Tunatafuta majina ya timu badala ya ubora? Mwaka 2016 uende zake tu!

ZIMEBAKI siku 16 kabla ya kumalizika kwa mwaka 2016 na kuingia mwaka 20178.

Hizi si siku nyingi. Ni siku chache ambazo ukizihesabu kwa vidole vya miguuni na mikononi unapata idadi kamili ya siku hizo na bado viungo hivyo vinabaki. Wacha mwaka 2016, uende zake tu.

Mwaka 2016 haukuwa na mafanikio ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Huu ulikuwa mwaka ulioichafua zaidi TFF kwa mipango yake kutofanikiwa. Mipango mingi mizuri ya TFF tuliishia kuiona kwenye makaratasi.

Suala la upangaji matokeo Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ratiba ya ligi kupanguliwa ovyo kwa sababu zisizo za msingi, kiwango chetu katika viwango vya FIFA kushuka kwa kiwango kkubwa mpaka kufikia nafasi ya 160, madeni na migogoro lukuki. Tunatakaje kuendelea na mwaka 2016? Tuuache uende zake.

Licha ya TFF kuwa na matukio mengi ya kumstaajabisha kila mpenda soka, lakini tukio la kutoa nafasi kwa wadau wa soka kupendekeza majina ya timu za Taifa za Vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 za wanawake na wanaume, linaweza kutufungia mwaka 2016 na kutukaribishia mwaka 2017.

Wadau wameombwa kupendekeza majina kwa ajili ya timu hizo. Hivi bado tuko katika dunia ya kutafuta majina ya timu za taifa na kuacha kujiuliza juu ya ubora wetu kisha tujiiulize tulikwamia wapi 2016 na tufanye nini 2017? Kama tuna akili za namna hii, tujue tuna safari ndefu kupata mafanikio.

Muda huu ambao tumebakisha siku 16 kumalizika kwa mwaka tulihitaji kuwa na mijadala mingi ya wazi kuuzungumzia mpira wetu na nini kifanyike, lakini kutaka wadau wapendekeze majina – kwa timu zipi tulizonazo mpaka tuanze kupendekeza majina ya timu wakati huu?

Suala la kutafuta majina ya timu ni jambo dogo tu ambalo haliwezi kuwafanya wadau kukaa chini na kukuna vichwa kwa ajili ya kutafuta majina ya timu husika, tunatakiwa kukuna vichwa kujiuliza juu ya ubora wetu unaozidi kudidimia badala ya kuinuka.

Ubora na miundombinu ya timu ndio unaotakiwa tuanze nao na mambo mengine yafuate. Tunaanzaje kutaka majina ya timu bila kutazama ubora wa kiwango tulichonacho?

Ina maana kupendeza uwanjani ndio kipaumbele chetu bila kujali tuna kiwango cha namna gani?

Moja ya shida kuu tuliyonayo sasa ni kuwa hakuna kiongozi anayetenga muda wake kwa ajili ya maendeleo ya soka, kila kiongozi amejikita katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa TFF, mwakani.

Hali ya uongozi wa juu wa TFF kuwa katika hali hii pamoja na viongozi wa Mikoa, Wilaya ndio kumefanya tufikie katika hali hii ambayo tumefikisha nafasi ya 160, lakini hakuna aliyejali wala kushituka.

Kushika nafasi ya 160, kulitakiwa kumshitua kila mmoja wetu, lakini kilicho mbele wakati huu ni uchaguzi mkuu ambao walioko ndani wanataka kutetea nafasi zao na walioko nje wanataka kuingia ndani,.

Katika mazingira haya, nani atakayetenga muda wake kuhoji nafasi yetu ya 160 FIFA? Wacha mwaka 2016 uende zake. Sitamani kuukumbuka.

Uendeshaji wa mpira wetu ndiyo umefikia eneo hili la viongozi wa juu kutojali nafasi tuliyoko na wote wamekuwa wakiwaza kuishi maisha ya kesho, wakati majukumu yao ya leo hawajamaliza bado.

Muda huu tunaotaka kuutumia kuhamasishana kuyatafuta majina ya timu za taifa wote tuulizane ni sahihi muda huu kutafuta majina ya timu na kuacha kujenga miundombinu ya mpira wenyewe?

Kama mpira wetu ukisimama vyema, kila kitu kitawezekana na tutakuja kupata hadi wadhamini wa vifaa vya michezo ambao watataka kutuvalisha, lakini inakuwaje tunawaza kutafuta majina wakati tuna timu dhaifu inayoshuka katika nafasi za FIFA kila mwezi?

Kupendekeza majina ya timu hakutakiwi kuwekewa mabango na kufikia kuitwa hadi wadau na wao kupendekeza majina yao, wadau waitwe katika masuala ya kujadili mpira na maendeleo yake kiujumla.

Septemba 3 mwaka huu, kulikuwa na kongamano kwa ajili ya kujadili matatizo na maendeleo ya soka la Tanzania ambalo lilifanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, lakini hakuna hata kiongozi mmoja wa TFF, aliyehudhuria kongamano hilo.

Jukwaa hilo lililenga kuimarisha misingi ya uendeshaji wa soka na  mambo mengi yalijadiliwa katika siku hizo mbili ikiwemo kufahamu namna gani ya kuendesha vilabu vya soka pamoja na mpira wa miguu.

Lakini hakukuwa na mtu yeyote wa TFF, aliyefika katika kongamano hilo na hata Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambaye kwenye ratiba alionekana, hakuonekana kwenye jukwaa hilo huku kukiwa hakuna sababu iliyotolewa.

Makongamano ya namna hii ndiyo yanayojenga na kuimarisha masuala ya maendeleo, lakini kwetu haiko hivi na tunayaona masuala ya kawaida.

Unadhani mpira wetu unatokaje hapa ulipo? Mwaka 2016 uishe tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *