza kufanikisha azima hii.
Mfano, mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha KANU nchini Kenya, haukuleta umoja wa kitaifa kwa sababu ya staili za uongozi. Chini ya KANU, uwezo wa mtu kuongoza katika ngazi yoyote, ulipimwa kutokana na kabila lake au uwezo wake wa kifedha. Ajabu, chini ya mfumo wa vyama vingi, idadi ya Wakenya wanaopima viongozi kutokana na uwezo wa kuongoza, na wala si kabila au fedha, inaongezeka kiasi cha kuleta matumaini ya umoja na mshikamano wa kitaifa.
Nilipata kusoma maandishi ya Ali Mazrui kuwa, Nyerere aliamini kwamba, demokrasia ya mfumo wa chama kimoja ingeweza kuwa bora na kuwafaa wananchi kama iwafaavyo, au pengine kuzidi demokrasia ya mfumo wa vyama vingi. Kwa upande mmoja, imani hii ina ukweli. Mfano, ingawa kuanzia mwaka 1990 mpaka 1992, Zaire ilikuwa na vyama rasmi vya siasa 123, lakini ubora wa demokrasia yao usingefua dafu mbele ya demokrasia ya chama kimoja nchini Tanzania. Hii inatokana na ukweli kwamba vyama vingi Zaire havikuwa tunda la msukumo wa Wazaire bali shinikizo kutoka nje.
Hata hivyo, binafsi naamini kuwa, hakuna demokrasia inayoweza kuwa bora na kuwafaa wananchi zaidi ya ile iliyotokana na msukumo wa wananchi wenyewe. Wananchi wakiona kuwa wakati fulani ni muafaka wa kuwapo demokrasia ya mfumo wa chama kimoja, vyama vingi, au mfumo wa jamii usio na chama chochote cha siasa, basi demokrasia ya namna hii itawafaa wananchi kuliko demokrasia inayotoka nje, hata kama ni nzuri kiasi gani. Hivyo basi, utashi wa wananchi unatakiwa usiwe na mbadala.
Mfano, ingawa Marekani ni mojawapo ya mataifa yaliyoshinikiza demokrasia ya vyama vingi katika Afrika, lakini msingi wa taifa la Marekani haukujengeka katika demokrasia ya chama chochote cha siasa. Wamarekani walifanikiwa kumung’oa mkoloni, na hata kuasisi taifa lao bila kuwapo chama chochote cha siasa. Rais wa kwanza George Washington, alimaliza kipindi chake cha urais bila ya kuwapo chama cha siasa. Hata hivyo, misingi mikubwa iliyowekwa na waasisi wa taifa la Marekani miaka 200 iliyopita, ndiyo inayoliongoza taifa la Marekani mpaka leo.
Ingawa sasa hivi Marekani inaendeshwa chini ya demokrasia ya vyama vikuu viwili vya siasa (Democratic na Republican), lakini ndani ya Katiba ya Marekani, hakuna mahala palipoandikwa maneno “vyama vya siasa” (political parties). Badala yake, maneno yanayotumika ni “wawakilishi wa wananchi” ambao ni wabunge. Muswada wa haki (bill of rights) umehifadhi haki za Wamarekani, kwa hiari yao, kujumuika katika umoja wa aina yoyote ili kutimiza malengo yao. Nafikiri tafsiri ya muswada wa haki ndio chimbuko la umoja wa vyama vya siasa.
Katika hotuba yake ya kustaafu, Rais George Washington alionya Wamarekani kutokuendekeza vyama vya siasa. Alikuwa na wasiwasi kuwa vyama vya siasa vingeweza kuwekwa kwapani na makampuni makubwa, hivyo kutelekeza kusudio la uongozi ambalo ni kuwatumikia wananchi. Naam! Wosia wa Rais Washington umekuwa kama jinamizi linalowatafuna Wamarekani ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Yamekuwapo malalamiko kutoka wa Wamarekani kuwa vyama vya siasa vimepoteza mwelekeo kwa sababu ya kutumikia mashirika na makampuni makubwa.
Kabla ya uhuru, raia wengi katika Afrika waliona umuhimu wa kuanzisha vyama mbalimbali ili kuunganisha juhudi zao za kumung’oa mkoloni. Azima yao ilifanikiwa kwa sababu msukumo wa kuanzisha vyama vingi vya siasa ulitokana na Waafrika wenyewe na si vinginevyo. Ndiyo maana naamini kwamba, demokrasia ya mfumo wa vyama vingi katika Afrika, isingeondolewa mara tu baada ya uhuru. Badala ya kufuta vyama vilivyoanzishwa na wananchi, ingewekwa kanuni ya kikatiba ambayo ingetoa dira kwa vyama vya siasa kupigania maslahi ya wananchi na kujenga umoja wa kitaifa.
Sasa tatizo linalozikabili nchi nyingi Afrika ni kwamba, mara tu baada ya uhuru, misingi iliyosimikwa ililenga kuimarisha demokrasia ya chama kimoja cha siasa. Raia waliandaliwa kisheria, kielimu, kiutamaduni, na mengineyo, kuukubali mfumo wa chama kimoja cha siasa. Watawala wengi wa Afrika hawakuwa na ndoto kwamba siku moja kunaweza kutokea mabadiliko na kuleta demokrasia ya vyama vingi. Hivyo basi, raia wengi wa nchi za Afrika pamoja na watawala wao walikuwa hawajajiandaa kuupokea mfumo wa vyama vingi. Mafuriko ya mashinikizo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kutoka nchi wafadhili na mataifa ya Magharibi, yalizikumba nchi za Afrika bila kuwa na maandalizi ya kutosha ya kubadili misingi iliyovilea vizazi vilivyofuatia baada ya uhuru.
Mashinikizo kutoka kwa wafadhili yaliyoambatana na ahadi za fungu la fedha, yaliziweka serikali nyingi za Afrika katika njia panda. Kama tunavyokumbushwa katika hadithi ya sungura mjanja, na fisi mlafi aliyekuwa na njaa, huku akitokwa na udenda baada ya kuona kipande kinono cha nyama choma. Sungura alimwambia fisi afumbe macho na kuachama ili awekewe kipande cha nyama choma mdomoni. Fisi alipotii amri ya sungura, hakuwekewa kipande cha nyama bali kaa la moto, kinyume cha makubaliano.
Kama bibi yangu alivyo nihadithia kwa Kihaya, fisi alibaki njia panda huku akiunguzwa na kaa la moto mdomoni. Sungura alimwambia fisi “chwa nu”, fisi alijibu “nchwe obunuzi”, sungura alisema “mila nu”, fisi alijibu “mile omulilo”. (Tafsiri isiyo rasmi; sungura alisema “tema basi”, fisi alijibu “niteme utamu”, sungura alisema “meza basi”, fisi alijibu “nimeze moto”).
Baada ya kaa la moto kudhoofisha mdomo wa fisi, sungura akaanza kujitafunia kipande cha nyama choma wakati fisi akimkodolea macho na hana la kufanya.
Serikali nyingi za Afrika zilikuwa mithili ya fisi mwenye njaa. Kaa la moto ni vyama vingi vya siasa. Kipande cha nyama choma ni burungutu la fedha kutoka kwa wafadhili. Na sungura mjanja ni nchi wafadhili. Serikali zilitamani donge nono la fedha (utamu), lakini hazikupenda mfumo wa vyama vingi vya siasa (moto). Matokeo yake, raia wa nchi za Afrika waliburuzwa kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Swali la msingi ni je, serikali za Afrika ziliwekewa kaa la moto badala ya fedha za misaada walizoahidiwa na wafadhili? Jibu lake ni ndiyo. Kumbuka wafadhili walikuja na mpango wa kujikwamua kiuchumi uitwao SAP (Structural Adjustment Program). Kama Waswahili wasemavyo, si vyote ving’aavyo ni dhahabu.
Kusudio la SAP lilikuwa kukusanya madeni ambayo nchi za Afrika zilikuwa zikidaiwa. Serikali zililazimishwa kubana matumizi, na kuwaamuru wananchi kuchangia huduma muhimu za jamii kama afya na elimu. Mpango wa SAP ulipokamilika, nchi nyingi za Afrika zilikuwa mahututi kiuchumi, wakati wafadhili wanajitafunia donge lao nono la fedha walizokusanya.
Kutokana na pupa ya kukimbilia fedha, vyama vingi vilikubaliwa bila kuwapo juhudi za dhati za kushauriana na wananchi ili kuweka misingi bora ambayo ingeweka mazingira mazuri ya ustawi wa mfumo mpya. Badala yake, mfano kwa Tanzania, Katiba iliwekewa viraka vinavyopingana na dhana nzima ya mfumo wa vyama vingi. Sheria nyingi za mfumo wa chama kimoja ziliendelea kutumika katika mfumo wa vyama vingi.
Mfano, bado sioni mantiki katika sheria iliyomzuia Abdulrahman Mohamed Babu (Mungu airehemu roho yake), asiweze kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa 1995 kama mgombea mwenza wa Augustine Mrema kupitia tiketi ya NCCR-Mageuzi. Au kwa nini Serikali haikuridhia mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya kufuta sheria zote 40 ambazo zisingetufaa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa?
Lazima tufikie mahala tukubali kuwa misingi iliyoambatana na kuja kwa vyama vingi vya siasa ni mibovu na haikutokana na mashauriano au ridhaa ya wananchi. Kudhani kuwa mabadiliko ya vyama vya siasa pekee katika usukani wa kuongoza nchi bila mabadiliko ya misingi mibovu isiyoweka mazingira ya haki kwa raia, yanaweza kuleta mabadiliko ya maana, ni sawa na kubadilisha mavazi kwa lengo la kuondoa harufu mbaya ya kikwapa.
Ndiyo maana hata vyama vya upinzani vinapochukua madaraka katika baadhi ya nchi, mambo yanabakia vilevile au wakati mwingine hali inakuwa mbaya zaidi, kwa sababu kinachobadilika ni vyama lakini misingi inabaki vilevile. Mfano, vyama kama UNIP chini ya Rais Keneth Kaunda wa Zambia na MCP chini ya Rais Kamuzu Banda wa Malawi vilikuwa na matatizo ya utawala wa kiimla. Lakini matatizo ya vyama vilivyowapokonya madaraka vya MMD chini ya Rais Fredrick Chiluba na UDF chini ya Rais Bakili Muluzi, yalikuwa makubwa zaidi yaliyogubikwa na rushwa ya kiwango cha juu.
Mzee Mwinyi aligusia suala la amani na utulivu akijaribu kulihusisha na misingi bora aliyoiweka. Si rahisi kuamini kuwa miaka si mingi iliyopita, Serikali iliwalipia karo na kuwasafirisha wanafunzi kutoka kona moja ya nchi mfano Karagwe kwenda kusoma kona nyingine ya nchi mfano Dar-es Salaam. Kwamba wanafunzi waligharamiwa kifungua kinywa kabla ya kuingia darasani na chakula bora cha mchana pamoja na matunda yaliyoliwa na kusaza. Kwamba kila shule ilikuwa na idadi ya kutosha ya vifaa vya maabara kwa ajili ya majaribio.
Kwamba ama ndani au maeneo ya karibu ya kila shule, kulikuwa na zahanati zilizokuwa na mganga pamoja na madawa ya huduma ya kwanza kwa wanafunzi. Kwamba kila mwanafunzi wa chuo kikuu alipewa fungu la fedha ya kujikimu, ambalo wakati mwingine, lilizidi mshahara ambao angeanza nao baada ya kuhitimu.
Kwamba viongozi wengi wa ngazi za juu serikalini kama Rashidi Kawawa, Salim Ahmed Salimu, Joseph Warioba, Edward Sokoine na wengineo, pamoja na udhaifu wao wa kibinadamu, hawakuwa na tamaa ya utajiri wa haraka. Waliaminiwa na wananchi na wakaaminika.
Kwamba maazimio mengi ya sera za chama tawala CCM yalitokana na wanachama wenyewe, na yalilenga kukuza ustawi wa jamii ya Watanzania. Mfano, Azimio la Musoma lililolenga elimu kwa wote na kukuza maarifa ya ufundi na sayansi, Azimio la Iringa ambalo mkazo wake ulikuwa ni kilimo, na Azimio la Arusha ambalo lilitilia maanani hasa siasa ya kujitegemea na kukataa dhana ya kwamba fedha ndio msingi wa maendeleo.
Waswahili wanasema usione vyaelea, vimeundwa. Sifa zote nilizotaja na nyinginezo zinazofanana na hizi, ndizo ziliwafanya Watanzania wakatulia tuli kama maji ya mtungi, wakiwa na matarajio ya hali bora za maisha yao ya baadaye. Hata familia zilizokuwa hohehahe, zilikuwa hazibughudhiwi na utajiri wa majirani. Kila mzazi aliweka jembe begani akiwa na uhakika kuwa watoto wake watapata elimu bora, na kuwa na matarajio kwamba, siku watoto wao wakimaliza shule, watapata kazi nzuri ili wajikwamue wenyewe pamoja na familia zao. Binafsi naamini hii ndiyo maana halisi ya amani na utulivu. Kinyume cha hapo, hakuna kitu kinaitwa amani na utulivu.
Lakini misingi iliyowekwa ya kufuata sera za kibeberu za SAP au maazimio ya wafadhili ya Rome na Paris, ilifuta matumaini na matarajio ya Watanzania. Chini ya SAP, wazazi walishindwa kuandikisha watoto wao shuleni kwa sababu ya ukosefu wa karo. Zahanati ziliondolewa shuleni na hospitali hazikuingilika tena. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, viongozi walianza kuweka misingi ya kujihusisha na matendo ya waziwazi ya uporaji mali ya wananchi, au wakati mwingine walishirikiana na makampuni ya nje kuwatapeli wananchi.
Mfano, madini ya dhahabu na fedha ya kigeni vilivyokuwa na thamani ya shilingi milioni 172.6 vilikamatwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Augustino Mrema (Sunday News June 23, 1991). Waziri Mrema alisema mali iliyokuwa inatoroshwa nje ilikuwa ni ya vigogo.
Ardhi ya Loliondo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 4666, iliuzwa au kukodishwa kwa raia wa nje kwa bei ya chee (Mfanyakazi Januari 20, 1993).
Ni kipindi hicho ambacho wananchi waliotumia silaha za kujihami kama visu, vijiko, umma, mapanga, na mashoka, tena bila mafunzo ya aina yoyote, walilazimishwa kulala nje chini ya mwavuli wa Sungusungu, ili kupambana na majangiri yaliyotumia bunduki aina ya SMG. Jeshi la Polisi ambalo kazi yake kubwa ni kulinda usalama wa raia, halikuwa na msaada wowote kwa wananchi. Ni kipindi hicho ambacho misingi ya amani na utulivu ilianza kubomolewa.
Ama kweli dalili ya mvua ni mawingu. Zamani tulijiaminisha kuwa ni Serikali za kidikiteta kama za akina Samwel Doe ndizo zilizoua raia wasiokuwa na hatia. Kumbe hata Serikali iliyochaguliwa na wananchi kama ya Benjamin Mkapa, inaweza kushindwa kuwa na uvumilivu wa kisiasa na kuua raia wasio na hatia kama ilivyokuwa Zanzibar. Zamani tulidhani kuwa ni jeshi la mamluki kama lile la Iddi Amini, ndilo liloua raia na kupora mali zao. Kumbe hata Jeshi letu la Polisi, ambalo ni la wananchi, linaweza kuwageuzia kibao raia wasio na hatia kama ilivyotokea katika mauaji ya Sinza, Kijiweni.
Ingawa muda umetutupa mkono, lakini naamini bado hatujachelewa. Tuache majigambo yasiyo na mantiki ya kudhani kuwa taifa letu limekalia misingi ya amani na utulivu, wakati ukweli ni kwamba tumekwisha kuibomoa. Tushauriane na wananchi jinsi ya kuweka misingi imara itakayo linusuru taifa kutoka katika ukingo wa shimo lisilo na kitako.
Toa maoni yako