Tahariri
Tunahitaji siasa CUF
John Bwire
Toleo la 217
14 Dec 2011

TUMEANZA safari ya kuelekea kuanza mwaka wa 51 baada ya kuadhimisha miaka ya 50 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika. Kwa sehemu kubwa, sote tunajivunia kubaki katika amani na utulivu kwa muda wa miaka yote 50.

Sote kama raia wa nchi huru tumepeana salamu za pongezi na hata lawama au ukosoaji, kuhusu mwenendo wa nchi, viongozi wetu na hata taasisi nyeti hususan, mihimili ya taifa.

Inashangaza, siku chache baada ya kukumbushana hayo na kutakiana heri kwenye safari mpya ndefu, baadhi ya wenzetu katika Chama cha Wananchi (CUF), wameonekana kukosa ustaarabu.

Achilia mbali wao ni raia wa nchi moja, lakini wao pia wanachama wa chama kimoja sasa wanawezaje kuacha kupambana kwa hoja za kisiasa na badala yake, wanapambana kwa silaha za jadi?

CUF jijini Dar es Salaam wameingia katika mvutano uliosababisha matumizi ya nguvu miongoni mwao kiasi cha kutiana ngeu.

Inaelezwa, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, anayetajwa kuwa na nia ya kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa CUF, inayoshikiliwa kwa sasa na Maalim Seif Shariff Hamad kwa muda mrefu, ametiwa misukosuko.

Hamad Rashid alikuwa katika ziara ya baadhi ya kata za chama hicho wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, ziara ambazo kwa mujibu wa taarifa zilizopo, haziwafurahishi baadhi ya viongozi wenzake wa CUF, wakiamini anafanya kampeni ili ashinde kiti cha Katibu Mkuu, dhidi ya Seif ambaye naye anatarajiwa kugombea tena.

Hatutaki kuingilia taratibu za CUF kuhusu ziara za viongozi wake au kuhusu namna ya kuendesha kampeni za kuwania madaraka ndani ya chama hicho.

Hatuna mpango wowote wa kujihusisha na siasa za ndani ya CUF, lakini hata hivyo, kama sehemu ya Watanzania, hatupendi kuona vyama vinavyotarajiwa kupewa uongozi wa nchi, vikishindwa hata kujidhibiti na kuvaa taswira ya amani, utulivu na siasa za kistaarabu.

Lazima tuwakumbushe kuwa, ili uheshimike binafsi au taasisi fulani iheshimike mbele ya umma ni lazima kwanza wao binafsi wajenge imani kwa umma kwamba ni wastaarabu miongoni mwao. Ni wenye kujali misingi ya demokrasia. Ni waumini wa siasa za kupingana kwa hoja bila kupigana.

Kitendo cha wana-CUF kushambuliana wao kwa wao si ishara nzuri katika mwelekeo wa siasa za Tanzania.

Hatutaki kuona madaraka yakitafutwa kwa mapanga au silaha yoyote, tena ndani ya vyama vya siasa. Tunataka kuona madaraka ya uongozi yanatafutwa kwa ushindani wa nguvu ya hoja na ahadi zenye kupimwa kama kweli zinatekelezeka.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
John Bwire
jbwire@raiamwema.co.tz

Maoni ya Wasomaji

Muandishi usiwe mnafiki kila chama kina matatizo yake ndani ya Chama musilichukulie hili la Hamad Rashid kuwa Big dial kwa vile wote ni Wazanzibar , muna yenu mengi yakujadili kama vile kifo cha Tanganyika na kuitawala Zanzibar kinguvu bila ridhaa za wananchi wenyewe.
 

Toa maoni yako