AYUB Rioba ni mwanazuoni aliyebobea katika sayansi ya ukusanyaji, uchakatuaji, utunzaji na usambazji wa habari kwa umma; ni mhadhiri wa siku nyingi katika sekta hii; na kwa sasa tayari analo taji la tasnifu ya uzamivu kichwani mwake.
Mwaka jana tulipokutana Humburg Ujerumani katika kongamano la wanahabari alikuwa na haya ya kusema :
“Wanazuoni mamboleo wanapenda kuhusisha vyombo vya habari na majukumu kama vile… kufanya doria za kikachero katika jamii, kuibua ajenda za maana, kuibua mijadala mtambuka kuhusu mitazamo anuai, kutoa nafasi ya watawala kuhojiwa na umma, kutumika kama jukwaa la wananchi kubadilishana mawazo, na kutoa motisha kwa wananchi ili wajifunze na kushiriki katika michakato ya kisiasa, (kiuchumi, kijamii, kijinsia, kiutamaduni na vinginevyo).
Hata hivyo, baada ya kusema hivyo, Rioba alionekana kusikitishwa sana na jambo moja kubwa kuhusu namna ambavyo vyombo vya habari vinatekeleza majukumu haya nchini na nje ya nchi pia.
Aliongeza Rioba: Vyombo vya habari… kwa sehemu kubwa, vinatoa mchango haba katika (ustawi wa) demokrasia kwa sababu ya udogo wa hadhira vinayoifikia kwa wakati mmoja, maudhui yasiyokidhi viwango stahiki, na kudhibitiwa na vyombo vya dola, (kama si kudhibitiwa na vyombo vya makanisa na/au misikiti).
Rioba yuko sahihi. Na kwa mtazamo wangu, miongoni mwa sababu hizi tatu alizozitaja, sababu kubwa kuliko nyingine mbili, ni ile ya “maudhui yasiyokidhi viwango stahiki”.
Anachokiongelea hapa Rioba ni tatizo la ufidodido wa fikra miongoni mwa wanahabari na watafiti baki.
Katika makala hii nataka kutumia mfano wa makala mbili za magazeti ili kuonyesha urefu na upana wa tatizo hili la “maudhui yasiyokidhi viwango stahiki”.
Makala ya kwanza iliandikwa katika gazeti la kiongozi toleo namba 44 ikiwa na kichwa cha maneno: “Viongozi wa Dini Wataja Vigezo Katiba Mpya”.
Katika makala hiyo mwandishi alieleza yafuatayo:
"Viongozi wa dini mbalimabli nchini wamesisitiza kuwa katiba inayotakiwa itumike Tanzania ni ile inayotambua umuhimu wa maadili ya kitaifa na hasa uwepo wa Mungu huku ikitoa fursa kwa wananchi kumiliki uchumi wao… Katika mjadala huo ulioandaliwa na Baraza la Madhehebu ya Dini Kuhusu Amani Tanzania (IRCPT), Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa IRCPT, Jaji Raymond Mwaikasu, alisema katiba ndiyo msingi wa nchi unaotoa mwongozo wa namna nchi itakavyoendeshwa kwa manufaa ya umma."
Kimsingi, makala hii, inaeleza kwamba, wajumbe wa IRCPT walikubaliana kwamba katiba mpya itambue "uwepo wa Mungu"; na kwamba katiba mpya yafaa itambue tunu muhimu zilizotufikisha hapa kama Taifa, kwa maana ya "maadili ya kitaifa" kama vile "uhai," "afya bora," "maarifa," "ndoa," "familia," "udugu," "amani," "uhuru wa kuabudu," na "uhuru wa dhamiri."
Miongoni mwa tunu hizi kuna "tunu elekezi" ("instrumental goods") kwa maana kwamba tunu moja inakuwa ni daraja kuelekea katika kufanikisha tunu nyingine. Mifano ni "maarifa," "uhuru wa kuabudu," na "uhuru wa dhamiri." Lakini, si kila tunu ni tunu elekezi. Tunu elekezi ni daraja kuelekea "tunu za msingi" ("basic goods").
Kwa mfano: elimu inatusaidia kupata ajira, ajira inatusaidia kupata pesa, pesa inatusaidia kununua chakula, na chakula kinatusaidia kujenga afya ya mwili. Mlolongo huu hauwezi kuendelea mpaka mbinguni.
Kwa hiyo, tunasema kwamba afya ni tunu ya msingi au tuseme tunu ya mwisho katika mlolongo huu.
Ukimwuliza mtu kwa nini unajenga afya ya mwili wako atakwambia "basi tu". Vivyo hivyo ukimwuliza mtu akwambie kwa nini hapendi wengine wamwue, atakwambia "basi tu". Uhai pia ni tunu ya msingi. Ziko tunu za msingi nyingine pia. Viongozi wa dini walikuwa wanaongelea tunu za aina hizi mbili.
Lakini, walipendekeza jambo lenye utata kwa sababu moja. Tanzania ya leo kuna Wakristo wapatao 30%, Waislam wapato 35%, na wafuasi wa dini za asili (African Traditional Religions) wapatao 35%.
Katika taifa la aina hii "uwepo wa Mungu" si tunu ya kitaifa kwa sababu moja kuu. Makundi haya tofauti yanaabudu "miungu" tofauti, kiasi kwamba katiba inayotambua "uwepo wa Mungu" itakuwa imechagua "muungu" mmojawapo na hivyo kuwakataa "miungu" wengine. Pia itakuwa imewalazimisha wasioamini katika "uwepo wa Mungu" kumkubali.
Hivyo, katika mazingira haya, tunu ya “uhuru wa dhamiri” ni "tunu elekezi" kwa maana kwamba ni daraja kuelekea tunu nyingine kama vile uhuru wa kila raia kuabudu miungu anaowamini ("freedom of worship"), na "uhuru wa kutoabudu miungu wowote kama raia haamini katika uwepo wa "miungu" ("freedom of non-worship").
Lakini, kama katiba ya nchi itatambua "uwepo wa Mungu" kama mwandishi huyu wa Kiongozi anavyoripoti, basi tunu hizi mbili zinaondoka. Mhariri wa gazeti la Kanisa Katoliki alipaswa kuliona jambo hili, na hivyo kujizuia kuchapa makala hiyo.
Makala nyingine iliandikwa na kuchapishwa katika gazeti hilohilo la Kiongozi toleo namba 49.
Makala hiyo ilibeba kichwa cha maneno "Tusidanganyane ushoga ni janga". Kupitia makala hii, mwandishi amewasilisha kwa umma hoja yenye muundo wa kimantiki ufuatao:
“Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron amesisitiza (kufuta) misaada kwa nchi ambazo sheria na katiba zao hazitambui (ushoga) na ndoa ya jinsia moja.
Nionavyo mimi, ushoga (na ndoa ya jinsia moja) ni janga”, kiasi kwamba, “si kitu cha kufumbia macho”, kwani, ni “utamaduni ambao si wetu” na (ni kitu ambacho) “kimekatazwa hata katika vitabu vitakatifu (vya) dini zote.
‘’Kwa hiyo, tunapoelekea kwenye kutafuta katiba mpya, jambo hili (la mashoga na ndoa ya jinsia moja), kama lilivyopendekezwa na Cameron, lisifikiriwe wala kuungwa mkono na kila mmoja anayeitwa Mtanzania na mwenye uchungu na nchi yake.”
Mwandishi huyu alikuwa akimjibu David Cameron, Waziri Mkuu wa Uingereza. Hivi karibuni, akiongea na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Cameron amenukuriwa kusema maneno yafuatayo yaliyowakera wengi:
"Britain is now one of the premier aid givers in the world. We want to see countries that receive our aid adhering to proper human rights, and that includes how people treat gay and lesbian people… British aid should have more strings attached, in terms of do you persecute people for their faith…, or do you persecute people for their sexuality (for example, through unjust discrimination against gay and lesbian people who want to contract same-sex marriage)? We don't think that's acceptable (on grounds of human dignity)."
Hoja ya Cameron nitaihakiki kupitia makala nyingine ili kuonyesha ubovu wake. Kwa sasa nitatumia muda mwingi kuihakiki hoja ya mwandishi yule wa Kiongozi. Kimuundo sina tatizo na hoja hiyo kwani vigezo vyote vya msingi vimezingatiwa.
Hata hivyo, katika muktadha wa maudhui, hoja hii imesheheni “maudhui yasiyokidhi viwango stahiki”. Kimsingi, hoja hii ina makosa makubwa matano ya kimaudhui.
Makala hii ni kwa ajili ya kuonyesha makosa yaliyo katika hoja hii, kubainisha hoja za watu wengine zenye makosa kama haya, na hatimaye kujazia pale ambapo mwandishi amepwaya.
Kosa la kwanza ni kwamba, ameshindwa kutofautisha kati ya “hali ya ushoga” (“homosexual condition”) na “matendo ya kishoga” (“homosexual acts”). Kwa sababu hii amejikuta anafanya kosa la kupinga “ndoa ya jinsia moja” na wakati huo huo kupinga “ushoga”. Jambo hili si sawa hata kidogo.
Inawezekana amefanya hivi kwa bahati mbaya. Lakini pia, inawezekana amefanya hivi kwa sababu zinazotokana na dhamira yake ya kutekeleza mkakati wa kusindika unyanyapaa dhidi ya ushoga (stigmatisation strategy against homosexuality).
Kama hili la pili ni kweli, basi, mkakati wake hauwezi kufanikiwa kuteka akili za binadamu kila mahali, kila wakati na kwa kila mtu. Ukweli ni kwamba, japo inawezekana kupinga “ndoa ya jinsia moja”, haiwezekani kabisa kupinga “ushoga.” Yaani, inawezekana kupinga “uhusiano wa kishoga” lakini haiwezekani kupinga “hali ya ushoga.”
Kosa la pili lililofanywa ni kushindwa kutofautisha kati ya “hali ya ushoga” (“homosexual condition”) na “utamaduni” wa kishoga (“gay culture”). Japo tunaweza kuwa na utamaduni wa kishoga, lakini ushoga si, na hauwezi kuwa utamaduni. Tuone utamaduni ni kitu gani kwa ufupi kabisa.
Utamaduni ni kusanyiko la imani zinazoshikiliwa na kikundi cha watu kuhusu mambo yafuatayo, kati ya mengine: namna ulimwengu wa maumbile unavyofanya kazi (ontological beliefs), jinsi ulimwengu wa wanadamu unavyofanya kazi (anthropological beliefs), malengo yanayopaswa kufukuziwa na wanadamu (axiological beliefs), jinsi wanadamu wanavyopaswa kuenenda katika sekta mbalimbali za maisha yao (moral beliefs), utaratibu wa kupata na kutofautisha kati ya maarifa ya kweli na maarifa ya uongo (epistemological beliefs), utaratibu wa kutofautisha kati ya hoja sahihi na hoja potofu (logical beliefs), na nafasi ya miungu katika ulimwengu na maisha ya wanadamu (theological beliefs).
Imani hizi kwa pamoja hujenga msingi wa mitazamo na matendo ya wana kikundi; na kwa pamoja, haya hukitofautisha kikundi kimoja cha watu na kingine. Hii ndiyo sababu tunasema kwamba utamaduni ni kitambulisho cha kabila, au taifa au jamii nyingine yoyote.
Tofauti na mwandishi wetu anavyofikiri, ushahidi wa kisayansi uliopo unaonyesha kuwa “hali ya ushoga", kwa maana halisi ya ushoga, si zao la utamaduni.
Hivyo, ushoga si mtazamo wala tabia za kimatendo. Ushoga ni maumbile. Kwa hiyo, kama “ushoga ni janga" kama mwandishi anavyodai, basi, hili litakuwa ni "janga" la kimaumbile (“physical evil”).
Na hakuna binadamu anayeweza kulaumiwa kutokana na uwepo wa majanga ya kimaumbile kama vile mafuriko, tetemeko la ardhi, u-makengeza, u-mashoto, uzeruzeru, na u-kigugumizi.
Sana sana tunapaswa kuwalaumu miungu, ambao tunaambiwa kwamba wanaweza kufanya kila kitu siku zote (“omnipotent”), kwa kushindwa kuingilia kati ili kuzuia majanga haya.
Kosa la tatu lililofanywa na mwandishi ni kushindwa kutofautisha kati ya “hali ya ushoga” (“homosexual condition”) tunaouongelea leo na “matendo ya kisodoma” yanayoripotiwa katika misahafu. Ni kweli kwamba, misahafu inakataza matendo kama vile "tendo la ulawiti", "tendo la ufelasio", n.k.
Lakini, katika misahafu hii hatuna ushahidi kama matendo haya ama waliokusudia kuyafanya au walioyafanya walikuwa mashoga au hapana.
Matendo kama vile "tendo la ulawiti" na "tendo la ufelasio", yanaweza kufanywa kati ya mwanamume na mwanamume au kati ya mwanamume na mwanamke. Wanaume wanaodai haki hewa ya kuoana wanakuwa wanakusudia kufanya “tendo la ulawiti”. Hawa ni mashoga na wanataka kufanya “tendo la kishoga.”
Na kwa upande mwingine, tafiti zangu zinaonyesha kuwa, kuna wake na waume ambao tayari wamekubaliana kuwa watakuwa wanapongezana kimapenzi mara tano kwa mwaka, yaani siku ya Pasaka, Krismasi, Mwaka Mpya, siku ya kuzaliwa Mume na siku ya kuzaliwa mkewe. Wanapongezana kwa kufanya “tendo la ulawiti”. Lakini hawa si mashoga na wala hawafanyi “tendo la kishoga.”
Itaendelea
Toa maoni yako