Tunamzomea Bocco kwa faida ya nani?

KATIKA mechi 18 alizoanza msimu huu, mshambuliaji wa Azam FC, John ‘Adebayor’ Bocco, amepachika wavuni mabao 15 katika Ligi Kuu ya Tanzania.

Hii ni rekodi bora zaidi kwa mshambuliaji wa Kitanzania msimu huu. Lakini, misimu miwili iliyopita, Bocco alifunga mabao 12 na 14 kwenye msimu mmoja na kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa msimu uliopita.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Bocco –ambaye ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu, alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi lililofanyika visiwani Zanzibar ambako timu yake ilitwaa kombe. Labda hapo bado hujapata picha kamili kumhusu huyu mchezaji!

Katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, Azam ilimleta nchini mshambuliaji hatari kutoka Ghana, Abdul Wahab Yahya, kucheza katika timu yao.

Kwa wasiofahamu, Wahab alikuwa mfungaji bora namba tatu katika Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita. Hata hivyo, raia huyo wa Ghana hakufua dafu kwa Bocco na ndiyo maana amerejea kwao baada ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza.

Michael Kipre Tchetche, mshambuliaji mahiri kutoka Ivory Coast aliyekuwa mfungaji bora wa Kombe la CECAFA mwaka juzi, anacheza timu moja na Bocco lakini hajafikia nusu ya mabao ambayo Mtanzania huyo amefunga msimu huu.

Bocco amefunga karibu katika mechi zote anazocheza dhidi ya vigogo wa soka Tanzania, yaani Simba na Yanga. Bocco alifunga pia katika fainali ya Kombe la Mapinduzi wakati timu yake ikitwaa kombe.

Sifa moja kubwa ya mchezaji mkubwa ni kwamba huwa anafanya mambo makubwa katika mechi kubwa. Huyu kijana tayari ana sifa hiyo.

Naomba nirudie, Bocco ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu. Hata hivyo, nimesikitishwa na vitendo ambavyo kijana huyu amekuwa akifanyiwa na wale wanaojiita mashabiki wa soka hapa nchini.

Kwa wanaokwenda Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi za timu ya taifa, watakuwa wamebaini namna mashabiki wa soka wanavyompa wakati mgumu kijana huyu kulitumikia taifa lake.

Bocco amekuwa akizomewa na mashabiki katika karibu mechi zote ambazo amepewa nafasi na walimu kucheza. Matokeo yake, kiwango chake katika timu ya taifa kimekuwa kikiathirika.

Na hapa ndipo linapokuja swali langu kubwa la makala hii ya leo, Watanzania wanamzomea Bocco kwa faida ya nani?

Bocco ni tumaini la Tanzania

Kwa maoni yangu, Bocco ni tumaini la Tanzania kwa miaka walau 10 ijayo kama atatumiwa vizuri. Hao wanaomzomea Bocco, wana mbadala wake? Je, ni Watanzania kweli? Kama ni Watanzania; je, uzalendo wao umejitosheleza mioyoni mwao?

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen, amekuwa akilalamika kwamba tatizo kubwa la Tanzania kwa sasa ni kukosa mshambuliaji wa maana.

Na hili ndilo tatizo pia alilokuwa nalo mtangulizi wake, Marcio Maximo. Tanzania haizalishi tena washambuliaji wa kutisha kama ilivyokuwa zamani.

Kwa bahati nzuri, kuna vijana watatu wamejitokeza hapa nchini ambao wanaonyesha kila dalili kuwa watakuja kuwafuta machozi Watanzania katika muda si mrefu kutoka sasa.

Vijana hao ni Bocco, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wote wa TP Mazembe ya DR Congo.

Najua wako vijana wengi wanaochipukia vizuri katika safu ya ushambuliaji hapa nchini lakini hawa watatu ni bora zaidi. Nilitarajia Watanzania wawape moyo vijana hawa lakini badala yake wanazomewa.

Nimemuona Bocco akifunga magoli magumu katika klabu yake ya Azam, lakini nimemuona akikosa magoli rahisi wakati akiichezea timu ya taifa. Hii yote ni kwa sababu ya kukosa kujiamini.

Na hawezi kujiamini wakati mashabiki wake wanamzomea kuanzia kosa lake la kwanza katika dakika ya kwanza ya mchezo hadi atakapotolewa. Naomba nirudie, ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu.

Makosa ni darasa kwa Bocco

Watu wanatarajia nini kutoka kwa kijana wa miaka 21 ambaye ndiyo kwanza anakua kama mwanasoka? Huu ndiyo umri ambao Bocco anaruhusiwa kufanya makosa na kujifunza kwayo.

Mashabiki wa kweli wa soka wanatakiwa kumpa kijana huyu kila aina ya uungwaji mkono inayohitajika. Uungwaji mkono kwa njia ya mawazo au ushauri na maelekezo ya kiufundi. Apewe sapoti si kumzomea.

Kwa maoni yangu, huyu ni mchezaji ambaye anatakiwa kuangaliwa na kuboreshwa kwa maslahi ya taifa letu hili. Miaka mitatu ijayo ambapo atakuwa amewiva zaidi kimwili na kiakili, Tanzania itajivunia kuwa na mchezaji kama yeye.

Lakini, kama tutaendelea na utaratibu wetu wa kumzomea, taifa letu linaweza kujikuta limepoteza mchezaji muhimu sana. Katika soka la Tanzania ambapo wataalamu wa saikolojia ya wachezaji ni kama vile hakuna, ni rahisi sana kumtoa mchezaji mchezoni.

Kwa wanaofuatilia soka la Tanzania, watabaini kuwa hiki ni kipindi cha mpito. Kuna kizazi kinaondoka na kuna kizazi kipya kinaingia.

Kizazi kipya ni akina Bocco, Samatta, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Hussein Javu, Mwinyi Kazimoto na wengineo wengi. Hawa wote wanahitaji sapoti kutoka kwa mashabiki na si kuzomewa kila wanapofanya makosa.

Kwa nini Bocco na si wengine?

Kuna mtakaouliza kwa nini nimetumia mfano wa Bocco pekee wakati kuna vijana wengi wanachipukia siku hizi. Majibu yangu ni kwamba huyu ndiye anayeongoza kwa kuzomewa na hili linaniuma kwa sababu ni kijana mwenye uwezo mkubwa sana.

Kwa wanaofuatilia soka la Uingereza, watakuwa wamepata habari kuhusu mchezaji anayeitwa Andrew Alexander Cole (Andy Cole). Huyu ni mshambuliaji mahiri katika historia ya Ligi Kuu ya England lakini hakupata mafanikio katika timu yao ya taifa.

Wachambuzi wanadai kwamba kilichomponza Cole ni kule kuzomewa kwake mara kwa mara na mashabiki kila alipopewa nafasi katika timu yao ya taifa.

Matokeo yake Cole akawa na sura mbili; kiwembe kwenye ngazi ya klabu lakini butu anapokuwa timu ya taifa. Bahati nzuri Waingereza walikuwa na Alan Shearer, Les Ferdinand, Ian Wright na Teddy Sheringham ambao wangeweza kutumika bila ya wasiwasi wowote kwa vile walikuwa na ama kiwango sawa na Cole au pengine kumzidi.

Tatizo ni kwamba, Tanzania hatuna mtu kama Bocco hivi sasa na pengine kwa miaka mitano ijayo. Habari njema ni kwamba kijana huyu atakuwa hatari zaidi huko tuendako.

Maana ya urefu wa Bocco

Wachezaji warefu kama Bocco wana tabia ya kuchelewa kushika kasi kwa sababu ya maumbo yao. Wanasaikolojia ya soka wanaamini kwamba kadri umri wa wachezaji wa aina hii unavyoongezeka, ndivyo ubora wao unavyoongezeka pia.

Kadiri umri unavyoongezeka, ndivyo wanavyokuwa na busara zaidi, uimara zaidi, shabaha zaidi na ujanja zaidi. Wanakuwa washambuliaji bora zaidi kuliko walivyokuwa vijana.

Sasa kwa nini tunataka kuipoteza bahati hii kwa Bocco? Tunataka kumfaidisha nani kwa kumzomea au kumfanyia kijana huyu vitendo visivyo vya kiungwana?

 

One thought on “Tunamzomea Bocco kwa faida ya nani?”

  1. laizer says:

    urefu wa boko sio tatitizo , ni muda anatkiwa kupewa kw umri wa miaka 21 ana mabao mengi yamebaki miguuni mwake what he needs is just time na mashabiki kuwa wavumilivu na kuwa na imani naye tujivunie ni moja wa soka chipukizi wa taifa letu .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *